Showing posts with label UTALII. Show all posts
Showing posts with label UTALII. Show all posts

 



Makamishna wasaidizi waandamizi wa Uhifadhi  wanawake kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wapo nchini Indonesia kushiriki mkutano wa mtandao wa wanawake maafisa waandamizi wa Polisi na vyombo vya vingine vya usalama unaofanyika nchini humo.


Wakiongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi -Rasilimali watu na Utawsla Salma Chisonga makamishna hao wanatarajia kutoa  uzoefu wao katika masuala ya ulinzi, uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.


Mkutano huo wa siku tano unawaweka pamoja  wanawake kutoka vyombo vya usalama wa nchi mbalimbali duniani kujadili fursa na changamoto katika vyombo vya usalama na vinavyolinda rasilimali za nchi.

 



Na Mwandishi wetu, Ngorongoro 


Ilinenwa “KATIKA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA”, ndivyo walivyofanya waumini  wa Parokia ya Mt. Petro Masanza  Kona mkoani Simiyu ambapo baada ya kulijenga kanisa kwa umoja wao waliamua kutembelea  hifadhi ya Ngorongoro kujionea uwezo wa mwenyezi Mungu katika uumbaji wa ulimwengu na vilivyomo.



Ziara hiyo imewashirikisha waumini 50 kutoka parokiani hapo wakiongozwa na  mapadri wanne na frateli mmoja ikiwa na lengo la kuwawezesha waumini kufanya utalii wa ndani na kujifunza juu ya urithi wa dunia ambao  upo ndani kasoko ya Ngorongoro.



Akiongoza ziara hiyo,Rev Fr. Furaha James ambaye ni Paroko wa Parokia ya Masanza  alisema kwamba ziara hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa kwa kuwa wamepata fursa ya kujifunza historia, utamaduni, mazingira na vivutio vya asili vilivyopo nchini.


“Tumekuja hapa kwa ajili ya kujifunza na kuona kile ambacho Mungu ametujalia katika nchi yetu. Naamini kuwa waumini wetu waliotembelea hapa wameongeza uelewa na watakuwa mabalozi wa kutunza na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwetu” alisema Fr. Furaha 



Aidha kwa upande wa WAWATA, akiwemo  Flora Nkolongo walieleza kufurahishwa na ziara hiyo, wakisema kuwa imewapa nafasi ya kujifunza na kuwaona wanyama mbalimbali kama Simba, Faru, Nyati, Tembo na wengine wengi ambao ni mara yao ya kwanza kuwaona kwa karibu.



Ziara hiyo ilihitimishwa  kwa kutembelea  makumbushi ya Urithi ambako walipata historia ya ardhi ya Ngorongoro, volkano, wanyamapori, maendeleo ya binadamu na tamaduni za jamii zinazozunguka eneo hilo ambao ni Wamasai, Wahadzabe, Wairaqw na Wadatoga na waumini hao kuhitimisha ziara yao kwa kuamini kuwa NGORONGORO NI NYUMBANI KWA KILA KIUMBE.









  


Happy Lazaro,Arusha .



MBALI na ubunifu wa teknolojia za kilimo na mifugo unaoendelea kuonyeshwa katika Maonesho ya Nanenane, wageni wanaotembelea viwanja hivyo wamepata pia nafasi ya kufanya safari ya kipekee ya ladha kupitia vyakula vinavyobeba utamaduni wa mataifa mbalimbali katika banda la Cheesy Bite lililopo Nanenane Njiro .


Katika kona moja ya maonesho hayo, harufu ya vyakula vinavyoandaliwa kwa ustadi huwavutia wageni kusimama, kuonja na kujionea namna sekta ya utalii wa chakula (food tourism) inavyozidi kukua nchini. Wengi huchukua muda kupumzika na kufurahia milo yenye mchanganyiko wa mapishi ya kisasa yanayokidhi ladha tofauti za wateja.



Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo ,Mmoja wa wafanyakazi katika katika hoteli hiyo, Maryam Mlau , amesema wameamua kuandaa menu inayowapa wageni uzoefu wa kuonja vyakula vya asili tofauti bila kulazimika kusafiri nje ya Tanzania.


 Maryam ameeleza kuwa wageni hupata fursa ya kufurahia vyakula kama Chicken Loaded Fries, Beef Loaded Fries, Halloumi Loaded Fries pamoja na burger za nyama ya ng'ombe na kuku ambazo zimekuwa zikivutia wengi.



Ameongeza kuwa, si Watanzania pekee wanaovutiwa na vyakula hivyo, bali pia wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaotembelea maonesho hayo, jambo linaloonyesha kuwa chakula kimeendelea kuwa sehemu muhimu ya utalii na uzoefu wa msafiri anapotembelea eneo jipya.



Amesema kuwa,mazingira mazuri, huduma zenye ukarimu na kuzingatia viwango vya usafi vimechangia kuwafanya wageni wengi kurejea tena, huku baadhi yao wakichagua kutumia huduma ya kusafirishiwa chakula pale wanaposhindwa kufika moja kwa moja.



"Wadau wa utalii wanaeleza kuwa utalii wa chakula unaendelea kushika kasi duniani, ambapo wageni hutafuta sio tu vivutio vya asili na utamaduni, bali pia ladha zinazotofautisha eneo moja na jingine"amesema Maryam.

 


"Hali hiyo imeifanya sekta ya huduma za chakula kuwa sehemu muhimu ya kuongeza thamani ya maonesho makubwa kama Nanenane."amesema Maryam .



"Kadri maonesho hayo yanavyoendelea, wageni wanaondoka wakiwa si tu na maarifa mapya kuhusu kilimo na mifugo, bali pia na kumbukumbu za ladha mbalimbali walizozionja, jambo linaloifanya Nanenane kuwa zaidi ya maonesho ya uzalishaji—bali pia jukwaa la kukutanisha tamaduni kupitia chakula."amesema 





Maafisa na askari  wa jeshi la Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro waliopoteza maisha, kujeruhiwa na kufanya kazi kwa uhodari wametunukiwa vyeti na fedha kutokana na kujitoa kwao kwa hali na mali kulinda rasilimali za wanyamapori na misitu.



Tuzo hizo zimetolewa tarehe 31 Julai 2026 kwenye maadhimisho ya  siku ya  askari wanyamapori duniani ambayo huadhimishwa kwa lengo la kuutambua mchango wa  askari hao katika kulinda rasilimali za nchi na kuenzi mchango wa Askari 10 waliopoteza maisha yao na kujeruhiwa wakiwa kazini katika hifadhi ya Ngorongoro.



Naibu kamishna wa Uhifadhi huduma za shirika Aidan Makala  amewapongeza askari wote wa jeshi la uhifadhi kutokana na  kujitoa kwa hali na mali katika kazi hiyo huku akiwasisitiza kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi ili kulinda matakwa ya haki jinai.



Naibu Kamishna Makala ameleza kuwa,  askari  wa  uhifadhi ni nguzo ya ulinzi wa rasilimali za wanyamapori  na misitu ambapo  kazi hiyo haiishii kukabiliana na ujangili pekee  bali inakwenda sambamba na kudhibiti uharibifu wa mazingira hususan vyanzo vya maji, ulinzi wa maisha na mali za watu dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuelimisha jamii kutunza rasilimali hizo.

 


Akielezea kuhusu maadhimisho ya siku ya  askari wanyamapori duniani, Afisa Uhifadhi mkuu anayesimamia idara ya huduma za Ulinzi Bw. Emmaanuel Kaaya amesema kuwa Siku hiyo ilianza kuadhimishwa mwaka 2007, kwa ushirikiano baina ya Shirikisho la Kimataifa la Askari wa Wanyamapori (International Rangers Federation - IRF) na mashirika mengine ya kimataifa. 


Lengo la kuanzishwa kwa maadhimisho haya ni kuutambua mchango wa Askari wa Wanyamapori na kuuenzi mchango wa Askari waliopoteza maisha wakiwa kazini. Ni siku ya kuwatambua na kuenzi mchango wa mashujaa wanaojitolea kila siku kuhakikisha hifadhi zetu zinaendelea kuwa salama kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.


Kwa upande wake kamishna msaidizi mwandamizi wa Uhifadhi Gloria Bideberi amebainisha kuwa katika maadhimisho haya, Mamlaka imetoa vyeti na fedha taslimu  kwa zaidi ya watumishi 30 ikiwa ni sehemu ya kuutambua mchango wao katika kazi kwa kipindi cha mwaka 2025/26.


Maadhimisho hayo yalipambwa na michezo mbalimbali iliyojumuisha  mpira wa miguu, kukimbiza kuku, mazoezi ya viungo na maonesho ya kwata mbalimbali.



SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeingia kwenye hatua kubwa ya kuimarisha ulinzi na doria angani baada ya Kamishna wa Uhifadhi, Massana G. Mwishawa, kukagua ndege ndogo mbili (2) mpya aina ya Savannah zilizonunuliwa hivi karibuni.



Ndege hizo zimenunuliwa kupitia mradi unaofadhiliwa na BMZ, uliotekelezwa chini ya Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani. Lengo kuu la ununuzi huo ni kuongeza nguvu katika doria na uhifadhi wa wanyamapori kwenye Hifadhi za Taifa za Serengeti na Nyerere.


Ukaguzi huo umefanyika leo katika Karakana iliyopo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar, ambapo ndege hizo zinaendelea kuunganishwa tayari kwa kazi.


Akiwa uwanjani hapo, Kamishna Mwishawa amewapongeza mafundi wanaoendelea na kazi ya uunganishwaji wa ndege hizo kwa umakini mkubwa.


Pia, ametoa pongezi za kipekee kwa marubani wawili (2) ambao ni Askari Uhifadhi wa TANAPA. Marubani hao kwa sasa wapo kwenye hatua za mwisho za mafunzo yao maalum ya kurusha ndege hizo ili kuhakikisha usalama na ufanisi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.


Ndege hizo za kisasa aina ya Savannah zinatarajiwa kuanza doria rasmi angani mwanzoni mwa mwezi Oktoba, 2026, hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujangili na kulinda rasilimali za taifa.

 



Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro Abdul-Razaq Badru ameuambia mkutano wa 48 wa kamati ya Urithi wa Dunia kuwa Ngorongoro ni sehemu pekee ambayo binadamu duniani kote wanaweza kupata ushahidi sahihi wa chimbuko la asili ya binadamu.



Akizungumza mjini Busan,Jamhuri ya Korea wakati akiongoza Mkutano wa pembeni (Side event) ulioandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja kuhusu hali ya uhifadhi wa eneo la  Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni eneo la Urithi wa Dunia, Badru amesema Ngorongoro ina ushahidi uliohifadhiwa wa nyayo za binadamu na masalia ya kale katika eneo la Laetoli na Olduvai zinazothibitisha suala hilo.


“Ngorongoro si tu eneo la utalii bali pia ni mahali ambapo historia ya binadamu wote kisayansi ilianzia”, alisema kamishna Badru.


Katika kikao hicho ameeleza kuwa kila nyayo iliyohifadhiwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro inawakumbusha kurudi nyumbani kuona historia hiyo.


Badru amefafanua  kuwa Ngorongoro ni sehemu ambayo binadamu alianzia kutumia zana mbalimbali za mawe kama teknolojia ya awali ya shughuli za kibinadamu na ndipo alipoanza kufanya harakati za kimaisha.


Mkutano wa kamati ya Urithi wa Dunia una lengo la kufanya maamuzi kuhusu maeneo mapya yanayopendekezwa kuingizwa kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia na kuimarisha juhudi za pamoja za kulinda, kuhifadhi, na kusimamia kwa uendelevu maeneo yenye thamani kubwa ya kiutamaduni na asili duniani.

 


Mwambata wa ubalozi wa Oman nchini Tanzania, Abdulrahman Salim Algaad akiwa na familia yake, ametembelea Hifadhi ya Ngorongoro na kushuhudia maajabu ya utalii yaliyopo katika kivutio namba moja cha utalii barani afrika

 


Akimpokea mwambata huyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Huduma za Utalii na Masoko Mariam Kobelo ameeleza kuwa jitihada za mamlaka hiyo kuwafikia wadau mbalimbali zimeendelea kuzaa matunda ambapo watumishi kutoka balozi mbalimbali ndani na nje ya nchi wamendelea kutembelea hifadhi hiyo.

 


Akiwa ndani ya hifadhi hiyo, Abdulrahman Algaad na familia yake walipata fursa ya kushuhudia wanyamapori adimu wakiwa katika mazingira yao ya asili, wanyamapori wakubwa watano, misitu, maporomoko ya maji, urithi wa utamaduni na mambo kale, makumbusho ya urithi geopark na kueleza kuwa ndoto na hisia alizokuwa nazo zimekutana na uhalisia.

 

Mwambata huyo ameonyesha kuvutiwa na uzuri wa Hifadhi ya Ngorongoro na vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na kupongeza hatua za uhifadhi zinazofanyika na kuifanya Ngorongoro kuendelea kuheshimika kimataifa na kuwa eneo la urithi wa dunia lenye hadhi tatu za kimataifa.

 


Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia huduma za utalii na masoko, Mariam Kobelo amebainisha kuwa ziara za viongozi na maafisa wa kidiplomasia wanaotembelea Ngorongoro zinachangia kuitangaza Tanzania kimataifa, kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii, kuongeza ushirikiano kupitia diplomasia ya uchumi.

 


Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro ikiongozwa na makamu Mwenyekiti Dkt. Harriet Mtae jana tarehe 11 julai, 2026 imekagua uboreshaji wa miundombinu ya utalii eneo la Nyayo za Laetoli lililopo hifadhi ya Ngorongoro 



Wakiwa Laetoli Wakurugenzi hao wamekagua uhifadhi wa Nyayo zilizogundulika katika eneo hilo miaka zaidi ya milioni 3.6 iliyopita na kuangalia hatua za utekelezaji wa mradi wa Geopark unaohusisha ujenzi wa jengo la kupokelea wageni, jengo la kupumzika wageni, jengo lililojengwa kwa ajili ya kuhifadhi Nyayo sambamba na miundombinu mingine.


Naibu Kamishna wa Uhifadhi Joas Makwati anayesimamia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii ameeleza kuwa ziara hiyo imelenga kutathmini utekelezaji wa miradi inayofanywa na mamlaka kwa lengo la kuimarisha shughuli za uhifadhi, kuboresha huduma za utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro.



Pamoja na kukagua miundombinu ya utalii wakurugenzi hao wamepokea taarifa ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na mipango ya kuendelea kuboresha mazingira ya utalii na shughuli za uhifadhi.


Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Dkt. Harieth Mtae, alisema miradi hiyo inaakisi dhamira ya mamlaka ya kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa vivutio vya utalii na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wageni.





Ameongeza kuwa maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza thamani ya vivutio vya utalii, kuvutia watalii zaidi na kuendelea kuitangaza Hifadhi ya Ngorongoro kama moja ya vivutio vinavyoongoza duniani.



 



Waziri wa maliasili na utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) leo tarehe 10 julai, 2026 amekutana na bodi ya wakurugenzi mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo Karatu mkoani Arusha na kusisitiza umuhimu wa bodi hiyo kufuatilia kwa karibu shughuli zote za utendaji ili kuanza mwaka mpya wa fedha 2026/2027 kwa kasi na ufanisi.


Mhe. Kijaji amesema  kuwa bajeti ya mwaka mpya wa fedha inaanza na utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 hivyo vikao vyake na bodi za taasisi zilizopo chini ya wizara vina lengo la kuanza utekelezaji wa dira, bajeti na ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa pamoja.


Ameitaka bodi hiyo kuongeza nguvu katika kuimarisha uhifadhi, kutangaza utalii  na kusimamia maendeleo ya jamii na kusisitiza kuwa jitihada hizo ziendane na kasi ya kukamilisha miundombinu wezeshi ikiwemo barabara kuu ya Loduare hadi Golini, kuimarisha mawasiliano ndani ya eneo lote la hifadhi, kukamilisha mradi wa fensi ya umeme ili kupunguza migongano kati ya wanyamapori na wananchi, kudhibiti ujangili na kuendelea kuimarisha mahusiano ya hifadhi na wananchi wanaoizunguka.


“Tulinde uhifadhi wa Ikolojia ya Ngorongoro kwa wivu mkubwa, tuendelee kubuni mazao mapya ya utalii na kuyatangaza, tujipange kikamilifu kuhakikisha Ngorongoro kama premium destination inawafikia na kuwashawishi wageni watakaohudhuria matukio ya AFCON, mkutano wa umoja wa Mabunge duniani, tuzo za  dunia za utalii na shindano la Miss world ambapo matukio yote yatafanyika Tanzania kati ya mwezi oktoba 2026 na Julai mwaka 2027”  amesisitiza Dkt. Kijaji.



Katibu wa Bodi, ambae ni kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Abdul-Razaq Badru amemueleza Mhe. waziri kuwa, Ngorongoro imepiga hatua ya kimageuzi kwenye mifumo ya kidijitali (ICT Transformation), uhifadhi endelevu kwa kuimarisha doria za kisasa, kuboresha miundombinu hasa barabara ya tabaka gumu kutoka geti la loduare hadi Seneto (km 29.5) kwa gharama ya TZS 80.3 bilioni  


Badru ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 eneo la Ngorongoro idadi ya watalii ilifikia 1,061,620 na fedha shilingi 269.5 Bilioni zilikusanywa. Ngorongoro imeendelea na jitihada za kulinda hadhi tatu za kimataifa kutoka UNESCO ambazo ni Urithi wa Dunia (World Heritage Site), Hifadhi ya Biosphere (Man and Biosphere Reserve), na Geopark ya Dunia (Ngorongoro-Lengai Global Geopark) ili ziendelee kuinufaisha nchi yetu.


Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Ngorongoro Dkt. Harriet Mtae amemueleza Mhe waziri kuwa, katika kipindi cha miezi sita (06) iliyopita bodi ya Ngorongoro imetekeleza majukumu  kwa kuzingatia sheria, kanuni pamoja na maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha Mamlaka inatekeleza kikamilifu dhamana yake ya kuhifadhi maliasili za Wanyamapori, malikale na urithi wa dunia, kuendeleza utalii endelevu na kuboresha shughuli za maendeleo ya jamii.

 


Tukio la Ngorongoro kuonesha vivutio vya utalii mubashara kupitia runings kubwa iliyofungwa katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii

limevutia wananchi wengi wanaotembelea  maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa jijini  Dar es Salaam kwa kuoneshwa maajabu yaliyopo Ngorongoro hususan Kreta ya Ngorongoro, makundi ya wanyama mbalimbali ikijumuisha pundamilia, nyumbu, swala, nyati na wanyama adimu kama  faru, simba, tembo na  na  chui na kujihisi kama wapo nyumbani Ngorongoro.



Afisa Uhusiano Mkuu wa Ngorongoro  Walter Mairo ameeleza kuwa  kupitia runinga iliyofungwa viwanja vya maonesho wageni wanaotembelea wanaona wanyama aina mbalimbali ndani ya Kreta, tambarare za Ndutu ambapo maisha ya Nyumbu kuzaliwa, kukua, kusafiri na kurejea na kuanza kizazi kipya kila mwaka


Mairo ameongeza kuwa, matukio mubashara yanaonesha wananchi jinsi teknolojia ya kidigitali na utalii wa asili vinavyoweza kushirikiana kuelimisha, kuburudisha na kuonyesha ushahidi kuwa Ngorongoro si tu hifadhi, bali ni jukwaa la kidunia linalounganisha urithi, biashara na teknolojia sehemu moja.


Karibu Sabasaba timu yetu yenye wabobezi na watopezi imejipanga kukupa  hadhithi za Ngorongoro zitakazokuduwaza kuwa Ngorongoro sio mahali pa kuangalia tu, bali mahali pa kuelewa, kujifunza na kuishi uzoefu usiosahaulika.



ARUSHA, TANZANIA – Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ametoa maagizo sita makuu kwa Kamishna mpya wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Gibril Mwishawa, akimtaka kuimarisha utendaji na kuhakikisha sekta ya utalii inaongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.


Waziri Kijaji alitoa maagizo hayo leo Julai 9, 2026, jijini Arusha wakati akiongoza hafla ya uapisho wa Kamishna Mwishawa. Kabla ya uteuzi wake uliofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo Julai 2, 2026, Mwishawa alikuwa akihudumu kama Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa shirika hilo. Anachukua nafasi ya Kamishna Mstaafu, CPA Musa Nassoro Kuji, ambaye amemaliza muda wake wa utumishi.

Maagizo Sita ya Waziri Kijaji



Katika hotuba yake, Waziri Kijaji alimtaka kiongozi huyo mpya kuelekeza nguvu na weledi katika maeneo yafuatayo:
  1. Kusimamia na kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi zote nchini.
  2. Kuvutia na kuongeza fursa za uwekezaji wa kimkakati.
  3. Kubuni na kuanzisha bidhaa mpya za utalii ili kuongeza mnyororo wa thamani.
  4. Kusimamia mapato kwa ufanisi mkubwa ili kuzuia upotevu.
  5. Kuimarisha uhusiano mwema na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
  6. Kusimamia nidhamu, uadilifu, weledi na ustawi wa watumishi, ikiwemo kulipa maslahi yao kwa wakati.
"Ushirikiano na wananchi wanaozunguka hifadhi ni nguzo muhimu sana katika kulinda rasilimali hizi za taifa," alisisitiza Waziri Kijaji.

Kauli ya Bodi ya Wadhamini



Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali George Waitara, aliahidi kuwa bodi yake itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo thabiti kwa menejimenti ili kufikia malengo yaliyowekwa. Jenerali Waitara aligusia pia umuhimu wa uwazi, akitaka utoaji wa mrejesho wa utendaji kazi uhusishe maafisa na askari wa ngazi zote ili kuongeza ufanisi.

Shukrani na Ahadi ya Kamishna Mpya



Akizungumza baada ya kula kiapo, Kamishna wa Uhifadhi, Massana Gibril Mwishawa, alieleza kuwa hifadhi za taifa ni hazina kubwa ya kiikolojia, kiuchumi na kijamii ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye mapato ya serikali na miradi ya kimkakati kama ufuaji wa umeme.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana hiyo kubwa, huku akiahidi kuiongoza TANAPA kwa misingi ya uzalendo, uwajibikaji na uadilifu.


"Nitaingiza nguvu mpya kwa kushirikiana kwa karibu na watumishi wote wa TANAPA ili kuendeleza na kuimarisha mafanikio ya taasisi yetu," alisema Kamishna Mwishawa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa dini, wadau wa utalii, pamoja na wakuu wa taasisi nyingine za uhifadhi nchini.



 



Katika Viwanja vya Sabasaba, timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi Abdul-Razaq Badru tarehe 6 June, 2026 ilivifunika viwanja hivyo huku macho na masikio ya wananchi waliotembelea yakijielekeza kwenye Kampeni ya Ngorongoro inayojulikana kama Karibu Nyumbani.



Akizungumza na Waandishi wa Habari katika siku maalum ya Ngorongoro, Kamishna Badru amewaeleza kuwa umuhimu wa kampeni hiyo inatokana na historia kwa kuainisha wazi kuwa binadamu wa kale kutembea kwa miguu miwili historia yake alipatikana ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.


Ameeleza kuwa ushahidi uliopo wa zaidi ya miaka milioni 3.6 unaonesha binadamu huyo aliweza kutembea na kufanya shughuli zake kwa kutumia zana za miaka hiyo, kuyatawala mazingira na kuishi bila shida yoyote.


Mhifadhi Mambokale wa Ngorongoro Ladislaus Kashaija akitoa maelezo kuhusu kwanini Ngorongoro inajivunia historia hiyo ameeleza kuwa inatokana na ushahidi wa wanazuoni duniani kote kuitaja Ngorongoro kama sehemu yenye ushahidi wa kutosha kuhusu historia ya binadamu.


Mchezaji wa timu ya soka ya Simba Shomari Kapombe amesema kuwa atakuwa chachu ya luwashawishi wanasoka wenzie kuitangaza Ngorongoro kuwa chanzo cha mpira wa miguu kwa kuwa historia ya binadamu kutembea kwa miguu miwili imeanzia hapo.


Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro imeshiriki tukio la siku ya Ngorongoro (Ngorongoro Day) katika viwanja vya sabasaba kwa kuhamasisha washiriki warudi Nyumbani Ngorongoro kwani mwenda kwao si mtumwa.

 


Usemi usemao hakuna marefu yasiyokuwa na ncha umetimia leo ambapo jumla ya maafisa na Askari 29 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) wamehitimu mafunzo ya mabadiliko ya kimuundo leo tarehe 20 Juni, 2026 katika Kituo cha Mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi kilichopo Mlele mkoani Katavi.



Akifunga mafunzo hayo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TAWA Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko amewataka wahitimu kuzingatia taratibu na sheria na amri zote za Jeshi la Uhifadhi



“Mmepata mafunzo ya kubadilika kimuundo kutoka raia kuwa Jeshi, matumaini yangu ni kuwa kila mmoja wetu hapa mtabadilika na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa katika kusimamia uhifadhi na rasilimali za nchi”,alisema Meja Jenerali (Mst) Semfuko.



Mkuu wa wilaya ya Mlele  Majid Mwanga amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kuwa mfano mwema wa uzalendo, maadili na ujasiri katika utendaji kazi.



Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Abdul-Razaq Badru amewahimiza wahitimu hao kutumia mafunzo waliyoyapata kuimarisha uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.



Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mlage Kabange amesema ushirikiano uliooneshwa kati ya TAWA na Ngorongoro katika kusimamia mafunzo hayo unaonesha kuimarika kwa Jeshi la Uhifadhi nchini na ari ya kusimamia rasilimali za Wanyamapori na Misitu.


Akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo mkuu wa mafunzo Meja Breyman Rulenguka amesema Jumla wa watumishi 29 wamefaulu na kupata alama za kuridhisha ambapo mwanafunzi mmoja pekee hakuweza kuhitimu kutokana na sababu za kiafya.


Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa katika kituo hicho kwa lengo la kuimarisha Jeshi la Uhifadhi na utendaji kazi wake.