Marekani yalaani Kauli za Kim

Marekani imelaani maoni ya afisa wa Korea Kaskazini kuwa nchi yake huenda ikafanya jaribio la bomu la haidrojeni kwenye Bahari ya Pasifiki.

Susan Thornton ambaye ni kaimu msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje kwa eneo la Mashariki mwa Asia na Pasifiki, aliwaambia waandishi wa habari jana Ijumaa kuwa kama jaribio hilo litafanyika litakuwa ni kitendo cha kichokozi ambacho hakijawahi kufanyika na kitasababisha jumuia ya kimataifa kuchukua kwa pamoja hatua kali na thabiti.

Kiongozi Mkuu wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alisema mapema kuwa nchi yake inaangazia kuchukua "msimamo wa jibizo la kiwango cha juu kuwahi kufikiwa katika historia" kama jibizo kwa hotuba ya Rais Donald Trump aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Alipoulizwa zaidi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini Ri Yong Ho aliashiria kuwa hatua za jibizo za Kim huenda ikawa ni jaribio la bomu la haidrojeni kwenye Bahari ya Pasifiki. 

Thornton alisisitiza kuwa Marekani itaendelea kuiwekea shinikizo na kuitenga Korea Kaskazini.

Wasiwasi unazidi kuongezeka kati ya Marekani na Korea Kaskazini.

0 Comments:

Post a Comment