Showing posts with label Ajali. Show all posts
Showing posts with label Ajali. Show all posts



SINGIDA: Watu 12, wakiwemo askari polisi watano na mahabusu, wamepoteza maisha kufuatia ajali mbaya iliyotokea leo asubuhi katika Mlima wa Sekenke, Wilayani Iramba, Mkoa wa Singida.

Ajali hiyo imehusisha lori la mafuta lililoligonga gari dogo la Jeshi la Polisi lililokuwa likisafiri kutoka Shelui kuelekea Kiomboi.

Akithibitisha kupokelewa kwa miili na majeruhi, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Dkt. Peter Luhega Janga, ameeleza kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi imepokea jumla ya maiti 12 (wanawake wawili na wanaume kumi) pamoja na majeruhi wawili wanaondelea kupata matibabu.

Askari Wote Watano na Mahabusu Wapoteza Maisha

Kwa mujibu wa taarifa za awali, gari la Polisi lilikuwa limebeba askari watano na mahabusu waliokuwa wakipelekwa mahakamani Kiomboi. Kwa masikitiko makubwa, askari wote watano pamoja na mahabusu waliokuwa ndani ya gari hilo walifariki dunia papo hapo kutokana na kishindo cha mgongano huo.

Dereva wa lori hilo la mafuta, ambaye ni raia wa nchi jirani ya Rwanda, pamoja na tingo wake, waliokolewa na wananchi na sasa hivi wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kiomboi, ambapo Dkt. Janga amethibitisha kuwa hali zao zinaendelea vizuri.

Miili Kuanza Kutambuliwa na Ndugu

Zoezi la utambuzi wa miili ya raia na mahabusu waliopoteza maisha linaendelea. Hadi sasa, baadhi ya waliofariki wametambuliwa na ndugu zao kuwa ni:

Hassan Onesmo Mbutu (26): Mkazi wa Kijiji cha Doromoni, Kata ya Tulya.

Vivian Saidi (60): Mkazi wa Kijiji cha Meli, Kata ya Old Kiomboi.

Timoth Lazaro Kimaro: Mkazi wa Doromoni.

Majonzi ya Mzazi: "Alienda Kama Mdhamini wa Laki na Nusu"

Kifo cha Hassan Onesmo Mbutu kimeacha simanzi nzito. Baba mzazi wa marehemu, Kapteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Onesmo Mbutu, ameeleza kwa majonzi makubwa jinsi mwanawe alivyochukuliwa na polisi kwenda mahakamani kwa makosa ya mkopo wa rafiki yake.

"Mimi nashangaa kuhusu kijana wangu ambaye inasemekana alimkopea rafiki yake fedha ya shilingi laki moja na nusu, na alikuwa anaenda kuelewana na mhusika ili amlipe. Lakini alishtukia yuko mikononi mwa Polisi na kuelezwa anapelekwa Mahakamani Kiomboi," alieleza Kapteni Mbutu huku akilengalenga machozi.

 

Endelea kufuatilia ukurasa wetu kwa taarifa rasmi zaidi kutoka kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida kuhusu majina ya askari waliopoteza maisha na taratibu nyingine zilizofuata.

 


Watu tisa wamefariki dunia, wakiwemo wanafunzi wanne, huku wengine 16 wakijeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea leo asubuhi katika eneo la Kambi ya Nyasa, wilayani Chemba, mkoani Dodoma.

Ajali hiyo imehusisha basi la abiria aina ya Tata mali ya Kampuni ya Babuu Trans lenye namba za usajili T129 DVX na lori la mizigo aina ya Fuso lenye namba T907 EJZ.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka husika, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori, ambaye alielezwa kuwa alipoteza mwelekeo na kuingia upande wa basi, na kusababisha ajali hiyo mbaya.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwatembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema mkoa umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo.

“Ajali hii ilisababisha vifo vya watu watano papohapo na majeruhi 20. Wakati wakiendelea kupatiwa huduma, wanne kati ya majeruhi hao walifariki dunia wakiwa njiani kuhamishiwa hospitali ya rufani, na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kufikia watu tisa, huku majeruhi wakibaki 16,” amesema Senyamule.

Ameongeza kuwa kati ya majeruhi 16, watu tisa wamepelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma ambako wanaendelea kupatiwa matibabu, huku wengine saba wakihudumiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chemba.

Senyamule ametoa pole kwa familia za marehemu na wote walioathirika na ajali hiyo, sambamba na kuwashukuru wananchi, viongozi wa wilaya, Jeshi la Polisi na wataalamu wa afya kwa msaada waliotoa katika shughuli za uokoaji na utoaji wa huduma kwa majeruhi.

“Natoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao na kuwaombea majeruhi wapone haraka. Pia nawashukuru wananchi, viongozi, Jeshi la Polisi na wahudumu wa afya kwa ushirikiano na msaada walioutoa kwa haraka,” amesema.

Taarifa zaidi kuhusiana na ajali hiyo zitaendelea kutolewa na mamlaka husika kadri uchunguzi unavyoendelea.

 


Ajali ya ndege ya Air India 171 iliyotokea mnamo Juni 12 mwaka huu katika jiji la Ahmedabad, magharibi mwa India, imeendelea kugusa hisia za watu wengi baada ya ripoti ya awali ya uchunguzi kutolewa. 



Ripoti hiyo, iliyotolewa na Ofisi ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege ya India (AAIB), imeeleza kuwa swichi mbili za kudhibiti mafuta kwenye injini za ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ziligundulika kuwa zimezimwa, jambo lililosababisha injini zote mbili kupoteza nguvu muda mfupi baada ya ndege hiyo kuruka.



Kwa mujibu wa data kutoka visanduku vyeusi vya ndege hiyo—ambavyo vinarekodi sauti na taarifa za safari—marubani waligundua kuwa swichi hizo hazikuwa katika nafasi yake ya kawaida wakati ndege tayari ilikuwa imeanza kupaa. Mmoja wa marubani anasikika kwenye kinasa sauti akiuliza, “Kwanini ulibadilisha swichi?” na mwenzake akijibu, “Sikuzibadilisha.”

Swichi hizo ziliporudishwa katika hali yake ya kawaida, injini moja ilianza tena kujaribu kujijengea msukumo huku nyingine ikiwa bado haijapata nguvu kamili. Wakati huo, ndege tayari ilikuwa angani kwa chini ya sekunde 40 kabla ya kupoteza uwezo wa kuendelea kuruka, na kuanguka katika kitongoji kilichojaa watu jijini Ahmedabad. Takriban watu 260 walipoteza maisha katika ajali hiyo, wakiwemo watu 19 waliokuwa ardhini. 

Mtu mmoja pekee alinusrika, akifanya ajali hii kuwa miongoni mwa ajali mbaya zaidi katika historia ya usafiri wa anga nchini India.

Ripoti hiyo haikufafanua ni rubani gani kati ya wawili aliyetoa ujumbe wa dharura wa “Mayday, Mayday, Mayday” wala kutambua ni nani aliyetoa amri ya mwisho ya kugusa swichi hizo za mafuta. 


Vilevile, haijafikia hitimisho kuhusu iwapo swichi hizo zilibadilishwa kwa bahati mbaya, kwa makusudi, au kwa kosa la kiufundi.

Air India imethibitisha kuwa inashirikiana kwa ukaribu na mamlaka za India katika uchunguzi unaoendelea, lakini imekataa kutoa maoni zaidi hadi ripoti ya mwisho itakapotolewa. 


Kampuni ya Boeing, ambayo ndiyo watengenezaji wa ndege hiyo, imesema inatoa usaidizi kamili kwa Air India na wachunguzi, huku ikisisitiza kuwa ripoti ya awali haikutoa mapendekezo yoyote ya moja kwa moja yanayolenga ndege zake au injini za GE.

Licha ya hatua za kiuchunguzi kuendelea, familia za waathirika zimeeleza kuwa taarifa hiyo ya awali imezua maswali zaidi kuliko majibu. Mume wa Ayushi Christian, mmoja wa wahanga, alikuwa miongoni mwa waliopoteza maisha. 


Ayushi anasema, “Hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya waliohusika.” Ndugu wengine wamesema wanapata faraja kidogo kwa kujua kilichotokea, ingawa hilo halibadilishi huzuni yao. Shweta Parihar, ambaye alipoteza mumewe, anasema, “Sasa nini maana ya uchunguzi huo? Kila kitu kimeshaharibika.”

Ripoti ya awali imeeleza wazi kuwa haina lengo la kutoa hitimisho la mwisho, bali ni kutoa mwelekeo wa uchunguzi zaidi. Wataalamu wanasema kuwa kitendo cha swichi za mafuta kuzimwa kimeleta dharura ya kupitiwa upya kwa taratibu za kiusalama ndani ya ndege, hasa kuhusu ulinzi wa swichi muhimu zisizopaswa kuguswa kwa urahisi wakati wa hatua za maandalizi ya kuruka.

Ripoti kamili ya uchunguzi huo inatarajiwa kutolewa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Kwa sasa, maswali yanabaki juu ya nini hasa kilitokea kwenye chumba cha marubani cha ndege ya Air India 171, na je, ajali hii ingeweza kuepukika? Majibu ya maswali hayo yatakuwa ya msingi si tu kwa familia za waathirika, bali kwa mustakabali wa usalama wa anga duniani kote.





Watu kadhaa wanahofiwa kupoteza maisha na wengine 16 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali mbaya ya barabarani leo asubuhi, Jumamosi Juni 28, 2025, katika eneo la Sabasaba, kata ya Same, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.



Ajali hiyo imehusisha basi kubwa la Kampuni ya Channel One lililokuwa likitokea Moshi kuelekea Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitoka wilayani Same kwenda Moshi. Magari yote mawili yamewaka moto mara baada ya kugongana uso kwa uso, hali iliyosababisha taharuki na vifo vinavyohofiwa kuwa vingi.



Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi, amethibitisha ajali hiyo na kueleza kuwa juhudi za uokoaji zimefanikisha kuokoa watu 16 hadi sasa.



"Watu 16 wameokolewa katika ajali hii iliyohusisha basi kubwa na dogo, ambayo yaliwaka moto. Tunashukuru kwa ushirikiano wa haraka kutoka kwa wananchi na vyombo vya uokoaji," amesema Mkomagi.

Akiendelea kufafanua, Kamanda huyo amesema:
"Tupo njiani kuelekea eneo la tukio, lakini taarifa za awali ni kwamba basi la Kampuni ya Channel One lililokuwa likitokea Moshi kuelekea mkoani Tanga na Coaster iliyokuwa inatoka Same kuja Moshi Mjini yamegongana na kuwaka moto."

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa mamlaka zipo kazini kuhakikisha kila mtu anapokea msaada unaohitajika haraka iwezekanavyo.

"Tunaendelea na juhudi za uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na wananchi wa maeneo ya jirani. Lengo ni kuhakikisha wote waliokumbwa na mkasa huu wanapatiwa msaada wa haraka," amesema Kasilda.

Hadi sasa idadi kamili ya watu waliopoteza maisha haijajulikana, huku kazi ya kuzima moto, kutoa miili na kuokoa manusura ikiendelea. Wahanga waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu katika vituo vya afya vilivyo karibu na eneo la tukio.

Wananchi wametakiwa kuwa watulivu na kuepuka kukaribia eneo la tukio ili kurahisisha kazi ya uokoaji, huku wakihimizwa kutoa taarifa sahihi pekee kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Tukio hili limeacha simanzi kubwa kwa wakazi wa Kilimanjaro na wasafiri wanaotumia njia hiyo, huku uchunguzi wa chanzo halisi cha ajali ukiendelea kufanywa na Jeshi la Polisi.

  


Katika tukio la kushtua lililotokea Juni 17, 2025, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Muhammed Shaib Saleh (35), mkazi wa Mbuyuni, Pemba, amenusurika kufa baada ya kujirusha baharini akiwa ndani ya boti ya mwendo kasi ya Zan Fast Ferries. 


Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Bandari ya Mkoani, Pemba kuelekea Bandari ya Malindi, Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo lilitokea majira ya saa nane mchana, kijana huyo alijitupa baharini katika mkondo wa bahari ya Nungwi. Mabaharia wa boti hiyo walichukua hatua za haraka kwa kuzima injini na kurusha vifaa vya uokozi, hatua iliyochangia kumuokoa kijana huyo ndani ya dakika 10.

Nahodha wa boti hiyo, Muhamed Khamis, amesema:

"Tulipoona kijana amejirusha, tulizima injini mara moja na tukarusha vifaa vya uokozi, tukafanikiwa kumtoa majini akiwa hai."

Baadhi ya mashuhuda waliokuwemo ndani ya boti hiyo wamesema kuwa kabla ya tukio hilo, kijana huyo alikuwa akiulizia mara kwa mara kama wamefika Nungwi.

Rashid Sultani, mmoja wa mashuhuda, amesema:

"Kijana hakuwa anaonekana kama ana matatizo ya akili, sijui alipatwa na nini hadi akachukua uamuzi wa kujitupa baharini."

Baada ya kuokolewa, Muhammed alikabidhiwa kwa askari wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi, huku hali yake ikiripotiwa kuwa nzuri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Mtumwa Said, amesema:

"Uwepo wa vifaa vya kisasa vya uokozi umechangia kuokoa maisha ya kijana huyo."

Boti ya Zan Fast Ferries huondoka Pemba majira ya saa saba mchana na huchukua takribani saa tatu kufika Unguja, ikiwa ni moja ya njia muhimu za usafiri baharini kati ya visiwa hivyo viwili.

Chanzo: Nipashe Digital

 


Idadi ya vifo kutokana na ajali mbaya ya ndege ya Shirika la Ndege la India imeongezeka na kufikia watu 270, huku majeraha ya kihisia kwa familia za waathirika yakiwa bado yanaendelea kuongezeka. Ajali hiyo, ambayo sasa imetajwa kuwa miongoni mwa majanga mabaya zaidi ya ndege duniani katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ilitokea siku ya Alhamisi jioni katika jiji la Ahmedabad, magharibi mwa India.

Ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, iliyokuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Gatwick nchini Uingereza, ilianza kushuka kwa ghafla sekunde chache tu baada ya kuruka. Hatimaye, iligonga jengo la bweni la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Udaktari cha B.J., na kusababisha mlipuko mkubwa wa moto ambao uliiteketeza kabisa ndege hiyo pamoja na majengo ya karibu.

Miongoni mwa watu 242 waliokuwa ndani ya ndege hiyo, ni mtu mmoja tu aliyenusurika kwa miujiza, huku wengine wote wakithibitishwa kufariki dunia. "Tumepokea miili 270 kutoka eneo la tukio," alisema Dhaval Gameti, rais wa Chama cha Madaktari Wanafunzi wa chuo hicho, akizungumza na waandishi wa habari mbele ya hospitali kuu ya mji huo.

Familia nyingi zimerundikana nje ya hospitali, zikiwa zimechoka kwa majonzi na kusubiri kwa hamu kukabidhiwa miili ya wapendwa wao. Hata hivyo, miili mingi haijafahamika kirahisi kutokana na kiwango kikubwa cha moto kilichoteketeza miili hiyo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa uchunguzi wa vinasaba, sampuli za meno zinatumika kuwatambua marehemu. "Tayari tumeshakusanya rekodi za meno za wahanga 135," alisema Jaishankar Pillai, daktari wa uchunguzi wa meno, na kuongeza kuwa watafanikisha utambuzi kupitia picha za mionzi, rekodi za awali na taarifa binafsi kutoka kwa familia.

Serikali ya jimbo la Gujarat imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, huku uchunguzi wa kiufundi ukiwa umeanza ili kubaini chanzo cha ajali. Mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo imesema kuwa itashirikiana na wazalishaji wa ndege hiyo pamoja na wataalamu wa kimataifa katika uchunguzi huo.

Wakati familia nyingi zikiendelea na msiba mzito, baadhi yao wameelezea hasira juu ya kucheleweshwa kwa taratibu za utambuzi na kukabidhiwa kwa miili. "Tunaelewa kuwa hali ni ngumu, lakini tunahitaji haki na heshima kwa wapendwa wetu," alisema jamaa mmoja wa waathirika aliyezungumza kwa uchungu.

Tukio hili limeacha maswali mengi kuhusu usalama wa ndege, utayari wa dharura katika viwanja vya ndege, pamoja na hatua za serikali kukabiliana na majanga ya aina hii. Wakati wote wakisubiri majibu, taifa linaomboleza vifo vya raia wake waliopotea katika tukio hili la kusikitisha.




Watu saba wamepoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali mbaya iliyohusisha gari la kubebea wagonjwa (ambulance) na guta lililokuwa limebeba watu 22 waliokuwa wakielekea shambani. 

Ajali hiyo imetokea leo, Aprili 19, 2025, katika barabara ya Mafinga kuelekea Luganga, karibu na ofisi za Halmashauri ya Mji wa Mafinga, mkoani Iringa.

Kwa mujibu wa taarifa ya mashuhuda wa ajali hiyo, guta hilo lilikuwa limebeba watu wengi kupita uwezo wake, na lilipofika eneo la tukio, liligongana uso kwa uso na gari la wagonjwa aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili STM 7840, ambalo lilikuwa linatoka Luganga.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, alipofika katika Hospitali ya Mji wa Mafinga alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza masikitiko yake kufuatia vifo hivyo.

"Watu hawa walikuwa wanakwenda shamba kwa kutumia usafiri ambao ni hatarishi kwao. Natoa wito kwa wananchi kuepuka kutumia vyombo vya usafiri visivyo salama ili kulinda maisha yao," amesema Dkt. Salekwa.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Mafinga, Dkt. Victor Msafiri, amethibitisha kupokea miili ya watu saba na majeruhi 15.

"Majira ya saa kumi na mbili asubuhi tumepokea majeruhi 15 na miili 7 ya marehemu wa ajali hii mbaya. Baadhi ya majeruhi wapo katika hali mahututi na wanaendelea kupatiwa matibabu," amesema Dkt. Msafiri.

Ajali hiyo imesababisha taharuki kwa wakazi wa Mafinga huku vyombo vya usalama vikiendelea na uchunguzi kubaini chanzo kamili cha ajali. 

Wakati huo huo, viongozi wa serikali wamewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapotumia vyombo vya usafiri, hasa katika maeneo ya vijijini.

 




Tukio la kusikitisha limetokea wilayani Geita, ambapo watu watano wamejeruhiwa baada ya mtambo maarufu kama Bulldozer, mali ya mgodi wa Bucreef, kuacha njia na kugonga nyumba za makazi katika kitongoji cha Isingilo, kijiji cha Lwamugasa. Inadaiwa kuwa dereva wa mtambo huu alikuwa akikimbizwa kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa mafuta kutoka kwenye mgodi, jambo ambalo linadaiwa kuwa lilichochea tukio hili la ajali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwamugasa, Mwita Amos, alieleza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa nane usiku wa kuamkia Aprili 3, 2025. "Kaya tatu zimeathiriwa na tukio hili, na majeruhi watano wameshafikishwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita, wengine wamelazwa katika kituo cha afya Katoro," alisema Mwita.

Tukio hilo linahusisha mtambo wa Bulldozer, ambao ulitokea kwenye mgodi wa Bucreef na kugonga makazi ya watu. "Mtambo huu ulipita bila kuwa na mwendeshaji ndaji yake, na kupelekea uharibifu kwenye nyumba za watu," aliongeza Mwenyekiti.

Athuman Charles, mmoja wa manusura wa ajali hiyo, alielezea tukio hilo: "Kabla ya tukio, tulisikia muungurumo wa kitu kinapita, lakini kwa sababu tunaishi karibu na mgodi, tulihisi ni mitambo ya mgodi. Ghafla tulisikia kama kuna kitu kinadondoka, kisha tukaona nyumba moja imeanguka na watu wakiwa wanalia. Kuna mzee alikuwa anapiga yowe kutufahamisha kuwa nyumba iliyokuwa na watoto sita imeanguka."

Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba, alithibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea ili kubaini kiini cha ajali hiyo. "Taarifa za awali zinaeleza kuwa dereva wa mtambo huo alikuwa akijihusisha na wizi wa mafuta, na alikuwa na baadhi ya watu waliokuwa wananunua mafuta. Wawili tayari wameshakamatwa," alisema Komba.

Komba alifafanua zaidi kwamba walinzi wa mgodi waligundua kuna wizi unaendelea, hivyo walianza kumfuatilia mwendeshaji wa mtambo. "Dereva alijua kuwa ufuatiliaji unaendelea, ndipo alikimbia na kutelekeza mtambo. Mitambo hii ina uwezo wa kujiendesha yenyewe, na ukiwasha unaweza ukatoa funguo na likendelea," alisema Komba. "Ndio maana mashuhuda waliokuwepo walielezea kuwa mitambo hiyo iliendelea kuunguruma eneo la tukio."

Tukio hili linazua maswali kuhusu usalama wa mitambo na majukumu ya kampuni za migodi katika kuhakikisha kuwa mitambo yao inasimamiwa kwa ufanisi ili kuepusha madhara kwa wananchi wa maeneo ya karibu. Uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo kamili cha ajali na hatua stahiki zitakazochukuliwa.




Ajali mbaya imetokea leo asubuhi katika kijiji cha Mamba, Kata ya Msangeni, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, ambapo basi la Kampuni ya Mvungi lililokuwa likitokea Ugweno kuelekea Dar es Salaam lilipinduka na kutumbukia bondeni. 



Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu nane na majeruhi 31.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Mrakibu Msaidizi Jeremiah Mkomagi, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyeshindwa kulimudu gari wakati alipojaribu kukwepa gari dogo katika kona kali ya mlima. 



Alisema, “Basi lilikuwa likitokea Vuchama Ugweno kuelekea Dar es Salaam, na wakati dereva alipokuwa akilikwepa gari dogo, alijikuta akielekea pembeni ya kingo ya mlima. Uzito wa gari ulizidi uwezo wa kingo, na hivyo basi lililokuwa likiendelea kushuka mlima, lilibingiria na kutumbukia bondeni.”




Majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa katika hospitali mbalimbali za wilaya na mkoa kwa matibabu. Baadhi ya hospitali zilizopokea majeruhi ni Hospitali ya Kifula, Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, Hospitali ya KCMC Moshi, na Hospitali ya Mkoa wa Mawenzi. Afisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Gabriell Chiseo, alithibitisha kupokea majeruhi saba, akisema, “Kati ya majeruhi hawa, mmoja alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali yetu.”

Katika taarifa yake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema kuwa chanzo cha ajali ni mchanganyiko wa mvua na uzembe wa dereva. Alisema, “Hii ni ajali mbaya, lakini tunashukuru kuwa baadhi ya majeruhi wanapata matibabu na tunaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha kuwa wote wanapata huduma bora.”

Miili ya watu saba waliopoteza maisha imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwanga kwa taratibu za mazishi. Majina ya waliopoteza maisha ni kama ifuatavyo:

  1. Ashura Omari Sakena (47) – Mkazi wa Vuchama, Mwanga

  2. Zaituni Hashimu Mwanga (52) – Mkazi wa Masumbeni, Mwanga

  3. Shabani Omari (62) – Mkazi wa Mwanga

  4. Judith Saifoi Mwanga (43) – Mkazi wa Mangio, Mwanga

  5. Hadija Omari (2) – Mkazi wa Mwanga

  6. Haji Abubakar (50) – Mkazi wa Kilifi

  7. Hamadi Hassani (64) – Mkazi wa Nagara, Ugweno

Kwa upande mwingine, wananchi na viongozi wa eneo hilo wameomboleza vifo vya ndugu zao huku wakieleza kutoridhishwa na hali ya barabara na usalama wa magari katika maeneo ya milima, hasa wakati wa mvua. "Tunahitaji kuwepo kwa hatua madhubuti za kuboresha barabara hizi, kwa sababu matukio kama haya yanaweza kuepukika kwa kupanua barabara na kuweka alama za tahadhari," alisema mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mamba.

Ajali hii inaendelea kushtua na kutoa somo kwa jamii juu ya umuhimu wa usalama barabarani, hasa katika kipindi cha mvua. 

 


Ajali mbili zilizotokea wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, zimelighubika eneo hilo kwa huzuni baada ya watu saba kupoteza maisha, wakiwemo wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Chome. 


Zaidi ya majeruhi 75 waliripotiwa, wakiwa na majeraha mbalimbali.


Ajali ya kwanza ilitokea majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo katika eneo la Njoro, ambapo basi la Kampuni ya Osaka, lililokuwa likielekea Dar es Salaam, lilihusika. 



Ajali hii ilisababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu 52. Maelezo kutoka kwa baadhi ya majeruhi wanasema kuwa chanzo cha ajali hiyo kilikuwa ni mwendokasi wa dereva, hali iliyosababisha gari kushindwa kutawala.



Ajali ya pili, inayohusisha basi aina ya Costa la Kampuni ya Mkokota, ilitokea majira ya saa mbili asubuhi leo katika milima ya Ilamba. 



Basi hili lilipinduka baada ya kushindwa kupanda mlima, na kusababisha vifo vya watu sita, wakiwemo wanakwaya wa KKKT walikuwa wakielekea Ndolwa kueneza Injili kwa njia ya nyimbo. 



Chanzo cha ajali hii kimeelezwa kuwa ni hitilafu ya mfumo wa usukani wa gari (steering rod).



Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, alithibitisha kupokea majeruhi 23 kutoka ajali ya pili, wakiwa na majeraha mbalimbali, baadhi wakiwa na mifupa iliyovunjika. 


Miili ya marehemu sita imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ya hospitali ya Same, ikisubiri utambuzi wa familia zao.



Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, alielezea masikitiko yake kuhusu vifo hivyo na kuhimiza madereva kuwa makini wanapopita katika wilaya hiyo, hasa kutokana na hali ya hewa yenye upepo mkali. Alisisitiza pia umuhimu wa abiria kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watabaini hali yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wao, kama vile mwendokasi au hali ya barabara.

Ajali hizi zinatoa zitumike kuwakumbusha madereva, abiria, na mamlaka za usalama barabarani kuwa makini na kufuata sheria ili kuepusha majanga kama haya

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia askari wa usalama barabarani, WP 8032 PC Victoria, kutoka Wilaya ya Igunga, kwa kushiriki katika uchotaji wa mafuta kutoka kwa lori lililopata ajali. 


Tukio hili linazua maswali mengi kuhusu maadili ya kazi ya polisi na usalama wa jamii, huku likikumbusha ajali kubwa ya mafuta iliyotokea miaka sita iliyopita mjini Morogoro.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, alieleza kuwa askari huyo alifika katika eneo la ajali, lakini badala ya kudhibiti wananchi waliokuwa wakichota mafuta kutoka kwa lori lililoharibika, alionekana akitoa dumu kwa mmoja wao ili aendelee kuhifadhi mafuta hayo. 


Kamanda Abwao alisema, "Askari huyu hajazingatia taratibu na maadili ya kazi yetu kwa sababu badala ya kuonya wananchi, yeye anashiriki."


Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Igogo, barabara ya Igunga-Nzega, ambapo lori la mafuta liligonga kwa nyuma lori la mahindi, kisha kupoteza mwelekeo na kugonga lori jingine. Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hili.

Tukio la Morogoro: Maafa ya Mafuta



Tukio hili linatupeleka nyuma mwaka 2019, ambapo ajali nyingine ya lori la mafuta ilitokea katika eneo la Msamvu mjini Morogoro. 

Ajali hiyo iligharimu maisha ya watu 60 na kujeruhi zaidi ya 65. Watu walikuwa wakichota mafuta kutoka kwa lori lililopinduka kabla ya kulipuka baada ya mwananchi mmoja kuchomoa betri, na kusababisha vifo vingi na majeraha makubwa. 

Polisi walieleza kuwa, "Watu hao walikuwa wakichota mafuta baada ya lori hilo kupinduka katika barabara kuu mapema Jumamosi."

Ajali hizi za mafuta zimeendelea kuwa tishio kubwa kwa usalama wa wananchi na majirani wa maeneo ya ajali. Hivyo, ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kuzuia uchotaji wa mafuta, ili kuepuka maafa yanayoweza kutokea.


Kudumisha Maadili na Usalama

Ushiriki wa askari katika tukio hili ni kielelezo cha changamoto ya maadili na utekelezaji wa taratibu zinazohusiana na usalama barabarani. 


Serikali na taasisi za usalama zinapaswa kuwa na mikakati madhubuti ya kudhibiti vitendo vya uchotaji mafuta, ili kuepuka maafa zaidi. Hali hii inatoa wito kwa wananchi na mamlaka husika kuwa makini na tahadhari kuhusu hatari zinazoweza kutokea kutokana na ajali za mafuta.

  


Mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chanika, SP Awadh Mohamed Chico, yamefanyika leo, Machi 18, 2025, baada ya kifo chake kilichotokea katika ajali ya gari jana akiwa anaelekea kazini.



Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi (DCP) Mkondya ameongoza waombolezaji katika ibada ya kuaga mwili wa marehemu, ambapo alitoa salamu za rambirambi kwa familia ya SP Awadh kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillus Wambura. 



Aliwahimiza waombolezaji kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu, akisema kuwa safari ya umauti ni ya kila mmoja wetu.



Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Gongolamboto mwisho, karibu na Kilima cha kuingia Pugu Sekondari, ambapo SP Awadh Mohamed Chico alipoteza maisha baada ya gari lake aina ya Prado kugongana na basi aina ya Eicher. 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Yustino Mgonja, alithibitisha kifo cha SP Awadh kupitia mitandao rasmi ya kijamii za Jeshi la Polisi.

Bofya kusoma zaidi

Kifo cha SP Chiko Kufuatia Ajali ya Gari: Maziko Kufanyika Kesho Kijitonyama




Ajali mbaya imetokea maeneo ya Gongolamboto mwisho, karibu na Kilima cha kuingia Pugu Sekondari, ambapo aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Chanika (OCD), SP Awadh Mohamed Chiko, amefariki dunia. Ajali hiyo ilihusisha basi aina ya Eicher ambalo lilitangulia na kugonga gari la SP Awadh, akiwa ndani ya Prado akielekea kazini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Yustino Mgonja, amethibitisha tukio hilo akitangaza kifo cha SP Awadh muda mfupi uliopita kupitia kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za Jeshi la Polisi Tanzania.

"Kwa masikitiko makubwa, SP Awadh Mohamed Chiko amefariki dunia leo asubuhi kufuatia ajali iliyotokea eneo la Pugu Sekondari, baada ya basi aina ya Eicher kugongana na gari lake aina ya Prado," alisema msemaji wa familia.

Kwa mujibu wa mashuhuda, basi hilo lilikuwa likitokea upande mmoja na kumgonga SP Awadh, ambaye alipoteza maisha kwenye tukio hilo.

Mwili wa marehemu umepelekwa katika Hospitali ya Kipolisi Barracks Kilwa Road kwa uchunguzi wa awali.

Maziko ya SP Awadh Mohamed Chiko yanatarajiwa kufanyika kesho, ambapo mwili wake utaswaliwa katika msikiti wa Akachube, uliopo Kijitonyama, kabla ya kusafirishwa kwa maziko. Familia inasema kuwa msiba huu umeleta huzuni kubwa katika jamii, huku wakimwomboleza kwa pamoja na kumuomba Mungu amuweke mahali pema peponi.

"Kwa sasa, msiba upo nyumbani kwa marehemu, Kijitonyama, Mtaa wa Bukoba, ambapo familia inajumuika kwa maombolezo na maandalizi ya maziko," aliongeza msemaji wa familia.

Polisi na maafisa wa usalama wameendelea kufanya uchunguzi juu ya ajali hii, huku familia ikisema itakuwa na mchakato wa kutoa taarifa kamili baada ya uchunguzi kukamilika.

Historia ya Familia: Baba wa SP Awadh Marehemu CP Mohamed Awadh Chiko

SP Awadh Mohamed Chiko alikuwa mtoto wa marehemu SACP Mohamed Awadh Chiko, ambaye pia aliwahi kushika wadhifa mkubwa katika Jeshi la Polisi la Tanzania. 

SACP Mohamed Awadh Chiko aliwahi kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, nafasi aliyoihudumu kwa kipindi kirefu na kuacha alama kubwa katika utendaji wa Jeshi la Polisi. 


Baada ya kustaafu, alihamishiwa Makao Makuu ya Polisi kabla ya kufariki dunia Januari 22, 2017. 

Marehemu SACP Mohamed Awadh Chiko alijulikana kwa juhudi zake za kukuza usalama na kudumisha amani katika mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine aliyopita.

 



Toronto, Canada – Abiria 80, wakiwemo watoto na watu wazima, wamenusurika kifo baada ya ndege ya Delta Air Lines 4819 kupata ajali wakati wa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toronto Pearson.

Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za uwanja wa ndege, ndege hiyo iliyokuwa ikitoka Minneapolis, Marekani, ilipata hitilafu ilipokuwa inatua, na kusababisha kupinduka huku moja ya mabawa yake likionekana kuharibika kabisa.

"Tunathibitisha kuwa ajali hii imehusisha ndege ya Delta Air Lines 4819 na kwamba abiria wote na wafanyakazi wa ndege wamepatikana," ilisema taarifa ya mamlaka za uwanja wa ndege wa Toronto Pearson.

Shirika la ndege la Delta lilithibitisha kuwa ndege hiyo ilikuwa na watu 80, wakiwemo abiria 76 na wafanyakazi wa ndege wanne.

"Tunashukuru kwamba abiria wote walifanikiwa kutoka salama licha ya hali hiyo ya kutisha," alisema msemaji wa Delta, Bi. Flint.

Majeruhi 18 walikimbizwa hospitalini, ambapo watatu kati yao – mtoto mmoja, mwanamume wa miaka 60, na mwanamke wa miaka 40 – waliripotiwa kuwa na majeraha makubwa.

"Kwa sasa, juhudi zinaendelea kuhakikisha kuwa wote waliokuwa ndani ya ndege wanapata msaada wa matibabu na msaada wa kiakili baada ya tukio hili," aliongeza Bi. Flint.

Uwanja wa Ndege wa Toronto Pearson ulifungwa kwa muda mfupi ili kuruhusu vikosi vya uokoaji kufanya kazi zao, lakini safari za ndege zilianza tena baada ya saa kadhaa.

Mamlaka zimeanza uchunguzi kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo.



Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani kimesema kuwa baada ya kuhitimisha zoezi la ukaguzi wa magari ya shule (School Bus) kwa kipindi cha likizo, ambacho kilitangazwa ili kuondoa usumbufu kwa wanafunzi wanaotumia vyombo hivyo, kimeanza kuwakamata wale wote walio kaidi agizo hilo huku kikosi hicho kikiwaomba wananchi kuweka uangalizi wa kundi hilo.



Akiongea katika zoezi hilo, Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed amesema kuwa kikosi hicho kilitangaza zoezi hilo na kueleza kuwa wameanza operesheni za ukamataji wa magari ambayo hayajakaguliwa na kikosi hicho.



"Kwa sasa tunaanza operesheni ya kuwakamata madereva na wamiliki wa magari ambayo hayajapitia ukaguzi huu, licha ya kuwa tulishatoa taarifa mapema," alisema SSP Zauda Mohamed.



Ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha kuna zaidi ya magari 563 ambayo yanatoa huduma kwa wanafunzi, na baada ya ukaguzi huo, imeonekana kuwa bado kuna magari 178 ambayo hayajakaguliwa.



 "Kuanzia leo Januari 13, 2025, tunaanza ukamataji wa madereva waliokaidi agizo hili," alisisitiza SSP Zauda.

SSP Zauda pia akatumia fursa hiyo kuwataka wamiliki na madereva wa magari ya shule, kupeleka magari yao katika kikosi cha Usalama Barabarani kwa ukaguzi ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi. 



"Watu wote waliokaidi watachukuliwa hatua za kisheria, kwa sababu tunataka kuhakikisha mazingira salama kwa watumiaji hawa," alisisitiza.

Sambamba na hilo, alisema kikosi hicho kinatambua kuwepo kwa kundi jipya la watumiaji wa barabara ambao ni wanafunzi wa shule za awali walioanza shule mwaka huu. Alisema, "Tunawaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwaelekeza watoto hawa kuhusu matumizi sahihi ya barabara na kuhakikisha wana wasimamizi wakati wa kwenda na kurudi majumbani."

Pia, SSP Zauda alitoa wito kwa madereva kutambua kuwa kuna kundi jipya la watumiaji wa barabara, akiwataka kuchukua tahadhari na kufuata sheria za usalama barabarani ili kundi hilo liendelee kuwa salama kipindi chote. "Ni jukumu letu sote kuhakikisha watoto hawa wanatumia barabara kwa usalama," aliongeza.

 


On January 4, 2025, a tragic accident occurred within the Ngorongoro Crater, resulting in one fatality and five people injured. 


The accident involved a safari vehicle owned by Wakali Safaris, which was carrying seven passengers, including six Israeli nationals and one Tanzanian driver. 


The incident took place around 8:45 AM between the Viewpoint and the main gate of Loduare, popular tourist areas within the park.


The Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA) confirmed that five people were injured in the accident, and one of the victims, a woman, tragically lost her life. 


The driver of the vehicle, a Tanzanian national, was reported to be in good condition and is recovering well after the incident.


NCAA Issues Official Statement

Hamis Dambaya, the Acting Public Relations Manager for the Ngorongoro Conservation Area Authority, issued an official statement about the incident, saying: “The accident has resulted in five injuries, and one of them, a woman, has passed away. 


The driver is in good health and is doing well. We continue to monitor the condition of the injured and will provide updates as soon as possible.”


Dambaya also reminded all safari vehicle drivers to exercise caution and adhere to traffic and conservation regulations, emphasizing that: “We continue to remind safari vehicle drivers to follow road safety laws and conservation regulations to ensure the safety of visitors and the vehicles they use while in the park.”

Injured Victims Transported to Hospitals for Treatment

Following the accident, the injured were rushed to the Lutheran and FAME hospitals in Karatu District for first aid. 


"After receiving initial treatment, the injured were transferred to the Lutheran Selian Hospital in Arusha for further medical care," the NCAA statement noted.

The Ngorongoro Conservation Area Authority has expressed condolences to the families of the victims and is praying for a speedy recovery for the injured. 


They also extended prayers for the deceased, wishing for them to rest in peace.



 


Ajali ya ndege iliyotokea katika mji wa Muan, Korea Kusini, imesababisha vifo vya abiria 179 na wafanyakazi wanne wa ndege. 


Watu wawili, ambao ni wafanyakazi wa ndege, walinusurika na walikolewa kutoka kwa mabaki ya ndege na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.



Kulingana na taarifa rasmi, ajali hiyo ilihusisha ndege aina ya Boeing 737-800 ya kampuni ya Jeju Air. 


Wote 175 wa abiria waliokuwa kwenye ndege walipoteza maisha, pamoja na wafanyakazi wanne wa ndege hiyo, ambao walikuwa sehemu ya wahanga wa ajali hii. 



Familia za waliokufa zimejumuika kwenye uwanja wa ndege kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho huku shughuli za uokoaji zikiendelea.



Picha za ajali zimekuwa zikisambaa kutoka eneo la tukio, ambapo wafanyakazi wa uokoaji wanajaribu kufukua mabaki ya ndege kwa matumaini ya kupata taarifa zaidi kuhusu chanzo cha ajali hiyo. 



Kaimu Rais wa Korea Kusini, Choi Sang-mok, alifika kwenye eneo la ajali akiongoza juhudi za kutoa msaada wa haraka, ikiwa ni pamoja na huduma za afya na vifaa vya kusaidia wahanga. 


Ofisi ya rais imesema kuwa serikali itahakikisha familia zilizofiwa zinapata msaada wa kutosha.


Ajali hii ni moja ya ajali mbaya zaidi katika historia ya Korea Kusini, nchi inayojivunia rekodi nzuri ya usalama wa ndege katika miaka ya hivi karibuni. 


Jeju Air, kampuni ya ndege ya bei nafuu iliyoanzishwa mwaka 2005, ni moja ya mashirika makubwa ya ndege nchini humo. 


Ajali hii ni ya kwanza katika historia ya Jeju Air, huku kampuni hiyo ikitoa rambirambi kwa waathiriwa wa ajali na kuahidi kuchukua hatua za dharura ili kusaidia familia zilizopoteza wapendwa wao.



Mkurugenzi Mtendaji wa Jeju Air, Kim E-bae, aliomba radhi hadharani kwa waathiriwa wa ajali hiyo akisema kuwa kampuni yake inashirikiana na mamlaka za uokoaji ili kukabiliana na madhara yaliyosababishwa na ajali hiyo. 


Alisisitiza kuwa msaada kwa waathiriwa na familia zao ndiyo kipaumbele cha kampuni kwa sasa.


Chanzo cha ajali hiyo bado hakijathibitishwa, ingawa vyombo vya habari nchini Korea Kusini vimeripoti kuwa huenda ilitokana na hitilafu kwenye mfumo wa ndege. 


Hata hivyo, uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini sababu kamili ya ajali



Ajali hii inahusisha ndege aina ya Boeing 737-800, ndege maarufu inayotumika sana na mashirika ya ndege duniani. 


Boeing imejibu kwa kutoa rambirambi kwa waathiriwa na kusema kuwa inawasiliana na Jeju Air ili kutoa msaada wa kiufundi na kujua zaidi kuhusu kilichosababisha ajali hiyo.


Kwa sasa, hii inabakia kuwa ajali ya ndege mbaya zaidi ya aina yake katika ardhi ya Korea Kusini, na inatoa changamoto kubwa kwa Jeju Air, ambayo imekuwa na sifa nzuri ya usalama hadi sasa. Huu pia ni mtihani mkubwa kwa sekta ya usafiri wa anga katika nchi hiyo.