WAKUU wa Nchi za Jumuiya yaAfrika Mashariki, (EAC), wameliagiza Baraza la Mawaziri la EAC, linaloundwa na Mawaziri wanaowakilisha nchi zao kwenye jumuiya hiyo kuwezesha kuanza mchakato wa uandishi wa katiba kwa ajili ya Shirikisho la Kisiasa kwa kuonyesha njia juu ya mambo muhimu yatakayohusika.
Aidha wamezindua mtandao wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EACJ), jambo litakalowezesha wananchi toka nchi wanachama kufungua mashauri wakiwa kwenye nchi zao bila kulazimika kuja zilipo ofisi za mahakama hiyo.
Hayo yamefanyika kwenye mkutano 12 wa wakuu wa Nchi za EAC, uliofanyika jijini hapa chini ya Mwenyekiti wao, Uhuru Kenyatta ambapo Marais waliohudhuria nia , Jakaya Kikwete wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda huku Rais wa Burundi, akiwakilishwa na Makamu wake, Prosper Bazombaza na Rais wa Rwanda akiwakilishwa na Waziri Mkuu, Pierre Habumuremyi.
Marais hao waliagiza baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo kufanya tathmini ya utekelezaji wa protoko zilizoanzishwa za Soko la pamoja , ushuru wa Forodha na Sarafu moja na kuwasilisha taarifa kwenye kikao kingine cha wakuu wa nchi kinachotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Kikao hicho kimewaapisha majaji wapya, Edward Rutakangwa na Aaron Ringera kutoka Kenya watakaoanza kazi rasmi June 3, mwaka huu kujaza nafasi za majaji wanaomaliza muda wao akiwemo Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, (EACJ), Harold Nsekela na makamu wake, Philip Tunoi.
Pia Kwenye mkutano huo wa jana jaji, Fakihi Jundu kutoka Tanzania aliapishwa kuwa jaji kuchukua nafasi ya jaji, John Mkwawa anayemaliza muda wake wa kuhudumu kwenye mahakama hiyo utamalizika juni 27,mwaka huu.
Wakuu hao wa nchi waliridhia, Jaji Dkt. Emmanuel Ugirashebuja kuwa Rais wa Mahakama ya Jumuiya hiyo na jaji Liboire Nkurunziza kuwa makamu wake huku wakihuyisha mkataba wa naibu Katibu Mkuu, Dkt. Enos Bukuku kwa kipindi kingine cha miaka mitatu ambacho ni cha mwisho.
Wameazimia vyombo vya usalama vya nchi wanachama kuungana katika kukabiliana na matukio ya uhalifu na ugaidi kwenye nchi wanachama pamoja na zile za maziwa makuu.
Wakuu hao wa nchi waliipongeza Tanzania kwa kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar huku wakiuelezea kuwa ni mfano wa kuigwa katika kuleta mtangamano na Umoja barani Afrika.
0 Comments:
Post a Comment