Japan na China kuboresha mahusiano yao


Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe ameahidi kuendelea kufanyia kazi kuendeleza zaidi maendeleo katika uhusiano wa nchi yake na China.

Abe alizungumza kwenye hafla iliyofanywa na ubalozi wa China jijini Tokyo jana Alhamisi. Tukio hilo lilikuwa la kuadhimisha siku ya taifa ya China na miaka 45 ya kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Japani na China.

Abe alisema yeye na Rais Xi Jinping wa China walikubaliana nchini Ujerumani mwezi Julai mwaka huu, kufanya majadiliano zaidi ya viongozi wakuu wa nchi hizo mbili. Huo ulikuwa ni mkutano wa tano wa viongozi hao wawili.

Abe alisema amelenga kufanya mkutano wa pande tatu utakaojumuisha viongozi wakuu wa China na Korea Kusini nchini Japani mwaka huu na kumkaribisha Waziri Mkuu wa China Li Keqiang kwenye mkutano huo.

Abe alisema anatamani kuitembelea China baada ya mkutano huo na angependa Rais Xi atembelee Japani pia hapo baadaye. Abe aliongeza kuwa anatumai kuendeleza mbele ushirikiano wa pande mbili kupitia kutembeleana kwa viongozi hao wakuu.

Akitilia maanani suala la Korea Kaskazini, alisema hali ya sasa huko kaskazini mashariki mwa Asia inamaanisha kuwa kuboresha ushirikiano wa Japani na China ni muhimu si tu kwa mataifa hayo mawili lakini pia kwa amani na uthabiti wa eneo hilo.

0 Comments:

Post a Comment