Showing posts with label Habari kitaifa. Show all posts
Showing posts with label Habari kitaifa. Show all posts




Mwandishi Wetu Dodoma



WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa na      viongozi wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) wamekutana na kujadili namna ya kutatua changamoto za wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini.



Kikao hicho kimefanyika jana Alhamisi Agosti 21 mwaka huu jijini Dodoma katika Ofisi ya Waziri Kikwete ambapo mjadala mkubwa ulijikita kwenye masuala ya  mikataba ya kazi na hali bora za kufanya kazi.



Akizungumza katika kikao hicho,Waziri Kikwete, amesema wizara yake hairidhishwi na hali za wafanyakazi walio wengi katika vyombo vya habari na lazima jambo hilo lipatiwe ufumbuzi kwa kuhakikisha wanapewa mikataba kama sheria inavyotaka.


"Nimewaita hapa leo tuzungumze pamoja kuhusu changamoto za kazi katika sekta yenu, kwa kweli mimi binafsi nazijua changamoto zenu na tunataka kuzifanyia kazi, naamini kupitia kikao hiki ambacho kamishna wa kazi ameshiriki tunaweza kupata muafaka kwa siku zijazo," amesema.


Amesema anajua wanahabari wengi hawana mikataba ya kazi na ajira na wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo lazima zifike mwisho kwani sheria ya kazi ni moja kwa wafanyakazi wote, lazima ionekane kwenye sekta zote.



"Kama tulivyozungumza Arusha, tulikubaliana leo kukutana tena hapa na Kamishna wa Kazi akiwepo ili kuona ni jinsi gani tunaweza kusaidia wanahabari nchini kufanya kazi katika mazingira bora, naomba kila mtu aende kutekeleza yale ambayo yanamuhusu tuangalie njia ya kupitia yenye maslahi kwa wote," amesema


Amesema ni lazima kila sekta nchini ifanyekazi kwa kuzingatia sheria za kazi zilizopo badala ya kufanyakazi kiujanja ujanja na mwisho uzeeni kuja kutaabika ama unapopata matatizo kushindwa kujisaidia.


Kwa upande wake Kamishna wa Kazi, Mkangwa amesema Ofisi yake ipo tayari kufanyakazi na JOWUTA kusaidia kutatua changamoto za wafanyakazi katika vyombo vya habari ambapo alisisitiza kushirikiana katika kutoa taarifa za changamoto zilizopo.


Mkangwa ametumia kikao hicho kuwaasa waandishi wa habari kuhakikisha wanafanya kazi baada ya kusaini mikataba ya kazi inayotambulika kisheria .


"Tunaweza kufanya ukaguzi lakini sekta yenu ina changamoto kadhaa za kimfumo ikiwepo uwepo wa wafanyakazi wanaoandika habari kwa  malipo baada ya habari kutumika (correspondent na freelance) wanahabari wenye mikataba ya muda (retainer), huu utaratibu ni mgumu sana na upo kwenu zaidi, unapaswa kuondoka ili tuwe kwenye njia moja kama sekta zingine," amesema.


Amesema ofisi yake imekuwa ikifanya ukaguzi mara kwa mara na kukuta mikataba ya walio katika ajira pekee hivyo ni vigumu kujua makundi mengine kama huna taarifa za kutosha na kutumia fursa hiyo kuomba waandishi watoe ushirikiano ili kubaini mapungufu yaliyopo.


"JOWUTA nawaomba tushirikiane ili kupata taarifa sahihi za hali za wafanyakazi katika kila chombo cha habari ili tuzifanyiekazi, " amesema


Amesema Ofisi yake pia itaendelea kutoa elimu ya sheria za kazi kwa wanahabari na wafanyakazi wengine ili wafanye kazi kwa kuzingatia sheria.


Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma aliomba Wizara hiyo kusaidia wanahabari kufanyakazi katika mazingira bora na sheria za kazi kufuatwa kama ilivyo katika sekta nyingine.


Amesema zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari nchini wanafanyakazi bila kuwa na mikataba ya kisheria, bima ya afya wala mifuko ya pensheni na zaidi ya miaka 10 katika hali hiyo jambo ambalo halikubaliki.


"Tunakuomba sana Kamishna usaidie sekta hii, ili waajiri wazingatie sheria za kazi na tunaomba pia ukaguzi wa mara kwa mara katika vyombo vya habari, kuhakikisha wamiliki wa vyombo vya habari wanafuata sheri0


a za kazi," amasema.


Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA, Seleman Msuya  amesema JOWUTA inashukuru serikali kwa kazi nzuri ambayo inafanywa na Bodi ya Ithibati Tanzania (JAB) kwa kuhakikisha wanaofanyakazi katika vyombo vya habari ni wale wenye sifa za kitaaluma.


Hata hivyo alisema ni muhimu mkazo wa kuwa na Ithibati kwa wanahabari uendane na kuboresha maslahi kwa wanahabari ikiwepo kupewa mikataba, kulipiwa bima na kuwa na stahili nyingine.


"Kwa sasa kila kukicha kuna michango ya wanahabari wagonjwa kwani wengi hawana bima wala hawapo kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Tunaomba nguvu hii ambayo imeoneshwa na JAB kwenye sifa za wanahabari ionekane kwa Kamishna wa Kazi kwenye eneo la mikataba," amesema.


Amesema waandishi wa habari ni nguzo muhimu katika huduma za kijamii, kiuchumi na kisiasa, hivyo ni vema wakapewa kipaumbele kama makundi mengine kwenye ajira.


"Tunaposema sekta inachangia kwenye pato la taifa, ni vema ikaonekana kivitendo, kwenye sekta hii ya habari yenye zaidi ya watu 30,000 mchango wake kwenye uchumi wa nchi bado ni mdogo sisi tunaamini iwapo sheria zitafuatwa mchango wetu utaonekana kila mwaka kama zilivyo sekta za utalii, uvuvi, ujenzi, kilimo na nyinginezo," amesema.


Mweka hazina wa JOWUTA Lucy Ngowi amesema sekta ya habari inapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma, ili kuhakikisha waandishi wananufaika na nchi kwa ujumla.




 

Kibaha, Pwani – Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imeweka lengo la kukusanya kiasi cha Shilingi trilioni 2 katika mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Shilingi bilioni 400 kutoka lengo la mwaka uliopita.


Hayo yalibainishwa Julai 28, 2025 na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, wakati wa uzinduzi wa mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi za umma yaliyoandaliwa na OMH kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi. Mafunzo hayo yamehusisha jumla ya watendaji wakuu 114 kutoka taasisi mbalimbali za umma, wakiwemo walioteuliwa hivi karibuni na wengine waliokuwa bado hawajapata mafunzo kama hayo licha ya kuwa kwenye nafasi kwa muda mrefu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mchechu alisema:
“Ili tuweze kufikia lengo letu la kukusanya Sh2 trilioni, itatubidi tuongeze bidii kwa asilimia 100 ya tulivyokuwa tunafanya mwaka wa fedha uliopita.”

Kwa mujibu wa taarifa za OMH, mwaka wa fedha uliopita (2024/25), ofisi hiyo ilifanikiwa kukusanya kiasi cha Sh1.028 trilioni kama mapato yasiyo ya kikodi, kiwango ambacho kilikuwa chini ya lengo la Sh1.6 trilioni lililowekwa na Serikali.

Mapato hayo yasiyo ya kikodi yanakusanywa kwa mujibu wa sheria mbalimbali za nchi na yanatokana na vyanzo kama gawio kutoka mashirika na taasisi za umma, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi, na mapato ya ziada ya taasisi, pamoja na marejesho ya mikopo, riba, na makusanyo kupitia mfumo wa TTMS (Telecom Traffic Monitoring System).

Kwa mujibu wa Kifungu cha 180 cha Sheria ya Makampuni (Sura 212) na Kifungu cha 15(2)(b) cha Sheria ya Mashirika ya Umma (Sura 257), mashirika ya umma yanayofanya biashara yanawajibika kutoa gawio kwa Serikali. Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 12(3) cha Sheria ya Fedha za Umma Sura 348, taasisi za umma ambazo hazihusiki moja kwa moja na gawio zinatakiwa kuwasilisha asilimia 15 ya mapato ghafi kwa Mfuko Mkuu wa Serikali.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Mchechu alisema:
“Tunaamini kuwa mafunzo haya yatakuwa chachu ya mageuzi katika mashirika ya umma, hasa kwa kuimarisha uongozi, maadili, uwajibikaji wa kifedha na usimamizi wa uwekezaji wa umma.”

Kufikia mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikuwa imewekeza takribani Sh86.25 trilioni katika taasisi za umma 252 na kampuni 56 ambazo Serikali ina hisa chache. Uwekezaji huu unahitaji usimamizi makini ili kuhakikisha unaongeza thamani kwa taifa na kuchangia kikamilifu katika mapato ya Serikali.

Kwa ujumla, jitihada za kuongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kikodi zinatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali kupanua wigo wa mapato ya ndani bila kuongeza mzigo kwa walipa kodi wa kawaida.


 


Serikali ya Tanzania inaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, huku ikijiandaa kupitia upya kanuni za malipo ya kifuta jasho na machozi kwa waathirika.



Katika ziara yake mkoani Tanga, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali inaongeza askari wanyamapori na kutumia teknolojia za kisasa kama ndege zisizo na rubani (drones) kudhibiti wanyama waharibifu.

"Tunaendelea kuongeza askari wanyamapori na kubuni mbinu mbalimbali za kufukuza wanyama, ikiwemo kutumia ndegenyuki (drones)," alisema Rais Samia wakati wa mkutano wake na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.



Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa chama na serikali, akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri Dunstan Kitandula, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, pamoja na watendaji kutoka taasisi za wizara hiyo.

Ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Mkomazi Kuanza Rasmi



Katika muendelezo wa ziara yake mkoani Tanga, Rais Samia ameweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji la Mkomazi wilayani Korogwe, akisema kuwa hatua hiyo inatimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ya kuboresha sekta ya kilimo nchini.



Bwawa hilo linatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 20,000 wa wilaya hiyo kwa kuwawezesha wakulima kulima mara mbili hadi tatu kwa mwaka bila kutegemea mvua.

"Dhamira ya serikali ni kumuinua mkulima kwa kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo," alisema Rais Samia.

Bwawa hilo litakuwa na tuta lenye urefu wa zaidi ya mita 300, barabara za mashambani zaidi ya kilomita 56, na litaweza kuhifadhi lita bilioni 17 za maji. Ujenzi wake unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 48 na utahusisha zaidi ya kata 20 wilayani Korogwe.





Akielezea mradi huo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema kuwa serikali kwa miaka mingi imekuwa na changamoto za kulitekeleza bwawa hilo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo masuala ya kisiasa na kifedha. Hata hivyo, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejidhatiti kuhakikisha mradi huo unakamilika.

"Serikali inalenga kuwavutia wawekezaji wakubwa wa mazao mengine kama vile kilimo cha chai, ili kutoa fursa kwa wakulima kupata nafasi ya kuuza mazao yao kwenye soko la ndani na nje ya nchi," alisema Bashe.



Hatua hii ya serikali inaashiria mwamko mpya katika kuboresha kilimo na usalama wa wananchi dhidi ya wanyamapori wakali, ikiwa ni juhudi za kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii kwa ujumla.

 


Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limeandaa kushiriki katika mazoezi mawili ya kijeshi ya pamoja, "Justified Accord" na "Cutlass Express", yatakayofanyika hapa nchini, yakishirikisha Jeshi la Marekani pamoja na majeshi kutoka nchi kumi na mbili rafiki. Mazoezi haya yanalenga kuongeza uelewa wa pamoja katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama, ikiwa ni pamoja na vitisho vya ugaidi na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, huku wakihakikishia wananchi usalama wao.

Zoezi la "Justified Accord" litafanyika katika eneo la Msata, Wilaya ya Chalinze, mkoani Pwani na Nanyuki, nchini Kenya, na kuanza rasmi Februari 10 na kumalizika Februari 21 mwaka huu. Katika zoezi hili, washirika watafanya mazoezi ya kijeshi yanayolenga kuongeza weledi na uelewa wa pamoja katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama.

"Mazoezi haya ni muhimu katika kuboresha uwezo wetu wa kijeshi na kuhakikisha tunakuwa tayari kukabiliana na changamoto za kiusalama," alisema Afisa Mkuu wa JWTZ. "Tunashirikiana na washirika wetu wa Marekani na nchi zingine ili kuimarisha ushirikiano wetu na kujifunza mbinu mpya za kupambana na vitisho."

Zoezi jingine, "Cutlass Express", litazingatia maeneo ya uwajibikaji baharini, linalolenga kuboresha ushirikiano katika kukabiliana na vitisho vya usalama baharini, ikiwa ni pamoja na kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya. Zoezi hili, linalofanywa pamoja na Jeshi la Wanamaji, litafanyika katika nchi za Tanzania, Madagascar na Ushelisheli; kwa upande wa Tanzania, zoezi hili litafanyika katika jiji la Tanga.

"Mashiriki katika zoezi hili yatatufundisha jinsi ya kuboresha ushirikiano wetu wa kiusalama katika maeneo ya baharini, na hili ni fursa muhimu ya kujifunza mbinu mpya za kukabiliana na vitisho vya usalama," alisema Afisa wa Jeshi la Wanamaji.


Wakala wa Jeshi la Marekani alisema, "Tunashirikiana kwa karibu na Tanzania na washirika wetu wengine ili kuboresha uelewa wetu wa pamoja na kuongeza ufanisi katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama. Ushirikiano huu ni wa kipekee na ni muhimu kwa usalama wa eneo letu."


Mazoezi haya yatashirikisha nchi 14, ikiwa ni pamoja na Kenya, Madagascar, Ushelisheli, Djibouti, Comoro, Georgia, Msumbiji, Malawi, Mauritius, Tunisia, Somalia na Senegal. Msimamizi wa mazoezi kutoka Kenya alisema, "Tumeungana kwa umoja katika zoezi hili ili kuhakikisha usalama wa maeneo yetu ya pande zote, na fursa hii inatupa uelewa mpya wa jinsi ya kukabiliana na changamoto za usalama."


Katika taarifa, ofisi ya uhusiano na vyombo vya habari iliongeza kuwa wananchi wametakiwa kutokuwa na taharuki kwani zoezi hizi zimepangwa kikamilifu na zinahusisha matumizi ya ndege vita na meli. "Wananchi wanasihiwa kutokuwa na taharuki kwani shughuli hizi ni mazoezi ya kijeshi yaliyopangwa vizuri ili kuepuka usumbufu kwa wananchi," alisema msemaji kutoka ofisi husika.


Mazoezi haya ya pamoja yanatarajiwa kuwa mchango mkubwa katika kuboresha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi husika na kuongeza uwezo wa kukabiliana na vitisho vya kiusalama katika muktadha wa mabadiliko ya kiutamaduni na kisiasa yanayoendelea.



Leo tarehe 17 Juni 2024, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameungana na waumini wengine katika kuswali Swala ya Idd El-Adh’haa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI BAKWATA, Kinondoni, Dar es Salaam. 



Baada ya sala, Majaliwa alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya Baraza la Kitaifa lililofanyika katika msikiti huo. Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.



Hafla hii ni sehemu ya maadhimisho ya Idd El-Adh’haa ambayo hufanyika kila mwaka kwa jamii ya Waislamu duniani kote.

  


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa pongezi kwa taasisi ambazo zimefanikiwa kutoa gawio, akithibitisha kuwa sera, miongozo, na mazingira yaliyowekwa na serikali yamewawezesha kufanya kazi. Amewataka taasisi zingine kufuata mfano huo.



 Akizungumza leo Ikulu Dar es Salaam alipokuwa akipokea gawio la Shilingi bilioni 637 kutoka kwenye mashirika na taasisi 145, Rais Samia ameonyesha furaha yake kutokana na mafanikio hayo. Amesema ni ishara nzuri kwa taasisi za umma kuongeza kasi ili kufikia mafanikio kama hayo.



Rais Samia ameelezea kufurahishwa kwake na mchango wa taasisi zilizo chini ya serikali ambazo zimefanikiwa kutoa gawio, hata kama serikali ina hisa chache katika taasisi hizo.



Amesema mfano wa Benki ya NMB, Kampuni ya Twiga Mineral Corporation, Airtel Tanzania, Puma Energy, na TPC Moshi unaweza kuwa kichocheo kwa taasisi nyingine kufanya kazi kwa bidii zaidi.


Kuhusu mifumo ya kusomana, Rais Samia ameagiza hatua zichukuliwe haraka ili kuhakikisha mifumo hiyo inafanya kazi ifikapo Desemba mwaka huu. Amesisitiza umuhimu wa mashirika ya umma kubadilika na kuchangia katika pato la taifa, na amefurahishwa na hatua zilizopigwa hadi sasa kwenye mageuzi ya mashirika hayo.



Akitoa taarifa mbele ya Rais Samia, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ameelezea juhudi zinazofanywa na ofisi yake katika kusimamia mageuzi ya mashirika. 

Ameeleza kuwa tija imeanza kuonekana, na kwamba zaidi ya taasisi 145 zimetoa gawio hadi sasa. 

Lengo ni kupokea gawio la Shilingi bilioni 850, na kwa sasa wamepokea Shilingi bilioni 637 kutoka taasisi 149. 

Mchechu ameongeza kuwa wako katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kuripoti taarifa za utendaji wa watendaji wakuu wa taasisi.


Rais Samia amesema amepokea mafanikio makubwa kutoka taasisi ambazo serikali ina hisa chache, hivyo ni ujumbe kwa taasisi za serikali kuongeza kasi ili kufikia mafanikio. Amesema hayo leo Ikulu Dar es Salaam wakati akipokea gawio la Shilingi bilioni 637 kutoka kwenye mashirika na taasisi 145 kati ya 304 zinazochangia asilimia 15 ya mapato ghafi na zile ambazo serikali ina hisa na kusimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.


“Tumeona Benki ya NMB, Kampuni ya Twiga Mineral Corporation, Airtel Tanzania, Puma Energy na TPC Moshi wametoa gawio kubwa na sisi tuna hisa chache nadhani kila shirika lifanye kazi kwa juhudi ili kufikia kampuni hizi,” alisema. Mh. Rais Samia


Aidha, Rais Samia amesema kilichofanywa na Mashirika ya Umma kama Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Wakala wa Huduma za Meli Tanzania (TASAC) na BRELLA ni ushahidi tosha wa kuweka mifumo mizuri na kushirikisha wawekezaji.


“Wapo ambao walipiga kelele kwamba Ooh.. mama anauza bandari, lakini gawio la Shilingi bilioni 153.9 ya TPA ni matokeo ya wawekezaji ambao wapo pale imani yangu ni mwakani wataongeza,” amesema.


Kuhusu mifumo kusomana Rais Samia ameagiza mamlaka husika kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu mifumo iweze kusomana na kwamba suala hilo limechukua muda mrefu. ambapo ameongeza kuwa hataki kusikia shirika ambalo mifumo yake haisomani na mingine.


Kiongozi huyo amesema alipoingia madarakani aliagiza mashirika ya umma na taasisi ambazo serikali ina hisa zibadilike na kuchangia katika pato la taifa, jambo ambalo limeanza kutekelezwa.


Awali akitoa taarifa yake mbele ya Rais Samia, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema ofisi yake inaendelea kusimamia mageuzi ya mashirika na tija imeanza kuonekana.


Mchechu amesema sheria inayosimamia ofisi ya Msajili wa Hazina inaelekeza mashirika kutumia si zaidi ya silimia 60 ya mapato yake iliyoyakusanya na kutoa gawio kwa serikali ambapo hadi sasa zaidi ya taasisi 145 zimetoa huku 159 zikitarajiwa kutoa kati ya 304.


Aidha, ameongeza kuwa taasisi zote zimeingia mkataba wa utendaji kazi kati ya bodi zao na ofisi ya Msajili wa Hazina na kwamba wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kuripoti taarifa za utendaji wa



Leo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma katika Ibada ya Jumapili. Ibada hiyo iliyoongozwa na Padre Dionis Paskal Safari ilikuwa na ujumbe wa amani na umoja.



Baada ya ibada, Dkt. Mpango ametoa wito kwa Watanzania kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji. Amesema matumizi mabaya ya mitandao hiyo yamesababisha madhara kwa watu wengi, hivyo ni muhimu kila mmoja kutumia mitandao hiyo kwa kuzingatia maadili na kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu.



Makamu wa Rais amewashukuru waumini kwa sala zao na kuwahimiza waendelee kumuombea ili awezoe kutimiza majukumu yake ipasavyo. 


Hii ni mara ya kwanza Makamu kuonekana hadharani  kwani kwa zaidi ya mwezi mmoja amekua haonekani hali iiyoibua minong'ono miongoni mwa wananchi waliotaka kujua alipo kiongozi huyo wa juu baada ya Rais .


Minong'ono hiyo ilimlazimisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa taarifa kuwa Makamu wa Rais yuko salama na anaendelea na majukumu yake kikamilifu.


Hii ni hatua muhimu inayojenga imani kwa umma kuhusu afya na utendaji wa Makamu wa Rais, na inaonesha umuhimu wa mawasiliano ya wazi na uwazi katika uongozi wa nchi.





Na Mwandishi wetu- Dodoma

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali katika ofisi yake, Paul Sangawe (wa kwanza kushoto) na baadhi ya watendaji katika ofisi yake pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo kutoka Shirika la Helen Keller Tanzania baada ya kikao hicho.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizumgumza katika kikao chake na wadau wa maendeleo kutoka Shirika  linalojishughulisha na masuala ya lishe la Helen Keller Tanzania walipotembelea ofisini kwake Jijini Dodoma.




Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa maendeleo  wa  Shirika  Helen Keller Tanzania  ofisini kwake Jijini Dodoma.


Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau hao katika kuhakikisha sekta ya lishe inapewa kipaumbele ili kuwa na Taifa lenye lishe bora kuanzia ngazi ya familia.


Dkt. Yonazi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kusirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha afua za lishe zinaboreshwa  kwa wananchi kuhamasishwa kula vyakula vyenye virutubisho kwa kuzingatia mazingira yao yanayowazunguka pamoja na wananchi kupewa elimu ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele ili kujikinga kwa ustawi wa Taifa.


"Ipo haja ya kushirikiana pamoja tuhakikishe wananchi tunabadilisha fikra za Jamii kuhusu masuala ya lishe na magonjwa kwa sababu itawasaidia kuacha kuishi kwa mazoea na badala yake wazingatie umuhimu wa kutunza afya zao ili waendelee kuwa sehemu ya uzalishaji katika familia zao na Nchi kwa ujumla,”Amesema Dkt. Yonazi.



Naye Mkurugenzi wa Shirika linalojishughulisha na masuala ya lishe la Helen Keller Tanzania, Dkt. Deogratius Ngoma ameeleza kwamba jukumu lao kubwa ni kujenga uelewa kwa jamii kuhusu vyakula hatarishi vinavyosababisha magonjwa yasiyoambukiza.


Aidha Mtaalam na Mshauri wa Masuala ya lishe Dkt. Theresia Jumbe kutoka Shirika hilo  amebainisha kuwa maazimio waliyofikia ni  kuendeleza shughuli za uratibu wa masuala ya lishe  katika kusimamia na kuchangia utekelezaji wa afua za lishe zilizoainishwa katika mpango jumuishi wa lishe wa Multisectoral  Nutrition  Action Plan  (NMMNAP).


(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI 

 


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa kampuni zote zilizopewa jukumu la upimaji wa viwanja katika Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba au hazikuwa nayo, zichukuliwe hatua kali za kisheria.


"Watumie makampuni yenye uaminifu badala ya kutumia makampuni yanayotuletea migogoro," alisema Waziri Mkuu.


Agizo hili limekuja baada ya kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, ambapo viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma walijadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.


"Kampuni nyingi hapa Dodoma zina watumishi wake wenyewe wakiwa ni sehemu ya mradi. Hatutaki hili liendelee," alisema.


Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha Kamishna Msaidizi wa Mkoa, Maafisa Mipango Miji wa Majiji, Halmashauri na Manispaa wanafanya kazi ya upimaji wenyewe bila kuchukua watumishi wa muda ili kuepusha mianya ya rushwa.


Pia, aliagiza kukamatwa kwa vibarua wanaotembea na nyaraka za Serikali na kuuza viwanja kwa niaba ya maofisa wa Jiji.


"Justin Albert, Freddy Mathias, Elias na Magige watafutwe, wachunguzwe na vyombo vya dola kuhusu nyaraka za Serikali walizonazo, na wazirejeshe nyaraka za Serikali wanazotumia vibaya kwa kuendelea kuuza viwanja maeneo ya Jiji la Ukanda wa Kijani, Mkonze, Ndachi, Chinyika, Ng’ong’ona na Mkalama."


"Hawa ni vibarua, lakini wanavijua viwanja vyote na wanafanya mauzo na kisha kuzipeleka hati kwa watu wao pale Jiji. Watafutwe na nyaraka hizo zinyang’anywe ili wasiendelee kuuza viwanja," aliagiza Waziri Mkuu




MAKAMU wa Rais,  Dkt. Philip Mpango ameyapongeza Mashirika Yasiyo ya Serikali, (NGOs) kwa kazi kubwa wanayoifanya, wakiigusa jamii kwa njia mbalimbali. 

Ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2023 wakati akifungua jukwaa la mwaka la NGOs jijini Dodoma.

Aidha amesisitiza nia ya Serikali kuweka mazingira mazuri ya kufanikisha shughuli za NGOs na kuondoa changamoto zinazowakabili. 

Pia, alitoa wito kwa NGOs kuzingatia maadili ya Kitanzania na kuepuka kutumiwa kinyume cha sheria na mila za nchi.


Dkt akizungumzia kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, aliwapongeza NGOs zinazoshiriki katika kukabiliana na suala hili na kuwataka kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira. 


Aliunga mkono pendekezo la kuimarisha ushirikiano baina ya NGOs za Tanzania na nyingine duniani.


Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima  alisisitiza jukumu la Wizara yake katika kusajili na kuratibu shughuli za NGOs ili ziweze kuleta mchango wenye tija katika jamii.

 Alizungumzia juhudi za kuongeza uelewa kuhusu sera na sheria za kodi zinazowaongoza NGOs. Pia, alitaja juhudi za Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa NGOs, ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya uratibu katika sekta mbalimbali.


Kwa upandw wake , mMuu wa Mkoa wa Dodoma,  Rosemary Senyamule alimshukuru na kumpongeza Rais wa Tanzania kwa kuimarisha ushirikiano kati ya NGOs na Serikali.

 Alitambua mchango muhimu wa NGOs katika Mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla huku akikumbusha kuwepo kwa NGOs 415 zinazofanya vizuri katika maeneo mbalimbali ya sekta za kijamii.


Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Seif Shekalaghe alitangaza mafanikio ya kukamilisha ramani ya kidijitali ya utambuzi wa mashirika yasiyo ya Kiserikali, lengo likiwa kusaidia kuondoa changamoto za utekelezaji wa miradi inayofanana katika maeneo yanayofanana.


Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Dkt. Lilian Badi aliwakumbusha washiriki juu ya ukuaji wa sekta ya NGOs na mchango wao muhimu katika maeneo mbalimbali. 

Aliahidi kuendelea kushirikiana na Wizara husika kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.


Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Serikali,  Mwantumu Mahiza,  aliongelea umuhimu wa Serikali kuwaunga mkono NGOs, na kuwataka viongozi wa mikoa na wilaya kushirikiana kwa karibu na mashirika hayo ili kuleta maendeleo ya Taifa.




Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amechukua hatua kali kuhusu migogoro ya ardhi iliyozidi kwenye majiji ya Mwanza na Dodoma. Amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza kusimamisha kazi watumishi wawili wa Jiji la Mwanza na kuchukua hatua dhidi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa huo. Pia, ametoa agizo la kuendelea na ujenzi wa ghorofa kwenye viwanja namba 194 na 195 jijini Mwanza.


Wakati huohuo, ameamuru Jeshi la Polisi na TAKUKURU wawachunguze na kuwarejesha Dodoma watumishi 11 wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma waliotuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha na uporaji wa maeneo ya wananchi. Amesema hatua hizi zinachukuliwa kwa lengo la kurejesha nidhamu na uwajibikaji kwenye utumishi wa umma.


Waziri Mkuu pia ametoa agizo la kuhakiki matumizi ya fedha za mkopo wa Mradi wa Kukuza Miji (KKK) uliotumika kulipa fidia kwa ajili ya upanuzi wa ujenzi wa hoteli jijini Dodoma. Ametoa wito wa kuhakikisha maeneo ya umma kama shule, vituo vya afya, bustani, na masoko hayabadilishiwi matumizi bila idhini rasmi.


Kwa ujasiri na azma ya kusimamia masuala ya ardhi, Waziri Mkuu ameonyesha dhamira ya kupambana na ukiukwaji wa sheria na utumishi mbaya wa umma. Hatua hizi zinatuma ujumbe mzito kuhusu uwajibikaji na haki katika matumizi ya ardhi nchini Tanzania


 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa agizo la kuanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa Wakuu wa Mikoa nchini Tanzania, na kuwapa muda wa miezi mitatu kutekeleza agizo hilo. Hii ni kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025, na lengo ni kukuza uwezeshaji na kupunguza umaskini nchini.


Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi na watendaji wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuhakikisha huduma za uwezeshaji zinaimarishwa ili kufikia malengo ya kupunguza umaskini na kuendeleza uchumi wa nchi. Hii ni sehemu ya juhudi za kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025.


Tukio hili limejiri wakati Waziri Mkuu alipofunga Kongamano la Saba la Uwezeshaji Kiuchumi huko Dodoma, na amesisitiza umuhimu wa kutekeleza Ilani ya Chama ili kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi. Jukumu la kuanzisha vituo vya uwezeshaji ni sehemu muhimu ya mkakati huu wa maendeleo.


Hii ni hatua muhimu kuelekea kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania, na tunasubiri kuona jinsi mikoa itakavyotekeleza agizo hili katika miezi mitatu ijayo.

 


28 Septemba 2023, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasisitiza viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini Tanzania kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Ametoa wito huu akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Maulid lililofanyika kitaifa jijini Dodoma.



Ameeleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya yana athari kubwa kwa taifa, hasa kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa. Athari hizi ni pamoja na madhara ya kiuchumi, kiafya, na kimazingira, na pia zinaweza kuathiri uwezo wa mtu kufikiri.



Waziri Mkuu pia ametoa mwito kwa viongozi wa dini kuendelea kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii na kuhamasisha waumini kushiriki katika shughuli za kuongeza kipato. Amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani nchini, kwani amani ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa.


Kuhusu masuala ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, Waziri Mkuu ameuhakikishia umma kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya wale watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo haramu.


Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Alhaj Nuhu Jabir Mruma, aliyekuwa miongoni mwa wasemaji, aliipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali. Pia, aliiomba Serikali kuongeza wigo wa kutoa elimu ya uraia kwa kushirikiana na viongozi wa dini, ikiwa ni pamoja na kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024





Serikali imezidi kuimarisha upatikanaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), huku ikiwekeza jumla ya shilingi bilioni 80 kwenye miradi ya usambazaji wa umeme mkoani Kagera. Hatua hii muhimu inalenga kuwaletea wananchi nishati bora na kuchochea maendeleo katika maeneo ya vijijini.



Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema hayo  leo, Septemba 27, 2023, wakati Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dkt. Doto Biteko, walipowasha umeme katika vijiji vya Mubaba na Nyantakara, Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera.


Akifafanua, Mhandisi Saidy alitaja miradi inayotekelezwa kuwa ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, upanuzi wa umeme pembezoni mwa miji, ujazilizi, kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo, na kutoa umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.


Kati ya vijiji vyote 662 vilivyopo mkoani Kagera, asilimia 77.3 ya vijiji, sawa na vijiji 512, vimeshapatiwa huduma ya umeme kupitia miradi ya awali kama vile REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya Kwanza.


Wakala wa Nishati Vijijini umejitahidi kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwenye mkoa wa Kagera, ukilenga kuwapelekea wananchi nishati, na hivyo kuboresha huduma za jamii katika maeneo ya vijijini na vijiji-miji. Hatua hii inaonesha dhamira ya serikali katika kufikia malengo ya kutoa nishati bora kwa kila mwananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Endelea kufuatilia ili kujua matokeo ya jitihada hizi muhimu




Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka viongozi mbalimbali nchini  kuzungumza na wananchi suala la ukomeshaji wa unyanyasaji wa kijinsia ili kujenga jamii iliyo bora na inayojiamini.


Dkt.Biteko ambaye pia  ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, amesema hayo tarehe 25  Septemba, 2023 wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Bulega wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni siku ya Pili ya ziara yake katika Jimbo hilo.


“Viongozi wakati mnazungumza na wananchi kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo mkumbuke kueleza suala la ukomeshaji wa vitendo unyanyasaji wa kijinsia ili watu wajue kuwa vitendo hivi vinakera Taifa na hivyo sisi tunawajibu wa kulikemea suala suala hili.” amesema Dkt.Biteko


Dkt.Biteko amesema kuwa, vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ukatili wa wanawake na watoto pamoja na ubakaji vinakera, hivyo Taifa linapaswa  kuvikemea na kumtaka kila mwananchi kuwa makini na malezi ya watoto ili kutowaweka katika mazingira hatarishi.


Akizungumzia maendeleo ya Jimbo la Bukombe, Dkt.Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kuendeleza miundombinu ya barabara, afya shule na kueleza kuwa nia ya Rais ni kupelekea maendeleo watu wake hivyo amewaomba wananchi kumuombea na kuendelea kumuunga mkono.


Aidha amewapongeza madiwani wote katika Jimbo la Bukombe kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kusimamia miradi kwenye Sekta za elimu, afya, barabara na kwamba anaona fahari kuwa na madiwani hao pamoja na wananchi ambao wameonesha kuwa na uchungu na maendeleo yao na kizazi kinachokuja.


Dkt. Biteko ameahidi kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo  ambapo katika Kijiji cha Bulega ameahidi kukarabati shule ya sekondari kabla ya mwezi Januari 2024, kupeleka gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya Bulega na kuendelea kusambaza umeme.

 

Na Mwandishi wetu - Dar es salaam





Vijana nchini wamehimizwa kuepuka kutumika na baadhi ya watu wasio na nia njema ili kuvunja Amani ya Nchi hatua itakayosababisha maendeleo ya Taifa kuzorota.



Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichoshughulikia masuala ya Demokrasia ya Vyama vingi nchini katika Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini na Wadau wa Demokrasia Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi  na hali ya Siasa Nchini uliofanyika Jijini Dar es salaam.



 Dkt. Yonazi amesema vijana wana sehemu kubwa ya kuwajibika kuhakikisha Taifa husika linapata maendeleo na siyo  kutumika  kwa lengo la kuvunja mshikamano, umoja na upendo ulioanzishwa na waasisi.


“Kuhusu ushiriki wa vijana katika Siasa, Demokrasia na Uongozi Kikosi Kazi kilipendekeza kuwa, juhudi zinazofanywa na Serikali kuhusu ushiriki wa vijana katika siasa, demokrasia, uongozi, uchumi, ulinzi na usalama wa nchi yetu ziendelee na mikakati mipya ibuniwe ili kuongeza ufanisi na tija,” Amesema Dkt. Yonazi.


Pia ameeleza kuwa  Serikali inaendelea kuboresha Mikakati iliyopo na mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Vijana pamoja na mipango ya kuhamasisha ushiriki wa vijana katika siasa, demokrasia, uongozi, uchumi, ulinzi na usalama wa nchi.


Kuhusu elimu ya uraia  Katibu MKuu huyo  amebainisha kwamba ipo haja ya elimu ya uraia kutolewa kwa wananchi ili kuwajengea uwezo  kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa na kuwa na uelewa wa pamoja wa walengwa na elimu ya mpiga kura ifundishwe katika ngazi zote za mfumo wa elimu kuanzia shule za awali mpaka katika vyuo vya elimu ya juu.


“Serikali na wadau wengine waongeze kiwango cha ufadhili katika kutoa elimu ya uraia ikiwemo elimu ya mpiga kura, ili kukabiliana na upungufu wa rasilimali fedha, watu na vifaa katika kutoa elimu hiyo,” Amebainisha Katibu Mkuu huyo.


Aidha amehimiza ushirikishwaji wa  Watu Wenye Ulemavu katika Siasa, Demokrasia na Uongozi   kwa kuzifanyia maboresho Sheria zisizozingatia ujumuishwaji wa Watu Wenye Ulemavu akisema huzuia ushiriki wao katika siasa, demokrasia na uongozi ndani ya vyama siasa.



MKUTANO wa Kimataifa wa ITU (Shirika la Mawasiliano la Kimataifa) unaolenga kujadili maendeleo na changamoto zinazohusiana na teknolojia za mawasiliano na habari katika ngazi ya kimataifa umeanza rasmi jijini Arusha ukileta pamoja wataalamu wa teknolojia na mawasiliano kutoka sehemu mbalimbali za dunia. 



Mkutano huo wa  siku kumi,  umefunguliwa rasmi leo Septemba 13,2023 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhandisi, Kundo Mathew kikundi cha Utafiti cha ITU-T namba 20, kinachosimamia masuala ya Internet of Things (IoT) na miji smart, kinashikilia vikao vyake katika eneo hili la kuvutia. 


Vikao hivi vinaleta pamoja wataalamu na wabunifu kutoka kote duniani kujadili mwelekeo wa IoT na jinsi teknolojia hii inavyoweza kubadilisha jinsi tunavyoishi na kufanya kazi katika miji na jamii zetu. Mkutano huu wa ITU ni muhimu sana kwa Tanzania, kwani ni fursa kwa nchi hii kuonyesha uwezo wake katika uga wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT). 

Serikali ya Tanzania imeonyesha dhamira yake ya kukuza uchumi wa kidigitali na kuleta maendeleo katika miji yake kwa kuzingatia teknolojia za IoT na miji smart. 

Katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano, Naibu Waziri, Mhandisi, Kundo amesisitiza umuhimu wa IoT na miji smart katika kuongeza ufanisi wa huduma za serikali na ubora wa maisha ya wananchi wa Tanzania. 



Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari, aliwakaribisha washiriki wa mkutano huo na kuonyesha matumaini yake kwamba mkutano utacha ngia katika kuimarisha uchumi wa kidigitali wa Tanzania.

Mkutano huu wa ITU pia ni fursa kwa Tanzania kujifunza kutoka kwa nchi nyingine na kushirikiana ujuzi wake katika uga wa IoT na miji smart. 

Wataalamu na wabunifu kutoka Tanzania wanapata nafasi ya kujadiliana na wenzao kutoka sehemu mbalimbali duniani, na hii inaweza kusaidia kuchangia maendeleo ya haraka ya teknolojia hizi katika nchi.


Naye, Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, amesisitiza umuhimu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Ameeleza jinsi TEHAMA inavyosaidia kuharakisha huduma za kijamii na kufanya serikali kuwa karibu zaidi na wananchi. 

Profesa Mwamfupe pia alisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika miundombinu ya TEHAMA ili kufikia malengo haya huku akisema  kuwa jiji la Dodoma linajitahidi kuwa kiongozi katika matumizi ya TEHAMA kwa manufaa ya jamii yake.


Pamoja na majadiliano kuhusu IoT na miji smart, mkutano pia unajumuisha masuala mengine muhimu kama usalama wa mifumo ya IoT na faragha, standardization ya teknolojia hizi, na faida za kiuchumi zinazotokana na maendeleo haya. Kwa ujumla, Mkutano wa ITU ni fursa muhimu kwa wataalamu wa teknolojia na mawasiliano kutoka duniani kote kubadilishana uzoefu, kujadili maendeleo ya kiteknolojia, na kusaidia kuweka viwango vya kimataifa kwa teknolojia za IoT na miji smart.

Tanzania inaamini kuwa mkutano huu utasaidia kuwezesha maendeleo na matumizi ya teknolojia hizi za kisasa kwa manufaa ya jamii na uchumi wa nchi.



Wataalamu wanatarajiwa kujadili mikakati ya kukabiliana na vitisho vya mtandao na jinsi ya kuhakikisha kuwa mifumo ya kimtandao inakuwa na nguvu dhidi ya mashambulizi.

Mkutano wa ITU Arusha unafungua milango ya ushirikiano wa kimataifa na mawazo mapya katika ulimwengu wa teknolojia. Kwa pamoja, washiriki wanabaliana kuwa teknolojia ina jukumu kubwa katika kuboresha maisha ya watu na kuleta maendeleo. Mkutano huu ulitoa fursa ya kuweka malengo na mikakati ya kufanikisha hilo.

Tutabaki kufuatilia jinsi matokeo ya mkutano huu yatakavyoathiri maendeleo ya teknolojia katika kanda yetu na ulimwenguni kwa ujumla. Teknolojia inaendelea kubadilika kwa kasi, na mkutano wa ITU Arusha ulithibitisha kuwa tuko tayari kukabiliana na changamoto zinazotujia katika zama hizi za utandawazi.