Tanzania imeweka wazi mikakati yake mikubwa ya muda mrefu ambapo inalenga kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika na kuingia kwenye orodha ya nchi 10 bora duniani kwa uzalishaji wa chakula ifikapo mwaka 2050.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akitoa mada kuu kwenye mjadala kuhusu Mustakabali wa Kilimo barani Afrika katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue) unaoendelea jijini Des Moines, Marekani.
Mambo Makuu Yaliyobainishwa na Waziri Mkuu:
- Ongezeko la Bajeti: Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kwa kasi kubwa kutoka shilingi bilioni 294 (2021/2022) hadi kufikia shilingi trilioni 1.241 katika mwaka wa fedha wa 2025/2026.
- Utoshelevu wa Chakula: Kutokana na uwekezaji huo, Tanzania imefikia utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130, jambo linaloifanya nchi kuwa na ziada kwa ajili ya soko la kikanda na kimataifa.
- Kukua kwa Mauzo ya Nje: Mauzo ya nje ya mazao ya kilimo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 (2021/2022) hadi kufikia dola bilioni 3.7 (2024/2025).
- Mhimili wa Uchumi: Kilimo kinachangia asilimia 24.6 ya Pato la Taifa (GDP), kinaajiri asilimia 65 ya nguvu kazi nchini, na kinazalisha takriban asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje.
Katika mjadala huo, wadau mbalimbali akiwemo Mwanzilishi na Mhariri Mkuu wa Jarida la Chakula la Afrika, Prof. Ruth Oniang’o, wameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa inayopiga, hususan kupitia programu bunifu kama 'Jenga Kesho Bora' (BBT), uboreshaji wa miundombinu, na ufanisi wa maafisa ugani.
Waziri Mkuu ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kuwekeza kwa wakulima, vijana, wanawake, na kwenye sayansi ili kujenga mifumo thabiti ya chakula kabla njaa haijatushinda.






0 Comments:
Post a Comment