Showing posts with label Michezo. Show all posts
Showing posts with label Michezo. Show all posts

 



Unaweza kusema dili limetiki kufuatia klabu ya Simba ya Jijini Dar es Salaam kuchagua kivutio namba moja cha utalii barani Africa kufanya uzinduzi wa wiki ya simba na jezi mpya ya mnyama kwa mwaka 2026.



Uzinduzi uliofanyika leo tarehe 1 Agosti, 2026 eneo la Ngoitoktok katika kasoko ya Ngorongoro ulipambwa na upepo mwanana unaotokana na mawimbi kutoka bwawa la Ngoitoktok likipambwa na Viboko wanaogelea huku ulinzi ukiimarishwa na familia za Simba waliosheheni kreta ya Ngorongoro.



Akizungumzia tukio hilo la kihistoria lililojumuisha uzinduzi wa logo ya miaka 90 ya Simba ulihudhuriwa na menejimenti ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro iliyoongozwa na Naibu Kamishna huduma za Shirika Aidan Makala na mashabiki zaidi ya 300 kutoka ndani na nje ya Nchi.



“Tukio hili ni matokeo chanya kati ya ushirikiano wa Klabu ya Simba na hifadhi ya Ngorongoro, tumetangaza utalii wa ndani, wanasimba wamerudi nyumbani lakini kubwa zaidi ni kuchagiza utalii wa michezo kuelekea mashindano ya AFCON ya mwaka 2027 yatakayofanyika hapa Nchini” Naibu Kamishna Aidan Makala.



Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba Ahmed Ally amebainisha kuwa Ngorongoro ni zaidi ya hifadhi, ina vivutio vingi vya utalii ambapo asili, urithi wa utamaduni na malikale vinaishi pamoja, hivyo Simba kufanya uzinduzi huo ndani ya hifadhi ni kurudisha mashabiki nyumbani na kuwadhihirishia kuwa ndoto, maono na hisia zao zinakutana na uhalisia uliopo Ngorongoro.




















 

Kikosi cha Klabu ya Simba kinatarajiwa kuondoka kesho alfajiri kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya mchezo muhimu wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya RS Berkane utakaochezwa Mei 17, 2025.



Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema maandalizi ya safari hiyo yamekamilika na msafara wa timu hiyo utaongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA.


"Tutaondoka kesho alfajiri, kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya mchezo wetu huo, tukiwa na malengo ya kushinda mchezo huo, wenye kauli mbiu Tunabeba," amesema Ahmed Ally.

Ameeleza kuwa msafara huo utajumuisha wachezaji 24 pamoja na benchi la ufundi, huku idadi ya mashabiki watakaosafiri pamoja na timu hiyo ikitarajiwa kutangazwa kabla ya kuondoka.

Aidha, Ahmed Ally amesema kuwa wanatarajia mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa RS Berkane ambao tayari wamecheza fainali nne na kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo.

"Mchezo huu utakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu RS Berkane ni timu yenye uzoefu mkubwa katika michuano hii, lakini sisi tumejipanga kuhakikisha tunashinda," amesema.

Pamoja na mchezo huo wa Mei 17, Simba pia itakuwa na faida ya kucheza mchezo wa marudiano nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Mei 25, 2025. Ahmed amesema wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye michezo yote miwili.

Kuhusu hali ya wachezaji, Ahmed amesema:
"Hali ya wachezaji wetu ni nzuri, saikolojia zao zipo juu na wamejipanga kupambana kwa ajili ya kutuletea ushindi."

Kwa upande wa mashabiki wanaotaka kusafiri pamoja na timu hiyo kwenda Morocco, Ahmed Ally amesema gharama ni Dola za Kimarekani 1,200 kwa kila mtu, kiasi ambacho kinajumuisha malazi, usafiri, na bima ya afya.

"Kila shabiki anayehitaji kusafiri anapaswa kulipa Dola 1,200 ambazo zitahusisha siku zote watakazokaa nchini humo, ikiwa ni pamoja na malazi, usafiri na bima ya afya," amefafanua.

Simba SC inasaka taji lake la kwanza la Kombe la Shirikisho baada ya kufika hatua ya fainali, na mashabiki wa timu hiyo wana matumaini makubwa kuwa mwaka huu utaandika historia mpya kwa klabu hiyo kongwe Tanzania.

 


Klabu ya Simba Sports Club imeandika ukurasa mpya katika historia ya soka barani Afrika baada ya kufuzu kwa fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup), kwa kuiondosha Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 1-0.

Katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja wa Moses Mabhida jijini Durban, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana (0-0). Matokeo hayo yaliihakikishia Simba tiketi ya fainali kwa faida ya ushindi wa bao 1-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Amaan, Visiwani Zanzibar.

Hii ni mara ya pili kwa Klabu ya Simba kufika hatua ya fainali katika michuano ya CAF, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 1993. Safari hii, Wekundu wa Msimbazi wanasubiri mshindi kati ya CS Constantine ya Algeria na RS Berkane ya Morocco.

Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho CAF imepangwa kuchezwa Mei 17, 2025, huku mchezo wa marudiano ukichezwa Mei 25, 2025.

Kombe la Shirikisho Afrika lilianzishwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa mashindano ya African Cup Winners' Cup (iliyodumu kuanzia mwaka 1975) na CAF Cup (iliyodumu kuanzia 1992).

RAIS SAMIA AIPONGEZA SIMBA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Klabu ya Simba kwa ushindi huo mkubwa na mafanikio ya kufuzu kwa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kupitia salamu zake, Rais Samia alisema:

"Pongezi za dhati kwa Klabu ya Simba kwa ushindi katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF Confederation Cup), na kuandika historia ya kufika fainali ya mashindano haya. Mmeipa nchi yetu heshima kubwa. Nawatakia kila kheri. Mnayo hamasa yangu wakati wote."

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba SC, alieleza furaha yake kwa mafanikio hayo akisema:

"Tumefanya kazi kubwa kama timu. Kila mchezaji alijitoa, na sasa tumefikia hatua ya kihistoria. Lengo letu ni kuhakikisha tunaleta kombe nyumbani."

Nahodha wa timu hiyo naye aliongeza:

"Tumeandika historia, lakini safari haijaisha. Tuna deni kwa mashabiki wetu, na tunataka kuhitimisha kazi tuliyoianza."

Mashabiki wa soka Tanzania sasa wana kila sababu ya kujivunia mafanikio ya Simba SC, wakisubiri kwa hamu fainali ya kihistoria ambayo huenda ikaleta kombe la kwanza la CAF nchini Tanzania.

 

Rais, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza, Sir Jim Ratcliffe, tarehe 11 Aprili, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam. 


Katika mazungumzo hayo, Rais Samia alimkaribisha rasmi Sir Jim kuwekeza nchini Tanzania, hususan katika sekta za michezo na utalii.

Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yalilenga kuangazia fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na klabu ya Manchester United, ambayo ina mashabiki mamilioni duniani kote, wakiwemo wengi kutoka barani Afrika.

Akizungumza katika kikao hicho, Sir Jim Ratcliffe alionesha nia ya kuitumia Manchester United kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kimataifa, hasa kupitia kampeni za utalii.

"Tunaamini Tanzania ina vivutio vya kipekee vya utalii ambavyo dunia inapaswa kuviona. Kupitia Manchester United, tunaweza kusaidia kuitangaza Tanzania kwa hadhira kubwa zaidi," alisema Sir Jim.

Katika ishara ya heshima na urafiki, Sir Jim alimkabidhi Rais Samia jezi ya Manchester United iliyosainiwa na wachezaji wa timu hiyo. Rais Samia alipokea zawadi hiyo kwa furaha na shukrani, na kutumia fursa hiyo kumualika mwekezaji huyo kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya mafunzo ya michezo (Sports Academies) nchini.

“Nakukaribisha uweze kuanzisha vituo vya kukuza vipaji kwa vijana wetu. Tuna vijana wengi wenye vipaji vya michezo, lakini wanakosa fursa. Kupitia ushirikiano huu, tunaweza kuwasaidia kufikia ndoto zao,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alitoa pongezi kwa Sir Jim kupitia Taasisi yake ya Six Rivers, ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) katika kuhifadhi mazingira na kudhibiti muingiliano wa wanyamapori na binadamu.

"Nashukuru kwa kazi nzuri mnayofanya kupitia Taasisi ya Six Rivers. Ushirikiano wenu na taasisi zetu umesaidia sana kulinda bioanuwai na kuhakikisha uhifadhi endelevu," aliongeza Rais Samia.

Kwa upande wake, Sir Jim alieleza dhamira ya Taasisi yake ya Six Rivers katika kurejesha hadhi ya Hifadhi ya Taifa ya Selous.

“Tunataka kuona Selous ikiwa na idadi kubwa ya wanyama wakubwa kama zamani. Ni dhamira yetu kuhakikisha hifadhi hii inakuwa kivutio kikubwa cha utalii wa kimataifa,” alieleza.

Manchester United imekuwa na historia ya kushirikiana na mataifa mbalimbali barani Afrika kupitia miradi ya kijamii inayotekelezwa na Manchester United Foundation. Hata hivyo, huu ni mwanzo wa aina yake kwa mmiliki wa klabu hiyo kuonesha nia ya kuwekeza moja kwa moja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ziara ya Sir Jim Ratcliffe nchini Tanzania inaonekana kuwa hatua muhimu ya kuimarisha diplomasia ya michezo na kufungua milango ya ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta ya michezo, utalii na maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.


 


Simba SC imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika Kundi A la Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya CS Constantine kutoka Algeria, katika mchezo wa kusisimua uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Katika mchezo huo, Simba ilipata mabao yote mawili kipindi cha pili, kupitia kwa Kibu Denis na Leonel Ateba. 


Denis alifunga bao la kwanza kwa mkwaju mkali kutoka ndani ya eneo la goli, huku Ateba akimaliza kabisa mchezo kwa shambulizi la kushtukiza, likiwa ni bao la pili kwa Simba na kuhitimisha matokeo katika dakika ya 79, huku dakika 11 zikisalia kumalizika kwa mechi hiyo.


Ushindi huo umeiwezesha Simba SC kumaliza nafasi ya kwanza katika kundi hilo kwa pointi 13, ikiwazidi wapinzani wao wa CS Constantine, ambao walikusanya pointi 12 na kumaliza nafasi ya pili. Hii ni ishara kwamba timu zote mbili zimefuzu kwa robo fainali ya mashindano hayo.


Simba SC inatajwa kuwa na nafasi nzuri ya kufika mbali katika michuano hiyo, huku mashabiki wake wakisubiri kwa hamu hatua inayofuata.


Mabingwa wa soka nchini, Simba SC, wameanza vyema kampeni yao ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) msimu wa 2024/25 kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola. Mchezo huo wa kundi A ulifanyika Novemba 27, 2024, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Jean Ahoua alifunga bao pekee kwa penalti dakika ya 27 baada ya beki wa Bravos, Edmilson, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. 


Penalti hiyo iliwaweka Simba mbele katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa, huku timu hiyo ikiimarisha uongozi wao kupitia ulinzi thabiti uliosimamiwa na Shomari Kapombe na Mohamed Hussein.


Kipa wa Simba alicheza kwa umahiri, akiokoa penalti ya Bravos katika dakika ya 48 na kuisaidia timu yake kuondoka na alama zote tatu. 


Ushindi huu unawaweka Simba kileleni mwa kundi A, wakisubiri mechi zijazo dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia na Constantine ya Algeria.



Yanga SC Yajikuta Katika Changamoto Hatua ya Makundi

Tofauti na watani wao, Yanga SC walikumbana na changamoto kubwa katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 


Wakiwa wenyeji wa Al Hilal Omdurman ya Sudan Novemba 26, 2024, Yanga walikubali kipigo cha mabao 2-0 katika uwanja huo huo wa Benjamin Mkapa.


Mshambuliaji Adama Coulibaly aliwapa Al Hilal uongozi kwa bao dakika ya 64, kabla ya Yasir Mozamil kufunga bao la pili dakika ya 90, na kuzima kabisa matumaini ya Yanga kuanza kampeni yao kwa ushindi nyumbani.



Kipigo hiki kinawaweka Yanga katika nafasi ya mwisho ya Kundi A, ambalo pia lina timu ngumu kama TP Mazembe ya DR Congo na MC Alger ya Algeria. 


Wana Jangwani sasa watalazimika kujipanga upya ili kurejesha matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.

Viwango Vya Makundi (Baada ya Mchezo wa Kwanza):
Kombe la Shirikisho Afrika - Kundi A:

  1. Simba SC – 3 Pointi
  2. CS Sfaxien – 0 Pointi (bado kucheza)
  3. Constantine – 0 Pointi (bado kucheza)
  4. Bravos do Maquis – 0 Pointi

Ligi ya Mabingwa Afrika - Kundi A:

  1. TP Mazembe – 3 Pointi
  2. Al Hilal Omdurman – 3 Pointi
  3. MC Alger – 0 Pointi (bado kucheza)
  4. Yanga SC – 0 Pointi


Timu zote mbili zinatarajiwa kupambana vilivyo katika mechi zijazo ili kuendeleza heshima ya Tanzania kwenye mashindano haya makubwa barani Afrika.



Yanga SC Yaangukia Pua Mchezo wa Kwanza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika 


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC Tanzania Bara, Yanga SC, wameanza kwa matokeo mabaya katika kampeni yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, baada ya kupoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi kwa kufungwa mabao 2-0 na Al Hilal Omdurman ya Sudan. Mchezo huo uliochezwa Novemba 26, 2024, ulifanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.  


Al Hilal walidhihirisha ukomavu wao kwa kufunga mabao kupitia mshambuliaji wao hatari Adama Coulibaly dakika ya 64, kabla ya Yasir Mozamil kufunga bao la pili dakika ya 90, na hivyo kuzima matumaini ya Yanga kuanza kwa ushindi nyumbani.  


Matokeo haya yanaifanya Yanga SC kushika nafasi ya mwisho katika Kundi A, ambalo lina timu nyingine ngumu kama TP Mazembe ya DR Congo na MC Alger ya Algeria, pamoja na Al Hilal Omdurman.  


Mashabiki wa Yanga wanatarajia kikosi chao kurekebisha makosa na kuonyesha makali katika michezo ijayo, hasa kwa kuwa hatua ya makundi bado ni ndefu na kuna fursa ya kurejea katika mbio za kufuzu hatua ya robo fainali.  


Yanga SC itahitaji kujipanga vyema na kutumia uzoefu wake wa kimataifa ili kupata matokeo chanya kwenye mechi zinazofuata dhidi ya wapinzani wake wa kundi A.  


Je, Yanga itaweza kujikwamua kwenye hatua hii ya makundi? Mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona mustakabali wa klabu yao kwenye michuano hii mikubwa barani Afrika.

 



Simon Msuva alifunga bao pekee katika kipindi cha pili na kuipa Tanzania ushindi muhimu wa 1-0 dhidi ya Guinea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumanne. Ushindi huo umeihakikishia Taifa Stars tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zitakazofanyika nchini Morocco.  


Kwa matokeo hayo, Tanzania imemaliza katika nafasi ya pili ya Kundi H ikiwa na pointi 10, hivyo kuwa nje ya uwezo wa Guinea iliyo nafasi ya tatu au Ethiopia inayoshika mkia kufikia alama hizo kwenye msimamo wa kundi.  


**Msuva Aibuka Shujaa wa Taifa Stars**  

Katika mechi hiyo ya ushindani mkubwa, Simon Msuva aling’ara kwa kufunga bao muhimu dakika ya 61 kwa kichwa safi kufuatia krosi ya Mudathir Yahya. Bao hilo liliibua shangwe kubwa kwa mashabiki wa nyumbani huku Tanzania ikijihakikishia nafasi ya kushiriki AFCON kwa mara ya nne katika historia yake.  


Msuva alithibitisha ubora wake kwa kufunga bao lake la tatu katika kampeni za kufuzu AFCON mwaka huu, akihitimisha mechi hiyo akiwa shujaa wa Taifa Stars. Hata hivyo, Tanzania ilikaribia kuongeza bao la pili, lakini shuti la Feisal Salum lilipaa juu ya lango dakika za mwisho za kipindi cha pili.  


Kwa upande wa Guinea, licha ya juhudi za kutafuta bao la kusawazisha, mchezaji wa akiba Kandet Diawara alikosa nafasi ya dhahabu dakika za lala salama. Ulinzi wa Tanzania, unaoongozwa na Dickson Job na Shomari Kapombe, ulidhibiti mashambulizi yote ya wapinzani kwa umakini mkubwa.  


**Matumaini ya Guinea Yatoweka**  

Licha ya kuingia kwenye mchezo huo wakiwa na ushindi wa mechi tatu mfululizo, Guinea walishindwa kupenya ulinzi thabiti wa Tanzania. Fursa yao bora zaidi ilitokea kipindi cha kwanza, ambapo Mady Camara alipiga shuti lililogonga mwamba wa juu, lakini walishindwa kutumia nafasi walizopata licha ya kumiliki mpira kwa muda mrefu.  


Kwa matokeo hayo, Guinea imekosa nafasi ya kufuzu baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu ya Kundi H wakiwa na pointi 9, huku Tanzania ikifuzu kwa mara ya pili mfululizo na mara ya nne katika historia.  


**Msimamo wa Mwisho wa Kundi H (Kwa Tanzania):**  

1. DR Congo – Pointi 12 (Mechi 5)  

2. Tanzania – Pointi 10 (Mechi 6, imefuzu)  

3. Guinea – Pointi 9 (Mechi 6)  

4. Ethiopia – Pointi 1 (Mechi 5)  


Ushindi huu ni hatua kubwa kwa Taifa Stars, na mashabiki wa soka nchini wanatarajia kuona timu yao ikiwakilisha vyema katika michuano ya AFCON mwaka 2025 nchini Morocco.  

 


Na Kassim Nyaki, NCAA.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye ametembelea timu za NCAA zinazoshiriki mashindano ya SHIMMUTA Jijini Tanga na kusisitiza wachezaji kuzingatia nidhamu katika michezo yote wanayoshiriki.



Akizungumza na wachezaji wa NCAA wanaoshiriki michezo mbalimbali katika mashindano hayo, Dkt Doriye amebainisha kuwa, watumishi  wa NCAA kushiriki michezo hiyo inachangia kuimarisha afya zao , kujikinga na magonjwa mbalimbali, kupanua mtandao wa ushirikiano na taasisi zingine na kuisaidia NCAA kutangaza utalii wa ndani kupitia vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro kupitia washiriki wa michezo hiyo.



"Nawapongeza kwa jinsi mnavyoendelea kujitoa katika michezo mnayoshiriki,  nimemabiwa baadhi ya timu kama Kamba (wanawake na wanaume) pamoja na timu ya mpira wa miguu za NCAA tayari zimefuzu kwenda hatua ya robo fainali huku michezo mingine ikiwa inaendelea, endeleeni kujitoa katika michezo hii lakini mhakikishe mnazingatia nidhamu kwa kila mchezo" amesisitiza Dkt. Doriye.



Michezo ya Shirikisho ya mashirika ya Umma na ya Sekta binafsi (SHIMMUTA) iliyofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko ilianza tarehe 11 Novemba na itahitimishwa tarehe 22 Novemba, 2024  jijini Tanga.

 





Klabu ya Yanga SC imetangaza rasmi kuachana na Kocha wake mkuu, Miguel Gamondi, pamoja na msaidizi wake, Moussa Ndaw, hii leo Ijumaa, 15 Novemba, 2024kupitia taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wa Instagram wa klabu hiyo.



Gamondi, raia wa Argentina, alijiunga na Yanga SC mwezi Juni 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia Nesreddine Nabi, ambaye alihamia AS FAR Rabat ya Morocco. Kocha huyo alisifika kwa mbinu zake za kufundisha mpira wa kushambulia na wenye burudani, akileta mtindo wa soka lenye ladha ya Amerika Kusini. Chini ya uongozi wake, Yanga iliweza kushinda Kombe la Shirikisho Tanzania, Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara, na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Hata hivyo, sababu zinazosemekana kupelekea Gamondi kuachishwa kazi ni kushindwa kudhibiti nidhamu ya wachezaji, kupoteza uwezo wa kushawishi wachezaji katika vyumba vya kubadilishia nguo, na kushuka kwa viwango vya wachezaji katika kikosi chake. Hali hii ilidhihirishwa zaidi baada ya Yanga SC kupoteza michezo miwili mfululizo katika Ligi Kuu dhidi ya Azam FC kwa goli 1-0 na Tabora United kwa 3-1, kabla ya mapumziko ya michezo ya kufuzu michuano ya AFCON 2025.


Habari zisizo rasmi zinadai kuwa klabu hiyo ipo mbioni kumpa nafasi kocha mpya, Sead Ramović, ambaye hivi karibuni aliifundisha TS Galaxy ya Afrika Kusini. Ujio wa Ramović umeongeza uzito kwenye tetesi za kuachishwa kazi kwa Gamondi.


Gamondi ataacha kumbukumbu muhimu, akiwa ndiye kocha pekee aliyeweza kuiongoza Yanga kushinda michezo minne mfululizo dhidi ya Simba SC katika Dabi ya Kariakoo, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na kocha mwingine.


Klabu ya Yanga inajiandaa kuanza upya chini ya uongozi mpya kwa lengo la kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho Tanzania, na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mechi yao ijayo baada ya mapumziko ya michezo ya timu za taifa itakuwa dhidi ya Al-Hilal Omdurman, tarehe 26 Novemba.


Happy Lazaro, Arusha .



Washiriki Elfu moja wanatarajiwa kushiriki katika mbio za "Dyslexia Awareness Run" zinazotarajiwa kufanyika oktoba 20 mwaka huu katika uwanja wa mgambo mkoani (karibu na Gymkhana) Arusha .




Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mwanzilishi na Mkurugenzi  wa Taasisi ya Dyslexia Tanzania , Caudence Ayoti ambao ndio waandaaji wa mbio hizo .




Amesema kuwa, lengo la mbio hizo ni kusambaza uelewa kuhusiana na Dyslexia kwani Taasisi hiyo inajihusisha na kusambaza uelewa kuhusu  changamoto za kujifunza kwa watoto. 



"Dyslexia ni changamoto ambayo inampata mtoto katika kujifunza ,kuandika, kusoma  na kuhesabu ambapo mbio hizo zitasaidia taasisi hiyo kuendelea kusambaza uelewa kuhusiana na changamoto hiyo kwenye jamii".amesema Ayoti. 



Ayoti ameongeza kuwa ,washiriki hao watakimbia mbio za kilometa 5 na 10 ambapo  washiriki kwenye mbio hizo watapata medali za kipekee kutoka Shanga Foundation ambazo zinatengenezwa  na walemavu ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaunga mkono pia.



Aidha amesema kuwa,kiingilio katika mbio hizo ni shs 35,000 ambapo ametoa wito kwa wananchi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ili waweze kuiunga  taasisi hiyo mkono katika kuendelea kusaidia watoto wenye changamoto hiyo.



Kwa upande  wake  Meneja Rasilimali watu kutoka Shanga Foundation ambao ndio   wamefadhili  medali hizo,Janet Steven amesema kuwa,Taasisi hiyo ya kijamii inashughulika na watu wenye ulemavu ambao wamekuwa wakitengeneza medali  hizo wa lengo la kujipatia kipato. 



Amesema kuwa, taasisi hiyo imechukua  uamuzi wa kufadhili  mbio hizo kwa lengo la kuwasaidia walemavu hao  na pia kusambaza uelewa kuwa wanaweza  ili waweze kuungwa  mkono kwani medali hizo  ndio wametengeneza wenyewe.


Kw upande wake Mwenyekiti chama cha riadha mkoa wa Arusha ,Gerald Babu ameipongeza  taasisi hiyo kwa kuanzisha mbio hizo ambazo zinalenga  kutatua changamoto  hiyo ya Dyslexia  kwa watoto kwani ni jambo zuri sana na ni mfano wa kuigwa na jamii.


Babu ametoa wito kwa wadau na jamii mbalimbali  kujitokeza kwa wingi katika mbio hizo kwa lengo la  kuwaunga mkono kwa ajili ya kusaidia  jitihada hizo .



 



TIMU ya Taifa ya Hispania imefanikiwa kunyakua Kombe la Euro 2024 baada ya kuichapa Uingereza mabao 2-1 katika fainali iliyochezwa kwenye dimba la Olympiastadion, Berlin nchini Ujerumani.


Hispania walianza kupata bao kupitia kwa Nico Williams dakika ya 47 ya kipindi cha pili, baada ya kupokea pasi kutoka kwa nyota Yamal.


Dakika ya 72, nyota wa klabu ya Chelsea, Cole Palmer, aliweza kuisawazishia timu yake kwa bao zuri baada ya kupokea pasi kutoka kwa Jude Bellingham.


Mikel Oyarzabal aliweza kufunga bao la pili na la ushindi kwa Hispania, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Marc Cucurella dakika ya 86 ya mchezo, na hivyo kumaliza hesabu kwenye fainali hiyo.


Mchezaji bora wa mashindano hayo alitangazwa kuwa ni nyota wa Manchester City, Rodri, kwa mchango wake mkubwa katika timu ya Hispania.

 Manchester City Yashinda Taji la EPL Misimu Minne Mfululizo



Manchester City iliifunga West Ham mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Etihad na kuwa timu ya kwanza kushinda taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) misimu minne mfululizo.


City walihitaji ushindi ili kuhakikisha wanawazuia Arsenal, ambao walianza siku ya mwisho wakiwa nyuma kwa pointi mbili lakini wakiwa na tofauti nzuri ya mabao. Phil Foden aliweka kikosi cha Pep Guardiola mbele baada ya dakika mbili pekee.


Nyota huyo wa Uingereza aliongeza jingine kabla ya mapumziko na ingawa Mohammed Kudus alirudisha goli moja, kiungo Rodri alirejesha tofauti ya mabao mawili kwa wenyeji kupitia shuti kali kutoka kwenye eneo la hatari baada ya dakika 59.


City walinusurika hofu ya dakika za lala salama wakati West Ham ilipopata bao la pili lililokataliwa na VAR baada ya mchezaji kuunawa mpira. Hata hivyo, ushindi wao haukuwa na shaka kamwe kwani ulikamilisha mwendo wa kushangaza wa ushindi 19 na sare nne tangu kushindwa kwao kwa mara ya mwisho kwenye ligi, huko Aston Villa mnamo 6 Desemba.


City sasa wameshinda mataji sita kati ya saba iliyopita ya Premier League. Muhula uliopita, waliungana na Huddersfield, Arsenal, Liverpool na Manchester United, mara mbili, kushinda ligi kuu miaka mitatu mfululizo. Sasa timu ya Guardiola imepata kitu ambacho hakuna upande mwingine imefanikiwa tangu Ligi ya Uingereza ilipoanzishwa mwaka 1888, miaka 136 iliyopita.


"Yanga Yatawazwa Mabingwa wa Ligi Kuu NBC Premier League Baada ya Ushindi Dhidi ya Mtibwa Sugar"


Na Said Humbe





Klabu ya soka ya yanga imetawazwa kuwa mabingwa wa ligi kuu soka NBC PREMIER LEAGUE baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 1-3 dhidi ya mtibwa sugar katika dimba la Manungu Turiani mkoani Morogoro.


Baada ya ushindi huo yanga wamefikisha point 71 ambazo haziwezo kufikiwa na klabu yeyote inayoshiriki ligi kuu msimu  huu wa 2023/2024 na kutawazwa kuwa mabingwa. 

Huku ukiwa ni ubingwa wao wa 30 tangu klabu hiyo ianzishwe katika ligi kuu mwaka 1936 magoli ya yanga yalifungwa na Kennedy Musonda, Clement Mzize pamoja na goli la kujifunga la Nasri Kombo huku goli la Mtibwa likifungwa na Charles Ilanfya .



RAIS, Samia Suluhu Hassan  ameikaribisha ikulu Timu ya Mpira wa Miguu ya Wanawake chini ya Umri wa Miaka 17 ( Serengeti Girls)  chakula cha mchana ikiwa ni muendelezo wa pongezi zake kwa  timu hiyo baada ya Kufuzu kucheza Kombe la Dunia nchini India.



Viongozi wa Serikali na Mpira wa Miguu  wakiongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbas  na wengine wamehudhuria tukio hilo lililofanyika leo Julai 05, 2022 Ikulu Dar es Salaam.





Hafla hiyo, imepambwa na Wasanii   wa Muziki wa kizazi kipya akiwemo Barnaba na Frida Amani.

LIGI i Kuu ya Uingereza ( EPL) imemuondoa mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich kuwa mkurungezi wa Klabu hiyo.


Kamati ya Ligi kuu ya Uingereza imechukua hatua hiyo kumuondoa kutoka klabu hicho kufuatia uamuzi serikali ya Uingereza kumuwekea tajiri huyo vikwazo kama njia ya kuijibu Urusi kwa kuivamia Ukraine.


Kwa sasa Chelsea imepatiwa kibali maalum cha kuhudumu na kuendelea na shughuli za mpira hata baada ya mali ya Abramovich kupigwa tanji na serikali ya Uingereza.


Ligi Kuu ya uingereza unasema ingawa Abramovich amepigwa marufuku lakini hatua hiyo "haitaathiri Chelsea kufanya mazoezi na kusakata mpira"


Bilionea huyo amekuwa akiiongoza klabu hiyo tangu 2003 lakini majaribio yake ya kutaka kuiuza klabu hiyo yalisitishwa na serikali ya Uingereza, ambayo imezuia mali yake.


Roman Abramovich awekewa vikwazo na UingerezaChelsea: Roman Abramovich anasema ana mpango wa kuiuza klabu hiyo


Abramovich aliwekewa vikwazo na serikali ya Uingereza siku ya alhamisi iliyopita kama sehemu ya majibu yake kwa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.


Serikali inaamini kuwa bilionea huyo amekuwa na "uhusiano wa karibu kwa miongo kadhaa" na rais wa Urusi Vladimir Putin, viungo ambavyo Abramovich amekuwa akikanusha.


Mbali na yaliompata tajiri Abramovich klabu chake cha Chelsea nacho kitakuwa chini ya marufuku ya uhamisho ikimaanisha kuwa haiwezi kununua wala kuuza wachezaji.


Chelsea vilevile haitaruhusiwa kujadili mikataba mipya kwa wachezaji wake, meneja na wafanyakazi wake wote


 Liverpool imetawazwa kuwa mabingwa wapya wa Kombe la ligi (Carabao Cup) msimu huu, baada ya usiku wa kuamkia leo kuitandika Chelsea kwa mikwaju ya penati 11-10 katika uwanja wa Wembley.

Mpaka dakika 120, timu hizo zilienda sare ya bila kufungana. Mlinda mlango wa Chelsea anayetajwa kama mtaalamu wa kuokoa penati Kepa Arrizabalaga, aliingizwa katika dakika za mwisho kwa ajili ya kuisaidia timu yake, alikosa penati muhimu baada ya mwenzake wa Liverpool Caoimhin Kelleher, kufunga mkwaju wake.

Wachezaji wote wa Liverpool walipata penatiki akiwemo Kipa Kelleher aliyefunga penati ya mwisho ya 11 lakini Kepa alipaisha juu penati yake, na kuhitimisha mchezo kwa machungu.

Katika mchezo huo, magoli 3 ya Chelsea yalikataliwa ikionekana wachezaji wamezidi (offside). Kiungo wake Mason Mount atakuwa na usingizi wa mang’amung’amu wiki hii baada ya kukosa nafasi mbili muhimu za kufunga, huku mlinda mlango wake Edouard Mendy, akiokoa michomo mengi ya Liverpool.

Liverpool wao walitengeneza nafasi nyingi katika mchezo huo, huku goli la Joel Matip likikataliwa kutokana na madhambo yaliyofanyika na kuotea kabla ya kufunga.

Ni kombe la kwanza kwa Liverpool msimu huu, likiweka rekodi kwa timu hiyo kulitwaa mara 9, wakiendelea kuwania pia makombe mengine ya ligi kuu, mabingwa Ulaya na FA Cup.

Gwiji wa soka nchini Brazil, Ronaldinho anatarajia kufunga ndoa katikati ya mwaka huu mwezi Agosti na kufanya sherehe moja na wachumba zake wawili, Priscilla Coelho na Beatriz Souza.

Watatu ambao wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani na furaha  kwenye jumba la kifahari la nyota huyo wa soka jijini Rio de Janeiro tangu Disemba mwaka jana.
Gazeti la O Dia la Brazil limeripoti kuwa Ronaldinho alianza mapenzi na Coelho miaka michache iliyopita kabla ya kumuona Souza mwaka 2016.
Hata hivyo imeripotiwa kuwa wachumba zake hao wanapokea posho ya dola 2000 za kimarekani sawa na Shilingi Milioni 4.5 na zaidi kwa pesa ya kitanzania kutoka kwa Ronaldinho na amekuwa akiwapa zawadi zinazolingana yakiwamo manukato yanayofannya

Ronaldinho hajawahi kuthibitisha uhusiano wake na wapenzi hao wawili lakini husafiri nao karibu katika matukio yote anayoalikwa limesema gazeti la  O Dia.
Aidha ndoa za wanawake wengi haziruhusiwi kisheria nchini Brazil, hivyo haijajulikana kwa gwiji huyo wa soka kama atafanikisha swala hilo la kufunga ndoa na wanawake hao ambao wameonesha kukubaliana na uamuzi huo.

Uongozi wa timu ya soka ya villa real inayo shiriki ligi kuu ya nchini Hispania, (LALIGA) umekabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya polisi mkoani Arusha inayoshiriki ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa.

mkurugenzi wa timu hiyo, Ammar Hayani, amesema wamefikia uamuzi huo baada ya   vutiwa na amani,usalama wa Tanzania huku akisisitiza michezo ambapo amesema ili soka la Tanzania liweze kupiga hatua ni wakati muafaka wa vilabu  kuongeza ushirikiano kwa vilabu vya soka kwa nchi nje ya mipaka ya tanzania.
Akizungumza viwanjani mara baada ya kupokea jezi kutoka kwa klabu hiyo ya uhispania kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'azi amesema vifaa hivyo vitaongeza chachu katika michezo kwa lengo la kujiweka katika nafasi nzuri katika mchezo wa soka kwa timu yao.

 Klabu ya polisi Morani imemaliza nafasi ya 6 kati ya timu 15 katika mashindano ya soka ngazi ya mkoa