Showing posts with label MAHAKAMANI. Show all posts
Showing posts with label MAHAKAMANI. Show all posts

 


Mahakama ya Wilaya ya Arusha  imetoa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa mtuhumiwa mmoja na kuwaachia wawili kwa masharti kufuatia makubaliano ya kukiri makosa ya kutengeneza na kukutwa na pombe bandia pamoja na stamp feki za TRA. 



Adhabu hizo zimetolewa kufuatia makubaliano ya maridhiano ya kukiri makosa (Plea Bargain) kati ya washtakiwa hao na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ambapo hatua hii imekuja baada ya washtakiwa wote kwa pamoja kukamilisha malipo ya faini ya Shilingi Milioni Tano (Tsh 5,000,000) kwa mkupuo mmoja kwenda kwenye akaunti ya DPP.




Katika uamuzi huo, Mahakama pia imeamuru kuteketezwa kwa vielelezo zikiwemo stamp feki za kielektroniki za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na pombe feki zilizokamatwa, huku ikitoa amri ya washtakiwa kurejeshewa magari yao aina ya Toyota IST yenye namba za usajili T 628 DDE na Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili T 308 EJU. 





Uamuzi huo umetolewa leo Septemba 17, 2026, na Hakimu Mkazi Devotha Msofe wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha aliyekuwa akisikiliza shauri hilo la jinai namba 14535/2026, 



Washtakiwa hao waliotiwa hatiani ni Thomas Godfrey Temu (35) aliyepata kifungo cha mwaka mmoja jela, pamoja na Sara Marko Laizer (22) na Lilian Godfrey Temu (47) ambao wameachiwa kwa masharti ya kutorudia makosa ndani ya mwaka mmoja.

Awali, Wakili wa Serikali Belinda Rwakatare aliwasilisha mahakamani hapo mkataba huo wa makubaliano baina ya washtakiwa na DPP ambapo baada ya mkataba kupokelewa, upande wa mashtaka ulibadili hati ya zamani na kuwasilisha hati mpya ya mashtaka yenye makosa matatu ambapo washtakiwa waliyasomewa upya na kuyakubali yote.


 Katika shtaka la kwanza, Sara na Thomas wanadaiwa kukutwa na rola tatu za stamp feki za TRA za kielektroniki za kodi (ETS) mnamo Machi 23, 2026, maeneo ya Lolovono Sokoni 1 jijini Arusha, ambapo shtaka la pili linawakabili Lilian na Thomas ambapo walikutwa na pombe feki, na shtaka la tatu ni kufanya biashara ya kutengeneza pombe bila kuwa na leseni.


Mchakato wa kutoa adhabu ulifanya mahakama ihamie kwa muda kwenye ghala (warehouse) la Mamlaka ya Mapato Arusha ili kuangalia vielelezo vinavyoshikiliwa ambavyo vinapaswa kuteketezwa pamoja na magari yanayopaswa kurejeshwa kwa washtakiwa.



Akiongea mara baada ya uamuzi huo, Meneja Upelelezi wa Kodi wa TRA Kanda ya Kaskazini, Thoddy Beanga aliwaonya wananchi kutofanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kwani vinalikosesha Taifa mapato na kuathiri afya za walaji.

"Ni vinywaji ambavyo vinazalishwa kinyume cha utaratibu, hivyo vinaathiri nguvu kazi ya nchi, kodi, na hata afya za wanywaji ambao ni wananchi," alisema Beanga huku akiwataka wananchi kutoa taarifa wanapowabaini watu wanaofanya vitendo hivyo mitaani.


Aliongeza kuwa washtakiwa walikuwa wakitengeneza pombe bila kuwa na leseni kinyume na sheria za nchi lakini pia wakifungasha chapa za makampuni mbalimbali, na alihitimisha kwa kusema kuwa ingawa wahalifu wana mbinu nyingi, mamlaka inajitahidi kuwa mbele yao kuwadhibiti na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria 


Hatua hiyo imechukuliwa ili kukomesha vitendo vya ukwepaji kodi, uhujumu uchumi, na uingizaji wa bidhaa hatari sokoni zinazohatarisha afya za walaji.








Jaji wa Mahakama Kuu, Hamidu Mwanga, amekataa ombi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho la kumtaka ajiondoe kusikiliza kesi ya mgawanyo wa mali kati ya pande mbili za chama hicho – Bara na Zanzibar.

Ombi hilo liliwasilishwa kwa Mahakama Kuu tarehe 23 Juni 2025 kupitia barua rasmi iliyotiwa saini na Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, wakidai kuwa Jaji Mwanga ana upendeleo, ana mgongano wa maslahi na kwamba amekiuka taratibu za utendaji wa mahakama.

Kauli ya Jaji Mwanga

Katika uamuzi alioutoa tarehe 28 Julai 2025, Jaji Mwanga amesema kuwa hakuna msingi wowote wa kisheria unaoweza kumlazimisha kujitoa katika usikilizaji wa shauri hilo.

Amesema: "Nikikubali kujitoa, itakuwa shida kwa kuonekana majaji wa Mahakama ya Tanzania wanaendeshwa na uamuzi wa mtu, kwamba anaweza kuamua kumtoa jaji pale anapohisi hajafurahishwa na uamuzi wa mahakama. Hivyo nakataa hoja hii."

Hoja za Walalamikiwa Zakataliwa

Jaji Mwanga amezikataa hoja mbalimbali zilizotolewa na CHADEMA na Bodi ya Wadhamini, zikiwemo:

  • Hoja ya upendeleo – Jaji amesema tuhuma za upendeleo hazina mashiko kwa kuwa zilitokana na uamuzi alioutoa Juni 23, 2025, kuhusu maombi madogo ya zuio la muda, ambapo upande wa walalamikiwa haukuwa na wakili aliyejitambulisha kisheria mahakamani.

  • Hoja ya Wakili Edson Kilatu – Amesema: "Kilatu hajawahi kufika mahakamani hata kujieleza kuhusu barua anayoaminika kuituma, na si sahihi kuzungumzia jambo hilo kwa niaba yake. Zaidi ya hapo, mahakama haimtambui kama wakili wa upande wowote katika shauri hili."

  • Historia ya ajira ya Jaji – Kuhusu madai kuwa aliwahi kufanya kazi katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji Mwanga amesema hajawahi kuwa mtumishi wa ZEC, bali aliwahi kuhudumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), na hiyo si sababu ya msingi ya kumtaka ajitoe katika kesi.

Mahakama Yaahirisha Kesi

Kesi hiyo, ambayo awali ilipangwa kusikilizwa mwezi Juni na kisha kupelekwa mbele hadi Julai 14, 2025, imeendelea kuahirishwa na Mahakama Kuu kutokana na sababu mbalimbali za kisheria na kiutaratibu, ikiwemo ukamilishaji wa maamuzi ya awali kama huu wa kutaka Jaji ajitoe.

Kwa mujibu wa taarifa utoka Mahakama Kuu, kesi kuu sasa imepangwa kusikilizwa tena tarehe 7 Agosti 2025, ambapo pande zote zinatarajiwa kuwasilisha hoja zao mbele ya Jaji Mwanga ambaye sasa ataendelea na usikilizaji.

Muktadha wa Kesi

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wenzake wawili, wakitaka mgawanyo wa mali za chama hicho kati ya Zanzibar na Bara, wakidai kutengwa na kunyimwa haki ya usawa ndani ya chama.

Kwa upande wake, CHADEMA kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu John Mnyika, imesema kuwa hatua ya Mahakama kuzuia vikao na maamuzi ya chama ni kuingilia uhuru wa chama cha siasa na kuvunja misingi ya utawala wa sheria.

Kwa msimamo aliouchukua Jaji Mwanga, kesi hii itaendelea chini ya usimamizi wake licha ya pingamizi kutoka kwa CHADEMA. Jambo hili linaonesha msimamo wa Mahakama juu ya uhuru wa majaji katika kutoa haki bila shinikizo kutoka kwa wahusika wa nje wa mashauri.

Kesi ya mgawanyo wa mali ndani ya CHADEMA sasa inaelekea kuwa mojawapo ya kesi zinazofuatiliwa kwa karibu zaidi katika historia ya mivutano ya kisiasa ndani ya vyama vya siasa nchini Tanzania.


 


Katika kisa kilichoteka hisia za watu kote duniani, Mahakama Kuu ya Victoria nchini Australia mnamo Jumatatu, Julai 7, 2025, ilimpata Erin Patterson na hatia ya kuwaua watu watatu na kujaribu kumuua mtu wa nne kwa kuwalisha chakula kilichochanganywa na uyoga wenye sumu hatari. 


Kesi hiyo imekuwa gumzo kwa zaidi ya miaka miwili, tangu tukio hilo kutokea mnamo Julai 29, 2023, katika mji mdogo wa Leongatha, ulioko eneo la mashambani kusini mwa Australia.

Tukio la Kushtua

Erin Patterson, mwanamke mwenye umri wa miaka 50, aliwaalika wageni wanne nyumbani kwake kwa chakula cha mchana: wazazi wa mumewe (Don na Gail Patterson), pamoja na mjomba na shangazi wa mumewe (Ian na Heather Wilkinson). Siku chache baada ya chakula hicho, watatu kati yao walifariki dunia kutokana na sumu inayopatikana kwenye uyoga wa porini aina ya Amanita phalloides, maarufu kama "death cap", huku Ian Wilkinson akiwa ndiye aliyenusurika baada ya kulazwa hospitalini kwa muda mrefu.

Katika utetezi wake mahakamani, Erin alidai kuwa hakujua kuwa uyoga aliotumia ulikuwa na sumu na kwamba aliununua kutoka duka la kawaida la vyakula au alipanda kutoka bustani ya nyumbani kwake. “Sikuwa na nia mbaya. Nilipika chakula hicho kwa mapenzi na ukarimu,” alisema mahakamani kwa sauti ya huzuni. Hata hivyo, upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi ulioonyesha kuwa Erin aliandaa chakula hicho kwa makusudi, kwa kutumia uyoga hatari, na kwamba alijaribu kuficha ushahidi, ikiwa ni pamoja na kutupa mashine ya kukaushia uyoga baada ya tukio hilo.

Mahakama ilielezwa kuwa muda mfupi kabla ya tukio, Erin alikuwa akipitia changamoto za kifamilia, ikiwa ni pamoja na mzozo wa malezi ya mtoto wao wa kiume na mumewe Simon Patterson, ambaye kwa wakati huo walikuwa wametengana bila talaka rasmi. Simon, aliyekuwa hajahudhuria chakula hicho, alisema: “Uhusiano wetu ulikuwa umeharibika, lakini sikuweza kudhani kuwa hali ingetokea kwa namna hii ya kusikitisha.”

Majaji na jopo la wataalamu wa sumu walithibitisha kuwa sumu ya Amanita phalloides ndiyo iliyosababisha vifo hivyo. Hakimu Mkuu, Christopher Beale, alisema katika hukumu yake: “Huu ni mfano wa kusikitisha wa kile kinachoweza kutokea pale ambapo uhusiano wa kifamilia unapoingia kwenye mizozo mikubwa, na mtu kuchukua hatua kali za uharibifu.”

Kauli za Wahusika

Katika ushahidi wake, manusura Ian Wilkinson alisema:

“Tulikuwa tumekusanyika kwa ajili ya chakula cha familia, haikuwahi kuvuka mawazo yangu kwamba kingeweza kuwa chakula cha mwisho kwa wengine. Nilihisi vibaya, lakini pia nilihisi kwamba jambo hili halikuwa la kawaida. Nilianza kuumwa masaa machache tu baada ya kutoka mezani.”

Wakati huo huo, Erin Patterson aliendelea kusisitiza kuwa alihisi hatia kwa yaliyotokea, lakini hakukubali kuwa alikusudia kuua.

“Naishi na huzuni hii kila siku. Nilipoteza watu waliokuwa familia kwangu. Sikuwa na nia ya kuwadhuru.”

Lakini upande wa mashtaka ulipinga kauli hizo, ukisema kuwa kulikuwa na ushahidi wa maandalizi ya kutosha unaoashiria nia ya uhalifu. Mwendesha mashtaka mkuu alisema:

“Aliandaa chakula hicho kwa utaratibu, akajua aina ya uyoga aliokuwa akitumia, na alifanya kila jitihada kuficha alama za ushahidi baada ya tukio. Hii haikuwa ajali.”

Hatima Yake

Erin Patterson sasa anakabiliwa na hukumu ya kifungo cha maisha gerezani, huku upande wa utetezi ukiwa na siku 28 kuwasilisha rufaa. Hadi sasa, hukumu rasmi haijatolewa, lakini matarajio ni kwamba itakuwa kali kutokana na uzito wa kesi hiyo.

Kesi hii imeibua maswali mengi kuhusu usalama wa chakula, uhusiano wa kifamilia, na jinsi chuki za ndani ya familia zinaweza kubadilika kuwa vitendo vya uhalifu mkubwa. Katika nchi ambayo mara chache husikia matukio ya sumu ya uyoga, kesi hii imeacha alama kubwa katika historia ya sheria za uhalifu wa Australia.

Kwa sasa, jamii ya Australia inaendelea kutafakari kwa kina tukio hili, huku wengi wakihoji: je, ni kweli ilikuwa ajali ya kusikitisha au ni njama ya mauaji iliyopangwa kwa utulivu na ushawishi wa ndani? Majibu hayo sasa yako mikononi mwa sheria.

 


Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, imemhukumu mchungaji Daud Nkuba maarufu kwa jina la Komando Mashimo, Nabii Nikaya, (Mchungaji Mashimo) kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili kati ya matatu aliyokuwa akishtakiwa nayo.

Mashimo ametiwa hatiani kwenye mashtaka ya kuingia kwa jinai na kuharibu mali, huku akiachiliwa huru kwenye shtaka la kutishia kwa vurugu.

Mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka matatu ambapo upande wa Jamhuri umethibitisha makosa mawili dhidi yake na kushindwa kuthibitisha shtaka la kutishia kwa vurugu.

Hukumu hiyo ilitolewa leo Machi 18, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhan Rugemalila, baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha makosa dhidi ya mshitakiwa bila kuacha shaka yoyote.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Rugemalila alisema, "Nimeridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa Jamhuri na vielelezo, ambapo wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo mawili. Hata hivyo, mshtakiwa ameachiliwa huru kwa shtaka la tatu kwa kuwa upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa alitenda kosa hilo."

Aidha, alisema, "Mshtakiwa katika kosa la kuingia kwa jinai, mahakama inakupa adhabu ya kwenda jela miezi sita, na kosa la kuharibu mali, mahakama inakutia hatiani na kukupa adhabu ya kwenda jela miaka miwili. Pia, mahakama inakuachia huru kwa kosa la kutishia kwa vurugu kwa sababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi yako. Hivyo, utatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani."

Kabla ya kusomewa adhabu, mshitakiwa alipata nafasi ya kujitetea, ambapo aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Rhoda Kamungu, uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kama sheria inavyoelekeza, ili iwe fundisho kwake na kwa jamii nzima.

Awali, ilidaiwa kuwa, Novemba 22, 2023, mchungaji Mashimo alifanya uhalifu katika maeneo ya Mbezi Luis Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, kwa kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Frola Mwashaa. Aidha, aliharibu ujenzi wa nyumba iliyokuwa eneo hilo, kinyume cha sheria.

Pia, ilidaiwa kuwa, katika shtaka la tatu, alimtishia Ramson Vicent kwa vurugu.

Mwekezaji Saleh Almamry (wa kwanza kusho) Wakili wa Kujitegemea, Sheki Mfinanga.


Mwekezaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii nchini, Salehe Salim Almamry, pamoja na wakili wa kujitegemea Sheki Mfinanga, wanakabiliwa na mashtaka 60, yakiwemo utakatishaji wa fedha na uhujumu uchumi, huku upande wa Jamhuri ukitarajia kuwasilisha mashahidi 80 katika kesi hiyo.


Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) ameidhinisha kesi hiyo kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Ndogo ya Arusha.

MAELEZO YA MASHTAKA



Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Erasto Philly, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Edga Bantulaki, akisaidiwa na waendesha mashtaka Jackline Mosha na Allawi Miraji, pamoja na Yona Msengi wa TAKUKURU, alieleza kuwa Jamhuri imekamilisha ushahidi na inatarajia kuwasilisha nyaraka 461 za ushahidi wa maandishi pamoja na nyaraka 12 za ushahidi unaoonekana.

Alisema miongoni mwa mashahidi hao ni wafanyabiashara wakubwa waliotumiwa na mtuhumiwa Salehe Almamry kupitia kampuni yake ya Tarangire Sunset Limited kutakatisha fedha.

Bantulaki aliieleza, “Mtuhumiwa Salehe Almamry anadaiwa kutakatisha zaidi ya bilioni 60 baada ya kuwadhulumu wabia wake wawili raia wa Saudi Arabia, Khalid Alraj na Abdulkarim Alraji, katika kampuni ya Tarangire Sunset Limited.”

Aliendelea kufafanua kuwa washtakiwa pia wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu, kughushi nyaraka, na kutoa taarifa za uongo kwa mamlaka za kiserikali kwa nia ya kujipatia fedha isivyo halali.

Mwekezaji Saleh Almamry 


Katika shtaka namba 16, Almamry anadaiwa kughushi nyaraka ikionyesha kuwa wabia wake Abdulkarim Mohamed Alraj na Khalid Alraj walikubali hisa zao za asilimia 18 kuchukuliwa, jambo ambalo si la kweli.

Makosa haya yanadaiwa kufanywa kati ya Machi 2019 na Mei 2024, katika mikoa ya Arusha, Manyara, Pwani, na Dar es Salaam.

HATMA YA WASHTAKIWA

Kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, Hakimu Mkazi Erasto Philly alisema: "Mtuhumiwa namba moja Salehe Almamry ataendelea kukaa mahabusu kwa kuwa kesi yake haina dhamana, huku mtuhumiwa namba mbili Sheki Mfinanga akiendelea na dhamana yake hadi kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi."

Aliendelea kusema kuwa "Mahakama yetu imesikiliza maelezo ya awali baada ya upelelezi kukamilika, na sasa tunasubiri taarifa rasmi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kuhusu tarehe ya usikilizaji wa kesi hiyo."

MAWAKILI WA WASHTAKIWA



Wakili Mosses Mahuna, na Faisal Rukaka.

MASHIHIDI WA JAMHURI

Miongoni mwa mashahidi wa Jamhuri waliotajwa ni mfanyabiashara na mkulima mkubwa Gerald James Milla, Said Iddi Kipingu, wakili John Beatus Kasegenya, Abdull Said Msalaam, Suleiman Nkya, Abdulkareem Mohamed Alraj, Khalid Alraj, na Abano Gilla.

Kesi hiyo sasa inasubiri tarehe rasmi ya kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi.



Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni imeelezwa kuwa vijana sita, wakiwemo mabondia wawili, walipanga kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo kwa lengo la kumlawiti na kumsababishia maumivu.




Kesi hiyo imeendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemalira, ambapo washtakiwa Fredrick Nsato (21), bondia Isaack Mwaifuani (29), Benk Mwakalebela (40), bondia Bato Twelve (32), dereva teksi Nelson Msela (24), na Anitha Temba (27) maarufu kama Jack, wanakabiliwa na mashtaka ya utekaji nyara.


Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema kuwa Anitha alihusika katika kumshawishi Tarimo kukutana naye hotelini kwa madai ya kujadili biashara. Hata hivyo, alipofika hotelini hapo, alinaswa kwenye mtego wa washitakiwa waliokuwa na mpango wa kumteka.


Ilidaiwa kuwa Novemba 11, 2024, Tarimo alipofika hotelini, Anitha alimwelekeza kusubiri katika kaunta ya baa. Baada ya muda mfupi, washtakiwa Mwaifuani, Mwakalebela, na Twelve waliwasili katika gari aina ya Toyota Raum namba T 237 EGE na kujitambulisha kama polisi.


Walipomvuta Tarimo kuelekea kwenye gari hilo, alipiga kelele, hali iliyowalazimu kumwachia na kumtishia kuwa wangempata tena. Taarifa zilifikishwa katika Kituo cha Polisi Gogoni, ambapo uchunguzi ulifanyika na hatimaye washitakiwa wakakamatwa.


Katika utetezi wao, washtakiwa wote walikana mashtaka dhidi yao, huku Anitha Temba akikataa jina lake maarufu la Jack. Mahakama ilikubali ombi la kubadilisha shtaka kutoka "jaribio la utekaji" hadi "utekaji nyara" baada ya ushahidi mpya kuwasilishwa.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, 2025, kwa ajili ya kusikilizwa zaidi.

 Mahakama Yawaachia Huru Mke wa bilionea Msuya na mwenzake.

Ndugu wa marehemu alia kwa uchungu 






Leo, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa uamuzi wa kesi iliyokuwa inamkabili Miriam Steven Mrita, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara mashuhuri wa madini mkoani Arusha, bilionea Erasto Msuya, pamoja na mshitakiwa mwenzake, Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray, ambao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia.


Katika hukumu iliyotolewa leo, Mahakama imefikia uamuzi wa kuwaachilia huru washitakiwa hao baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao. 



Miriam na Ray walidaiwa kuhusika katika mauaji ya kikatili ya Aneth Elisaria Msuya, wifi wa Miriam, ambayo yalidaiwa kutokea Mei 26, 2016, huko nyumbani kwa Aneth Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam.


Kesi hiyo, ambayo ilianza mwaka 2018, imekuwa ikiendelea kwa miaka kadhaa huku washitakiwa wakiwa mahabusu. Hata hivyo, leo wamepata afueni baada ya Mahakama kuwakuta hawana hatia.


Uamuzi huu wa Mahakama umekuja baada ya kipindi kirefu cha kusikilizwa kwa ushahidi na hoja kutoka pande zote mbili. Familia za washitakiwa na jamii kwa ujumla zimepokea habari hii kwa furaha na utulivu.


Hukumu hii imepokelewa kwaa hisia tofauti ambapo wakati ndugu wa wshitakiwa hao wakifurahi na kuimba nhimbo za kumsifu !ungu ndugu wa marehemu Aneth walionekana wakilia kwa jchunhi.



Antuja Msuya ambaye ni Dada wa Marehemu Bilionea Erasto Msuya ameangua kilio  Mahakamani hapo jioni ya leo na kupaza sauti “ushahidi wote unaonekana Mtu anaambiwa hana hatia, niueni... niueni, niueni, bora nife” 


“Hakuna haki iliyotendeka maana ushahidi wote unaonekana na ushahidi upo na jinsi ilivyofanyika mwanzo hadi mwisho ila wameamua maamuzi yao Mahakama haijatenda haki, kuanzia Arusha wanapaka nyumba rangi, upare wanapaki nyumba rangi wanasema anatoka kwa gharama yoyote leo ametoka, Mungu ataamua,”  Antuja ameyasema hayo wwkati akisaidiwa na ndugu yake pamoja na polisi kutoka nje ya chumba cha mahakama.

 

Hata hivyo wakati Miriam wakitoka Mahakamani hapo, Ndugu na Jamaa waliofurahishwa na kuachiwa huru kwa wawili hao walisikika wakitamka baadhi ya maneno ya kumshukuru Mungu mbele ya Antuja “Yesu ni bwana, amefanya” 

https://habaritanzaniagracemacha.blogspot.com/2024/02/hukumu-ya-kesi-ya-mke-wa-bilione-msuya.html



Hukumu ya Kesi ya Mke wa bilione Msuya kutolewa leo



Hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili Miriam Steven Mrita, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, bilionea Erasto Msuya, inatarajiwa kutolewa leo na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Kesi hii, ambayo imekuwa ikiendelea kwa miaka minane sasa, inamhusisha Miriam pamoja na mshitakiwa mwenzake, Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray, ambao wanadaiwa kumuua kwa kumchinja, Aneth Elisaria Msuya, wifi ya Miriam.


Tukio hili la kusikitisha lilitokea Mei 26, 2016, huko nyumbani kwa Aneth, Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam. Aneth, ambaye alikuwa mdogo wa marehemu bilionea Erasto Msuya, alipoteza maisha yake kikatili katika tukio hilo la mauaji ya kukusudia. Kufuatia tukio hili, Miriam na Ray wamekuwa wakisubiri hukumu huku wakiwa mahabusu.


Kukumbuka historia ya kesi hii, bilionea Erasto Msuya pia alifariki kwa njia ya kutatanisha baada ya kuuawa kwa kupigwa risasi kwa kutumia bunduki ya kivita aina ya SMG, eneo la Mijohoroni, Barabara Kuu ya Moshi-Arusha wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 7, 2013. Kifo chake kilizua maswali mengi na kutia doa kwenye taswira ya amani katika jamii.


Hukumu hii inayotarajiwa kusomwa na Jaji Edwin Kakolaki itakuwa muhimu sana kwa familia za marehemu na washitakiwa wenyewe. Kwa mujibu wa sheria za nchi, iwapo watapatikana na hatia, adhabu inayotolewa kwa mauaji ya kukusudia ni kunyongwa hadi kufa. Hata hivyo, iwapo watapatikana hawana hatia, wanaweza kuachiwa huru.



MAHAKAMA imewahukumu kifungo cha miaka 30 jela watu wanne baada ya kukutwa na hatia kwenye kesi ya ugaidi ya kulipua mgahawa wa Traditional Indian Cusine uliopo jijini Arusha.


Aidha imemhukumu Idd Salim Abdallah miaka 18 jela kwa kosa la kuwahifadhi  watuhumiwa wa ugaidi.

Uamuzi huo umetolewa faragha leo Desemba 15,2023 na jaji ,Stephen Magoiga aliyesikiliza shauri hilo la jinai (criminal session case)  namba 66/2022 ambalo lilianza kusikilizwa kwa faragha Novemba 15, 2023 kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.


Waliohukumiwa miaka 30 jela ni pamoja na Yusuph Ally Hutta, Aman Mussa  Pakasi, Rajab Ayub Abdallah na Abashari Hassan Omary ambapo kwa kuwa walikuwa mahabusu miaka tisa hivyo watatumikia kifungo kwa miaka 21.

Awali kwenye shauri hilo kulikuwa na washitakiwa sita waliokuwa wakikabiliwa na mashitaka 17 ya vitendo vya ugaidi ambapo mmoja, Shaban Iddi maarufu kama baba Tuna aliachiwa huru baada ya mahakama kumuona hana kesi ya kujibu,

Washitakiwa hao kila mmoja alikuwa akitetewa na wakili wake akiwemo, Simon Mbwambo, John Shirima, Jabir Wahira 

Washitakiwa hao walihusishwa na tukio la mlipuko  bomu uliolipuka usiku wa Julai 8,2014  jijini Arusha  katika mgahawa wa  Traditional Indian Cusine uliopo pembezoni mwa Klabu ya Gymkana ambapo jumla ya watu nane walijeruhiwa.


Tukio hilo lilitokea kati ya saa nne na tano usiku ambapo aliyekuwa  kaimu mgamna mkuu wa hospitali ya Seliani Dr. Paulo Kisanga  alisema walianza kupokea majeruhi hao kuanzia majira ya saa tano kasoro na saa tano usiku .

Alisema kuwa walipokea wagonjwa nane ambao waliumia sana katika maeneo ya miguu ambapo alibainisha kuwa katika wagonjwa hao nane kuna mmoja ambaye aliletwa akiwa na hali mbaya sana kitu ambacho kiliwalazimu kumfanyia upasuaji usiku huo huo.


"Kati ya wagonjwa hao nane mmoja aliletwa akiwa mahututi sana kwani mguu wake ulikuwa umeadhiriwa sana na bomu hilo ivyo ikatulazimu  kumkata mguu mmoja wa kushoto ,kwakweli mgonjwa huyo ambaye tumemkata mguu anaitwa  Deepak Gupta (25) mwanaume na sasa hivi anaendelea vyema kidogo na yupo katika chumba cha ICU ndani ya hospitali hii yetu ya Seliani,"alisema Kisanga.


Aliwataja majeruhi hao kwa majina kuwa ni pamoja na  Vinod Suvesh(37), Ritwik Khandelval (13), Raj Rajin(30), Prateck Saver, Manci Gupta, (14), Manisha Gupta (36), Mahush Gupta(42) pamoja na Deepak Gupta (25)  wote wakiwa na asili ya kiasia

Kisanga alisema kuwa kwa mujibu wa wagonjwa hao walio  waliofika hapo hospitali walidai kuwa   bomu hilo lilirushwa kwa kupitia dirishani.!


DEREVA toyo, Maico Silvesta, (28) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la  kumbaka mtoto wa wa kike wa miaka 10 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Olomitu.


Mkazi huyo wa Maloloyi, Moshono,  Arusha amekutwa na hatia ya kumbaka mtoto huyo ambaye alimpatia pipi kisha akamwingiza kwenye chumba cha bibi yake na kumbaka huku akitishia kumuua endapo ataendelea kupiga kelele. 


Uamuzi huo umetolewa leo, Septemba 26,2023 na Hakimu, Itikija Nguvava wa Mahakama ya wilaya Arumeru aliyekuwa akisikiliza shauri hio la jinai namba 37/2023.

Akisoma uamuzo huo Hakimu Nguvava amesema kuwa amefikia uamuzi huo  baada ya kusikiliza hoja za pande zote ambapo upande wa jamhuri walileta mashahidi wanne huku mshitakiwa Maico akijitetea mwenyewe.

Awali, mahakama hiyo ilielezwa kuwa mnamo mwezi January mwaka huu mhanga akiwa anaishi na bibi yake , mjomba yake alikuja na rafki yake  (mshtakiwa Maico) nyumbani.

" Alimpa pipi (mhanga/mtoto) na kuondoka na baada ya kuondoka kesho yake (Maico) alirudi peke yake ambapo alimpeleka mhanga chumbani kwa bibi yake na akamvua nguo za ndani na kumbaka, mhanga alipiga kelele ila mshtakiwa alimziba mdomo na akamtishia akisema atamuua,".


Siku inayofuata ndipo ilipogundulika kufanyika kwa tukio hilo kwani mtoto huyo alikuwa hatembei vizuri ambapo alipohojiwa alisema kuwa amebakwa na mshitakiwa Maico.

Maico alikamatwa Februari 20,2023 ambapo alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 15,2023.

MAHAKAMA imesema kuwa Waziri wa Maliasili na utalii hakuzingatia sheria kwenye mchakato wa kutangaza pori Tengefu la Pololeti kwani wananchi wa vijiji vilivyopo ndani ya eneo hilo hawakushirikishwa.


Hata hivyo mahakama hiyo ilishindwa kutoa amri ya kumtaka waziri kurudia mchakato huo kwa kile ilichoeleza kuwa tayari Rais ameshalipandisha hadhi eneo hilo kuwa pori la akiba.


Hayo yameelezwa leo, Septemba 19,2023 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Joachim Tiganga wakati akisoma uamuzi kwenye shauri la mapitio namba 21/2022 ambalo limekuwa likifuatiliwa kwa karibu na wananchi wengi hasa jamii ya wafugaji ambao walijitokeza kwa wingi mahakamani hapo.



Amesema kuwa Waziri alikiuka haki ya kushirikisha wahusika ambao ni wananchi wa vijiji vilivyokuwa ndani ya pori tengefu la Loliondo na kusisitiza kuwa jambo lolote linalofanywa dhidi ya mtu anapaswa kushirikishwa hivyo  ilitakiwa kuzingatiwa.



"Waziri alikosea kwa kushindwa 'kuconsult' wale waliotakiwa kuwasiliana nao kama sheria inavyoelekeza. ..Eneo husika limeshapandishwa hali kuwa  'game reserve' pori la akiba kutoka kutoka 'game controlled area' poro tengefu ambapo Rais alilipandisha hadhi kwa mujibu wa sheria," ameeleza Jaji Tiganga akisoma uamuzi huo na kuongeza 

... Mahakama inajiuliza kuwa inaweza kumrejesha waziri kushuhulikia suala hilo wakati aliye juu yake ameshafanya mamuzi na sheria inampa mamlaka Rais kupandisha hadhi ya eneo,".

"Basi kama kuna upingaji basi unapaswa kupinga uamuzi huo wa Rais wa kutangaza eneo hilo kuwa pori la akiba  ....kutoa amri kuwa waziri narudie arekebishe itakuwa si sahihi kwa sasa Tangazo la serikali la waziri halipo kwani Rais ameshalifuta na kutangaza Pololeti kuwa Game Reserve kwa GN namba ....ya Oktoba 14,2022,".

Hata hivyo Jaji Tiganga alitupilia mbali hoja nyingine tisa zilizowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa waleta maombi watano, Latang'amwaki Ndwati, Ndamalia Taiwap, Megwari Moko, Ezekiel Sumare na Latajewo Sayari.



Waleta maombi hao waliwakilishwa na mawakili wa kujitegemea, Joseph Ole Shangai, Yonas Masiaya, Joseph Alais na Dennis Mosses huku wajibu maombi ambao ni Waziri wa Maliasili na Utalii na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwakilishwa na mawakili Mkama Msalama na Ian Mbise.

Kwenye shauri hilo waleta maombi hao walikuwa wanaiomba iiagize Serikali kuondoa zuio dhidi ya  Wananchi  kuingia kwenye eneo la Kmilometa za mraba  1,502 ambalo wamekuwa wakitumia kwa ajili ya malisho ya mifugo yao na kufanyia shughuli za imani yao.

Aidha walikuwa wanaiomba  mahakama itengue Tangazo la Serikali namba 421  (GN421) la Juni, 17  2022  kwa kuwa ni batili na limetangazwa kinyume na sheria na pia haikuwashirikisha wananchi kama sheria inavyotaka

Ombi lao la tatu walikuwa wanaiomba mahakama itamke kuzuia Serikali na Mawakala wake wasifanye oparesheni zote kwenye eneo hilo.


WAKILI wa kujitegemea, Peter Madeleka, ameibwaga serikali baada ya mahakama Kuu Kanda ya Arusha kukubaliana na maombi yake ya kupatiwa haki ya dhamana.

Aidha mahakama hiyo imempa marshati ya dhamana kuwa ni kuweka dhamana ya shilingi milioni moja na kudhaminiwa na mtu mmoja anayeaminika.

Uamuzi huo wa Jaji, Yohane Masara, aliyesikiliza rufaa hiyo namba 87/2023 umesomwa leo, Septemba 9, 2023 na Kaimu Msajili wa Mahakama hiyo, Boniface Semroki. 

Akisoma uamuzi huo, Semroki ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi, amesema kuwa baada ya mahakama kupitia hoja za pande zote mbili umejiridhidha pasipo na shaka kuwa kesi inayomkabili Madeleka ni yankujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambayo kimsingi mashitaka hayo yana dhamana.


Kwenye shauri hilo upande wa Jamhuri umewakilishwa na Mawakili wa Serikali, Elidineni Njiro, Tusaje Samuel na Joyce Mafie huku mleta maombi, wakili, Madeleka amekiwakilishwa na mawakili, Boniface Mwabukusi, Revocatus Myela,  Simon Mbwambo na Jonas Masiaye 

Uamuzi huo wa jaji Masara umesema kuwa kwenye shauri la msingi DPP alifanyia marekebisho hati ya mashitaka akaondoa mashitaka ya kutakatisha fedha ambayo hayana na dhamana na kuacha mashitaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambayo yana dhamana.

Baada ya kufanya makubaliano na ofisi ya DPP ya plea bargaining  alilipa shilingi milioni mbili ambapo mahakamani alikiri kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu au faini ya shilingi laki mbili ambapo alilipa faini hiyo.

Semroki amesema  mahakama  kuwa kimsingi hati ya mashitaka iliyokuwa hai (exist) mahakamani ni ile ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwani ndiyo iliyotumika kufanya uamuzi wa mwisho wa mahakama kwenye shauri hilo namna 40/2020.

Awali Madeleka ambaye amekaa mahabusu kwenye gereza la  Kisongo siku 57 kuanzia julai  17,2023 baada ya  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Fadhil Mbelwa, kutoa  uamuzi huo mdogo kuhusiana na hatima ya dhamana ya Madeleka anayekabiliwa na makosa 10 ikiwemo utakatishaji fedha.

Hakimu Mbelwa alisema kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Julai 17,2023,ambao uliondoa zoezi la makubaliano ya kukiri kosa 'plea bargain', hivyo akasema na hati ya mashitaka iliyofanyiwa marekebisho ambayo ilikuwa na makosa yenye dhamana imefutwa.

Alisema kilichoamuliwa na Jaji Aisha Bade wa Mahakama hiyo ni kuondoa zoezi la makubaliano hayo na kuwa kufutwa kwa mwenendo huo hati inayomshitaki ni ya awali ambayo ina makosa 10 ikiwemo la utakatishaji fedha ambalo halina na dhamana kisheria hivyo mshitakiwa ataendelea kukaa mahabusu.


Agosti 1,2023  ya Hakimu Mkazi Arusha,ilitoa uamuzi mdogo ambao ulitupilia mbali ombi la dhamana ya wakili huyo lililowailishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanne wanaoongozwa na Wakili, Mwabukusi


WAKILI wa kujitegemea, Peter Madeleka ameondoka mahakamani kwa staili ya aina yake ambapo alibadili nguo kisha kutoka kwa kasi  na kupanda bodaboda iliyokuwa ikimsubiri nje ya lango kuu la mahakama mara baada ya mahakama kuu kanda ya Arusha kumuachia kwa dhamana.



Hayo yametokea leo Septemba 8, 2023 majira ya saa tisa alasiri mara baada ya Jaji, Yohane Masara wa mahakama kuu kanda ya Arusha aliyesikiliza rufaa namba 87/2023  kumuachia kwa dhamana.

Madeleka ameamua kutumia mbinu hiyo baada ya yeye na mawakili wake kuhofia kuwa huenda akakamatwa na polisi waliokuwa wamevaa kiraia walionekana  ndani na nje ya mahakama  tokea majira ya mchana mara baada ya  mahakama kutoa uamuzi wa kumuachia kwa dhamana.

Wakili huyo ambaye kesi yake inafuatiliwa na wengi akiwa mahakamani alikuwa amevaa shati la bluu lenye mistari meupe ambapo mara baada ya kuachiwa kwa dhamana alitoka nje ya chumba cha mahakama akiwa amefuatana na mawakili wake kisha wakaingia kwenye moja ya vyumba vya mahakama.

Baada ya muda Madeleka alionekana akitoka nje ya jengo la mahakama akiwa kavaa koti jeusi miwani meusi na kofia akitembea kwa mwendo wa haraka hali ambayo haikuwa rahisi kutambulika.


Mwandishi wa habari hizi alimshuhudia Madeleka akitoka mahakamani hapo akifuatiwa na mdhamini wake ambapo walipokaribia lango kuu la dhamana walitimua mbio na  bodaboda iliyokuwa karibu na lango kuu kisha kuondoka kwa mwendo wa kasi.

Hata hivyo mawakili wa Madeleka, Boniface Mwabukusi alipoulizwa ni sababu ya hatua hizo, amesema  wamelazimika kutumia mbinu hizo alizoziita za kimedani kutokana na hofu huku akionya vyombo vya dola vinapokuwa mahakamani viuache muhimili huo utende kazi zake.


"Lakini ni vema wanapokuwa kwenye maeneo ya mahakama basi waiache mahakama ifanye kazi yake na watu waweze kuona ile sura ya mahakama. Mahakama ni sehemu ambayo inatafsiri vitabu inatafsiri sheria," amesema Mwabukusi.

"Mimi sifurahi,  mimi ni mmoja wa watu wanaosikitika sana kuona lundo la watu wanaojaribu kuufanya mchakato wa  mahakama kuwa wa kijeshi,"  

...Ila najua polisi wetu wana weledi basi watumie weledi kufanya kazi kwenye maeoneo yao na ya wengine wayaache katika sura yake na wanapolazimika kuwepo wajitahidi wawe katika sura inayomwalika kila raia  kwenye hilo eneo,".

Kuna wakati kwa kutumia mbinu za medani mtu anaweza kufa kwa kihoro anaweza kuruka dirishani vitu ambavyo  si sawa kabisa,".

Awali mahakama hiyo iliporejea majira ya mchana mbele ya Kaimu Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Boniface Semroki  Madeleka alitimiza masharti ya dhamana ambapo alisaini dhamana ya shilingi milioni moja na kudhaminiwa na mtu mmoja, Mzambia Amon Kabuje  ambaye naye alisaini dhamana ya shilingi milioni moja

Dk John Pima na washitakiwa wenzake wakiongea na wakili wao, Moses Mahuna

ALIYEKUWA Mkurugenzi  wa jiji la Arusha dkt John Pima na wenzake wawili wamehukumiwa  kifungo cha miaka 20 jela  baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya uhujumu uchumi yaliyokuwa yakiwakabili.


Wengine waliohukumiwa pamoja na Pima ni pamoja na aliyekuwa Mwekahazina wa jiji la Arusha Mariam Mshana na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango,Takwimu na Ufuatiliaji, Innocent Maduhu.


Hukumu hiyo imetolewa leo Agosti 31,2023 na Hakimu Mkazi, Saraphina Nsana wa mahakama ya hakimu mkazi Arusha aliyekuwa akisikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi  namba 5 /2022.


Hakimu Nsana amesema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili imejiridhisha pasipo shaka na  ushahidi wa upande wa mashtaka na kuwatia hatiani.


"Kwa kuzingatia ushahidi huo na kwamba kama washtakiwa wanarekodi ya makosa ya jinai ,na utegemezi wa familia mahakama inawahukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja na iwapo kama hamjaridhika na adhabu hiyo nafasi ya kukata rufaa ipo wazi".


Hata hivyo bado Dk. Pima na wenzake wanakabiliwa na kesi nyingine mbali na kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi ,namba 5/ 2022. 


Awali,Katika kesi hiyo namba 5/2022 Dk Pima na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashitaka sita  ya uhujumu uchumi na  mawili ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.


Mashitaka mengine ni kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri ,ufujaji na ubadhirifu ambayo Dk Pima na wenzake walisomewa Juni 21, mwaka huu mbele ya hakimu Mkazi wa mahakama hiyo , Bittony Mwakisu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022.

Dk Pima na wenzake kwani Juni 17, 2022 walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa nane ya ufujaji wa mali ya umma na kughushi nyaraka katika kesi mbili za uhujumu uchumi.


Ambapo kesi hiyo inawakabili washitakiwa watano wakiwemo   waliokuwa wachumi katika jiji hilo, Nuru Ginana na Alex Daniel.


Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022, iliyosemwa Juni 21, 2022 huu washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita ambapo kosa la kwanza linalowakabili ni ufujaji na ubadhirifu wa Sh103 milioni, kosa la pili na la tatu ni kutumia nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri.



Kosa la tano linalomkabili Maduhu peke yake  ni utakatishaji fedha huku la sita likiwa ni la utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote watatu.


Akiwasomea mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Charles Kagilwa alieleza mahakamani hapo kuwa shitaka la kwanza linawakabili washitakiwa wote watatu ambapo ni la ufujaji na ubadhirifu kinyume cha sheria ya uhujumi uchumi na sheria za kuzuia na kupambana na rushwa.


lidai mahakamani hapo kuwa  washitakiwa wote katika tarehe tofauti kati ya Machi 28, 2022 na April 14,2022 huu wakiwa wameajiriwa wa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI wakiwa kama mkurugenzi wa halmashauri jiji la Arusha, Mkuu wa Idara ya Fedha na  mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango waliweza kutumia milioni 103 ambazo zimekuja kwao kupitia nafasi zao.


Wakili wa serikali Kagilwa alieleza kuwa  shitaka la pili linawakabili washitakawa wote watatu ambapo wanadaiwa  walituma  nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri wao kinyume cha sheria za kuzuia na kupambana na rushwa na uhujumi uchumi.


Alidai kuwa mnamo tarehe 27 machi mwaka huu katika jiji wilaya na mkoa wa Arusha washitakuwa hao  wakiwa wameajirikiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutumia nyaraka, dokezo walitoa taarifa zao uongo kuonyesha kwamba Maduhu aliomba masurufu kwa ajili ya kununua mchanga moramu shilingi milioni 103 kwa nia ya kutengeneza matofali wakati wakijua ni uongo.

Katika kosa la tatu ilidaiwa mahakamani hapo kuwa  washitakiwa wote walitumia nyaraka kumdanganya mwajiri wao ambapo mnamo tarehe 27 machi, huu katika jiji wilaya na mkoa wa arusha kwa nafasi ya mkurugenzi  wa jiji la Arusha, Mkuu wa kitengo cha fedha na Mkuu wa  kitengo cha mipango na uchumi waliweza kumdanganya mwajiri.


lidaiwa waliandaa maombi ya masurufu ya safari zikiwa na taarifa za udanganyifu wakijifanya bwana, Innocent Maduhu ambaye ni mchumi aliomba malipo ya kiwanda cha ujenzi wa kiwanda cha matofali kiasi  cha shilingi milioni 103.


Ilidaiwa katika shitaka la nne washitakiwa hao walitumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri wao ambapo mnamo Aprili 28, mwaka huu walijifanya kuonyesha Maduhu alirejesha fedha za ununuaji 'material' kwa ajili ya ununuaji wa vifaa vya kujenga kiwanda cha matofali wakati wakijua si kweli.

Shitaka la tano la utakatishaji fedha linalomkabili, Madihu peke yake ambapo anadaiwa  mnamo Aprili , mwaka huu alijipatia gari yenye namba za usajili T 844 DYY aina ya Subaru Forester kwa fedha ambazo ni zao la uhalifu la  kumdanganya mwajiri wake

Wakili Kagilwa alisoma shitaka la sita la utakatishaji fedha linalowakabili washitakiwa wote watatu   wanadaiwa kuwa katika terehe tofauti kati ya Machi 23, mwaka huu na Mei 25, mwaka huu walijipatia fedha taslim sh milioni 103 wakati wakijua fedha hizo zilitokana na zao la uhalifu la kumdanganya mwajiri wao.



Awali Juni 17,2022, Dk Pima na wenzake wanne walifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Bittony Mwakisu, wakikabiliwa na makosa nane katika kesi mbili za uhujumu uchumi.




Dk Pima na wenzake watatu Innocent Maduhu (aliyekuwa mchumi wa Jiji), Nuru Ginana (mchumi), Alex Daniel (mchumi), 




Hata hivyo mshitakiwa mwingine ni Mshana ambaye alikuwa Mwekahazina wa Jiji hilo  hakuwepo mahakamani hapo, hivyo upande wa Jamhuri ukaomba  mahakama kutoa hati ya wito na kukamatwa kwa mshitakiwa huyo ambaye ni wa pili katika kesi zote.


Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Akisa Mhando na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Hamidu Simbano huku Dk Pima na Maduhu wakiwakilishwa na Wakili Valintine Nyalu.


Katika kesi ya kwanza,  Dk Pima, Mariam, Maduhu na Ginana wanakabiliwa na mashitaka manne ambayo ni ufujaji na ubadhirifu huku makosa mengine yakiwa ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.


Aidha washitakiwa hao wataendelea kukaa mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ambapo kila mmoja anapaswa kuwa na wadhamini wawili watakaoweka kiasi cha shilingi 32 milioni au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ambapo hawakuweza kukamilisha masharti hayo.




Awali katika kesi ya kwanza ya uhujumu uchumi namba 3/2022 inawakabili Dk Pima,Mariam,Maduhu na Ginana wanakabiliwa na mashitaka manne ambayo ni ufujaji na ubadhirifu huku makosa mengine yakiwa ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.


Kosa la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu ambapo kwa pamoja wanadaiwa kati ya Aprili 14 hadi 16 mwaka huu,katika wilaya na Mkoa wa Arusha wakiwa waajiriwa wa serikali,walitenda  kosa la ufujaji na ubadhirifu wa fedha  Sh67 milioni.


Shitaka la pili ni matumizi ya nyaraka kwa malengo la kumdanganya mwajiri ambapo wanadaiwa kutumia nyaraka iliyokuwa na kichwa cha habari dokezo lenye maelezo kuwa Nuru amenunua na kusambaza moramu yenye thamani ya Sh65 milioni kwa ajili ya Soko la Samunge huku wakijua nyaraka hiyo siyo ya kweli na wakimdanganya mwajiri.


Shitaka la tatu ilidaiwa kuwa ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri,ambapo wanadaiwa Aprili 14,2022 wakiwa na nia ovu walitumia nyaraka ya maombi ya masurufu(safari) ikionyesha Nuri amenunua na kusambaza moramu ya Sh65 milioni huku wakijua wanamdanganya mwajiri wao.


Alitaja shitaka la nne kuwa ni matumizi mabaya ya nyaraka kwa malengo ya kumdangaya mwajiri ambapo wanadaiwa Aprili 28,mwaka huu wakiwa na nia ovu ua kumdanganya mwajiri walitumia nyaraka ya marejesho ya masurufu ikionyesha Nuru amefanya marejesho ya Sh65 milioni ikiwa ni malipo maalum ya  kazi za nje ya kituo chake cha kazi.


Katika kesi ya pili ya uhujumu uchumi namba 4/2022 washitakiwa ni Dk Pima,Mariam,Maduhu na Daniel wanakabiliwa na makosa manne ikiwemo la ufujaji na ubadhirifu pamoja na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.


Akiwasomea mashtaka hayo,Wakili Akisa alidai kosa la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu ambapo kati ya Aprili 14 hadi 16,mwaka huu wakiwa waajiriwa wa serikali kwa pamoja na kwa nia ovu walifanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kwa matumizi yao binafsi Sh65 milioni iliyokuwa imetolewa kwa ajili ya matumizi ya umma.


Alitaja shitaka la pili katika kesi hiyo kuwa ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri kinyume na sheria ambapo wanadaiwa Aprili 14,mwaka huu walimdanganya mwajiri kupitia nyaraka yenye dokezo lililokuwa linahusiana na shughuli za kila siku za mwajiri ambapo walidanganya Daniel amenunua na kusambaza moramu yenye thamani ya Sh65 milioni huku wakijua kwa kufanya hivyo ni kumdanganywa mwajiri.


Alidai shitaka la tatu kuwa ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri ambapo,Aprili 14,mwaka juu wakiwa na nia ovu walitumia nyaraka ya maombi ya masurufu,ikiwa na maelezo ya uongo yakionyesha Daniel amesambaza moramu kwa ajili ya matengenezo ya barabara hivyo adai Shilingi 65 milioni huku wakijua wanamdanganya mwajiri wao.

Shitaka la nne ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri ambapo wanadaiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu kupitia nyaraka iliyokuwa na kichwa cha habari marejesho ya masurufu iliyoandikwa Aprili 26,2022 iliyohusiana na shughuli za mwajiri.




Alidai nyaraka hiyo ilikuwa na maelezo ya udanganyifu kuwa Alex anafanya marejesho ya Shilingi 65 milioni ikiwa ni matumizi ya kusambaza moramu katika taasisi mbalimbali za serikali kwa ajili ya kutengeneza barabara huku wakijua kwa kufanya hivyo wanamdanganya mwajiri.


Aidha washitakiwa hao walikana kutenda makosa hayo ambapo Mahakama ilitoa masharti ya dhamana kuwa kila mshitakiwa awe na wadhamini wawili kila mmoja adeposit Sh32.5 milioni au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani kama hiyo.


Washitakiwa hao walitakiwa kutokusafiri nje ya mipaka ya  Tanzania na kuwasilisha hati zao sa kusafiria ambapo pia walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kuwa wataendelea kukaa mahabusu hadi watakapotimiza masharti hayo.


Mashauri haya yamekuja baada ya Mei 24,2022, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwasimamisha kazi maafisa sita wa Jiji hilo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za jiji na tuhuma za kughushi nyaraka.