MAHAKAMA ya hakimu mkazi Arusha imewahukumu kifungo cha miaka 235 jela washitakiwa sita waliokuwa wafanyakazi wa benki ya Exim tawi la Arusha baada ya kuwatia hatiani na makosa 15 ya utakatishaji fedha haramu na 40 ya kughushi na kuharibu nyaraka za benki.
Washitakiwa , Daudi Nhosha na Genes Masawe wamehukumiwa kwenda jela miaka minne kila mmoja baada ya kukutwa hatiani na kosa moja la kughushi huku mshitakiwa wa saba Dorothi Chijana akihukumiwa miaka 72 jela kwa kukutwa na hatia na makosa 18 ya kughushi.
Aidha imewaachia huru washitakiwa wengine saba baada ya kukosekana ushahidi wa kuwaweka hatiani.
Uamuzi huo umetolewa leo na Kaimu hakimu mkazi mfawidhi, Desder Kamugisha aliyesikiliza shauri hilo la jinai namba 309/2013 ambaye alitumia zaidi ya saa nne kusoma uamuzi huo kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa nane mchana.
"Hii ni organized crime na yamefanyika kwa series ya muda mrefu natunataka kudiscourage ualifu wa namna hii. Hivyo kwa makosa yote ya utakasaji fedha haramu kila kosa wataenda jela kwa miaka mitano kulingana na walivyotiwa hatiani," alisema hakimu Kamugisha.
Alisema kwa makosa ya kugushi na kuharibu nyaraka za benki kila kosa wataenda jela miaka minne.
Kulingana na uamuzi huo mshitakiwa namba mbili, Lilian Mgeye anaenda jela miaka 98 kwa kutiwa hatia kwenye makosa 10 ya kutakatisha fedha haramu na 12 ya kughushi nyaraka za benki .
Mshitakiwa Deusdedit Chacha amehukumiwa miaka 45 jela baada ya kutiwa hatiani kwenye makosa matano ya kutakasa fedha haramu na matano ya kughushi nyaraka za benki.
Mshitakiwa mwingine Christopher Lyimo alihukumiwa kwenda jela miaka 12 baada ya kuwekwa hatiani kwenye makosa manne ya kughushi nyaraka za benki.
Hata hivyo alisema kuwa adhabu zote zinaenda pamoja hivyo watatumikia kifungo cha juu cha miaka mitano kwa waliotiwa hatiani kwa makosa ya kutakatisha fedha haramu na miaka minne kwa walikutwa na hatia kwenye makosa ya kughushi na kuharibu nyaraka.
Washitakiwa hao alikuwa wanakabiliwa na mashitaka 318 utakatishaji fedha haramu,kughushi nyaraka,kuharibu nyaraka na wizi wa zaidi Shilingi Biloni Saba katika benki hiyo.
Washitakiwa walioachiwa huru ni Bimal Gondalia, Neema Kinabo, Livingston Julius, Evance Kashebo, Tuntufye Agrey, Josephat Neki na Gervas Lubuva.
Aidha katika kesi hiyo jamhuri walikuwa na vielelezo 20 ikiwemo benki slip za malipo ya wateja wa kampuni mbalimbali za kitalii,zilizokuwa zikilipwa katika benki hiyo kwa ajili ya wageni wa nje waliokuwa wakienda katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA),vocha na nyaraka nyingine ziliwasilishwa.
0 Comments:
Post a Comment