Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imezindua mashindano bab kubwa ya mchezo wa mpira wa miguu yatakayojulikana Kama _Rhino Cup_ kutoa hamasa kwa jamii ya tarafa ya Ngorongoro  yenye vijiji 25 na Kata 11  kutoshana nguvu katika mchezo wa kabumbu.



Mashindano hayo yamefunguliwa jumanne hii katika viwanja vya shule ya msingi Makao Ngorongoro na kocha wa zamani wa timu ya taifa (Taifa Stars ) na Yanga Charles Boniface Mkwasa.



Akifungua mashindano hayo Mkwasa amewataka vijana wa tarafa ya Ngorongoro kutumia michezo Kama fursa ya ajira na kujenga afya zilizo bora na kuhimiza uhifadhi shirikishi kupitia michezo.



Naibu kamishna wa Uhifadhi NCAA Aidan Makalla amesema Mamlaka imeamua kuanzisha kombe hilo litakalochezwa kila mwaka ili kutoa hamasa ya mchezo wa mpira wa miguu ndani ya tarafa ya Ngorongoro na kuhamasisha jamii juu ya ulinzi wa faru na rasilimali mbalimbali zilizopo ndani ya hifadhi.


Mashindano hayo yatashirikisha kata 11 za tarafa ya Ngorongoro na bingwa wa mashindano hayo pamoja na zawadi nyingine ataenda kushuhudia mtanange wa ligi kuu baina ya Simba na Yanga kwa msimu wa mwaka huu.

 


Na Mwandishi wetu, Ngorongoro 


Hayawi hayawi sasa yamekuwa, tarehe 22 Septemba, 2026 wahifadhi Duniani kote wanaungana kuadhimisha siku ya Faru ambapo Hifadhi ya Ngorongoro inaadhimisha siku hii huku ikikumbuka jinsi faru Vicky alivyomchanganya faru Telele mpaka akamwacha faru John.



Faru Vicky alikuwa na mahusiano na faru John, lakini tabia ya faru John ilikuwa ni ukorofi uliopitiliza na hasa kupigana na madume ya faru wenzie na kujipa utawala wa majike mengi.


Siku moja faru Vicky akiwa na faru Telele alitokea faru John na kuanzisha vurugu za kumpiga faru Telele, hata hivyo faru Telele hakutaka kupambana na faru John alitulia kimya kama maji ya mtungini.



Baada ya vurugu hizo faru Telele aliamua kuondoka eneo la tukio na kumuacha faru Vicky akiwa na na faru John, kwa bahati mbaya faru John akapitiwa na usingizi.


Faru Vicky alipoona faru John amelala hoi alimtoroka na kwenda kwa Faru Telele na kisha kuanzisha mahusiano na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa enzi kwa uhusiano wa faru Vicky na faru John.



Faru Telele anapendwa na majike ya faru kutokana na utulivu na upole wake kwani yeye kwenye mahusiano hatumii nguvu zaidi ya nyama ya ulimi, kubembeleza, kudekeza na upole wake.

 


Matukio ya kuvutia kama haya ndiyo yaliwavutia wageni wakiwemo wanafunzi wa shule ya sekondari Embaraway iliyopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kufika hifadhi ya Ngorongoro kujifunza shughuli za uhifadhi wa Faru.


Wakiwa katika Bonde la Ngorongoro , wanafunzi hao walipata fursa ya kujionea uhifadhi wa wanyama mbalimbali na kujifunza uhifadhi wa Faru, tabia, mwenendo na umuhimu wake kiuhifadhi, elimu, utafiti na utalii.



Afisa Uhifadhi Mwandamizi na Mratibu wa Faru Ngorongoro Deogratius Maige alisema kuwa, kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi wa faru imekuwa ni sehemu ya juhudi za Mamlaka hiyo katika kuimarisha uelewa na ushiriki wa jamii katika uhifadhi, na kuhakikisha kuwa wanajenga kizazi cha baadae cha wahifadhi bora. 



Kauli mbiu ya Siku ya Faru Duniani ni “Keep the Five Alive”



SINGIDA: Watu 12, wakiwemo askari polisi watano na mahabusu, wamepoteza maisha kufuatia ajali mbaya iliyotokea leo asubuhi katika Mlima wa Sekenke, Wilayani Iramba, Mkoa wa Singida.

Ajali hiyo imehusisha lori la mafuta lililoligonga gari dogo la Jeshi la Polisi lililokuwa likisafiri kutoka Shelui kuelekea Kiomboi.

Akithibitisha kupokelewa kwa miili na majeruhi, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Dkt. Peter Luhega Janga, ameeleza kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi imepokea jumla ya maiti 12 (wanawake wawili na wanaume kumi) pamoja na majeruhi wawili wanaondelea kupata matibabu.

Askari Wote Watano na Mahabusu Wapoteza Maisha

Kwa mujibu wa taarifa za awali, gari la Polisi lilikuwa limebeba askari watano na mahabusu waliokuwa wakipelekwa mahakamani Kiomboi. Kwa masikitiko makubwa, askari wote watano pamoja na mahabusu waliokuwa ndani ya gari hilo walifariki dunia papo hapo kutokana na kishindo cha mgongano huo.

Dereva wa lori hilo la mafuta, ambaye ni raia wa nchi jirani ya Rwanda, pamoja na tingo wake, waliokolewa na wananchi na sasa hivi wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kiomboi, ambapo Dkt. Janga amethibitisha kuwa hali zao zinaendelea vizuri.

Miili Kuanza Kutambuliwa na Ndugu

Zoezi la utambuzi wa miili ya raia na mahabusu waliopoteza maisha linaendelea. Hadi sasa, baadhi ya waliofariki wametambuliwa na ndugu zao kuwa ni:

Hassan Onesmo Mbutu (26): Mkazi wa Kijiji cha Doromoni, Kata ya Tulya.

Vivian Saidi (60): Mkazi wa Kijiji cha Meli, Kata ya Old Kiomboi.

Timoth Lazaro Kimaro: Mkazi wa Doromoni.

Majonzi ya Mzazi: "Alienda Kama Mdhamini wa Laki na Nusu"

Kifo cha Hassan Onesmo Mbutu kimeacha simanzi nzito. Baba mzazi wa marehemu, Kapteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Onesmo Mbutu, ameeleza kwa majonzi makubwa jinsi mwanawe alivyochukuliwa na polisi kwenda mahakamani kwa makosa ya mkopo wa rafiki yake.

"Mimi nashangaa kuhusu kijana wangu ambaye inasemekana alimkopea rafiki yake fedha ya shilingi laki moja na nusu, na alikuwa anaenda kuelewana na mhusika ili amlipe. Lakini alishtukia yuko mikononi mwa Polisi na kuelezwa anapelekwa Mahakamani Kiomboi," alieleza Kapteni Mbutu huku akilengalenga machozi.

 

Endelea kufuatilia ukurasa wetu kwa taarifa rasmi zaidi kutoka kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida kuhusu majina ya askari waliopoteza maisha na taratibu nyingine zilizofuata.

 



Makamishna wasaidizi waandamizi wa Uhifadhi  wanawake kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wapo nchini Indonesia kushiriki mkutano wa mtandao wa wanawake maafisa waandamizi wa Polisi na vyombo vya vingine vya usalama unaofanyika nchini humo.


Wakiongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi -Rasilimali watu na Utawsla Salma Chisonga makamishna hao wanatarajia kutoa  uzoefu wao katika masuala ya ulinzi, uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.


Mkutano huo wa siku tano unawaweka pamoja  wanawake kutoka vyombo vya usalama wa nchi mbalimbali duniani kujadili fursa na changamoto katika vyombo vya usalama na vinavyolinda rasilimali za nchi.




Wilaya ya Ngorongoro ipo katika hatua za mwisho ya mapitio na kupitisha mkakati mpya wa miaka mitano unaodhamiria kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kasi ya maendeleo unaokwenda sambamba dira ya taifa ya maendeleo 2025-2050.



Akifungua kikao maalum cha kupitia mkakati huo mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Brigedia Jenerali Wilson Sakulo amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kutumia fursa hiyo kwa kupanga vipaumbele vitakavyogusa maisha ya wananchi.



“Leo tumekutana hapa kupanga mipango yetu kwa miaka mitano, hakikisheni mnapanga vipaumbele vinavyopimika kwa kuangalia maslahi ya wananchi wa wilaya hii ili waweze kupata huduma bora za kijamii, miundombinu na kuboresha shughuli zao za kiuchumi”,alisema Brigedia Jenerali Sakulo.


Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Manja Sironga Yaile aliipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo kutokana na kushiriki kikamilifu katika kuchangia mipango mbalimbali ya kijamii ya Tarafa ya Ngorongoro na wilaya hiyo.



Wakichangia kuhusu mpango mkakati huo baadhi ya madiwani walisisitiza umuhimu wa kujikita katika ujenzi wa barabara,malisho, maji na uimarishwaji wa huduma za kijamii.






 


Na Mwandishi Wetu, Tanga.


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imewezesha ziara ya mafunzo kwa Viongozi wa Mila (Malaigwanani), Wazee Mashuhuri na kinamama  33 kutoka kata 11 za tarafa ya Ngorongoro kutembelea kiwanda cha kuzalisha na kuchakata mazao ya maziwa cha Tanga Fresh, kilichopo jijini Tanga.



Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Malaigwanani Ngorongoro na Diwani wa Kata ya Olbalbal, Mhe. Metui Shaudo alisema, ziara hiyo imewapa fursa ya kuona kwa vitendo hatua mbalimbali zinazofanyika katika uchakataji wa maziwa, kuanzia ukusanyaji wa maziwa, uzalishaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali zilizoongezewa thamani.



 “Tumetembelea kiwanda hiki kujifunza na kuona mambo mengi ambayo tunaweza kuyatumia tunaporudi Ngorongoro, tumeona kuwa maziwa yanaweza kuwa na thamani kubwa zaidi yakichakatwa vizuri badala ya kuuzwa yakiwa ghafi kama ambavyo mara nyingi inafanyika kwa wananchi wetu, baada ya ziara hii tutapelekeaa elimu hii kwa wananchi wenzetu ili kuwaongezea tija na kipato kinachotokana na ufugaji,” alisema  Shaudo 


Kina mama walioshiriki ziara hiyo  wameelezea kufurahishwa na manufaa yanayotokana na  mifugo na kuwaongezea ujuzi wa uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya mifugo na kuahidi kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa Ngorongoro ili waendelee kujikwamua kiuchumi.


Kiongozi wa mila kutoka kata ya kakesio Ole Kotika ameeleza kuwa ziara hiyo  inaendelea kuimarisha mahusiano mazuri kati ya hifadhi ya Ngorongoro na wananchi hasa kuwaongezea fursa ya kujifunza shughuli za ufugaji wa kisasa, usindikaji wa bidhaa za maziwa zenye ubora na kuongeza mnyororo wa thamani ambao unasaidia kukuza uchumi wa wananchi.



Ziara ya viongozi hao ni sehemu ya jitihada za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii ya kuwawezesha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kupata ujuzi na uzoefu unaoweza kuboresha shughuli zao za kiuchumi na kuongeza thamani ya rasilimali walizonazo.

 



Na Mwandishi wetu, Ngorongoro 


Ilinenwa “KATIKA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA”, ndivyo walivyofanya waumini  wa Parokia ya Mt. Petro Masanza  Kona mkoani Simiyu ambapo baada ya kulijenga kanisa kwa umoja wao waliamua kutembelea  hifadhi ya Ngorongoro kujionea uwezo wa mwenyezi Mungu katika uumbaji wa ulimwengu na vilivyomo.



Ziara hiyo imewashirikisha waumini 50 kutoka parokiani hapo wakiongozwa na  mapadri wanne na frateli mmoja ikiwa na lengo la kuwawezesha waumini kufanya utalii wa ndani na kujifunza juu ya urithi wa dunia ambao  upo ndani kasoko ya Ngorongoro.



Akiongoza ziara hiyo,Rev Fr. Furaha James ambaye ni Paroko wa Parokia ya Masanza  alisema kwamba ziara hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa kwa kuwa wamepata fursa ya kujifunza historia, utamaduni, mazingira na vivutio vya asili vilivyopo nchini.


“Tumekuja hapa kwa ajili ya kujifunza na kuona kile ambacho Mungu ametujalia katika nchi yetu. Naamini kuwa waumini wetu waliotembelea hapa wameongeza uelewa na watakuwa mabalozi wa kutunza na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwetu” alisema Fr. Furaha 



Aidha kwa upande wa WAWATA, akiwemo  Flora Nkolongo walieleza kufurahishwa na ziara hiyo, wakisema kuwa imewapa nafasi ya kujifunza na kuwaona wanyama mbalimbali kama Simba, Faru, Nyati, Tembo na wengine wengi ambao ni mara yao ya kwanza kuwaona kwa karibu.



Ziara hiyo ilihitimishwa  kwa kutembelea  makumbushi ya Urithi ambako walipata historia ya ardhi ya Ngorongoro, volkano, wanyamapori, maendeleo ya binadamu na tamaduni za jamii zinazozunguka eneo hilo ambao ni Wamasai, Wahadzabe, Wairaqw na Wadatoga na waumini hao kuhitimisha ziara yao kwa kuamini kuwa NGORONGORO NI NYUMBANI KWA KILA KIUMBE.









 


Mahakama ya Wilaya ya Arusha  imetoa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa mtuhumiwa mmoja na kuwaachia wawili kwa masharti kufuatia makubaliano ya kukiri makosa ya kutengeneza na kukutwa na pombe bandia pamoja na stamp feki za TRA. 



Adhabu hizo zimetolewa kufuatia makubaliano ya maridhiano ya kukiri makosa (Plea Bargain) kati ya washtakiwa hao na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ambapo hatua hii imekuja baada ya washtakiwa wote kwa pamoja kukamilisha malipo ya faini ya Shilingi Milioni Tano (Tsh 5,000,000) kwa mkupuo mmoja kwenda kwenye akaunti ya DPP.




Katika uamuzi huo, Mahakama pia imeamuru kuteketezwa kwa vielelezo zikiwemo stamp feki za kielektroniki za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na pombe feki zilizokamatwa, huku ikitoa amri ya washtakiwa kurejeshewa magari yao aina ya Toyota IST yenye namba za usajili T 628 DDE na Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili T 308 EJU. 





Uamuzi huo umetolewa leo Septemba 17, 2026, na Hakimu Mkazi Devotha Msofe wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha aliyekuwa akisikiliza shauri hilo la jinai namba 14535/2026, 



Washtakiwa hao waliotiwa hatiani ni Thomas Godfrey Temu (35) aliyepata kifungo cha mwaka mmoja jela, pamoja na Sara Marko Laizer (22) na Lilian Godfrey Temu (47) ambao wameachiwa kwa masharti ya kutorudia makosa ndani ya mwaka mmoja.

Awali, Wakili wa Serikali Belinda Rwakatare aliwasilisha mahakamani hapo mkataba huo wa makubaliano baina ya washtakiwa na DPP ambapo baada ya mkataba kupokelewa, upande wa mashtaka ulibadili hati ya zamani na kuwasilisha hati mpya ya mashtaka yenye makosa matatu ambapo washtakiwa waliyasomewa upya na kuyakubali yote.


 Katika shtaka la kwanza, Sara na Thomas wanadaiwa kukutwa na rola tatu za stamp feki za TRA za kielektroniki za kodi (ETS) mnamo Machi 23, 2026, maeneo ya Lolovono Sokoni 1 jijini Arusha, ambapo shtaka la pili linawakabili Lilian na Thomas ambapo walikutwa na pombe feki, na shtaka la tatu ni kufanya biashara ya kutengeneza pombe bila kuwa na leseni.


Mchakato wa kutoa adhabu ulifanya mahakama ihamie kwa muda kwenye ghala (warehouse) la Mamlaka ya Mapato Arusha ili kuangalia vielelezo vinavyoshikiliwa ambavyo vinapaswa kuteketezwa pamoja na magari yanayopaswa kurejeshwa kwa washtakiwa.



Akiongea mara baada ya uamuzi huo, Meneja Upelelezi wa Kodi wa TRA Kanda ya Kaskazini, Thoddy Beanga aliwaonya wananchi kutofanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kwani vinalikosesha Taifa mapato na kuathiri afya za walaji.

"Ni vinywaji ambavyo vinazalishwa kinyume cha utaratibu, hivyo vinaathiri nguvu kazi ya nchi, kodi, na hata afya za wanywaji ambao ni wananchi," alisema Beanga huku akiwataka wananchi kutoa taarifa wanapowabaini watu wanaofanya vitendo hivyo mitaani.


Aliongeza kuwa washtakiwa walikuwa wakitengeneza pombe bila kuwa na leseni kinyume na sheria za nchi lakini pia wakifungasha chapa za makampuni mbalimbali, na alihitimisha kwa kusema kuwa ingawa wahalifu wana mbinu nyingi, mamlaka inajitahidi kuwa mbele yao kuwadhibiti na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria 


Hatua hiyo imechukuliwa ili kukomesha vitendo vya ukwepaji kodi, uhujumu uchumi, na uingizaji wa bidhaa hatari sokoni zinazohatarisha afya za walaji.





 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, ameeleza kutoridhishwa kwake na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu mkoani Lindi inayotekelezwa na kampuni ya KIKIM Contractors Limited ikishirikiana na mbia wake AMACO Enterprises. Miradi hiyo inayofadhiliwa kupitia Mradi wa Ustawishaji Miji Tanzania (TACTIC) inahusisha ujenzi wa barabara za kilomita 5.3, Stendi ya Mabasi Mitwero, na Soko Kuu la Matopeni.



Waziri Shemdoe alitoa kauli hiyo Septemba 15, 2026 baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi hiyo na kubaini kuwa utekelezaji wake umefikia asilimia 23 tu, huku kukiwa kumesalia miezi mitano pekee kabla ya muda wa mkataba kuisha.

Kufuatia kusuasua huko, Prof. Shemdoe amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Kighoma Malima, kuchukua hatua kali za kisheria na kimkataba dhidi ya wakandarasi hao ambao amewataja kama "wababaishaji."

 Maagizo Mazito ya Waziri:


* Mpango Kazi: Wakandarasi wanatakiwa kuwasilisha mpango mkakati wa kukamilisha mradi ifikapo Septemba 23, 2026.

* Mrejesho: Waziri anataka kupatiwa ripoti ya maendeleo ya mradi kila baada ya wiki mbili.

* Hatua za Mikataba: Mkuu wa Mkoa ametakiwa kusimamia kikamilifu masharti ya mkataba bila kufanya mchezo.



 Sababu za Kuchelewa kwa Mradi

Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Interconsult Ltd, Mhandisi Rashidi Abdallah, alitaja sababu za kusuasua kwa mradi huo kuwa ni pamoja na:


   1. Mkandarasi kutojipanga vyema kiutendaji.

   2. Ukosefu wa rasilimaliwatu (wafanyakazi) wa kutosha.

   3. Matumizi mabaya ya fedha za awali za mradi (advance payment).



Wakandarasi Wakiri Uzembe

Mmoja wa Wakurugenzi wa kampuni hizo, John Daniel, amekiri wazi kuwepo kwa uzembe upande wao. Hata hivyo, ameahidi kuwa wamejipanga kufanya kazi usiku na mchana kufidia muda uliopotea na amemwomba Mkuu wa Mkoa kuwawekea malengo ya muda mfupi.



Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, amesisitiza kuwa katika kikao chao atakachofanya nao, wakandarasi hao itabidi waridhie kutoa mkataba mdogo (sub-contract) kwa kampuni nyingine kama wataona hawana uwezo wa kumaliza kazi hiyo kwa wakati.

Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe alikagua pia miradi mingine ikiwemo ujenzi wa Daraja la Ng’uni (Nanganga), shule mpya ya msingi ya Kitandi, na Kituo cha Afya Chiola mkoani humo.