Showing posts with label Teknolojia. Show all posts
Showing posts with label Teknolojia. Show all posts

 


ARUSHA: Serikali imewahimiza watengeneza maudhui nchini kuchangamkia fursa za uwezeshaji zinazotolewa ili kukuza taaluma zao na kujiimarisha kiuchumi kupitia sekta ya ubunifu inayokua kwa kasi.



Rai hiyo imetolewa jijini Arusha Aprili 8, 2026  na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Kelvin Kanje, wakati akifunga mafunzo maalum yaliyoshirikisha zaidi ya watengeneza maudhui 450. 



Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania.



Kanje Aliwapongeza watengeneza maudhui hao kwa kushiriki mafunzo kwa awamu ya kwanza, akiahidi kuwafikia watengeneza maudhui katika mikoa mingine.



Aidha, amewataka Watengeneza Maudhui walioshiriki mafunzo kwa awamu va kwanza kutumia mafunzo havo kuboresha kazi zao ili ziwaingizie kipato.



"Kwa wale mnaoanza mafunzo haya yatawasaidia kuinuka na wale ambao tayari mmeanza mfanye vizuri zaidi," amesema Kanje.



 Nidhamu ya Fedha na Mikopo

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Wasanii, Dk. Asha Mshana, alibainisha kuwa ongezeko la watengeneza maudhui ni fursa kubwa ya ajira, lakini mafanikio yake yanategemea nidhamu ya kifedha na uelewa wa kibiashara.

"Mfuko wa Utamaduni na Sanaa unatoa mikopo bila upendeleo kwa lengo la kuwawezesha wabunifu. Ni wajibu wa wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili kuendeleza mzunguko wa kuwainua wengine," alisisitiza Dk. Mshana.



Ubora wa Maudhui na Maadili

Mbali na usimamizi wa fedha, washiriki walihimizwa:


 Kuzingatia ubora wa kazi zao ili kushindana kimataifa.

 Kutumia lugha za kimataifa ili kupanua wigo wa soko lao.

 Kulinda maadili na usalama wa taarifa binafsi katika majukwaa ya kidijitali.



 Balozi wa Nishati Safi ya Kupikia

Katika hatua nyingine, Mhandisi Benezeth Kabunduguru kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, aliwaomba wabunifu hao kutumia ushawishi wao kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.

Alieleza kuwa kupitia video fupi na vichekesho, wasanii wana nafasi kubwa ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.



Akihitimisha mafunzo hayo, Kanje aliwapongeza washiriki kwa kujitokeza kwa wingi na kuwasisitiza kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi ili kuboresha kazi zao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

 


Panya mmoja wa kiume anayenusa mabomu ya ardhini nchini Cambodia ameweka rekodi mpya ya dunia, kwa kuwa panya wa kwanza kufichua zaidi ya mabomu mia moja ya kutegwa ardhini na mabaki mengine ya zana za kivita ambayo yanaweza kusababisha maafa. 


Ronin, panya kutoka Tanzania, amethibitisha umuhimu wa wanyama hawa katika mchakato wa kutoa msaada wa kipekee katika maeneo yaliyoathiriwa na vita.

Shirika la kutoa misaada ya kutegeua mabomu yaliyotegwa ardhini lililo na makao yake nchini Ubelgiji, la APOPO, limetangaza kuwa Ronin amefanya kazi kubwa katika jimbo la Preah Vihear, kaskazini mwa Cambodia, kwa zaidi ya miaka mitatu. 


Katika kipindi hicho, amegundua mabomu 109 na vifaa vingine vya kivita vyenye hatari. 


Mafanikio haya yamefanya Ronin kuwa panya wa kwanza kufikia rekodi hiyo, akivunja ile ya awali iliyoshikiliwa na panya mwingine maarufu, Magawa, ambaye pia alitoka Tanzania.

Magawa aligundua mabomu 71 katika kipindi cha miaka mitano kabla ya kustaafu mwaka 2021. 


Magawa alitunukiwa medali ya dhahabu kwa ushujaa wake, lakini alifariki mwaka 2022. Kwa sasa, Ronin ameendelea na jukumu hili la kugundua mabomu kwa ufanisi, huku akiwa na uwezo wa kufanya kazi kwa miaka mingine miwili, kulingana na taarifa za APOPO.


Panya huyu mwenye umri wa miaka mitano amepewa taji la Rekodi za Dunia za Guinness kwa kugundua mabomu mengi zaidi ya ardhi. 


"Mafanikio yake ya kipekee yamemfanya apate taji la Rekodi za Dunia za Guinness kwa kuwa panya aliyegundua mabomu mengi ya ardhini," ilisema taarifa ya APOPO.


Cambodia inakabiliana na madhara ya mabomu yaliyosalia kutoka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwishoni mwa miaka ya tisini. 


Maelfu ya mabomu ya kutegwa ardhini bado yapo kwenye maeneo mbalimbali, yakitishia maisha ya raia, hasa watoto. Vifo vinavyosababishwa na milipuko ya mabomu ni jambo la kawaida, na takribani vifo 20,000 vimetokea tangu 1979. 


Watoto wawili waliuawa mwezi Februari mwaka huu wakati guruneti lililokuwa limeachwa kutoka kwa vita lililipuka karibu na makazi yao kaskazini magharibi mwa mkoa wa Siem Reap.

Nchini Tanzania, shirika la APOPO linatumia panya wa kunusa pia katika kugundua magonjwa kama kifua kikuu, ambapo panya hawa hutumika kutambua watu wanaougua ugonjwa huu kwa haraka na ufanisi. 


Hii ni sehemu ya juhudi za shirika hili kutoa huduma muhimu ya kiafya na usalama kwa watu wa maeneo mbalimbali.

Kwa hivyo, panya hawa wa kunusa ni wanyama wa kipekee na mashujaa, kwani wanasaidia katika kupambana na hatari zinazotokana na vita, silaha zilizotegwa ardhini na magonjwa hatari. 


Ufanisi wa Ronin unathibitisha uwezo wa wanyama hawa katika kutoa msaada muhimu na kuokoa maisha duniani kote.


Chanzo; BBC 

 


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amewataka wananchi kulinda mawasiliano yao ya simu kwa umakini kama wanavyolinda mali zao zenye thamani. 


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 21, 2025, jijini Arusha, Waziri Silaa amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watu kuacha kufanya mazungumzo na watu wasiowafahamu kupitia simu au mitandao ya kijamii kwani wanapofanya hivyo wanajikuta wakitoa fursa kwa matapeli.



Katika kikao hicho kilichofanyika pembeni ya uzinduzi wa kampeni ya Sitapeliki, Waziri Silaa alieleza kuwa ulinzi wa simu unapaswa kuwa kipaumbele cha kila mtu ili kuepuka kutapeliwa.


"Usijiunge na link usizozifahamu, ukijiunga nayo kwa mfano kwenye Facebook, imetengenezwa kwa mfumo unaoiwezesha kuchukua akaunti yako. 


Wakishachukua akaunti yako wanaitumia kuomba watu fedha kwa kuandika vibonzo vya kulaghai watu," alisema Waziri Silaa.



Aliongeza kuwa, "Kuclick link usiyoifahamu ni kama kugongewa mlango nyumbani kwako usiku na mtu usiyemfahamu kisha umfungulie. Yaani mtu anagonga unamuuliza nani hakujibu au anakwambia mimi mbunge wako au nakwambia mimi mwanamaombi halafu umfungulie unakuta umemfungulia mwizi ndiyo hivyo hivyo utakavyoclick link usiyoijua unakua umefungulia wezi."


Waziri Silaa alisisitiza kuwa watanzania wanapaswa kutoa taarifa kwa polisi pindi wanapojitokeza matukio ya utapeli kupitia mitandao ya simu. 


Alihimiza wananchi kuwa na tahadhari na kutoa taarifa haraka wanapopoteza simu au kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa mawasiliano yao.



"Watanzania wakipoteza line waone ni jukumu lao kutoa taarifa kwa mtoa huduma ili line ifungwe. 


Mtu ana simu ndogo ya 20,000 anapoipoteza haoni sababu ya kutoa taarifa kwa mtoa huduma na ni rahisi simu hiyo kuokotwa, na simu hiyo haina namba ya siri au una namba ya siri rahisi unakuta 1234," aliongeza.


Akiendelea kutoa wito wa kuchukua tahadhari, Waziri Silaa alisema kuwa mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha uhusiano kati ya matapeli na makampuni ya simu. 


Hata hivyo, alisisitiza kuwa kuna ushirikiano wa aina fulani unapotokea wakati matapeli wanapopiga simu kwa kutumia namba za simu za wahanga.


Kuhusu kampeni ya Sitapeliki, Waziri Silaa alitoa wito kwa kila mtanzania kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya utapeli kwa kutokutoa ushirikiano kwa matapeli. 


Alisisitiza umuhimu wa kuweka namba za siri na kuepuka kufungua links ambazo hazijulikani.


"Kampeni ya Sitapeliki ni ya kila mmoja wetu kuweza kuamua kwamba hatapeliki, kwa kutokutoa ushirikiano, kuweka namba za siri, ambazo zina ugumu wa aina fulani wa mtu kuweza kubaini," alisema.


Pia, alitoa wito kwa watanzania kutambua kuwa hakuna pesa za bure zinazoweza kutolewa kupitia mitandao ya simu, hivyo wanapaswa kuwa makini na jumbe za utapeli ambazo hutumwa kwa njia ya links.

Baadhi ya waandishi wa habari walitoa maoni yao kuhusu huduma za simu na mitandao. 


Walishauri kampuni za simu kutoa huduma za haraka kwa watumiaji ili kurahisisha utoaji wa taarifa na kuimarisha huduma nzuri kwa wananchi.


Kampeni ya Sitapeliki imezinduliwa kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu hatari ya utapeli kupitia mitandao ya simu na kuhakikisha kuwa jamii inakuwa na uelewa zaidi kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya matapeli.

 

Serikali, watoa huduma za simu na intaneti kushirikiana kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na utapeli mtandaoni



Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amezindua kampeni ya taifa ya "SITAPELIKI" iliyolenga kutoa elimu kwa umma kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli mtandaoni na jinsi ya kujikinga na udanganyifu huo. 



Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Februari 20,2025 jijini Arusha na kuhudhuriwa na wadau umuhimu kutoka sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari, wakiwemo viongozi kutoka Wizara ya Mawasiliano, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT), na makampuni ya simu.



"Leo hii, tupo katika mkutano huu wa kuzindua kampeni ya pamoja ya utoaji elimu kwa umma na kuwa na mpango mahususi wa kushughulikia masuala ya utapeli mtandaoni iitwayo 'SITAPELIKI.'


Kampeni hii inalenga katika kuongeza uelewa kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni na kuwapa wananchi maarifa zaidi ya jinsi ya kujikinga dhidi ya majaribio mbalimbali ya ulaghai," alisema Waziri Silaa.

Katika hotuba yake, Waziri Silaa alieleza kuwa kampeni hii ni sehemu ya jitihada za serikali kushirikiana na watoa huduma za simu na intaneti kutoa elimu na kuongeza ufanisi katika kupambana na utapeli mtandaoni. 

Aliongeza kuwa utapeli huu unahujumu maendeleo ya nchi kwa kuwatia hofu watumiaji wa huduma za mtandao, na hivyo kudumaza juhudi za serikali za kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijiti na kujenga uchumi wa kidijiti.

"Kampeni hii ya SITAPELIKI ina lengo la kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuchukua hatua mahususi katika kushughulikia masuala ya utapeli mtandaoni," alisisitiza.

Kampeni hii pia inatarajiwa kuwawezesha wananchi kujua jinsi ya kulinda taarifa zao mtandaoni, kama vile nywila (neno la siri), na kujiepusha na viunganishi (links) visivyojulikana. Waziri Silaa alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwa makini na maswala haya ya usalama mtandaoni.

"Linda taarifa zako kwa kutumia nywila thabiti na tofauti kwa kila akaunti, yenye mchanganyiko wa maneno, namba, alama na herufi kubwa na ndogo. Usifuate maelekezo na kutoa nywila (neno siri) au namba yako ya uthibitisho (OTP) kwa mtu yeyote," aliongeza.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuhakiki namba zao za simu kwa kutumia namba *106# ili kudhibiti wizi wa taarifa na kuongeza usalama. 


Alivipongeza pia vyombo vya habari kwa kushirikiana na serikali katika kusambaza elimu hii kwa wananchi.

"Tunahimiza kuhakiki namba zako za simu kupitia 106#. Bofya 106# kisha chagua kuona namba zilizo sajiliwa na kitambulisho chako cha NIDA. Iwapo utakuta namba usizo fahamu tafadhali fika kwenye duka la mtoa huduma wako ili waifute," alisisitiza Waziri Silaa.



Waziri alikumbusha kuwa watoa huduma wa mawasiliano ya simu wanapaswa kuwasiliana na wateja wao kupitia namba 100 pekee na si vinginevyo, akitoa wito kwa wananchi kutojibu simu za kutoka namba nyingine ambazo hazijulikani.

Katika kufafanua kuhusu ushirikiano wa taasisi za kifedha, Waziri Silaa alitolea mfano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambayo inaendelea kushughulikia masuala ya usalama wa fedha mtandaoni, ikiwemo kuimarisha Dawati Maalumu la Malalamiko (Complaints Resolution Desk) na Kituo cha Kuitikia Majanga ya Kompyuta cha kisekta (TZ-FinCERT).


"Ninawapongeza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuendelea kushughulikia masuala yote yanayohusu fedha katika mitandao ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa Dawati Maalumu la Malalamiko (Complaints Resolution Desk) kwa ajili ya kutatua malalamiko ya wateja wa huduma za Kifedha," alisema.


Vilevile, Waziri Silaa alikishukuru Jeshi la Polisi Tanzania kwa juhudi za kukabiliana na wahalifu wa mtandaoni na kutoa rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuendelea kuchukua hatua madhubuti ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la uhalifu mtandaoni.


"Ninatoa rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kupitia Jeshi letu la Polisi kuendelea kuchukua hatua stahiki kwenye yale maeneo ambayo yanaripotiwa mara kwa mara kwa kuongoza katika viashiria vya Uhalifu mtandaoni," aliongeza.


Kwa upande wa malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano, Waziri Silaa alikumbusha wananchi kuwa wafuate utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao kwa watoa huduma kupitia namba 100, na kama hawatapata ufumbuzi, basi waendelee na malalamiko kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba ya bila malipo 0800008272.


"Hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano. Tunawahimiza wananchi wafuate utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao kwa watoa huduma kupitia namba 100," alisema.

Waziri Silaa alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau wote ili kufanikisha kampeni hii na kuhakikisha kuwa elimu inafika kwa kila mtumiaji wa huduma za mawasiliano, hivyo kupunguza vitendo vya utapeli mtandaoni.


"Ni matumaini yangu kwamba baada ya kuzindua kampeni hii kila mdau ataenda kutekeleza kwa wakati mpango huu mahususi ambao utafanikisha lengo la kupeleka elimu na uelewa katika jamii juu ya kujikinga dhidi ya utapeli mtandaoni," alisistiza Waziri Silaa.


Uzinduzi wa kampeni ya “SITAPELIKI” unalenga kuongeza usalama wa mitandao na kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia huduma za kidijiti kwa usalama zaidi, na hivyo kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa kidijiti wa taifa.


Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla, amesema kikao kazi hicho kimejikita katika kutathmini utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10, kuanzia 2024 hadi 2034.


Ameongeza kuwa mkakati huu utakuwa na nguzo sita muhimu, ambazo ni: kuwezesha miundombinu ya kidijitali, utawala na mazingira wezeshi, uelewa wa kidijitali na maendeleo ya ujuzi, utamaduni wa ubunifu wa kidijitali, teknolojia wezeshi na kukuza ushirikishwaji wa kidijitali na upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali.


 

Serikali yatoa mwanga kuhusu changamoto za hisa za Vodacom na mwelekeo mpya wa sekta ya mawasiliano



Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amesema ni wakati muafaka kwa serikali kufanya mapitio ya sheria na mikakati ya uwekezaji katika sekta ya mawasiliano, ili kuhakikisha kuwa inawafaidi wananchi na kuwa na mazingira bora ya biashara kwa watoa huduma za simu na intaneti. 


Kauli hiyo ameitoa leo Februari 20, 2025 jijini Arusha wakati akijibu maswali yaliyoulizwa kwenye majadiliano wakati wa uzinduzi wa kampeni ya "SITAPELIKI".


Waziri Silaa alieleza kuwa serikali ipo tayari kurejea kwenye meza ya mazungumzo na wadau wa sekta hiyo ili kutathmini hatua zilizochukuliwa awali na kurekebisha miongozo na sheria ili kuendana na mabadiliko ya soko na mazingira ya uwekezaji.


"Ni wakati muafaka wa sisi kukaa na kuangalia tulipofika na kutengeneza njia bora zaidi ya kampuni hizi kujiendesha hasa tukiweka mazingatio kwenye miongozo na vision aliyonayo Rais Samia Suluhu Hassan.


 Rais Samia amefanya kazi kubwa kukuza mazingira ya uwekezaji, sisi tunaomsaidia hatuna budi kuangalia namna ya kusaidia utekelezaji wa mikakati hii muhimu kwa manufaa ya Watanzania wote," alisema Waziri Silaa.


Waziri Silaa alikiri kuwa baadhi ya hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha nyuma, ikiwemo sheria iliyolazimisha Vodacom kujisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2017, hazikuzalisha matokeo yaliyotarajiwa. 


Alisema kuwa wazo la serikali kuhamasisha wananchi kununua hisa za Vodacom lilileta matumaini makubwa lakini utekelezaji wake haukuwa mzuri, na hivyo kuleta changamoto kwa watanzania waliowekeza.


"Mimi nadhani njia bora zaidi ya kukuza sekta yoyote kwenye uchumi huu wa soko ni kuacha sekta zitawaliwe na nguvu ya soko. 


Kama serikali, tukianza kutengeneza shuruti kwenye baadhi ya mambo, matokeo yake ndio haya unayosema. Sina tathmini sahihi, lakini ndio hiki ulichokisema," alisema.


Aidha, Waziri Silaa alisema kuwa ni muhimu serikali kufanya mapitio ya sheria zilizopitishwa na kurekebisha mikakati ya sekta hiyo kwa manufaa ya pande zote, akiongeza kuwa hakuna mfumo wa sheria unaoweza kuwa kamili kila wakati. 


Aliweka wazi kuwa kupitia vikao vya wadau, serikali itachukua hatua za kuboresha mazingira ya biashara na kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya mawasiliano unakua.


"Lakini ambacho naweza kusema ni kwamba ni wakati wa kufanya mapitio na kujua tulipo, na kutengeneza utaratibu bora zaidi kwa ajili ya sekta hii," aliongeza.


Katika majadiliano hayo, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Absalom Kibanda, aliuliza maswali kadhaa muhimu kuhusu hatima ya wawekezaji wa Vodacom baada ya serikali kuhamasisha wananchi kununua hisa za kampuni hiyo kupitia sheria zilizowekwa mwaka 2017. 


Kibanda alikosoa hatua ya serikali ya kuhamasisha wananchi kuwekeza kwenye kampuni za simu kabla ya kuandaa mazingira rafiki ya uwekezaji.


"Serikali imechukua hatua gani ili kuwasaidia wanahisa waliohamasishwa na serikali mwaka 2017 kununua hisa za Vodacom ambao hadi leo hawajui hatima ya uwekezaji wao katika hiyo kampuni?" alihoji Kibanda.


Alitilia mkazo pia changamoto zinazojitokeza kutokana na kushuka kwa thamani ya hisa za Vodacom, akisema kuwa wananchi wengi ambao walijitokeza kuwekeza wameshindwa kuelewa jinsi gani thamani ya hisa zao ilivyoshuka kutoka TZS 850 hadi TZS 740.


"Je, serikali haioni kwamba uamuzi ule wa kuilazimisha Vodacom kusajiliwa katika soko la hisa kabla ya kuandaliwa kwa mazingira rafiki ndiko ambako kumesababisha sintofahamu iliyopo?" alihoji Kibanda.

Alitahadharisha kuhusu hatari ya kuwa na hali hii ambayo inaweza kuleta hasara kwa wananchi, akizungumzia kuhusu uwekezaji wa umma ambao ulifanywa bila ya mazingira mazuri ya biashara, na kuuliza serikali itachukua hatua gani sasa ili kuwanusuru wananchi walioshawishiwa kuwekeza.

"Je, serikali itachukua hatua gani sasa ili kuwanusuru na hasara kubwa Watanzania walioshawishiwa na serikali kuwekeza katika kampuni ya Vodacom?"

Kibanda alihoji pia iwapo serikali imejifunza kutokana na makosa ya awali, hasa katika kulazimisha kampuni za simu kujiingiza sokoni kabla ya kuwa na mazingira ya soko bora.


"Je, serikali imejifunza nini kutokana na kosa hilo la kuzilazimisha kampuni za simu kuchukua hatua za kiuwekezaji kama ilivyoifanyia Vodacom mwaka 2017 kwa kujisajili DSE huku ikijua kwamba hakukuwa na mazingira mwafaka ya kufanya hivyo?" alihoji Kibanda.


Vodacom na Hisa Zake

Vodacom Tanzania ilikuwa ya kwanza kutekeleza sheria ya EPOCA ya 2010 na Sheria ya Fedha ya 2016 kwa kuuza hisa 25% kwa umma kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2017.


 Hisa hizo ziliuzwa kwa shilingi 850, na serikali ilijivunia hatua hiyo ya kuwapa Watanzania fursa ya kuwekeza katika kampuni kubwa ya mawasiliano. 


Hata hivyo, thamani ya hisa hizo imeshuka kwa kiasi kikubwa, ambapo kwa mujibu wa hesabu za Vodacom PLC zinazoishia mwezi Machi 2024 hisa moja inauzwa kwa shilingi 740, jambo ambalo limetokea kama changamoto kubwa kwa wawekezaji wa Vodacom, hasa wale walionunua hisa hizo kwa bei ya juu.


Hali ya soko inavyoendelea kuonyesha kushuka kwa thamani ya hisa kwa shilingi 110  kumebainisha udhaifu wa utekelezaji wa mpango huu.


Waziri Silaa alisisitiza kuwa serikali itachukua hatua zinazofaa kuhakikisha maslahi ya Watanzania yaliyowekeza katika kampuni hiyo yanahifadhiwa kwa kuangalia namna ya kuboresha utaratibu wa uwekezaji na usajili wa kampuni za simu nchini.


"Sheria hatuzitungi sisi kutu control. Sheria tunazitunga ku regulate na kupeleka mambo yetu mbele," alisema Waziri Silaa, akisisitiza umuhimu wa kuboresha sheria na miongozo ili sekta ya mawasiliano iweze kutoa matokeo bora kwa Watanzania wote.


Kwa ujumla, Waziri Silaa alikiri kuwa ingawa hatua zilizochukuliwa awali zilikuwa na nia nzuri, ni muhimu sasa kurekebisha mikakati ili kuhakikisha kuwa sekta ya mawasiliano inakuwa imara na inatoa fursa kwa kila mtu.

 


Katika juhudi za kuimarisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) serikalini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amezitaka taasisi za umma kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa haraka na gharama nafuu.





Waziri alitoa wito huo Februari 13,2024 akifunga Kikao Kazi cha 5 cha Serikali Mtandao kilichofanyika katika jijini Arusha. 


Kikao hicho kiliwakutanisha washiriki takribani 1,500, wakiwemo maafisa masuuli, wakurugenzi, wakuu wa vitengo vya TEHAMA, na wataalamu wa sekta hiyo. Lengo kuu lilikuwa kujadili changamoto na mikakati ya kuboresha matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma.

Mikakati ya Kuimarisha Serikali Mtandao


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Mulula Mahendeka, alisisitiza kuwa mijadala na mapendekezo yaliyotolewa yatasaidia kuimarisha jitihada za serikali mtandao. 


Alibainisha kuwa ofisi yake itahakikisha maazimio yaliyofikiwa yanatekelezwa kwa wakati ili taasisi zote zifanye maboresho yanayohitajika.



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Benedict Ndomba, aliwashukuru washiriki kwa ushirikiano wao na kueleza kuwa maoni yao ni chachu ya maendeleo ya serikali mtandao. 


Aliahidi kuwa mamlaka hiyo itayafanyia kazi mapendekezo yote kwa lengo la kuongeza ufanisi wa mifumo ya TEHAMA nchini.


Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa e-GA, Dkt. Jasmine Tiisekwa, aliwatambua wadhamini wa kikao kazi hicho kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha mkutano huo. 


Pia alitoa shukrani kwa waandishi wa habari kwa kueneza taarifa kuhusu kazi mbalimbali za mamlaka hiyo.


Maelekezo kwa Taasisi za Umma

Katika hotuba yake ya kufunga kikao kazi hicho, Simbachawene aliwataka viongozi wa taasisi za umma kuongeza juhudi katika matumizi ya TEHAMA ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa njia ya kidijitali kwa urahisi zaidi.


Aliagiza taasisi zote za umma kuandaa taratibu za utendaji kazi kwa maandishi ili kuwezesha mifumo ya TEHAMA kubadilishana taarifa kwa ufanisi. 


Pia alieleza kuwa serikali kupitia e-GA imejipanga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za mtandao na kuboresha mawasiliano ya simu nchini kote.


"Idadi ya watumiaji wa simu za mkononi na intaneti inaongezeka mwaka hadi mwaka. Ongezeko hili linatupa chachu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za serikali kupitia simu za mkononi," alisema Simbachawene.


Katika kikao kazi hicho, washiriki walijadili mada mbalimbali kuhusu hali ya utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao, changamoto zilizopo, na mikakati ya kuzitatua.


Simbachawene alihitimisha kwa kusema kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha huduma za umma zinapatikana kwa njia ya kidijitali kwa urahisi na kwa gharama nafuu. 


Alitoa wito kwa taasisi zote za umma kushirikiana na e-GA ili kufanikisha azma hiyo kwa ufanisi zaidi.


"Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanaboreshwa kwa manufaa ya wananchi. 


Ni lazima tuchukue hatua thabiti ili kujenga serikali ya kidijitali yenye ufanisi," alisisitiza Simbachawene.



Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, ameagiza mikoa ambayo bado haijaanza kutumia utaratibu wa Ofisi ya Kielektroniki (e-Office) kuhakikisha inaanza kutumia mfumo huo ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu. 

Aidha, ameagiza kituo cha utafiti kuimarishwa na kuongezewa eneo la ufanyaji kazi ili kuongeza ufanisi katika shughuli za Serikali Mtandao.






Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Tano cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kinachofanyika jijini Arusha, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA na kada nyingine kwa kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.



Amesisitiza kuwa taasisi zote za umma zinapaswa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao katika hatua zote za ujenzi au ununuzi, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya TEHAMA.


"Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji katika vyuo vikuu na taasisi za serikali ili kuleta ukomavu katika utoaji wa huduma," amesema.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akipokea tuzo iliyotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba



Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema kikao hicho kinawakutanisha wadau mbalimbali wa Serikali Mtandao kutoka taasisi na mashirika ya umma pamoja na sekta binafsi ili kujadili hatua iliyofikiwa na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa jitihada hizo.


"Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kidigitali ambapo ilishika nafasi ya pili barani Afrika kwenye Ripoti ya Utafiti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2022 kuhusu Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Duniani katika utoaji wa huduma za serikali," amesema Simbachawene.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu,  Mululi Mahendeka, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).


Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba, amesema mamlaka hiyo imeiwezesha serikali kuwa na udhibiti wa moja kwa moja wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA inayotumika serikalini pamoja na kulinda usalama wa taarifa za serikali.




Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu itaadhimishwa kwa wiki nzima, badala ya siku moja kama ilivyozoeleka.



"Sherehe ya Siku ya Wanawake Kitaifa Arusha tunafanya kitu cha tofauti. Hatutafanya tu tarehe 8 Machi, bali tumeamua kuanza tarehe 1 Machi kwa wiki nzima ya shughuli mbalimbali za kuwawezesha wanawake," amesema Makonda.


Ameeleza kuwa shughuli hizo zitahusisha utoaji wa huduma za afya, msaada wa kisheria, elimu ya fedha na michezo kama mpira wa miguu kwa wachezaji wa kike kutoka timu za Simba Queens, Yanga Queens, JKT Queens na Fountain Gate FC.



Kikao Kazi cha Tano cha Serikali Mtandao kimehudhuriwa na zaidi ya washiriki 1,300 kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi. 


Kauli mbiu ya kikao hicho ni "Jitihada na Ubunifu wa Serikali Mtandao kwa Utoaji wa Huduma za Umma kwa Ufanisi."



Ross Ulbricht ni jina linalojulikana sana katika historia ya Bitcoin na teknolojia ya blockchain, lakini pia ni jina linalohusishwa na utata mkubwa kutokana na matukio ya kisheria yaliyomwandama.

 Aliyezaliwa mwaka 1984, Ross alianzisha tovuti maarufu ya Silk Road mnamo mwaka wa 2011. 


Tovuti hii ilikuwa soko la mtandaoni lililofanya biashara ya bidhaa haramu, hasa madawa ya kulevya. 


Silk Road ilijulikana kwa kuwa moja ya tovuti za kwanza kutumika kwa njia ya Bitcoin kama mfumo wa malipo, na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kueneza matumizi ya sarafu hii ya kidijitali.


Silk Road ilileta changamoto kubwa kuhusu uhuru wa mtandao, faragha, na matumizi ya Bitcoin. Ulbricht alikusudia kuanzisha jukwaa la biashara huria, akiamini kwamba watu wanapaswa kuwa na haki ya kufanya biashara bila kudhibitiwa na serikali. Hata hivyo, matumizi ya tovuti hii yalipelekea biashara ya bidhaa haramu, hali ambayo ilizua maswali kuhusu usalama wa mtandao na ufanisi wa sheria za kimataifa.


Mnamo mwaka 2013, Ross Ulbricht alikamatwa na kukutana na mashtaka makubwa, akiwemo kuendesha biashara haramu, ukiukwaji wa sheria za madawa ya kulevya, na kushiriki katika uhalifu wa mtandaoni. 


Alikataa tuhuma hizi, akieleza kwamba alianzisha Silk Road kama jukwaa la biashara huria, lakini alikubaliana kwamba matumizi mabaya ya tovuti hiyo yalipelekea madhara makubwa kwa jamii. 


Hata hivyo, alihukumiwa kifungo cha maisha jela bila uwezekano wa kupunguziwa adhabu, jambo lililosababisha mjadala mkubwa kuhusu haki za binadamu na usawa katika utoaji wa adhabu.


Wakati wa utawala wa Rais Donald Trump, kulikuwa na maombi ya mara kwa mara kutoka kwa wafuasi wa Ulbricht wakiomba msamaha kutoka kwa Rais. 


Walidai kuwa adhabu aliyopewa ilikuwa kali kupita kiasi, na kwamba aliweza kufundisha umma kuhusu umuhimu wa faragha mtandaoni. Mnamo mwaka wa 2025, Rais Trump alitumia mamlaka yake kumsamehe Ulbricht, na hatua hii ilileta mjadala mkubwa kuhusu haki za kibinadamu, matumizi ya mtandao, na sera zinazohusiana na Bitcoin na fedha za kidijitali.


Hadithi ya Ross Ulbricht ni mfano mzuri wa mafanikio ya mtandao na Bitcoin, lakini pia inawakilisha changamoto na utata wa kisheria unaoweza kutokea wakati wa kuanzisha miradi ya kidijitali. Ingawa alikumbwa na matatizo makubwa, hadithi yake inaendelea kutoa funzo kuhusu mabadiliko ya kidijitali, umhimu wa faragha, na athari za sheria katika dunia ya mtandao.