MNYIKA ANENA MAZITO AKIWAFARIJI WAFIWA MSIBA WA AQUILINA



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezidi kulaani vikali mauaji ya kikatili ya Acquiline Akwilini yaliyotokea siku ya Ijumaa, Februari 16 mwaka huu, huku kikisema kuwa kimebaini uwepo wa njama za kutaka kuwabambikia kesi baadhi ya viongozi wakuu wa chama kuwa wanahusika na risasi iliyokatisha uhai wa binti huyo ili kumnusuru mtuhumiwa mkuu ambaye ni Jeshi la Polisi.

Akizungumza na familia ya marehemu Acquiline pamoja na waombolezaji wengine nyumbani kwao marehemu, Mbezi Louis, jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasilisha rambirambi ya CHADEMA msibani hapo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama (Bara) Mh. John Mnyika amesema kuwa Bi. Acquiline tukio hilo linapaswa kulaaniwa na kila mpenda haki nchini.

"Ndugu wafiwa familia ya Acquiline na waombolezaji wote mlioko hapa nimefika kuwapatia pole kwa nafasi mbili...kama Mbunge wa eneo hili ambako msiba kwa hapa Dar es Salaam upo na kama Naibu Katibu Mkuu wa Chama kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CHADEMA.

"Nimekabidhi rambirambi ya chama ya shilingi laki tano kwa hapa Dar es Salaam, kule nyumbani Rombo ambako pia tunajua msiba unaendelea chama tumetoa rambirambi ya shilingi milioni moja," amesema Mnyika na kuongeza;

"Ninaomba mniruhusu niondoke mapema kwa sababu wakati niko njiani nimepokea taarifa kuwa Jeshi la Polisi limeleta barua ya wito kuwa wanatuhitaji baadhi ya viongozi wakuu tufike Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

"Barua hiyo nimeambiwa inatutaka tufike polisi saa 11 jioni hii lakini cha ajabu ni kwamba barua yenyewe imefika kwa kuchelewa huo muda ukiwa umeshapita. Kwa hiyo nalazimika kuondoka ili kwenda kushughulikia suala hilo muda huu."

Mhe. Mnyika amewaambia wafiwa na waombolezaji hao kuwa CHADEMA inatambua hakuna kiasi chochote cha fedha za rambirambi au salaam za pole zinaweza kuziba pengo la msiba hasa kwa namna kifo cha Aquiline kilivyotokea kiasi cha kugusa na kuibua hisia za maumivu kwa watu wengi.

"Tunatambua kuwa muda huu mnahitaji sana faraja kwa msiba huu mkubwa. Lakini kiuhakika kuna vitu vingi vingine vinaendelea kuhusu tukio hili. Hata huu wito wa Jeshi la Polisi tulioletewa jioni hii ni sehemu ya mkakati wa jeshi hilo kutaka kugeuza kesi ya polisi kufyatua risasi zilizowajeruhi watu kadhaa na kusababisha mauaji ya Acquiline, iwe kwamba sisi viongozi ndiyo tunahusika na risasi hizo.

"Badala ya kufanyika kwa jitihada za kuchukua hatua za uwajibikaji kwa wahusika, sasa zinafanyika jitihada za kutaka kumweka pembeni mtuhumiwa mkuu ambaye ni Jeshi la Polisi katika tukio hilo la mauaji ambapo mimi binafsi nilishuhudia baadhi ya watu wakiwa wamepigwa risasi," amesema Mnyika.

Amesisitiza kuwa marehemu Acquiline anastahili kutendewa haki ikiwemo uchunguzi wa haki na huru juu ya kifo chake, maziko ya heshima na stahiki zingine hata baada ya kuzikwa.

Mhe. Mnyika amemuomba shemeji yake na marehemu Damiani Swai kufikisha salaam za chama kwa ndugu wengine wa familia ambao kwa wakati huo walikuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kabla ya kuelekea kwenye kikao kujadili masuala yanayohusu msiba huo.

0 Comments:

Post a Comment