Showing posts with label Ngorongoro. Show all posts
Showing posts with label Ngorongoro. Show all posts




Wilaya ya Ngorongoro ipo katika hatua za mwisho ya mapitio na kupitisha mkakati mpya wa miaka mitano unaodhamiria kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kasi ya maendeleo unaokwenda sambamba dira ya taifa ya maendeleo 2025-2050.



Akifungua kikao maalum cha kupitia mkakati huo mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Brigedia Jenerali Wilson Sakulo amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kutumia fursa hiyo kwa kupanga vipaumbele vitakavyogusa maisha ya wananchi.



“Leo tumekutana hapa kupanga mipango yetu kwa miaka mitano, hakikisheni mnapanga vipaumbele vinavyopimika kwa kuangalia maslahi ya wananchi wa wilaya hii ili waweze kupata huduma bora za kijamii, miundombinu na kuboresha shughuli zao za kiuchumi”,alisema Brigedia Jenerali Sakulo.


Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Manja Sironga Yaile aliipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo kutokana na kushiriki kikamilifu katika kuchangia mipango mbalimbali ya kijamii ya Tarafa ya Ngorongoro na wilaya hiyo.



Wakichangia kuhusu mpango mkakati huo baadhi ya madiwani walisisitiza umuhimu wa kujikita katika ujenzi wa barabara,malisho, maji na uimarishwaji wa huduma za kijamii.






 


Na Mwandishi Wetu, Tanga.


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imewezesha ziara ya mafunzo kwa Viongozi wa Mila (Malaigwanani), Wazee Mashuhuri na kinamama  33 kutoka kata 11 za tarafa ya Ngorongoro kutembelea kiwanda cha kuzalisha na kuchakata mazao ya maziwa cha Tanga Fresh, kilichopo jijini Tanga.



Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Malaigwanani Ngorongoro na Diwani wa Kata ya Olbalbal, Mhe. Metui Shaudo alisema, ziara hiyo imewapa fursa ya kuona kwa vitendo hatua mbalimbali zinazofanyika katika uchakataji wa maziwa, kuanzia ukusanyaji wa maziwa, uzalishaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali zilizoongezewa thamani.



 “Tumetembelea kiwanda hiki kujifunza na kuona mambo mengi ambayo tunaweza kuyatumia tunaporudi Ngorongoro, tumeona kuwa maziwa yanaweza kuwa na thamani kubwa zaidi yakichakatwa vizuri badala ya kuuzwa yakiwa ghafi kama ambavyo mara nyingi inafanyika kwa wananchi wetu, baada ya ziara hii tutapelekeaa elimu hii kwa wananchi wenzetu ili kuwaongezea tija na kipato kinachotokana na ufugaji,” alisema  Shaudo 


Kina mama walioshiriki ziara hiyo  wameelezea kufurahishwa na manufaa yanayotokana na  mifugo na kuwaongezea ujuzi wa uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya mifugo na kuahidi kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa Ngorongoro ili waendelee kujikwamua kiuchumi.


Kiongozi wa mila kutoka kata ya kakesio Ole Kotika ameeleza kuwa ziara hiyo  inaendelea kuimarisha mahusiano mazuri kati ya hifadhi ya Ngorongoro na wananchi hasa kuwaongezea fursa ya kujifunza shughuli za ufugaji wa kisasa, usindikaji wa bidhaa za maziwa zenye ubora na kuongeza mnyororo wa thamani ambao unasaidia kukuza uchumi wa wananchi.



Ziara ya viongozi hao ni sehemu ya jitihada za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii ya kuwawezesha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kupata ujuzi na uzoefu unaoweza kuboresha shughuli zao za kiuchumi na kuongeza thamani ya rasilimali walizonazo.

 


Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu  (HESLB) imetoa elimu kwa jamii ya Ngorongoro kuhusu  mfuko wa  Ngorongoro Scholarship Fund  unaolenga kuwezesha wanafunzi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kupata fursa ya masomo ya elimu ya juu kupitia ufadhili Ngorongoro Fund.  




Elimu hiyo iliyotolewa katika ofisi za Ngorongoro ilijumuisha wadau muhimu wanaoguswa na mpango huo ambao ni viongozi wa jamii, wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali ambao wamepewa uelewa kuhusu vigezo vya mkopo, sifa za waombaji pamoja na kupitia na kujadili mwongozo wa programu ya Ngorongoro Scholarship Fund.



Katika kikao hicho, viongozi wa jamii wamepongeza hatua ya Mamlaka ya kushirikiana na HESLB katika kuandaa na kuboresha mwongozo wa mfuko huo, wakieleza kuwa utasaidia kuweka utaratibu unaozingatia usawa, uwazi na mahitaji ya wakati katika kuwawezesha wanafunzi wenyeji kupata fursa za elimu ya juu.



Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro,  Edward Maura, aliipongeza Mamlaka ya Ngorongoro na HESLB kwa kutoa elimu kuhusu Ngorongoro Scholarship Fund hasa jinsi wanufaika wanavyoweza kutambua fursa, kujaza fomu na kufuata taratibu za kuomba ufadhili.



“Tunawapongeza Ngorongoro na Bodi ya Mikopo kwa kutoa elimu hii kwa jamii na wanafunzi na kusaidia kuwaondolea wanafunzi changamoto na uelewa mdogo wa namna ya kuomba na kupata mikopo huu, tunaamini maamuzi haya ya Serikali yanalenga  kuimarisha mahusiano kati ya jamii na Ngorongoro na tunaamini wanafunzi na jamii  watatumia  fursa zinazotolewa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa” alisema Mh. Maura.



Utekelezaji wa program hii unalenga kuimarisha ushirikiano na kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wa Ngorongoro ambapo elimu wanayopata itasaidia ushiriki wao katika program za uhifadhi endelevu na kuvutia wageni kupitia vivutio vya utalii vilivyopo.



 


Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania Ephraim Balozi Mafuru kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii ameongoza timu ya wizara hiyo kwenye kikao cha kimkakati na viongozi wa wizara ya Utalii kutoka Jamhuri ya Zambia huku Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikijinasibu kwa upekee  wa vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo ambapo asili, urithi na maajabu yanakutana eneo moja.



Mkurugenzi Mafuru ameeleza ujumbe huo kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Waasisi wa Tanzania na Zambia kuunganisha mshikamano wa kiuchumi na kijamii.



Mafuru amesema Tanzania inasonga mbele katika sekta ya utalii kutokana na kuimarisha  uhifadhi,miundombinu ya utalii pamoja na utafutaji wa masoko ya kimkakati ndani na nje ya nchi.



Akitoa wasilisho la Mamlaka ya Hifadhi  ya Ngorongoro Afisa Masoko Mwandamizi Selestine Saitabau alisema Ngorongoro ni kama kikapu cha zawadi ambapo kimebeba vivutio vingi kuanzia historia ya chimbuko la binadamu, wanyamapori, mazalia ya Nyumbu, mchanga unaohama, misitu, ndege, hali ya hewa ya kuvutia na uoto wa asili wenye mandhari yanayonawirisha ikolojia ya Ngorongoro, Serengeti hadi Masai Mara.



Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru aliwashukuru wageni hao wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Kiongozi na katibu Mkuu wa wizara ya Utalii Zambia na kuwaeleza kuwa Ngorongoro ina sifa zote za kuwa Bustani ya Eden na kuwahakikishia wageni hao kuwa wamerudi nyumbani kwenye asili ya Mababu zao wa takriban miaka zaidi ya milioni 3 iliyopita.

 



Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) leo tarehe 13 Machi, 2026 Karatu  imedhihirishiwa kuwa Ngorongoro ni sehemu pekee duniani yenye  ushahidi timilifu wa mwanzo wa binadamu wa kale.


Umwamba huo wa kihistoria ulioainishwa na wabobezi wa mambo kale umehifadhiwa katika makumbusho ya Urithi Geopark Museum iliyopo Karatu mkoani Arusha.



Akijinasibu mbele ya kamati ya bunge kuhusu ukweli huo Afisa Mhifadhi Mkuu wa mambo kale Dkt.Agness Gidna amesema muunganiko wa maisha ya binadamu kutoka zaidi ya miaka Milioni Mia tatu iliyopita hadi kizazi cha sasa  inapatikana katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro.


Wabunge wa kamati hiyo wamefurahishwa na uwepo wa makumbusho hiyo ni kuitaka mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kutangaza makumbusho hiyo na kazi zake za kihistoria duniani.


Mwenyekiti wa kamati hiyo Timotheo Mnzava ameishauri wizara ya Maliasili na Utalii kutanua wigo wa matangazo ya vivutio vya utalii ikiwemo makumbusho hiyo.



Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameeleza Kamati hiyo kuwa Wizara na taasisi zake inaendelea mkakati wa kutangaza utalii kwa kupitia masoko mbalimbali ya kimkakati Ulaya, Asia, Amerika ili kufikia malengo ya Serikali na kufikia zaidi ya watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030 kw akuhakikisha kuwa kila mwaka bidhaa moja mpya inapelekwa sokoni.



Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Abdul-Razaq Badru amesema mikakati ya kuboresha eneo la makumbusho hiyo kwa kuongeza miundombinu mbalimbali ya kuvutia wageni wanaotembelea inaendelea ili kwenda sambamba na chapa ya Ngorongoro kama Premium Safari Destination.

 


Swahili wisdom says 'tembea uone' -walk and you will see, and that no journey is ever wasted. Near the Olduvai Gorge, within the Ngorongoro Conservation Area, there is a wonder that proves this truth: the Shifting Sands.


Beside the cradle of human history, a crescent-shaped dune of black sand slowly journeys across the land. Each year, thousands of visitors come not to collect the elusive black sand, but to stand in awe of it. This sand, darkened by iron minerals and volcanic ash from eruptions of Mount Oldoinyo Lengai, is alive with movement.


Driven by the wind, the dune advances quietly, about 15 to 29 metres each year, rising nearly five metres high and stretching a hundred metres wide. It moves without hurry, without noise, teaching patience to those who stop to watch.


These are the wonders of Ngorongoro. If you wish to understand them, walk and see, for the pride of the eyes is in seeing, and that pride never empties the shop.

  


Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro.


Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA), Abdul-Razaq Badru ameongoza kikao cha kimkakati kilichojumuisha waheshimiwa Madiwani,  Viongozi wa Mila, watendaji wa kata, wenyeviti wa Vijiji na watendaji wa vijiji kwa lengo la kudumisha mahusiano na uboreshaji wa huduma za kijamii na uboreshaji wa shughuli  za Uhifadhi shirikishi.



Kamishna Abdul-Razaq Badru ameeleza kuwa kikao hicho ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka hiyo kukutana na makundi mbalimbali kujadili uboreshaji wa shughuli za kijamii na huduma za wananchi kama Maji, shule, Malisho, barabara, mawasiliano, afya na mengineyo.



"Viongozi na Wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro ni wadau muhimu katika hifadhi, tunakutana nao kama sehemu ya kuboresha uhusiano na kuwaeleza mikakati ya Serikali dhidi yao. 



kwa sasa tunaboresha miundombinu ya huduma za maji, ujenzi wa Barabara kwa tabaka gumu kutoka Loduare hadi Golini, kujenga minara mipya ya mawasiliano 9 ndani ya hifadhi ili kufikisha huduma kwa wananchi na wadau mbalimbali" amefafanua Kamishna Badru.



Kwa upande wa Viongozi waheshimiwa Madiwani, viongozi wa Mila wameiomba Serikali kupitia Mamlaka hiyo kuendelea kuboresha mahusiano, huduma za kijamii kama  miundombinu ya Maji, barabara, ukarabati wa vituo vya afya na shule, mahitaji  ya baraza la wafugaji, chunvi za mifugo na mpango wa malisho ya mifugo hawa wakati wa kiangazi.



Tofauti na vijana wa mjini hasa wa Dar es Salaam ambao wengi wao hutahiriwa wakiwa wadogo hospitalini tena kwa ganzi, tohara kwa vijana wa kimasai hufanyika wakiwa mabarobaro na mashabaro na tena bila ganzi na hivyo kusikia maumivu makali ya kitendo hicho.



Katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeungana naye kwa kupanda miti aina ya Olorien katika kijiji cha Oloirobi Wilayani Ngorongoro.



Miti hiyo hukatwa na hutumika mara baada ya vijana wa kimasai kufanyiwa Jando/kutahiriwa, kijana akishatahiriwa miti huo huwekwa mlangoni wa nyumba yenye kijana aliyetahiriwa kisha akina mama huzunguka ulipowekwa mti husika huku wakiimba kwa furaha na vigelegele kuashiria kwamba zoezi la tohara limefanyika na kukamilika.



Kwa mujibu wa imani ya kabila hilo nyimbo za shangwe na faraja zinazoimbwa na kina mama kwa kuzunguka mti huo ukiwa kwenye nyumba humfanya kijana kuwa na faraja kutofikiria maumivu aliyoyapata wakati wa tohara.



Tohara katika kabila la wamasai inahusisha mafundisho yote ya msingi kwa mwanaume ikiwa ni pamoja na kuwafanya wawe majasiri na shujaa wanaoweza kukabiliana na changamoto zozote za kimaisha tofauti na vijana wanaozaliwa mjini maarufu kama vijana wa elfu mbili (2000) ambao wengi wao maumivu ya jando hawayafahamu kutokana na kutahiriwa wakiwa wadogo tena wengi wao wakifanyiwa tohara hospitali.



Akizungumza mara baada ya zoezi hilo la upandaji wa miti Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayesimamia Idara ya Maendeleo ya Jamii Gloria Bideberi amesema kuwa mamlaka itaendelea kuithamini miti hiyo na kushirikiana na jamii ya kabila hilo kuhakikisha miti hiyo haitoweki



Kiongozi wa kimila wa kata ya Ngorongoro bwana Sembeta Ngoidiko amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti na kusema na wananchi wa kijiji cha Oloirobi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wameamua kupanda miti hiyo pamoja na miti mingine inayotumika kama miti dawa ili kuendelea kudumisha uhifadhi,mila na desturi.

 


Mwandishi wetu Endulen Ngorongoro.

Tarehe  20 Desemba, 2025


Uhusiano kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na jamii inayoishi ndani ya eneo la hifadhi umeendelea kuimarika kufuatia ziara za Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Bw. Abdul-Razaq Badru katika vijiji mbalimbali vilivyoko tarafa ya Ngorongoro ambapo leo tarehe 20 Desemba,2025  ametembelea Kata ya Enduleni, wilayani Ngorongoro.



Akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ngorongoro na Diwani wa Kata ya Endulen Mhe. Elias Sakara Nagol, Kamishna Badru ameeleza kuwa, lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya Uongozi wa hifadhi ya Ngorongoro na jamii, pamoja na kukagua maboresho ya miundombinu ya maji inayotumika kwa  matumizi ya wananchi, mifugo na wanyamapori.



Katika ziara hiyo Kamishna Badru amewaeleza wananchi wa vijiji vya Kata ya Enduleni kuwa Mamlaka inatekeleza Miradi ya Maji katika kata za Endulen, Kakesio, Olbalbal na maeneo mengine na  aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika usimamizi na utunzaji wa miradi hiyo ambayo inagharimu fedha za Serikali.



Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Enduleni, Dkt. Elias Sakara Nagol, amempongeza Kamishna Badru na wasaidizi wake kwa kuendeleza uhusiano  ya karibu na jamii inayoishi ndani  kwa kuwatembelea mara kwa mara, kusikiliza kero zao na kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kijamii na kuahidi kuwa wananchi wataendelea kuwa mabalozi wazuri wa kutunza na kulinda hifadhi kupitia programu ya uhifadhi shirikishi.



Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.


Jamii ya kabila la Wahadzabe inayopatikana pembezoni mwa Ziwa Eyasi Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha ni miongozi mwa makabila yaliyopo katika mzunguko wa Jiopaki ya Ngorongoro Lengai. Jamii hii ni wanufaika wa mradi wa makumbusho mpya ya kijiolojia (Urithi Geopark) iliyopo katika mji wa Karatu.



Nchi ya Tanzania na barani Afrika kwa ujumla zipo kanuni na taratibu mbalimbali ambazo jamii au makabila hujiwekea kama njia ya kuenzi na kutunza mila na desturi zao.


Katika kabila la Wahadzabe (Watindiga) kwa wanandoa (mke na mume) kufanya tendo la ndoa na mtu mwingine nje ya ndoa (Kuchepuka) inatafsiriwa kuwa ni laana kubwa kwa kabila hilo ambapo mtu anayefanya kosa hilo na ikathibitika adhabu yake ni kuuwawa na mtu aliyewafumania (aliyewashuhudia) kisha akishatekeleza mauji anapiga ukunga au yowe ili jamii ikusanyike na wazee wa kimila kutoa taarifa rasmi kwa jamii kuhusu kitendo hicho ambacho kinatafsiriwa kuwa ni kuleta laana na nuksi kwenye familia. 



Njia inayotumika kuwaua waliochepuka ni kuchomwa na mishale yenye sumu mwilini Mithili ya mnyama anayewindwa, Mishale inayotumika ina sumu kali ambayo huenea haraka kwenye mwili wa mwanadamu na kupoteza maisha ndani ya muda mfupi.


Katika maisha ya mapenzi na ndoa kwa jamii ya wahadzabe zipo kanuni mbalimbali ambazo wamejiwekea ikiwemo kila mwanaume anayeoa na mwanamke anayeolewa kuheshimu ndoa yake na kuepuka kwa vyovyote vile kushiriki tendo la ndoa na mwanamke au mwanaume mwingine.



Baada ya kuoana bibi na bwana harusi hutakiwa kuishi kwa upendo na jamii hufuatilia ndoa hiyo ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu miongoni mwao anayefanya tendo la ndoa nje ya mwenza wake, jamii hiyo ipo makini katika kufuatilia mienendo ya wanandoa ili kuhakikisha kuwa usalama wa familia unakuwepo katika kipindi chote cha ndoa hiyo.


Mchakato wa kuwaua wanandoa waliochepuka haufanyiki kwa kukurupuka bali uchunguzi na ufuatiliaji wa kina hufanyika mpaka pale watu wanaoaminika watakapowashuhudia watuhumiwa wakiwa katika kilele cha ndoa hiyo.


Kwa mujibu wa Kiongozi wa Mila za Wahadzabe Mzee Shagembe Gambai Jamii hiyo imeweka utaratibu huo wa kuwaua watu wanaochepuka ili kuimarisha nidhamu za familia, ukoo na jamii kwa ujumla ndio maana hadi sasa utaratibu huo umezoeleka na kuheshimiwa hivyo ni nadra sana kusikia mhadzabe akichepuka.


Katika kuhakikisha kuwa kila mmoja anajifunza ubaya wa kuchepuka zoezi la kuwaua waliofumaniwa hufanyika hadharani likishuhudiwa na jamii yote ya eneo hilo wakiamini kuwa kitendo hicho kinatoa darasa kwa wanandoa wengine kuacha tabia hiyo.


Mzee Shagembe anasimulia kuwa Ndoa kwa jamii ya wahadzabe si suala la kufa na kuzikana laah hashaa, jamii hiyo huruhusu kuachana na ikitokea hivyo unaruhusiwa kuoa au kuolewa na mtu mwingine hata kama huyo unayeanza naye uhusiano upya ni mtu wako wa karibu au rafiki wa aliyekuwa mwenza wako.


Jamii ya Wahadzabe hawaamini katika ndoa za mke zaidi ya mmoja, Kwao ndoa ya mke na mume mmoja tu na hairuhusiwi mwanaume kuoa mke zaidi ya mmoja sababu kubwa ikiwa ni kuimarisha upendo kwa wale walioamua kuishi kama mke na mume.

 


Wananchi wa Kitongoji ya Ormekeke Kijiji cha Nasipaoriong tarafa ya Ngorongoro wameanza kunufaika na mradi wa maji baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuchimba kisima chenye uwezo wa kuzalisha lita 13,00 kwa saa na kujenga tanki  lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 135,000 kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo.



Akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Abdul-Razaq Badru ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kümeleta  manufaa makubwa  kwa wananchi wa maeneo ya Ormekeke, Nasipaoriong na Olduvai yaliyopo hifadhi ya Ngorongoro ambao kipindi cha kiangazi walilazimika kuhamishia mifugo maeneo ya mengine kufuata maji


“Mradi huu tuliuanza kwa  kuwashirikisha wananchi ikiwa ni utekelezaji wa kuboresha mahusiano ya NCAA na jamii kwa kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ambalo moja wapo ni maji, umeshakamilisha na kitongoji cha Ormekeke wameanza kutumia maji, rai yangu kwa wananchi ni kulinda na kusimamia miundombinu ya mradi huu kupitia kamati za maji na mazingira ambazo wameshaziunda” alisema  Kamishna Badru.



Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ormekeke Bw.  Oreteti Olenjorio ameeleza kuwa eneo la kitongoji hicho ni kame na halina chanzo chochote cha maji hivyo uamuzi wa Serikali kupitia mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kuchimba maji ni msaada mkubwa kwa matumizi ya wananchi na mifugo na kuahidi kulinda miundombinu ya mradi huo  kupitia jumuiya za maji na kuzingatia sheria za hifadhi.



Kwa mujibu wa Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Godlove Sengele pamoja na mradi huo kunufaisha wananchi na mifugo yao pia utahudumia Makumbusho ya Olduvai, Leakey Camp, Mtui Camp, Nyumba za Maaskari pamoja na jamii ambayo imejengewa vituo vinne vya kuchotea maji na vituo vitatu vya kunyweshea mifugo.