JAJI RWAKIBARILA ATUBA OMBI LA KUVIBANA VYOMBO VYA HABARI

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha jana ilitupilia mbali ombi lililolenga kuminya uhuru wa vyombo vya habari lililowasilishwa mahakama na wakili wa wadai kwenye shauri la kupinga ubunge wa Godbless Lema , Alute Mungwai . Jaji wa mahakama hiyo , Gabriel Rwakibarila alitupa ombi la wakili huyo aliyetaka mahakama itoe karipio kwa vyombo vya habari kutokana na vichwa vya habari vinavyoandikwa kwenye magazeti kuhusiana na shauri hilo alivyodai kuwa vinaweza kuingilia maamuzi ya mahakama hiyo . Jaji huyo alisema kuwa kimsingi mahakama haifanyi maamuzi kwa kuangalia yaliyoandikwa magazetini huku akisisitiza kuwa ndiyo sababu kila wiki mawakili wa pande zote wanapewa nakala ya mwenendo wa kesi hiyo . “Umeisoma taarifa hiyo , umesoma kilichoandikwa mpaka mwisho? , je baada ya kuisoma habari yote inasema shahidi huyo ni muongo mpaka mwisho , kwanza mimi huwa sisomi magazeti hivyo usiwe na wasiwasi juu ya hilo na mahakama haifanyi maamuzi kupitia vyombo vya habari ndiyo sababu kila wiki nawapa nakala ya mwenendo wa kesi” . “Kabla sijawaonya waandishi au kuwakaripia nianze na nyingi mawakili , maneno yanayochukuliwa na waandishi mnayatamka ninyi nakumbuka vizuri mmoja wa mawakili ndiye alimwita shahidi muongo siyo kosa kwa mwandishi kuchukua maneno hayo kama habari” alisema jaji Rwakibarila . Jaji huyo alimkumbusha wakili Mungwai kuwa hata Februari ,9 mwaka huu walipokutana faragha kwa pamoja mawakili na waandishi wa habari ofisini kwake na kuzungumzia suala la uandishi wa vichwa vya habari magazetini , waandishi hao walilifafanua vizuri kuwa jukumu la kuweka vichwa vya habari si la kwao bali ni la wahariri na wasaidizi wao ambao ni wengi . Awali wakili Mungwai alilalamika mahakamani hapo kuwa vichwa vya habari kwenye magazeti vilikuwa vinaingilia mwenendo wa kesi huku akionyesha gazeti la Nipashe la Februari 24 , mwaka huu lililokuwa na kichwa cha habari “ kesi ya Lema Shahidi muongo” . Hata hivyo wakili huyo alisema kuwa anakubaliana na melezo yaliyokuwa kwenye taarifa hiyo kuwa ni sahihi isipokuwa kichwa cha habari ndicho alidai kuwa kinaweza kuingilia maamuzi ya mahakama kwenye shauri hilo . Wakili wa Lema , Method Kimomogoro alimwita shahidi wa sita , Said Athuman muongo baada ya kudai kuwa alihudhuria mikutano ya vyama vya CCM na TLP katika eneo la Kwa Mromboo mwezi Agosti, mwaka juzi, wakati ratiba inaonyesha vyama hivyo havikuwa na mikutano eneo hilo mwezi huo wote . Katika hatua nyingine shahidi wa nane kwenye shauri hilo , Agrey Mushi aliieleza mahakama kuwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo waliochangia chama hicho kupoteza jimbo la Arusha Mjini . Shahidi huyo aliyasema hayo wakati alipokuwa akihojiwa jana na wakili wa lema , Kimomogorombele ya jaji Rwakibarila ambapo alisoma taarifa toka kwenye mtandao wa Vijimambo iliyokuwa ikimnukuu katibu wa CCM mkoani hapa , Mary Chatanda akikanusha madai ya yeye kuhusika na kupoteza jimbo la Arusha mjini na kuwatumpia mzigo aliyekuwa katibu wa CCM wilayani hapa , Salum Mpamba na msimamizi wa uchaguzi . “ Mimi nilikuwa mtendaji wa wilaya zote mkoa wa Arusha hivyo kama ni lawama walipaswa kupewa aliyekuwa katibu wa CCM wilaya ya Arusha , Salum Mpamba na mkurugenzi wa uchaguzi “ Mushi alinukuu taarifa hiyo iliyotolewa na Chatanda miezi saba baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu . Kesi hiyo iliyofunguliwa na wapiga kura watatu , Mussa Mkanga , Agenss Mollel na Happy kivuyo inaendelea leo kwa shahidi wa tisa kuendelea kutoa ushahidi wake . MWISHO

0 Comments:

Post a Comment