LOWASSA KIGWANGALA HAPATOSHI





SAKATA la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangala kuwataja Mawaziri Wakuu Wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kuwa ni miongoni mwa wakazi 83 waliovamia eneo la Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro limechukua sura mpya baada ya kumuibua msemaji wa familia ya Lowassa, Fredrick Lowassa aliyedai waziri huyo anakutupuka na anatumia madaraka yake vibaya.

Msemaji huuo ambaye ni mtoto wa Lowassa alitoa tamko hilo jana muda mfupi baada ya kusambaa kwa video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Waziri Kigwangala akimtaja Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa kuwa ni miongoni mwa watu waliovamia eneo hilo.

Alisema anauhakikishia  umma kwamba yote aliyosema Waziri Kigwangala hayapo na endapo kama yapo wako tayari Waziri huyo afanye lolote lililo chini ya mamlaka yake badala ya kurejea miaka ya nyuma alikodai Waziri huyo  na wenzake kadhaa walifanya bila mafanikio kuchafua heshima za viongozi wote anaowataja bila sababu .


Fredick alidai Waziri  Kigwangalla alimtaja Lowassa kama mmoja ya watu walioshiriki kupora ardhi  Arusha jambo alilodai kuwa amesikitishwa na matamshi hayo kutolewa na  waziri ambaye kwa wadhifa wake hakupaswa kutoa kauli zisizo na msingi wowote na zilizolenga kulaghai Umma.

"Nimemfahamu Mhe Kigwangalla kwa miaka mingi, tangu wakati anavurugana na mbunge mwenzake wa Nzega na rafiki yangu Mhe Hussein Bashe kule Nzega.Kwa maoni na mawazo yangu nimekuwa nikiamini kwamba Kigwangalla atakuwa mtu aliyebadilika na kujifunza kutoka na makosa yake ya nyuma," alisema Msemaji wa familia ya Lowassa na kuongeza.

Kauli yake ya leo ni ushahidi kwamba bado ana matatizo yale yale ya kukurupuka. Ni wazi hata baada ya mambo mengi kubadilika na pengine nyakati za kuchafua watu kukoma, ndugu huyu bado anaishi nyakati zile zile,".

Ni wazi Kigwangalla anatumia vibaya dhamana aliyopewa na Rais Magufuli , kwa mambo ambayo Wizara ya Ardhi ina Wataalamu na uwezo wa kuchukua hatua stahiki kwenye mgogoro wowote.Nikiwa kama Msemaji wa Familia  ninazo katika kiganja cha mikono yangu taarifa zote za umiliki wowote unaomgusa Lowassa,".

Ninaweza kuuhakikishia umma kwamba yote aliyosema Waziri Kigwangala hayapo, na kama anayo basi sisi tuko tayari afanye lolote lililo chini ya mamlaka yake badala ya kurejea kule tulikopita ambako yeye na wenzake kadhaa walifanya bila mafanikio kuchafua heshima za wote anaowataja bila sababu .

ALICHOZUNGUMZA KIGWANGALA

"Inabidi wewe uzifumue kama mimi hapa najua kuna Sumaye, kuna Lowassa, kuna Ole Njolai, (Daniel , aliwahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha), sijui kuna Mshana, inabidi niseme wazi, nikisema watu watasema duh kumbe anajua zaidi ya kile alichokisema," anasikika Waziri Kigwangala akiongea kwenye video hiyo wakati akiongea na Mkurugenzi Mkuu wa NCAA, Dk Freddy Manongi akiwa na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa NCAA aliyoizindua rasmi jana na kuongeza

Wakishaelewa hivyo sasa watakaa kwenye mstari ukishaamua  kufanya unafanya lakini sasa hivi hawawezi kukuonyesha mfano kama watu wako tokea jana wapimaji hawakuja leo nimesema paandaliwe ili bodi waone hawaleti vipimo,".


Awali juzi Waziri Kigwangala Waziri Kigwangala alidai kuwa  kuna taarifa kwamba kati ya mwaka 1995 na 1996 eneo  la ekari 20 kati ya 40 zinazomilikiwa na NCAA liligawanya  kinyemela kwa hizo kaya 83 lakini walioshiriki kugawa ambapo mpaka sasa hawajathibitisha  ila taarifa alizo nazo ni kwamba ni watu wa ndani wa taasisi hizohizo tatu ambazo zina mgogoro wa eneo hilo.

"Taarifa tulizo nazo ni kuwa ilitengenezwa 'syndicate' ya maafisa kutoka  Bodi ya Utalii Tanzania na maafisa kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro lakini pia maafisa kutoka Wizara ya Ardhi. Ni taarifa ambazo hatujazithibitisha ... lakini maafisa hao walitengeneza taratibu za kihuni za kugawana eneo hilo," alisema  Waziri Kigwangala huku akisisitiza kuwa muda si mrefu ukweli utajulikana.

Alisema amewasiliana na Waziri wa Ardhi, William Lukuvi ambaye amemuagiza Kamishina wa Ardhi aitishe watu wote ambao wanamgogoro na eneo hilo la Serikali wapeleke nyaraka zao kwa kamishina wa ardhi zoezi linalotarajiwa kufanyika wiki ijayo.

"Na sisi tutabaini ukweli kwamba hawa waliopo hapa ni kina nani manake kuna maneno yanasemwa kuna baadhi ya Mawaziri Wakuu Wastaafu wawili wanamaeneo yao, baadhi ya maafisa waliokuwepo zamani wa hifadhi ya Ngorongoro, kuna baadhi ya maafisa wa Bodi ya Utalii zamani wanayo maeneo yao hapa lakini kwa sababu hatujui majina yao hatuwezi kusema ni akina nani lakini tuna taarifa hizo," alisema Kigwangala.

Alisema kuwa watu hao majina yao yatakajulikana kwa kamishina wa ardhi watachukuliwa hatua za kisheria kwa kutumia vibaya madaraka yao na wavamizi wengine wataondolewa kwenye eneo hilo walilovamia au watatakiwa kulipa fidia.

Hata hivyo alisema kuwa wanaangalia kama wataona eneo lililobaki la ekari 20 linawatosha NCAA kwa mipango waliyojiwekea basi watakubaliana na kulipwa fidia lakini ikiwa watahitaji eneo lote la ekari 40 itawabidi kuwandoa wakazi hao na kuvunja nyumba hizo.

"Eneo hili ni 'potentia' sana ni very 'prime' kwa hapa Arusha lina 'attract' bei ya juu sana kwa mauzo kwa mimi binafsi hainishangazi kuona viongozi wa zamani wakishirikiana na maafisa wa zamani wali 'conspire' kugawana eneo hili kinyemela ni jambo la kawaida tu ambalo kwa watu wenye tamaa wanaweza kufanya," alisisitiza Waziri Kigwangala.

Kiwanja hicho namba 4091 kilichopo Njiro  kilikuwa chini ya shirika la Utalii Tanzania, (TTC) ambapo mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati wa ubinafsishaji iliamriwa mali zote sasa Bodi ya Utalii nchini,(TTB).

Waziri Kigwangala alisema kuwa mwaka 2006 Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma,(PSRC ), walitangaza kuuza mali zilizokuwa chini ya TTB ikiwemo kiwanja hicho ambacho kilinunuliwa na  NCAA kwa shilingi bilioni 1.8 ambapo kwenye eneo hilo kulikuwa na nyumba na vitu vingine lakini mpaka sasa hawakuliendeleza.

Alisemamkuwa Mwaka 2016 wakati ngorongoro wanataka kuendeleza eneo hilo kuliibuka migogoro miwili, TTB waliendelea kutambua eneo hilo kama mali yao huku eneo lingine likigawanywa na halmashauri ya manispaa ya Arusha kwa ajili ya makazi ya wananchi.

"Ikalazimika ifanyike 'official search' kwa Kamishina wa Ardhi wa kanda hii (Kaskazini) ambaye ofisi zake ziko Moshi. Ramani aliyo nayo ni ya ekari 40  na umiliki wake uko kwa jina la TTB ambalo hili liliuzwa kwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kule haitambuliki hizi ekari 20 zilizopo hapa zipo kwa makazi ya wananchi na kuwa  na kuna wakazi wamegaiwa.," alisema Waziri Kigwangala na kuongeza.

Hivyo ni wazi kabisa eneo hili la hekta 10 karibu ekari 20 imegawanywa kwa matumizi ya makazi ambayo ndani yake kuna kaya 83 ambazo ziligawanywa na Halmashauri ya manispaa ya Arusha ni eneo la uvamizi.Hivyo hizi familia 83 ambazo zimevamia hapa hata kama wanahati yoyote ni hati ya kihuni ni hati isiyotambulika hivyo ni wavamizi kama wavamizi wengine tu,"



0 Comments:

Post a Comment