HABARI KAMILI TUKIO LA BOMU ARUSHA

MATUKIO ya milipuko ya mabomu yameendelea kulitikisa jiji la Arusha baada ya watu 17 waliokuwa wakiangalia mpira kwenye baa ya Arusha Night Park, iliyopo maeneo ya Mianzini kujeruhiwa vibaya na kitu ni kinachosadikiwa kuwa ni bomu.

Tukio hilo lilitokea April 13, mwaka huu majira ya saa kati ya saa 1:30 na saa 2:00 usiku ambapo kitu hicho kinachodhaniwa kuwa bomu kililipuka eneo la katikati ya baa hiyo kulipokuwa na mkusanyika mkubwa wa watu.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas aliyekuwa eneo la tukio  na kikosi cha ukaguzi wa mabomu,aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamekubaliana Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo ndiye atakayetoa taarifa rasmi juu ya tukio hilo.

Hata hivyo waandishi wa habari walioenda kwenye ofosi za mkuu huyo wa mkoa ili kupata taarifa hiyo, Mulongo aliwataka watawanyike mpaka majira ya 7:00 mchana anapotarajia kutoa taarifa rasmi kupitia afisa habari wa mkoa ambapo mpaka tunaenda mitamboni hakuwa ameitoa.

Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa na mganga mkuu wa mkoa, Dk.Frida Mokiti alisema kuwa kwenye hospitali ya mkoa ya Mount Meru walipokea majeruhi 17.

Alisema kuwa kati ya hao watano walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka, mmoja alihamishiwa hospitali ya Selian na 11 wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo ambao wengi majeraha yao makubwa yapo miguuni na kwenye mapaja huku mmoja kati yao hali yake ikidaiwa kuwa mbaya.
Dk Mokiti ambaye hakuwa tayari kutaja jina la mgonjwa huyo ambaye hali yake ni mbaya alisema kuwa mfupa mdogo kwenye mguu wake mmoja umesagika hivyo wanafanya  mawasiliano na Wizara ya Afya ili watapate maelekezo ya kufanya ikiwemo kumwamisha hospitali aende nyingine itakayomuwezesha kupata matibabu zaidi.

Aliwataja  majeruhi wanaoendelea kupata matubabu hospitali ya hapo  kuwa ni pamoja na Christian Mmasi, Ally Sudi, Evarest Kaaya, Evance Maleko, (24)Pius Shayo, Peter Mkereme, (25), Obeid Mbasha, Anteriue Mganda, Loice John, (29), Suzan Jacob (31) na Joyce William, (29).
Kwa upande wake mganga wa zamu kwenye hospitali ya Selian, Dk. Peter Mabula, alithibitisha kuwa walipokea majeruhi mmoja na hali yake inaendelea vizuri ingawa hakuwa tayari kutaja jina lake.
MAJERUHI WAZUNGUMZA
Majeruhi, Obeid Mbasha, ambaye amelazwa kwenye wodi ya majeruhi ya hospitali ya Mt Meru alisema kuwa yeye alikwenda kwenye baa hiyo kwa lengo la kuangalia mpira kombe la Ulaya ambapo wakati mpira ukiendelea alisikia mlio mkubwa uliombatana na kishindo.

Alisema kuwa alishangaa kuona watu wamelala chini wengine wakilia huku baadhi yao wakikimbia huku kukiwa kumetapakaa damu kila mahali.
"Niliinuka ili na  mimi nikimbie lakini sikuweza badala yake nilianguka chini hapo sasa nikaanza kuhisi maumivu kwenye goti nilipogusa nikaona damu nyingi zinatoka ndipo baada ya muda walikuja watu kunibeba na kunileta hapa hospitali,"alisema Mbasha.



MMILIKI AZUNGUMZA
Kwa upande wake Mkurugenzi  wa baa hiyo, Joseph Karugendo alisema kuwa anaamini waliohusika na tukio hilo lililojeruhi wafanyakazi na wateja wao watapatikana kwani wamefunga mitambo ya kufuatilia matukio wa CCTV.

"Baada ya tukio lile polisi walifika wakazingira eneo lile hivyo leo asubuhi (jana) polisi wameondoka na 'monitor' ya CCTV pamoja na mfanyakazi wetu mmoja kwa lengo la kwenda kufanyia uchunguzi wa picha hizo," alisema mkurugenzi huyo wakati akiongea na Tanzania Daima kwa njia ya simu.

Alisema kuwa mpaka sasa hajajua ni hasara kiasi gani wamepata kutokana na tukio hilo alilodai kuwa pia limewaharibia biashara kwani bado polisi hawajawaruhusu kuingia ndani ya eneo hilo.
"Kwa juu juu vitu nilivyoona vimeharibika ni pamoja na makabati ya kuwekea vyombo, viti, meza, sehemu ya dari nimeona limeshuka, fedha za vinywaji na vyakula walizokuwa wamekunywa wateja.
"Fedha nyingine za mauzo walikuwa nazo wahudumu ambao kwa sasa ni wagonjwa na wako hospitalini hivyo si uungwana kuwafuata hospitali kuwauliza mauzo," alisema Karugendo.

Alisema kuwa wakati tukio hilo la kusikitisha likitokea hakuwepo ambapo alisema kuwa wafanyakazi wake saba wamejeruhiwa pamoja na wateja kadhaa waliokuwepo.

Kwa upande wake mmoja wa wahudumu wa baa hiyo, Aneth Mushi, alisema kuwa wakati wa tukio alikuwa amekwenda jikoni kuchukua chakula cha wateja wake ambapo wakati akibeba sahani,ghafla alisikia kishindo na kelele za watu wakomba msaada jambo lililomfanya  alimwage chakula na kukikmbia.

"Kwa kweli nasikitika sana watu wameumia na mimi ni Mungu tu kaniokoa vinginevyo na mimi ningeweza kuwa i mmoja wa majeruhi,"alisema Mushi.

Awali Mkuu wa Mkoa , Mulongo, alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari juzi  mara baada ya kutokea kwa tukio hilo akidai kuwa  kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi wa awali ni kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.
MBUNGE WA ARUSHA MJINI ANENA
Kwa upande wake mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA) alitoa salamu za pole kwa familia za wahanga wa tukio hilo alilodai kuwa linaongeza mashaka makubwa miongoni mwa wananchi wa jiji hilo juu ya usalama wao.
"Maisha yanaendelea kuwa magumu katika fikra za Watu kwani milipuko kama hii ilianzia Kanisani halafu ikafuata katika Mkutano wa hadhara wa Chadema na sasa ni kwenye Bar za Pombe , sijui ni nini kinaendelea Arusha , lakini ni vyema muda wa kutafakari ukaongezewa nafasi . Kama Mbunge sina neno zaidi mpaka nitakapokuwa nimefika Arusha  nakuona na kutafakari'" alisema Lema.

Hili ni tukio la tatu la bomu kutokea kwenye jiji la Arusha kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo jumla ya watu saba wamepoteza maisha huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa.

Katika tukio la April 4, mwka jana bomu lilirishwa kwenye kanisa la Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi ambapo jumla ya watu watatu walifariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Tukio la pili ni lile la juni 15, mwaka jana ambapo bomu lilirushwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) kwenye viwanja vya Soweto ambapo jumla ya watu wanne walifariki dunia akiwemo mwanamke mmoja na watoto watatu.

Hata hivyo tayari mtu mmoja amefikishwa mahakamani kuhusiana na tukio la bomu kanisni ambap kwa upande wa wale waliohusika na bomu la mkutano wakiwa hawajapatikana licha ya chama hicho kutoa tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la polisi kuhusika hali waliyoshinikiza Rais kuunda tume ya kimahakama ili wawataje ma kutoa uthibitisho wa picha za video jambo ambalo halijafanyika.

Hata hivyo, Desemba 18, mwaka jana wakati wa uzinduzi wa kanisa la Olasiti Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mulongo alijigamba kuwa yeye kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama eneo hilo liko salama.

"Tunahesabu kosa pale linaporudiwa, nawaambia wale waliolipua siku ile wangejaribu tena wangeona, naomba niwahakikishie kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa huu kuwa mko salama" alisisitiza Mulongo

0 Comments:

Post a Comment