Showing posts with label KILIMO. Show all posts
Showing posts with label KILIMO. Show all posts

 



Happy Lazaro,Arusha 



WAKULIMA  wametakiwa kutumia mbegu bora, mbinu za kisasa za kilimo na mbolea zenye ubora ili kuongeza uzalishaji na kuondokana na changamoto ya mavuno duni jambo linalokwamisha maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.




Rai hiyo imetolewa na Mbunifu wa mbolea ya asili ya mazao mbalimbali , Albert Ssamawa Salimu  kutoka halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro  katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Themi ,Njiro.


 Ssamawa amesema  kuwa,banda hilo  linatoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbegu bora, mifumo ya umwagiliaji wa matone (drip irrigation) pamoja na teknolojia mbalimbali zinazoongeza tija shambani.



Ssamawa amesema moja ya ubunifu waliouleta katika maonesho hayo ni mbolea ya asili ya Sama Agro, ambayo imeandaliwa kutokana na samadi za wanyama na ndege bila kutumia kemikali na inafanya vizuri sana kwenye mazao kwani tayari wakulima wameshaanza kuitumia na kuona matokeo makubwa sana .


Amesema mbolea hiyo inaweza kutumika kwenye mazao mbalimbali ikiwemo mboga mboga, nafaka na mazao mengine ya biashara.



"mavuno madogo yanayotokana na wakulima wengi hutokana na ukosefu wa utaalamu wa matumizi ya mbolea pamoja na kutotumia virutubisho vinavyohitajika na mazao kwa wakati sahihi."amesema Ssamawa.


 Amesisitiza  kuwa, kama binadamu wanavyohitaji chakula, vivyo hivyo mimea huhitaji virutubisho vya kutosha ili kustawi na kuzalisha kwa kiwango kikubwa.



"mbolea ya Sama Agro imetengenezwa kwa kutumia mchanganyiko wa mbolea za kuku, popo, mbuzi na ng'ombe, na imeboreshwa kwa njia ya kitaalamu ili kuongeza ufanisi wake natoa wito kwa wakulima kutoka maeneo mbalimbali kufika kwenye banda hili kwa lengo la kuja kujionea teknolojia mbalimbali pamoja na mbolea hiyo ya asili."amesema .


 Ameongeza kuwa, matumizi yake hupunguza kiasi kikubwa cha mbolea kinachohitajika shambani kwani mkulima anaweza kutumia kiwango kidogo na kupata matokeo mazuri.



Amesema kuwa ,lengo la kuileta teknolojia hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane ni kuwapa wakulima fursa ya kujifunza, kuifahamu na kuanza kuitumia ili kuongeza uzalishaji na kipato chao. 


Ssamawa amefafanua  kuwa ,baada ya kuona matokeo chanya, wakulima wengi watanufaika na teknolojia hiyo na kuchangia kukuza kilimo chenye tija nchini.



 



Happy Lazaro,Arusha .



KAMPUNI ya  EFTA Tanzania imewazawadia  wakulima waliokopa zana za kilimo na kurejesha mikopo yao kwa uaminifu, kwa kuwarejeshea nusu ya riba waliyoilipa wakati wa marejesho ya mikopo hiyo.



Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA Tanzania, Nicomed Bohay wakati akizungumza katika hafla ya kukabithi hundi za rejesho la asilimia 50 ya riba kwa wateja waliorejesha mikopo yao kwa nidhamu hafla iliyofanyika katika maonesho ya nanenane Njiro.



Bohay amesema Taasisi hiyo imeamua kurejesha takribani shilingi milioni 100 kwa wateja wake nchini kama motisha ya ulipaji mzuri wa mikopo.



"jumla ya wateja 37 nchini tayari wamenufaika na mpango huo mwaka huu, huku kila mmoja akipokea kiasi tofauti cha fedha kulingana na kiwango cha riba alicholipa."amesema  Bohay .



 Amesema kuwa, mpango huo unawahusu wakulima waliokopa matrekta, matrela na zana nyingine za kilimo na kutekeleza masharti ya mikopo bila kuchelewa.


Bohay  amesema EFTA, ambayo hutoa mikopo ya zana mbalimbali bila kuhitaji dhamana na inaofisi nane nchini, inashiriki Maonesho ya Nanenane katika kanda tano za Arusha, Dodoma, Morogoro, Mbeya na Mwanza. 


Amesema  kuwa,mwaka huu taasisi hiyo imeamua kutumia maonesho hayo kuwatambua wateja wake bora na kuonyesha kuwa uaminifu katika ulipaji wa mikopo una manufaa ya moja kwa moja.


Amefafanua  kuwa mafanikio ya wateja katika ulipaji yameifanya EFTA kupunguza kwa kiwango kikubwa mikopo chechefu (NPL), ambayo kwa sasa ipo asilimia moja pekee.


Bohay ameongeza kuwa,kiwango hicho ni cha kuvutia katika sekta ya fedha na kimeiwezesha taasisi hiyo kuelekeza sehemu ya fedha ambazo zingetengwa kwa ajili ya mikopo chechefu kurudi kwa wateja wake kama zawadi.


Aidha, amewahimiza wakopaji wote nchini kujenga utamaduni wa kulipa mikopo kwa wakati, akisema rekodi nzuri ya mkopaji huwekwa kupitia mfumo wa Credit Reference Bureau wa Benki Kuu ya Tanzania na humrahisishia kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha siku zijazo.



 Amesema hatua hiyo inalenga kujenga uhusiano wa kudumu kati ya taasisi za fedha na wakulima, pamoja na kuhamasisha matumizi ya mikopo yenye nidhamu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo.


Wakizungumza mara baada ya kukabithiwa mfano wa hundi hizo wakulima hao walishukuru kwa namna taasisi hiyo inavyowajali na kuwapa motisha wa kuendelea kukopa zaidi.


"Kitendo kilichofanywa na Taasisi hii ni mfano wa kuigwa na taasisi zingine kwani kinatupa moyo wa kuendelea kukopa zaidi zana za kilimo ambapo taasisi hii imekuwa mkombozi mkubwa sana kwa wakulima."amesema .



Kwa upande wao wateja walionufaika na mkopo huo , Sebastian Gwalku kutoka  Mkoa wa Manyara amesema kuwa ,amekuwa  mteja wa EFTA kwa kupata mkopo uliomwezesha kukuza shughuli  za biashara ambapo kupitia mkopo huo ameweza  kuendeleza biashara na kuongeza kipato.


"Leo ninafurahi sana kuwa miongoni mwa wanufaika wanaokabidhiwa hundi kama ishara ya kutambua uaminifu wetu katika kurejesha mikopo kwa wakati na nawashukuru sana EFTA kwa fursa hii na kwa kuendelea kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kufikia malengo yao."amesema .


"Ninawahamasisha wafanyabiashara wengine kutumia fursa zinazotolewa na EFTA na kuhakikisha wanarejesha mikopo yao kwa wakati ili nao waweze kunufaika na fursa kama hii."amesema .



 



Happy Lazaro,Arusha .


WAKULIMA  kanda ya kaskazini wametakiwa kutembelea banda la kampuni ya Kibo Seed katika maonesho ya nanenane ili kuweza kupata elimu  kuhusu matumizi ya  mbegu bora za mahindi na mbogamboga ili kuongeza uzalishaji.




 Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Afisa Uzalishaji wa Mbegu wa  kampuni ya Kibo Seed Co.Ltd ,Marko Msheishiwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya  nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Taso Njiro.


 Amesema  kampuni hiyo inashiriki Maonyesho ya Nanenane 2026 ikiwa na lengo la kuwaelimisha wakulima kuhusu matumizi ya mbegu bora za mahindi na mbogamboga ili kuongeza uzalishaji.



Ameongeza kuwa ,kampuni hiyo  inazalisha na kusambaza mbegu za mahindi kwa kanda mbalimbali za kilimo nchini, zikiwemo kanda ya chini, ya kati na ya juu, ili kuhakikisha kila mkulima anapata mbegu zinazolingana na mazingira yake.



Akizungumzia maandalizi ya maonesho ya mwaka huu, Msheishiwa amesema yameboreshwa zaidi kuliko miaka iliyopita, ambapo mazao ya maonesho yalipandwa kwa wakati, yakatunzwa vizuri na sasa yanaonyesha matokeo halisi ambayo yatawawezesha wakulima kujifunza kwa vitendo.


Ameongeza  kuwa, moja ya sifa zinazotofautisha mbegu za Kibo Seed na kampuni nyingine ni ubora wake, hususan kwa mahindi yanayofaa kuchomwa na kukobolewa, ambayo ni matamu na yanakubalika na watumiaji wengi.


Kwa upande wa uzalishaji, amesema mavuno hutegemea ukanda na aina ya mbegu inayotumika. Mbegu za ukanda wa chini zinaweza kutoa tani 2 hadi 2.5 kwa ekari, ukanda wa kati tani 3 hadi 3.5, huku ukanda wa juu ukifikia tani 4 hadi 5 endapo mkulima atafuata kanuni bora za kilimo.


Aidha, amesema changamoto kubwa inayowakabili baadhi ya wakulima ni kutokuchagua mbegu sahihi kulingana na ukanda wao wa kilimo pamoja na kutofuata kanuni za uzalishaji, ikiwemo kupanda kwa wakati, kutumia mbolea stahiki na kutunza shamba ipasavyo.


Aidha Msheishiwa ametoa wito kwa wakulima na wananchi kutembelea banda la Kibo Seed katika maonyesho ya Nanenane jijini Arusha ili kupata elimu kuhusu mbegu bora, kuona mashamba ya mfano na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa kampuni hiyo.


 Jumla ya wafugaji wa ng'ombe wa maziwa na wadau wa mnyororo wa thamani 92,831 (asilimia 30 wakiwa wanawake) kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamefaidika na Mradi wa Ushirikiano Jumuishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa Tanzania (TI3P). Mafanikio hayo yamefikiwa tangu kuzinduliwa kwa mradi huo mnamo Machi 2022.

Mradi huu unafadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Taasisi ya Bill & Melinda Gates. Unatekelezwa kwa ushirikiano na mashirika ya Heifer International, Land O’Lakes Venture37, na Tanager. Lengo kuu ni kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa, kuongeza tija, na kuboresha kipato cha wafugaji wadogo.

Uwekezaji na Miundombinu

Tangu kuanza kwake, mradi umefanikisha utoaji wa mikopo na ufadhili wa zaidi ya shilingi bilioni 42 kwa wasindikaji, wakulima, wasambazaji wa pembejeo, na wadau wengine. Fedha hizo zimesaidia:
  • Kuanzishwa kwa viwanda vipya vya kusindika maziwa.
  • Upanuzi na uboreshaji wa viwanda 17 vilivyopo kwa uwekezaji wa bilioni 22.8.
  • Ununuzi wa mitamba bora ya maziwa 3,330 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 11.09, hatua iliyoongeza uzalishaji wa maziwa nchini.

Huduma za Ugani na Uwezeshaji Viwanda

Mradi umeongeza upatikanaji wa huduma za ugani, pembejeo bora, masoko, na fursa za kifedha. Jumla ya viwanda 19 vya maziwa vimeshiriki katika programu za kukuza biashara (Enterprise Acceleration Interventions) ili kuongeza ufanisi wa utendaji, faida, na matumizi ya uwezo wa viwanda hivyo kusindika maziwa.

Kukuza Usawa wa Jinsia

Katika kuleta ukuaji jumuishi, TADB ilitoa ruzuku za ulinganifu (matching grants) za shilingi bilioni 1.4 kwa wafugaji wadogo 1,216, wakiwemo wanawake 397. Hatua hii imepunguza vikwazo vya kupata mikopo ya mitamba na kupanua uwekezaji.
Aidha, viwanda vitano vya maziwa vinavyomilikiwa na wanawake vilipokea vifaa vya kupatisha maziwa (pasteurization equipment) vyenye thamani ya shilingi milioni 75. Wanawake wengine watano wasindikaji walipokea ruzuku za TI3P, huku wasindikaji 12 wakipata ruzuku maalum za kukuza usawa wa jinsia katika biashara zao.

Ukusanyaji na Ubora wa Maziwa

Ili kuboresha mifumo ya ukusanyaji na ubora wa maziwa, mradi umeanzisha na kuimarisha Vikundi vya Wakulima (FPOs) 45 na Vikundi vya Wadau wa Maziwa. Vikundi hivi sasa vinakusanya zaidi ya lita 25,664 za maziwa kila siku, hatua inayoshirikisha masoko vizuri na kuongeza nguvu ya wakulima kupanga bei.
Akizungumza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Maziwa mkoani Iringa, Kuratibu wa Mradi wa TI3P, Joseph Mabula, alisema mradi umefanikisha ujenzi wa vituo 23 vya kukusanyia maziwa nchini kwa gharama ya uwekezaji ya shilingi bilioni 1.157. Utekelezaji huo ulifanyika kwa ushirikiano na wasindikaji, vyama vya ushirika, na washirika wa mradi.
Mabula alibainisha kuwa mradi huo pia unashughulikia changamoto za kisera na kisheria zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo. Unasisitiza pia masuala ya mtambuka kama usawa wa kijinsia na lishe ili kuhakikisha maendeleo endelevu. Alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana ili kutatua changamoto za tasnia ya maziwa na kutumia kikamilifu fursa zilizopo.

 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dr. Fabian Madele, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya maziwa nchini Tanzania kuimarisha ushirikiano ili kuongeza tija katika uzalishaji, usindikaji, na masoko ya maziwa. 

Hatua hiyo inalenga kuongeza kipato cha wafugaji na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.



Dr. Madele aliyasema hayo alipotembelea banda la maonesho la shirika la Heifer International Tanzania wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maziwa ya Kitaifa yanayofanyika mkoani Iringa.
Katika ziara hiyo, alijionea jinsi Heifer Tanzania inavyoshirikiana na serikali pamoja na wadau wengine katika kukabiliana na njaa na umaskini kupitia mbinu bora za ufugaji wa ng'ombe wa maziwa na maendeleo endelevu ya sekta ya mifugo.
Heifer Tanzania ilionyesha mafanikio ya miradi yake mbalimbali inayowasaidia wafugaji wadogo wa maziwa kuongeza uzalishaji, kupata masoko ya uhakika, na kuboresha maisha ya familia zao. Aidha, shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa maziwa kupitia mafunzo, uwezeshaji wa kifedha, na uimarishaji wa vikundi vya ushirika.

Dr. Madele alilipongeza shirika la Heifer Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya maziwa. Alisisitiza kuwa ushirikiano thabiti kati ya Serikali, sekta binafsi, na washirika wa maendeleo ni nguzo muhimu katika kufikia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu: “Boresha Biashara ya Maziwa, Linda Afya ya Mlaji, Ongeza Kipato na Changia Ukuaji wa Ochumi.”

Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa ya Kitaifa yanafanyika mkoani Iringa kuanzia tarehe 28 Mei hadi 1 Juni, yakikutanisha wadau wakuu kutoka sekta nzima ya maziwa kujadili fursa, changamoto, na mikakati ya kukuza uzalishaji, unywaji wa maziwa, na maendeleo ya masoko nchini Tanzania.




MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imetoa mafunzo kwa Mawakala wa Forodha waliopo Mpaka wa Namanga, wilayani Longido mkoani Arusha, kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa maombi ya vibali vya kuingiza na kutoa mazao nchini kupitia Dirisha Moja la Mfumo wa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS), uliounganishwa kutoka mfumo wa awali wa e-Kilimo.



Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Disemba 18, 2025 Namanga wilayani Longido, Afisa Kilimo wa COPRA Kanda ya Kaskazini, 

 Peter Kabelelo, alisema kuwa katika kuboresha utoaji wa huduma za vibali, Wizara ya Kilimo imeunganisha Mfumo wa e-Kilimo na Mfumo wa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS) ili mifumo hiyo iweze kusomana.


Alisema lengo la hatua hiyo ni kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za vibali ambazo hapo awali zilikuwa zikiombwa kupitia mfumo wa e-Kilimo. Alifafanua kuwa hapo awali mteja alihitajika kutumia mifumo mbalimbali kutoka taasisi tofauti ili kupata huduma moja, kama vile COPRA, TPHPA na TANCIS.


“Maboresho yaliyofanyika yamewezesha kuunganishwa kwa mifumo hiyo ili mteja atumie mfumo mmoja tu wa TANCIS kupata huduma kutoka taasisi mbalimbali kama COPRA, hivyo kurahisisha zaidi utoaji wa huduma,” alisema Kabelelo.

Aliongeza kuwa faida nyingine ya matumizi ya mfumo huo ni kupatikana kwa takwimu sahihi za mazao yote yanayosafirishwa nje au kuingia nchini, pamoja na kujua thamani ya mazao hayo kwa usahihi.


Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Rajabu Mmunda, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kusikiliza maoni na changamoto za Mawakala wa Forodha kuhusu matumizi ya mfumo wa TANCIS.


Aliwashukuru mawakala hao kwa kushiriki mafunzo hayo na kueleza kuwa changamoto walizozitaja zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha mfumo huo unawarahisishia utendaji wa kazi kama ilivyokusudiwa na Serikali.


Naye Wakala wa Forodha wa Kampuni ya A & ED Co. Ltd, Bw. Robynson Masai, aliishukuru COPRA kwa kuwapatia elimu hiyo, akisema kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kuufahamu vizuri mfumo wa TANCIS na namna unavyofanya kazi.


Hata hivyo, aliomba COPRA kuendelea kuwa karibu na mawakala hao ili kusaidia kutatua changamoto za kimfumo pindi zinapojitokeza na wanapohitaji msaada wa haraka.


Aidha, Wakala wa Forodha wa Kampuni ya Njechele Co. Ltd, Petro Mveyange, aliomba COPRA kufungua ofisi katika Mpaka wa Namanga ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa maombi ya vibali.

 



Na Wandishi Wetu


ZAIDI ya wakulima 62,000 wa mbogamboga na matunda nchini wamenufaika na mafunzo ya kilimo hicho yaliyotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga – Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable Center – WorldVeg) kwa lengo la kusaidia kuongeza uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.



Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kufunga rasmi utekelezaji wa mradi huo unaoitwa Accelerated Innovation Delivery Initiative (AID-I), wenye kauli mbiu isemayo "Kusherehekea ushirikiano, matokeo, na ubunifu katika mifumo ya mbegu, minyororo ya thamani, na lishe”, Meneja wa Programu wa WorldVeg – Tanzania, Colleta Ndunguru, amesema mradi huo umekuwa na tija toka kuazishwa kwake mwaka 2023 katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro pamoja na  Zanzibar.


“Mradi huu umegusa maeneo mbalimbali ikiwemo kusaidia wakulima kurasimisha biashara zao ili zitambulike kisheria, sambamba na kusambaza mbegu bora za mbogamboga kwa zaidi ya kaya 10,500,” amesema Ndunguru.


Aliongeza kuwa zaidi ya wakulima 62,000 wamenufaika toka mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Uboreshaji wa Mahindi na Ngano (CIMMYT) uanzishwe hapa nchii, huku takriban wazalishaji wa mbegu 10,684 wakipatiwa mafunzo,  asilimia 52 kati yao wakiwa wanawake na asilimia 29 vijana.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar, Dk Abdallah Ibrahim Ali, aliipongeza WorldVeg kwa mchango huo mkubwa katika kuinua kilimo cha mbogamboga na matunda hapa nchini.


“Kupitia mradi huu, maelfu ya vijana wamenufaika , huku zaidi ya miche 446,021 ya mboga ikisambazwa katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Dk Ali.


Amesisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa mradi huu katika maeneo ambayo bado haijafikiwa ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaikan na kuongeza tija ya kilimo katika uchumi wa taifa.



Naye Mratibu wa Nchi kutoka CIMMYT, Peter Ojukwu, amesema sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, ambayo huathiri usalama wa chakula.


Amesema kuwa kutokana na changamoto hizo, CIMMYT ilimua kuanzisha mradi huo wa AID-I ili kukabiliana na tatizo la njaa na lishe duni kwa kutoa elimu na mafunzo bora juu ya uzalishaji wa mbegu na uongezaji thamani wa mazao, hasa mbogamboga na matunda.


“Awali tulikuwa tunazalisha gunia 40 za vitunguu kwa heka moja, lakini baada ya kupewa mafunzo haya, hivi sasa tunazalisha gunia kati ya 100 hadi 120 kwa heka,” alisema Bw. Slaa.


Naye Maryam Salim kutoka Wilaya ya Chake Chake Pemba, alisema mradi huo umemuwezesha kupata kipato endelevu kwa kuzalisha mbegu za mchicha lishe na kuziuza kwa wakulima wenzake.


Mradi wa AID-I umewezeshwa na ushirikiano kati ya WorldVeg na mashirika washirika mbalimbali ikiwemo  RIKOLTO, IDP, World Vision, HollandGreentech, Kilimo Trust, SAIPRO, Froresta, Milele Zanzibar Foundation, na Wizara ya Utalii na Urithi – Zanzibar.





Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla, ametembelea Maonesho ya Wakulima (NaneNane) yanayofanyika kitaifa katika uwanja wa Nzuguni, Jijini Dodoma, leo tarehe 8 Agosti 2025.



Katika ziara hiyo, Kihulla alifika katika banda la WMA na kuwapongeza watumishi wa Wakala kwa kazi nzuri ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya vipimo, tangu kuanza kwa maonesho hayo. Alieleza kuridhishwa na namna Wakala unavyoshiriki kikamilifu katika kutoa elimu ya vipimo kwa wananchi.



Akiwa bandani hapo, alisema:
"Tuendelee kutumia majukwaa mbalimbali kutoa elimu ya vipimo kwa wananchi ili waelewe haki yao ya kupata huduma kwa vipimo sahihi, lakini pia na wajibu wao wa kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi katika sekta mbalimbali."


Aidha, alisisitiza kuwa utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo haupaswi kuishia kwenye maonesho pekee, bali uendelezwe katika ngazi zote za jamii kwa lengo la kuhakikisha haki inapatikana kwenye mnyororo mzima wa biashara na huduma.

"Ni muhimu jamii ikaelewa ni kwa namna gani Serikali kupitia WMA inawalinda kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika sekta mbalimbali ni sahihi na vinatumika kwa usahihi," aliongeza.


Mbali na kutembelea banda la WMA, Kihulla pia alifanya ziara katika mabanda mengine mbalimbali, yakiwemo ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ili kujionea huduma na bidhaa zinazotolewa kwa wananchi.

Maonesho ya NaneNane hutoa fursa kwa taasisi za serikali, binafsi na wananchi kushiriki katika kubadilishana maarifa, teknolojia na huduma mbalimbali zinazolenga kuendeleza sekta ya kilimo na viwanda nchini.



Na Mwandishi Wetu, Arusha
TANZANIA inategemewa kuzalisha wataalamu wa uzalishaji wa mbegu bora chotara za mazao mbalimbali baada ya Chuo Kikuu cha Taiwan kuonesha utayari wa kuanzisha programu za mafunzo katika Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendeshaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika ‘World Vegetable Centre’ kilichopo Tengeru mkoani Arusha.
 

Akiongea wakati wa mafunzo yanayohusu uzalishaji mbegu bora ya mazao mbalimbali yanayohimili magonjwa na ukame, Dk. Sognigbe N’Danikou, mtaalamu wa uzalishaji mbogamboga asili na utunzaji kutoka katika taasisi hiyo jijini hapa, amesema kuwa ushirikiano na chuo hicho unalenga  kukuza kilimo hapa nchini kupitia maeneo mbalimbali.
 
 
Amesema miongoni mwa maeneo hayo ni kufanya tafiti mbalimbali kuhusiana na uzalishaji na utunzaji wa mbegu ‘chotara’ zenye kukua kwa haraka na kuhimili magonjwa na ukame.
Amesema kupitia mpango wa Taiwan wa kukuza Kilimo cha Mbogamboga barani Afrika ( Taiwan-African Vegetable Initative (TAVI), kituo hicho kitashirikiana na taasisi nyingine hapa nchini ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kukuza sekta ya kilimo, kuzalisha wataalam wa kutosha na kuwafikia wakulima wengi zaidi.  
 
Amesema maeneo mengine ambayo Tanzania itafaidika kupitia ushirikiano huo ni pamoja na uzalishaji wa wataalamu wa kutosha, kuongeza uwezo wa kufanya utafiti na ubadilishanaji wa programu za mafunzo (scholarships) juu ya uzalishaji chakula bora na lishe. 



 

 
Naye Profesa Chau-Ti Ting kutoka Chuo Kikuu cha Taiwan amesema kuwa Tanzania itakuwa kitovu cha uzalishaji mbegu bora na uhifadhi kupitia ushirikiano huo wenye lengo la kukuza sekta ya kilimo hapa nchini.
 
“Pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano huu, tunategemea chuo chetu kikuu cha Taiwan kuanzisha kozi maalum katika taasisi hii ya kimataifa hapa Arusha,” amesema Profesa Ting.


 
Naye Profesa Hung –Vi Wang amesema ushirikiano huu una lengo la kuangalia njia bora za uzalishaji wa mbegu bora kupitia tafiti mbalimbali na kuangalia namna wanavyoweza kuanzisha program za mafunzo katika taasisi hiyo mkoani Arusha.
 
Mmoja wa wanaohudhuria mafunzo hayo, Daktari Aloyce Kundy kutoka Benki ya Vinasaba vya Mimea iliyo chini ya Mamlaka ya Viuatilifu na Mimea (TPHPA) amesema Tanzania imekua na mahusiano mazuri na Taiwan katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo kwa kufanya tafiti zenye kukuza sekta hiyo hapa nchini.
 
Naye Magdalena Kiungo, mwanafunzi wa Chuo cha Taasisi ya Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela anayesomea uzalishaji wa mbegu bora za kisasa amesema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya kilimo, hasa katika uzalishaji wa mbegu bora zenye kutoa mazao mengi na kuhimili ukame.
 
“Nimefurahi kuwa mmoja wa washiriki wa mafunzo haya na ushirikiano huu utakuwa na tija na kutuwezesha sisi maofisa wa kilimo wa miaka ijayo kuwa na utaalamu wa kimataifa,” amesema Bi. Magdalena.
 

 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa Watanzania kutumia ipasavyo fursa ya maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane 2025), ili kujifunza mbinu bora za uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya taifa.



Akizungumza tarehe 4 Agosti 2025 katika viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma, Dkt. Chana alisema maonesho hayo yanaelimisha wananchi kuhusu uzalishaji bora wa mazao, pamoja na kukuza utalii wa vyakula.

"Naomba nitoe rai kwa Watanzania tutembelee maeneo haya ya maonesho, kuna bidhaa nzuri, kuna utafiti, kuna elimu, kuna mbegu, vivutio vya kila aina na pia unapokuja katika maonesho haya unapata elimu ya aina mbalimbali," alisema Dkt. Chana.



Aliongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mazao na kuongeza mapato kwa taifa na wananchi, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

"Tunapozalisha bidhaa tunaongeza thamani, tutapata na mapato, lakini tunataka watalii waje kuona utajiri wa Tanzania wa vyakula mbalimbali. Ndiyo maana leo tumekuwa na mabanda mahali hapa kuonesha bidhaa zetu za Wizara ya Maliasili na Utalii. Tunataka waje kuona utalii wa vyakula, kama ni chai yote hiyo ni aina ya utalii," alieleza.



Katika hatua nyingine, Waziri Chana alibainisha kuwa wizara yake inaendelea kutekeleza mikakati ya kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyama wakali kwa kutumia teknolojia rafiki na kutenga maeneo maalumu ya kuwalinda wananchi.

"Wizara itaendelea kutenga maeneo maalumu na kutumia ndege nyuki ili kuepusha mwingiliano na migogoro ya mara kwa mara kati ya wananchi na wanyama pori, hususan wale wakali na waharibifu," alisema Dkt. Chana.



Aidha, alitoa pongezi kwa Wizara ya Kilimo kwa kufanikisha maonesho hayo katika kanda mbalimbali nchini, hatua inayowapa fursa Watanzania wengi kujifunza mbinu bora za kilimo, ufugaji na uvuvi.

"Ni jambo la kupongeza kuwa sasa hivi tuna maonesho ya Nanenane katika kanda zaidi ya nane. Hii ni fursa kwa Watanzania wengi zaidi kupata elimu, kushiriki ubunifu, na kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi," alisema.

Maonesho ya Nanenane huandaliwa kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti kwa lengo la kuhamasisha maendeleo ya sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kutumia maarifa ya kitaalamu, ubunifu na teknolojia ili kuongeza uzalishaji na tija kwa taifa.



Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, ametoa wito kwa Watanzania kutoka kada mbalimbali kutembelea maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) yanayoendelea kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, pamoja na kwenye kanda nyingine nchini, ili kujifunza kuhusu vivutio vya utalii, shughuli za uhifadhi na fursa za uwekezaji katika sekta ya maliasili na utalii.



Akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika viwanja hivyo, Chana alisema maonesho ya mwaka huu yamekuwa ya kipekee kwa kuwa yameunganisha sekta mbalimbali zinazochangia maendeleo ya nchi kupitia ushiriki wa taasisi za serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.


“Natoa wito kwa Watanzania kutembelea maonesho ya Nanenane katika kanda zote yanapofanyika ili wapate elimu ya vivutio vya utalii tulivyonavyo, fursa za uwekezaji, elimu ya uhifadhi, na ufugaji nyuki. Wizara inaendelea kuongeza mazao mbalimbali ya utalii ikiwemo utalii wa vyakula na utalii wa kilimo kwa kuwa maonesho haya yamefunganisha sekta mbalimbali ili tuendelee kutangaza nchi yetu na kupata maendeleo kwa pamoja,” alisema Dkt. Chana.



Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake imekuwa ikishiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa rasilimali za taifa, matumizi endelevu ya maeneo yaliyohifadhiwa, pamoja na kutangaza vivutio adimu vya utalii vilivyopo nchini.


Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki maonesho hayo, ikitangaza vivutio mbalimbali vya kipekee vinavyopatikana ndani ya eneo hilo. Vivutio hivyo ni pamoja na Kreta ya Ngorongoro, Empakai, Olmoti, Mlima Lolmalasin (wa tatu kwa urefu nchini), Maporomoko ya Maji ya Endoro, na Mapango ya Tembo.


Aidha, mamlaka hiyo inatangaza vivutio vya utalii wa malikale kama Makumbusho ya Olduvai, Nyayo za Laetoli, mchanga unaohama, pamoja na utalii wa anga kupitia Kimondo cha Mbozi na Mapango ya Amboni mkoani Tanga. Mapango haya yana historia ya kipekee ikiwa ni pamoja na mchango wake katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika, na kuonesha urithi wa kihistoria wa watu wa mkoa wa Tanga.


Wageni wanaotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii pia wanapata fursa ya kuona mubashara baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro kupitia skrini kubwa ya televisheni iliyofungwa katika banda hilo.


Kaulimbiu ya maonesho ya Nanenane kwa mwaka 2025 ni: *“Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”*, ikiwa ni mwendelezo wa kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za uzalishaji pamoja na uongozi bora kwa maendeleo ya taifa.


 
Wataalamu wa kilimo na wadau mbalimbali wameitaka serikali kulitangaza rasmi ugonjwa wa Fungashada unaoshambulia migomba, kama janga la kitaifa, wakieleza kuwa hali hiyo itasaidia kuongeza jitihada za kudhibiti maambukizi na kulinda zao hilo muhimu kwa usalama wa chakula na kipato cha wakulima.


Hemadi Msofe, mchambuzi wa mbegu na mtaalamu kutoka Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), alisema kuwa uzalishaji wa mbegu bora za migomba bado uko chini kutokana na ukosefu wa wazalishaji wa kutosha pamoja na rasilimali.
“TOSCI ilianza kuandaa viwango tangu mwaka 2020 kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha mbegu bora zinapatikana,” alifafanua.
Kwa upande wake, Filbert Luhunga kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) aliwahimiza wakulima kutumia taarifa za kisayansi kufanya maamuzi sahihi, huku akitoa tahadhari dhidi ya matumizi ya miche isiyothibitishwa.
“Matumizi ya miche isiyokaguliwa ndiyo chimbuko la maambukizi mapya,” alisema.
Katika kuonyesha uzito wa tatizo hili, mmoja wa wataalamu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea Tanzania (TPHPA), ambaye hakutaka jina lake litajwe, alieleza kuwa bado kuna mapungufu ya kimkakati katika kukabiliana na janga hilo.
“Tunaendelea kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili kama USAID. Hatujaitangaza BBTV kama janga la kitaifa, na huo ni udhaifu mkubwa wa kimkakati,” alisema.
Aidha, Godfrey Amba, mkulima kutoka Kata ya Kauzeni, Manispaa ya Morogoro, alisema kuwa ugumu wa kupata miche bora umesababisha kuenea kwa kasi kwa magonjwa ya migomba.
“Tunahitaji msaada wa haraka kutoka serikalini ili kulinda zao hili muhimu,” alisema.
Kwa sasa, kila mgomba unaoambukizwa ni sahani ya chakula inayopotea, kipato kinachofifia, na familia inayosogea karibu zaidi na umaskini. Wadau wanaamini kuwa hatua ya kuitangaza rasmi Fungashada kama janga la kitaifa itafungua milango ya rasilimali, mafunzo, na teknolojia itakayosaidia kupambana na ugonjwa huo kwa mafanikio.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi kiwanda cha uzalishaji wa mbolea cha ITRACOM Fertilizers Ltd kilichopo Nala, jijini Dodoma tarehe 28 Juni 2025. 


Uzinduzi huo utahusisha uwekaji wa jiwe la msingi, upandaji miti kama ishara ya kuhifadhi mazingira na kuhimiza kilimo endelevu, pamoja na ukaguzi wa miundombinu ya kisasa ya kiwanda hicho. Hafla hiyo ya kihistoria inatarajiwa kuhudhuriwa na Marais wa nchi jirani akiwemo Rais wa Jamhuri ya Burundi, Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye, pamoja na Viongozi Wakuu wa Serikali, wakiwemo Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani.



Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 11 Juni 2025 kuelekea uzinduzi huo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema, “Kaulimbiu ya hafla hiyo ni ‘Kilimo ni Mbolea na Mbolea ni FOMI’.” Alisema kuwa kiwanda cha ITRACOM ni matokeo ya uwekezaji mkubwa ulioanza mwaka 2021, kikilenga kuongeza uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mbolea kutoka nje, na kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.



Waziri Bashe alieleza kuwa kiwanda hicho tayari kimeajiri wafanyakazi wapatao 1,805 huku ajira zisizo za moja kwa moja zikikadiriwa kuwa zaidi ya 5,000. Aliongeza kuwa matarajio ya baadaye ni kufikia zaidi ya ajira 3,000 za moja kwa moja na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 15,000.

“Ujenzi wa kiwanda ulianza mwaka 2021 na kina uwezo wa kutengeneza aina mbalimbali za mbolea kulingana na udongo na aina ya mazao. Hadi sasa kimeshasajili aina 14 za mbolea zinazotumika kwa mazao yote yanayolimwa nchini,” alisema Bashe. Aliongeza kuwa kiwanda hicho pia huzalisha chokaa-kilimo kwa ajili ya kurekebisha udongo ulioathiriwa na tindikali.

Kuhusu mbolea zinazozalishwa, Bashe alisema kuwa “Mbolea za Fomi Otesha, Fomi Kuzia na Fomi Nenepesha zilianza kuingia sokoni mwezi Desemba 2022. Mbolea hizi hutumika kuboresha afya ya udongo na kuongeza mavuno kwenye mazao ya chakula na biashara.”

Katika kuhakikisha kuwa viwanda vya ndani vinapata soko la uhakika, serikali imepanga kununua tani 200,000 za mbolea pamoja na tani 50,000 za chokaa kutoka viwanda vya ndani. Bashe alisisitiza kuwa hatua hiyo haitavuruga mfumo wa ruzuku uliopo.

“Tutanunua mbolea kutoka viwanda vya ndani na kupeleka kwenye maeneo ambayo mbolea hazitumiki sana ili Watanzania waanze kuzitumia na kuona matokeo yake,” alisema. Aidha, alieleza kuwa kwa sasa Tanzania ilikuwa ikiagiza hadi tani milioni 1.2 za mbolea kutoka nje ya nchi, lakini uwepo wa kiwanda cha ITRACOM na uwekezaji mwingine unaoendelea unalenga kupunguza uagizaji huo kwa kiasi kikubwa.

Waziri Bashe aliwataka wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo wa kihistoria na kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua sekta ya kilimo.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanda cha ITRACOM Fertilizers Ltd, Nazaire Nduwimana, alisema kuwa kiwanda hicho kinazalisha mbolea kwa kushirikiana na taasisi za serikali kama Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).

“Mpaka sasa tunazalisha aina 14 za mbolea. Kiwanda chetu kina uwezo wa kuzalisha mbolea kulingana na eneo, zao na hata hitaji la mkulima,” alisema Nduwimana. Aliongeza kuwa mbolea zinazozalishwa zinatumia mchanganyiko wa chumvi chumvi pamoja na malighafi za asili kama samadi na nyinginezo, jambo linalolenga kuongeza tija na kuimarisha afya ya udongo.

Uzinduzi wa kiwanda hiki unakuja miaka mitatu na nusu tangu uwekezaji kuanza kutekelezwa jijini Dodoma, na unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.



Serikali ya Tanzania imeondoa rasmi zuio la kuingiza bidhaa za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi, hatua inayolenga kutoa nafasi kwa majadiliano ya kidiplomasia na kiutaalamu kati ya pande hizo tatu.

Zuio hilo lilitangazwa awali na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kupitia mitandao ya kijamii, ambapo alieleza kuwa kuanzia Aprili 17, 2025, Tanzania ingezuia uingizaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini. Hata hivyo, baada ya siku mbili za utekelezaji, serikali imeamua kuliondoa.

Kupitia taarifa rasmi ya Wizara ya Kilimo iliyotolewa Aprili 25, 2025 na kusainiwa na Bashe, imeelezwa kuwa:
"Kwa misingi hiyo, Wizara ya Kilimo inaondoa mazuio yote yaliyowekwa kwa nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia Aprili 26, 2025 tukiamini majadiliano yanayoendelea yataleta suluhisho."

Bashe amesema kuwa kutokana na zuio hilo, Serikali za Malawi na Afrika Kusini ziliwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Kilimo ya Tanzania, kwa lengo la kutafuta njia ya pamoja ya kushughulikia changamoto zilizojitokeza.

"Makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba Serikali ya Malawi itatuma ujumbe wake Mei 2, 2025, utakaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje akiambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo ili kukutana na ujumbe wa Tanzania jijini Dodoma," amesema Bashe.

Kuhusu Afrika Kusini, amesema kuwa mazungumzo yanaendelea baina ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na mamlaka husika kutoka Afrika Kusini zinazoshughulikia masuala ya afya ya mimea na masoko.

Bashe amesisitiza kuwa serikali itaendelea kulinda maslahi ya wakulima na wananchi wa Tanzania, huku ikiheshimu misingi ya biashara huria na mahusiano ya kimataifa.

"Serikali inawahakikishia wakulima na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kuwa, uhuru wa biashara ya mazao ya kilimo utaendelea kwa kuzingatia matakwa ya afya ya mimea, usalama wa rasilimali za nchi na uhusiano wa kidiplomasia kwa manufaa ya wote," amesema.

Hatua hii inaonesha dhamira ya Tanzania katika kutafuta suluhisho la amani kupitia mashauriano, bila kuathiri usalama wa kilimo na maslahi ya taifa.

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa muda wa siku sita kwa nchi za Afrika Kusini na Malawi kuondoa vikwazo vya kibiashara vinavyokwamisha wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza mazao yao katika nchi hizo.



Akizungumza leo Aprili 17, 2025 jijini Dodoma katika mkutano wa wadau wanaotekeleza miradi ya kuwawezesha vijana na wanawake katika sekta ya kilimo, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema:

"Hakuna zabibu zozote wala apples pamoja na mazao mengine kutoka Malawi na Afrika Kusini yatakayoingia hapa nchini bila wao kuondoa vizuizi ili mazao ya Tanzania yaingie kuuzwa," amesema.

Ameongeza kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kuwa muathirika wa vikwazo ambavyo haina hatia navyo, huku akisisitiza msimamo wa serikali:

"We are not losers kwenye hili game, kama hawaondoi, hakuna zao lolote la kwao litaingia hapa nchini. Niwaambie tu wafanyabiashara, kwenye hilo hakuna kitakachoendelea."

Bashe amefafanua kuwa serikali ya Tanzania haijawahi kuweka vizuizi kwa mazao kutoka nchi hizo kuingia nchini, hivyo haoni sababu ya wao kufanya hivyo kwa Tanzania:

"Haijawahi kutokea serikali kuzuia mazao yao kuingia hapa nchini. Sasa iweje wao wazuie mahindi kutoka Tanzania halafu wanyamaze? Kitu hicho hakiwezekani."

Amesisitiza kuwa hakuna madhara yatakayompata Mtanzania kutokana na kutoingia kwa baadhi ya bidhaa kutoka nje:

"Hakuna Mtanzania yoyote atakayepoteza maisha kwa ajili ya kukosa kula apple kutoka Afrika Kusini au zabibu za nchi hizo. Wataendelea kutumia mazao ya hapa nchini."

Ameeleza pia kuwa Tanzania imekuwa jirani mwema, ikisaidia hata wakati nchi hizo zina uhaba wa chakula, lakini sasa hali imebadilika:

"Nchi haijawahi kumsumbua jirani yoyote kwenye soko la mazao. Mara nyingi wakiwa na njaa wanapiga hodi na kusaidiwa. Sasa safari hii hakuna ndizi wala bidhaa yoyote ambayo itaingia hapa nchini."

Aidha, amewapa pole wafanyabiashara wa Tanzania waliopata usumbufu katika kuuza mazao yao nje, huku akiwahakikishia kwamba hatua madhubuti zimechukuliwa:

"Wafanyabiashara wasiwe na wasiwasi wowote, kila kitu kita kaa sawa. Safari hii hakuna bidhaa yoyote ya kilimo ambayo itapokelewa kama nchi hizo hazitafungua mipaka hiyo."

Bashe ametamatisha kwa kuonya wafanyabiashara wa ndani:

"Wafanyabiashara wasibebe kitu chochote kutoka katika nchi hizo."

 


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kufanya mabadiliko makubwa katika uzalishaji na udhibiti wa zana za kilimo, huku akisisitiza matumizi sahihi ya fedha na kuhakikisha taasisi hiyo haipati hati chafu. 



Dkt. Jafo alitoa maelekezo hayo Januari 24, 2025, wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya CAMARTEC jijini Arusha.


Waziri Jafo alisisitiza kuwa Bodi hiyo inapaswa kuhakikisha zana za kilimo zinawafikia wananchi wengi, hasa wakulima, na kuendelea kutoa ushauri ili kuboresha ubunifu na maendeleo ya taasisi hiyo. Aliongeza kuwa CAMARTEC inatakiwa kuwa na mabadiliko makubwa ili kuendana na teknolojia ya kisasa na kusaidia sekta ya kilimo kupata tija.


Vilevile, alizitaka Taasisi zote chini ya Wizara yake kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya Kitengo cha Habari na Mawasiliano ili kutejeleza majukumu yake katika kuelimisha umma kuhusu maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara.


Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Needpeace Wambuya, alieleza kuwa Bodi hiyo itahakikisha tafiti na majaribio ya teknolojia yanahusishwa na zana za kilimo kutoka nje ya nchi.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CAMARTEC, Injinia Godfrey Mwinama, alifafanua kuwa Kituo hicho kimefanikiwa kuunda zana mpya 42 zinazozalisha zana mbalimbali zinazolenga kuongeza tija katika kilimo.


Mwenyekiti wa Bodi ya CAMARTEC, Profesa Valerian Silayo, alithibitisha kupokea maelekezo yote na kusema Bodi iko tayari kutekeleza majukumu hayo kwa kuhakikisha CAMARTEC inafikia malengo yake.

 SKIMU ZA NDUNGU,KIHURIO YAJAYO NI FURAHA TUU...


Na Gift Mongi


Same


WAKULIMA zaidi ya elfu tatu katika skimu za umwagiliaji Ndingu na Kihurio katika Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro wataenda kunufaika na kilimo baada ya serikali kutoa Bilioni 7 kwa ajili ya kukarabati skimu hizo. 


Hatua hiyo imekuja baada ya mvua zilizonyesha na kupelekea kuharibu miundombinu ya skimu hizo ambazo zinategemewa kwa kiasi kikubwa kuilisha wilaya ya Same. 



Akitambulisha wakandarasi watakaojenga skimu hizo ambazo ni kampuni ya Hamieri (T) Ltd na Ansil (T) Ltd, Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alisema kuwa lengo la serikali chini ya Rais Dkt. Sami Suluhu ni kuhakikisha wananchi wananufaika na kujikomboa katika umaskini. 



Alisema kuwa, ukarabati wa skimu hizo unatarajiwa kukamilika baada ya mwaka mmoja na nusu na kuwataka wakandari kuhakikisha wanatoa ajira zisizohitaji utaalam kwa vijana wazawa ili waweze kunufaika na mradi huo