FAMILIA ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu imeelezea kusikitishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linavyowapiga danadana kulipia matibabu ya ndugu yao licha ya kutekeleza masharti yote waliyowapa.
Wamekitaka chombo hicho cha kutunga sheria kugharamia matibabu hayo hata kama wanamuona Lissu ni mwiba kwao kwani ni haki yake kutibiwa na bunge kwa mujibu wa sheria
Aidha wameeleza kuwa Lissu anaendelea vizuri na wanajadiliana kuona namna watamsafirisha nje ya bara la Afrika kwa matibabu zaidi.
Msemaji wa familia, wakili, Alute Mughwai ameyasema hayo leo jijini Arusha ikiwa ni siku 100 zimepita tokea Lissu ashambuliwe kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiofahamika wakati akiingia nyumbani kwake mjini Dodoma.
“Lisu anaendelea vizuri, amepona hana bandeji wala hatumii dawa na bado yuko kwenye uangalizi wa madaktari akifanya mazoezi madogo,” amesema Mughwai
Amesema jumapili anaenda Nairobi akakutane na Lissu pamoja na mke wake ili wajadili kuona kama asafiri kwa matibabu nje ya bara la Afrika kwa sasa au atasubiri msimu wa sikukuu upite ili mapema mwakani ndiyo aende kwa matibabu.
Akizungumzia danadana ya bunge katika kugharamia matibabu ya Lissu, wakili Mughwai anasema licha ya uongozi wa bunge kufanya kikao na familia pamoja na Chadema Oktoba 2, mwaka huu lakini mpaka sasa hawajalipa.
“Wakatuambia tuandike barua ya kuanza mchakato tuliandika hiyo barua, tukawapatia bunge tukapeleka nakala kwa spika akanianiambia alikuwa ziarani Urusi ni kweli akaniambia subirini nirudi,” alisema Mughwai na kuongeza.
Aliporudi akaniambia kuna kuna mabadiliko ya katibu wa bunge hivyo Katibu mpya, Steven Kigaigai atatakiwa kueleweshwa jambo hilo baada ya muda nilipofuatilia kwa katibu mpya akasema yeye hajaona barua, yetu ya oktoba 18 na tuliipeleka kwa DHL na ilipokelewa”.
Wakili Mughwai anasema walipofuatilia zaidi wakambiwa hiyo barua imepatikana ila katibu wa bunge kwani hayupo ameenda Songea kwenye msiba wa mbunge Leonidas Gama.
“Baadaye wametuletea barua nyingine wakisema wameipata barua yetu ya awali wakatutaka tufafanue haki za Lissu tunazozitaka ..tumetoa ufafanuzi tunasubiri hatutarijii kutatokea kisingizio kingine kutoka uongozi wa bunge,”. anasema Mughwai na kuongeza.
Lissu atakuwa ni mbunge wa kwanza katika nchi hii atakuwa amelazwa hospitalini kutokana na shambulio la kihalifu lakini atakuwa si mbunge wa kwanza kuhitaji kutibiwa kwa gharama za bunge baada ya kuugua ,”.
Wakili Mughwai amesema Desemba 4,mwaka huu ndiyo bunge wamewaandikia wakihoji ni haki zipi wanazidai ambapo wameijibu leo na wameipeleka kwa njia ya DHL.
“Kama familia hatukuona kama familia ya bunge kututaka tuainishe haki anazostahi Tundu kuzipata kama mgonjwa wakati kwenye barua tuliwaeleza haki zote kulingana na sheria za bunge na katiba ya nchi,” alisisitiza Mughwai ambaye pia ni wakili maarufu jijini hapa.
Haki ya matibabu, posho za mbunge huyo na mke wake anayemuuguza ambazo alisema hawezi kutaja kiwango kwa kuwa inajulikana kwa mujibu wa sheria na kanuni za bunge ambapo alifafanua hakuna haki ya ziada ambayo Lissu anadai .
0 Comments:
Post a Comment