Showing posts with label Muziki. Show all posts
Showing posts with label Muziki. Show all posts

 


Tuzo za muziki za Trace Afrika, zilizofanyika kwa mara ya kwanza Visiwani Zanzibar, Tanzania, usiku wa kuamkia leo, zilikatizwa ghafla baada ya maji kujaa karibu na jukwaa, hali iliyosababisha sintofahamu kwa mashabiki na wageni waalikwa.


Tamasha hilo lilianza kwa kuchelewa kutokana na upepo mkali na mawimbi, na waandaaji walilazimika kusogeza muda wa kuanza hadi saa 4 usiku. Msanii wa Tanzania, Marioo, alikuwa wa kwanza kutumbuiza kabla ya wasanii wengine kuendelea na burudani. Hata hivyo, shughuli hiyo ilikatizwa ghafla mnamo saa 9:20 usiku, ikiwa bado katika hatua za mwanzo za kutangaza washindi wa tuzo hizo.

Ingawa sababu rasmi haikutangazwa jukwaani, tukio hilo lilizua minong’ono na malalamiko kutoka kwa waliohudhuria. Kabla ya kusitishwa, msanii Rema kutoka Nigeria alitangazwa kuwa Msanii Bora wa Kiume wa Mwaka na pia kushinda Tuzo ya Albamu Bora kupitia albamu yake Heis.


Tuzo zingine zilimwendea P. Prime kutoka Nigeria kama Mtayarishaji Bora wa Muziki, Josey kutoka Ivory Coast kama Msanii Bora wa Nchi zinazozungumza Kifaransa, Joe Dwet File (Ufaransa/Haiti) kama Msanii Bora wa Diaspora, na Duquesa kutoka Brazil.


Licha ya changamoto hiyo, tamasha hilo lilishuhudia burudani ya nguvu kutoka kwa wasanii wakubwa wa Afrika, akiwemo Diamond Platnumz wa Tanzania, Harmonize, na Bien wa Kenya.

MSANII wa muziki wa hip hop, Ibrahim Mussa, ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watatu wamepatikana wakiwa wazima wa afya huku bado kukiwa na maswali mengi yanayohitaji majibu juu ya kutoweka kwao kwa takriban siku tatu.
Msanii Roma

Msanii huyo akiwa na wenzake, Monii Central Zone, Bin Laden pamoja na Imma ambaye ni msaidizi wa kazi katika studio za Tongwe Records walitekwa na watu wasiojulikana na kushikiliwa kwa siku tatu bila ya taarifa zozote.
Hali hiyo iliibua taharuki kwa wasanii na familia zao na hasa mke wa Roma aitwae Nancy ambae amekuwa akizunguka kwenye vituo kadhaa vya Polisi kumsaka mumewe. Jana taarifa za kuonekana kwa msanii huyo akiwa na wenzake hao zilipatikana takriban saa nane mchana ambapo walishikiliwa kwa zaidi ya saa tano katika kituo cha Polisi Oysterbay.
Gazeti hili lilitumia zaidi ya saa sita kumngoja msanii huyo na wenzake kwa lengo la kujua ni nini kiliwakuta lakini hata hivyo hawakupata nafasi ya kuzungumza nao kituoni hapo.
Saa moja usiku aliwasili wakili wao Peter Kibatala ambae aliingia moja kwa moja kituoni humo kuzungumza na wasanii hao. Baada ya takribani dakika 10 walitolewa wasanii hao bila ya kuonana na waandishi wa habari na wakapelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Mwananyamala kufanyiwa vipimo.
Licha ya vyombo mbalimbali vya habari ‘kupiga kambi’ kituoni hapo tangu mchana lakini Polisi walishindwa kuzungumzia hilo.