Showing posts with label Uhalifu. Show all posts
Showing posts with label Uhalifu. Show all posts

 

Serikali imekamata almasi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.7 ikisafirishwa kinyume cha sheria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.



Akizungumza na waandishi wa habari Mei 24, 2025 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alithibitisha kuwa madini hayo yalinaswa Mei 18, yakisafirishwa na raia wa kigeni wakiwa na mabegi manne yaliyokuwa yamefichwa madini hayo.

"Madini haya yamekamatwa yakisafirishwa kinyume na utaratibu na raia wa kigeni, yakiwa kwenye mabegi manne katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza," alisema Mavunde.

Ameeleza kuwa Serikali imesikitishwa sana na kitendo hicho na kwamba haitavumilia kabisa tabia ya baadhi ya watu kujaribu kuiba rasilimali za nchi.

"Serikali inalaani vikali vitendo vya namna hii vya utoroshwaji wa madini. Hatutavumilia kuona mali ya nchi ikiporwa kwa maslahi ya watu wachache," alisisitiza.



Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alieleza mafanikio ya Serikali katika ukusanyaji wa mapato kupitia sekta ya madini, akifichua ongezeko kubwa la mapato ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 tulikusanya bilioni 162 kutokana na biashara ya madini. Lakini kutokana na udhibiti mkubwa dhidi ya utoroshaji wa madini, hadi kufikia Mei mwaka wa fedha 2024/2025 tumeshakusanya shilingi bilioni 925, na lengo letu ni kufikisha trilioni moja,” alisema.

Tukio hilo limeendelea kuonyesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ulinzi wa rasilimali za taifa na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu katika sekta ya madini.



Familia moja ya baba na mtoto imehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kusafirisha bangi kinyume cha sheria, kutoka wilayani Nzega mkoani Tabora kwenda mkoani Shinyanga. Tukio hilo limetajwa kuwa ni sehemu ya biashara haramu ya dawa za kulevya inayozidi kushamiri katika baadhi ya maeneo nchini.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega, chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Saturini Mushi, iliwatia hatiani jana washBaba na Mtoto Wahukumiwa Kifungo cha Maisha kwa Kusafirisha Bangiitakiwa hao kwa kosa la uhujumu uchumi baada ya kupatikana na ushahidi wa kutosha wa kuhusika na usafirishaji wa bangi.

"Hii iwe fundisho kwa wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Sheria ipo wazi, na haitavumilia uhalifu huu," alisema Hakimu Mushi wakati akisoma hukumu.

Aliwataja waliohukumiwa kuwa ni Ally Thabit (45) na mtoto wake Jonas Ally Thabit (23), wote wakazi wa Nzega. Alisema kuwa ni muhimu hukumu hii iwe mwanzo wa kukomesha vitendo vya kilimo na usambazaji wa bangi kinyume na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Mwendesha Mashtaka Meshaki Lyabonge kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya alieleza kuwa tukio hilo lilitokea mnamo Machi 13, 2024, katika Msitu wa Mabatini, Kijiji cha Kigandu, Kata ya Mogwa, ambapo watuhumiwa walikamatwa na magunia ya bangi wakiwa wanayapeleka mkoani Shinyanga kwa kutumia pikipiki.

"Naomba mahakama itoe adhabu kali iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na biashara hii haramu," alisema Lyabonge, akiwasilisha kesi namba 7152 ya mwaka 2024.

Watuhumiwa hao waliiomba Mahakama iwapunguzie adhabu kwa madai kuwa ni kosa lao la kwanza na kuahidi kutorudia tena, lakini Hakimu Mushi alikataa ombi hilo na kutoa hukumu ya kifungo cha maisha jela.

"Sheria inatakiwa ifuatwe. Uhalifu huu hauwezi kuvumiliwa. Mnayo haki ya kukata rufaa kama hamkuridhika na hukumu hii," alihitimisha.


Chanzo:
Mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya ndani 


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeomba uchunguzi wa haraka na wa wazi
kuhusu tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Padre Charles Kitima, lililotokea usiku wa tarehe 30 Aprili 2025 katika Makao Makuu ya TEC yaliyopo Kurasini, Temeke – Dar es Salaam.



Katika taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa na TEC, Baraza limesema tukio hilo ni la kusikitisha na la kinyama, na linahitaji kushughulikiwa kwa haraka ili kurejesha imani kwa wananchi. "Padre Kitima alipata majeraha makubwa na amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam," imeeleza taarifa hiyo.

TEC imeeleza kuwa tayari Serikali na vyombo vya usalama vimeonyesha ushirikiano mzuri, lakini ikaongeza kuwa "Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukua hatua za haraka za kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huu wa kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria."

Aidha, TEC imetoa rai kwa vyombo husika kutoa taarifa sahihi na kwa uwazi kwa umma kuhusu maendeleo ya uchunguzi ili kuondoa upotoshaji na kuweka wazi ukweli wa tukio hilo. Baraza pia limewashukuru wote waliomsaidia Padre Kitima kufikishwa hospitalini na wanaoendelea kumuhudumia.

"Tunaomba Waamini na watu wenye mapenzi mema muendelee kumuombea neema ya uponyaji Padre Kitima, na pia kuliombea Taifa letu amani na umoja," amesema Askofu Eusebius Nzigilwa, Makamu wa Rais wa TEC, katika taarifa hiyo ya Mei 1, 2025.



Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nalo limetoa taarifa ya awali kuhusu tukio hilo, likieleza kuwa tukio hilo liliripotiwa rasmi majira ya saa nne usiku wa tarehe 30 Aprili 2025.

Kwa mujibu wa Polisi, Padre Kitima alihudhuria kikao na viongozi wa dini mbalimbali kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni, kisha alielekea kwenye kantini ya Baraza hilo na kuendelea kupata kinywaji hadi saa nne na robo usiku. 


Akiwa njiani kuelekea maliwatoni, alishambuliwa kichwani kwa kitu butu na watu wawili wasiojulikana.

"Alipelekwa hospitali ya Aga Khan na anaendelea vizuri na matibabu. Mtu mmoja Rauli Mahabi @Haraja, mkazi wa Kurasini, anashikiliwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo," imesema taarifa ya Jeshi la Polisi.

Polisi wameeleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika. Wananchi wametakiwa kuwa na utulivu wakati uchunguzi unaendelea.


Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima, ameripotiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake ndani ya ofisi za TEC, eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Aprili 30, 2025.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo katika mgahawa mmoja ndani ya viunga vya TEC, Padri Kitima alionekana akiwa katika mazungumzo na baadhi ya watu kabla ya kuinuka kuelekea msalani. Dakika chache baadaye, watu wasiojulikana walitokea ghafla na kumshambulia kwa muda mfupi kisha kutoweka mara moja.
Baada ya tukio hilo, Padri Kitima alikutwa akivuja damu sehemu mbalimbali za mwili na kuomba msaada. Alipatiwa huduma ya kwanza katika kituo kidogo cha afya kilichopo ndani ya eneo hilo kabla ya kusaidiwa kupandishwa kwenye gari na kupelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi. Hadi taarifa hii inaandaliwa, bado haijafahamika rasmi hospitali alikokimbizwa.
Padri Kitima ni mmoja wa viongozi mashuhuri wa Kanisa Katoliki nchini, na amekuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti dhidi ya ukandamizaji wa haki, ukiukwaji wa sheria, na katika kupigania demokrasia na haki za binadamu. Umaarufu wake katika kuzungumzia masuala ya kijamii na kisiasa umemfanya kuwa sauti yenye ushawishi mkubwa katika jamii ya Watanzania.
Tukio hilo limelaaniwa vikali na watu mbalimbali mashuhuri nchini, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, wanaharakati na wanasheria.

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche, ameandika kwenye ukurasa wake wa X:
"Nimepokea taarifa mbaya za kushambuliwa kwa Mwalimu wangu Dr Kitima usiku huu.
Hii ni habari mbaya sana kwa nchi yetu, tumefikaje hapa?
Get well soon Father, tunakuombea."

Wakili Jebra Kambole naye ameandika:
"Get well soon Father Dr. Charles Kitima! Shambulio dhidi yako, ni shambulio dhidi ya wapigania haki!!! Hatuko salama!!!"

Wakili Paul Kisabo amesema:
"Pole sana Padri Kitima, alaaniwe mtu yule aliyekushambulia."

Kwa upande wake, Dawson Kagine ameandika kwa masikitiko:
"Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya kushambuliwa kwa Fr. Kitima. Namuombea kwa Mwenyezi Mungu apone haraka."


 


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 19 hadi 25 Machi 2025. 



Katika operesheni hiyo, ekari 285.5 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa na watuhumiwa saba (7) wamekamatwa, akiwemo kinara wa biashara haramu ya mirungi nchini aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, Interindwa Zinywangwa Kirumbi, maarufu kwa jina la mama Dangote.



Akizungumza baada ya operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema: "Mama Dangote ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini. Kwa zaidi ya miaka 30, amekuwa akiendesha mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hizo za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya kujua kuwa ni kinyume cha sheria."


Kamishna Lyimo aliongeza kuwa, mwaka juzi Mamlaka ilifanya operesheni wilayani humo na kutoa elimu kwa wananchi ili waachane na kilimo cha mirungi na badala yake wajikite katika kilimo cha mazao mbadala pamoja na ufugaji. Alisema: "Mwaka juzi tuliteketeza jumla ya ekari 535 za mashamba ya mirungi. Kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya, tulitoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya, ikiwemo mirungi. Lengo lilikuwa kuwawezesha wakazi wa eneo hili kujikita katika kilimo cha mazao mbadala na ufugaji kama njia ya kujiongezea kipato."


Aidha, Kamishna Lyimo alieleza kuwa, pamoja na jitihada hizo, uongozi wa wilaya ya Same na Wizara ya Kilimo na Mifugo walitekeleza miradi ya ufugaji wa nguruwe na kugawa miche ya kahawa, iliki na mazao mengine kwa wananchi. Alisema: "Kutokana na juhudi hizo, wananchi wengi wameachana na kilimo cha mirungi na kuanza kulima mazao mbadala, japo wapo wananchi wachache waliokaidi na kuendelea na kilimo na biashara ya mirungi."


Kamishna Lyimo alisisitiza kuwa Mamlaka itaendelea kufanya operesheni kuhakikisha wananchi wote wanaojihusisha na biashara ya mirungi wanakamatwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao. Alisema: "Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunatokomeza biashara na matumizi ya mirungi hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa, eneo hili la Same ni kitovu cha uzalishaji mirungi nchini hali inayohatarisha ustawi wa taifa letu ndio maana tunafanya operesheni hizi endelevu nchi nzima kuhakikisha tunadhibiti uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya za mashambani na viwandani ili zisiendelee kuathiri wananchi."


Kwa upande wake, Agness Mshana, mtendani wa kata ya Ekondi, alikiri kutambua uwepo wa watu wanaojihusisha na kilimo cha mirungi na kusema kuwa serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya mirungi. Alisema: "Tumejitahidi kuwaletea mradi wa nguruwe pamoja na miche ya miparachichi na kuwapa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa maana mirungi inamadhara mengi yakiwemo kuchanganyikiwa, kupoteza nguvu za kiume, kushindwa kuhudumia familia vizuri, kupata kansa na kadhalika."


Naye Bi. Hawa, mwananchi wa kata ya Tae wilaya ya Same, alisema kuwa, hajui sababu ya watu kuendelea kujihusisha na kilimo cha mirungi kwani, kuna mazao mengi yanayostawi kama vile vitunguu, karoti na iliki pamoja na miradi ya nguruwe iliyoletwa na serikali. Aliongeza: "Aidha, ameiomba serikali kuimarisha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayozalishwa kupelekwa sokoni, hali itakayosaidia wananchi kuwa na uhakika wa masoko ya mazao yao na hivyo kuachana na biashara ya mirungi."


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wazalishaji, wasambazaji, na watumiaji wa dawa za kulevya. Ushirikiano huu utasaidia kutokomeza kabisa biashara hii haramu na kulinda ustawi wa jamii. Kamishna Lyimo alimalizia kwa kusema: "Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika ili kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa salama na lenye maendeleo endelevu."


 


Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, imemhukumu mchungaji Daud Nkuba maarufu kwa jina la Komando Mashimo, Nabii Nikaya, (Mchungaji Mashimo) kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili kati ya matatu aliyokuwa akishtakiwa nayo.

Mashimo ametiwa hatiani kwenye mashtaka ya kuingia kwa jinai na kuharibu mali, huku akiachiliwa huru kwenye shtaka la kutishia kwa vurugu.

Mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka matatu ambapo upande wa Jamhuri umethibitisha makosa mawili dhidi yake na kushindwa kuthibitisha shtaka la kutishia kwa vurugu.

Hukumu hiyo ilitolewa leo Machi 18, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhan Rugemalila, baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha makosa dhidi ya mshitakiwa bila kuacha shaka yoyote.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Rugemalila alisema, "Nimeridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa Jamhuri na vielelezo, ambapo wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo mawili. Hata hivyo, mshtakiwa ameachiliwa huru kwa shtaka la tatu kwa kuwa upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa alitenda kosa hilo."

Aidha, alisema, "Mshtakiwa katika kosa la kuingia kwa jinai, mahakama inakupa adhabu ya kwenda jela miezi sita, na kosa la kuharibu mali, mahakama inakutia hatiani na kukupa adhabu ya kwenda jela miaka miwili. Pia, mahakama inakuachia huru kwa kosa la kutishia kwa vurugu kwa sababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi yako. Hivyo, utatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani."

Kabla ya kusomewa adhabu, mshitakiwa alipata nafasi ya kujitetea, ambapo aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Rhoda Kamungu, uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kama sheria inavyoelekeza, ili iwe fundisho kwake na kwa jamii nzima.

Awali, ilidaiwa kuwa, Novemba 22, 2023, mchungaji Mashimo alifanya uhalifu katika maeneo ya Mbezi Luis Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, kwa kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Frola Mwashaa. Aidha, aliharibu ujenzi wa nyumba iliyokuwa eneo hilo, kinyume cha sheria.

Pia, ilidaiwa kuwa, katika shtaka la tatu, alimtishia Ramson Vicent kwa vurugu.

 



Polisi: "Hatutasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria"

Dar es Salaam, Machi 9, 2025 – Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limemkamata na baadaye kumjeruhi kwa risasi mtuhumiwa wa utekaji mtoto, Stanley Dismas Ulaya (18), mkazi wa Kata ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumteka mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 8, mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mbezi, Ubungo, jijini Dar es Salaam. Tukio hilo lilitokea Machi 6, 2025, wakati mtoto huyo aliposhuka kwenye daladala kuelekea shuleni, ndipo mtuhumiwa alimkamata na kumpeleka hadi Bagamoyo, mkoani Pwani, ambako alimficha vichakani huku akitumia namba ya simu ya mzazi iliyokuwa kwenye madaftari ya shule ya mtoto huyo kudai pesa kwa vitisho.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, alisema kuwa Jeshi la Polisi lilifanya juhudi kubwa za ufuatiliaji hadi kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa mnamo Machi 8, 2025, majira ya saa 1:00 usiku.

"Baada ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, mtuhumiwa alijaribu kutoroka kwa kukimbia. Askari walilazimika kupiga risasi hewani kwa tahadhari, lakini alipokaidi, walimlenga kwa risasi mguuni na pajani ili kumzuia," alisema Kamanda huyo.

Mtuhumiwa alipelekwa hospitalini kwa matibabu kutokana na majeraha aliyopata, huku hali ya mtoto ikiendelea kuwa nzuri chini ya uchunguzi wa madaktari.

Jeshi la Polisi limeendelea kulaani vikali vitendo vya utekaji nyara na limeahidi kuchukua hatua kali kwa wahusika wote kwa mujibu wa sheria. "Hatutasita kuwashughulikia wahusika wa vitendo hivi kwa mujibu wa sheria. Tunatoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu," aliongeza Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.





Na Prisca Libaga Arusha


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa niaba ya Kamishna Jenerali tarehe 13.09.2024 imeteketeza kwa mujibu wa sheria vielelezo vya dawa za kulevya aina ya mirungi kilogramu 23.74 zilizokamatwa katika operesheni zilizotekelezwa hivi karibuni. Uteketezaji wa vielelezo hivyo ulifanyika katika dampo la Murieti jijini Arusha. 



Zoezi hilo limeshuhudiwa na wawakilishi kutoka Mahakama ya Wilaya Arusha, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Arusha, Ofisi ya Mkemia Mkuu Arusha kulingana na Matakwa ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. 





■Watano wakamatwa na vifaa vya kutengeneza vilipuzi vya baruti  vya uvuvi haramu wa baruti.


■Majahazi wawili yakamatwa na Mifuko ya sukari  550 kwa kukwepa ushuru.


■Mmoja akamatwa kwa utapeli na kujifanya Askari Polisi Kikosi cha Wanamaji.



Katika kipindi cha operesheni maalumu iliyotekelezwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji Dar es Salaam kuanzia Januari 15, 2024, hadi sasa, jumla ya watuhumiwa watano wamekamatwa na kushikiliwa kutokana na tuhuma za kuhusika katika vitendo vya uvuvi haramu baharini pamoja na matumizi ya vilipuzi na mbolea ya Ammonium salfeti. Watuhumiwa hawa wanashikiliwa kwa makosa ya kuhatarisha usalama wa baharini na kukiuka sheria za uvuvi.


Miongoni mwa watuhumiwa hao, baadhi yao walikutwa na mbolea aina ya Ammonium salfeti yenye uzito wa kilogramu 200 na vilipuzi (detonators) aina mbalimbali, jumla yake ikiwa vipande 443. Operesheni hii inaonesha dhamira ya jeshi letu katika kukabiliana na vitisho vinavyotokana na uvuvi haramu kwa kutumia njia hatari kama milipuko.


Tutakapopata maelezo zaidi kuhusu mashtaka yao, tutahakikisha kuwafikisha mahakamani ili haki iweze kutendeka. Watuhumiwa hawa ni sehemu ya mtandao unaoshukiwa kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu ambavyo vina athari kubwa si tu kwa mazingira bali pia kwa uchumi wa nchi yetu.