UNDANI SABABU ZA MAWAKILI WA LEMA KUKATAA VIELELEZO VYA JAMHURI VISIPOKELEWE MAHAKAMANI


Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema akitoka mahakama ya wilaya ya Arusha akiwa ameambatana na Mke wake, Neema.

MAWAKILI wa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), kwenye kesi ya uchochezi anaodaiwa kuufanya kupitia  ndoto yake dhidi ya Rais John Magufuli, wamewasilisha   pingamizi kuitaka mahakama isipokee vielelezo viwili mkanda wa video, (video cassette) na CD vilivyotaka kuwasilishwa  na shahidi waliyedai hana sifa kisheria kwani hakuhusika katika kupiga picha hizo.


Wakili wa Lema, John Mallya aliwasilisha pingamizi hilo Februari 23, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Devota Msofe, anayesikiliza shauri hilo namba 440/2016 wakati shahidi wa sita wa Jamhuri kutoka idara ya uchunguzi wa picha za video na kawaida, kupiga picha za matukio ya uhalifu, kufanya uchunguzi wa ajali na sauti,  Inspekta Aristides Kasigwa alipotaka kuwasilisha vielelezo hivyo.

Wakili Mallya alidai shahidi ameshindwa kuonyesha mahusiano yaliyopo baina yake na vielelezo anavyotaka kuwasilisha kama sheria inavyotaka kielelezo kiwasilishwe na aliyekirekodi kwenye tukio na kukiaanda.

Kwa upande wake Wakili wa utetezi, Sheki Mfinanga alisema shahidi huyo hastahili kuwasilisha vielelezo hivyo kwani sheria inataka shahidi anayetoa kielelezo cha vifaa vya kielektroniki anatakiwa aeleze historia ya kielelezo hicho kuanzia kilipochukuliwa mpaka kilipohamishiwa  na hatakiwi kutoa ushahidi wa kuambiwa jambo alilodai kuwa shahidi huyo hakuwa eneo iliporekodiwa mkanda huo wala hakuhusika kuusafirisha mpaka Dar es Salaam hivyo hawezi kukithi matakwa ya sheria.

Kwa upande wake wakili wa Serikali, Agnes Hyera, ambaye aliomba mahakama iharishwe kwa nusu saa ili aweze kuwasilisha hoja za majibu ambapo aliporejea alipinga hoja za mawakili wa utetezi kwa madai kuwa shahidi wao yuko sahihi kisheria kuwasilisha vielelezo hivyo kwani ndiye aliyevifanyia kazi.

"Wanasema shahidi wa nne (H 2261 Mongo) ndiyo alipaswa kuutoa mahakamani kwa kuwa ndiyo alipiga picha lakini shahidi huyo wa nne aliieleza mahakama baada ya kurekodi mkanda wa video aliupeleka kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa, (RCO), kisha ukapelekwa Dar es Salaam kwa uchunguzi," alidai wakili Hyera na kuongeza.

Shahidi wa sita (inspekta Aristides) ameeleza alipokea kielelezo hicho akakifanyia uchunguzi, akakiweka kwenye bahasha akafunga na seal  (lakiri) akairudisha kwa RCO, sasa shahidi wa nne kingemfikiaje? Shahidi wa sita ameonyesha hapa mahakamani akifungua lakiri baada ya kupatiwa kielelezo hicho kutoka ofisi ya RCO kikiwa kimefungwa,".

Hata hivyo wakili Hyera alisema wako tayari kumrejesha mahakamani hapo shahidi wa nne, PC Mongo ili awasishe kielelezo hicho cha mkanda wa video na shahidi wa sita inspekta Aristides atoe kielelezo cha CD ambacho alikiandaa.

Wakiwasilisha hoja za ziada wakili wa Lema, Mallya huku alirejea maamuzi ya mahakama ya mahakama ya Rufaa yaliyotolewa na Jaji Bernad  Luanda kwenye rufaa iliyofunguliwa na Lema dhidi ya waleta maombi, Mussa Mkakanga na wenzake wawili ambapo jaji aliamua kuwa mmiliki wa kielelezo ndiyo anapaswa kukiwasilisha mahakamani.

"Hii concept ya kielelezo kuwekwa seal na kuletwa mahakamani ni mpya kwenye masikio yangu na mahakama za jumuiya ya madola. Huyu shahidi siyo aliyepiga picha wala siyo mhifadhi nyaraka na vielelezo vya polisi. Mheshimiwa hakimu mahakama yako ni ya sheria naomba ikataze mchezo huu," alidai wakili Mallya akiomba vielelezo hivyo visipokelewe.


Awali katika  kesi hiyo Lema anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi  Oktoba 22 Mwaka jana,katika maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro,katika mkutano wa hadhara anadaiwa kutoa maneno yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii.

Miongoni mwa maneno anayodaiwa Lema kutoa ni kuwa: “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu,…. “Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria,mipaka ya Katiba,Rais huyo  ataingiza taifa katika majanga na umwagaji damu,watu watajaa vifua,wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”

Shauri hilo limeahirishwa mpaka Februari 16, mwaka huu mahakama itakapoamua endapo vielelezo hivyo vipokelewe au vitupwe.




 

0 Comments:

Post a Comment