Mshitakiwa David Nchemba (mwenye shati nyekundu)
MWALIMU wa shule ya ya msingi ya St Thomas ya jijini hapa, David Nchemba, (25), amefikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi Arusha kwa makosa mawili ya kumbaka na kumlawiti mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 8 anayesoma shuleni hapo.
Wakili wa Serikali, Rose Sule, leo ameieleza mahakama hiyo mbele ya hakimu Mkazi, Nestory Barro kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti mwezi februari na Juni, mwaka jana.
Alidai kuwa Mwalimu huyo alikuwa akiwafuata watoto wakicheza na kuwaita mmoja mmoja kwa zamu wamfuate darasani kisha aliwafunika macho kwa kutumia tai yake na kuwaziba mdomo kwa kutumia mkono wake kisha kuwabaka na kuwalawiti.
Wakili Sule aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa wazazi wa mtoto huyo walibaini tatizo kwa mtoto huyo wakati wa likizo ambapo walimuuliza ndipo akawaeleza kuwa alibakwa na mwalimu wake ambaye ndiyo mshitakiwa huyo.
Alidai mahakamani hapo kuwa baada ya hapo wazazi walichukua hatua kwa kuamua kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi ambao baada ya kuchukua maelezo waliongozana mpaka shule ya St Thomas na kumkamata mshitakiwa kisha alipelekwa kituo cha polisi kwa mahojiano.
Sule aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa baada ya hapo mtoto alipelekwa hospitali ya mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi.
Awali waandishi waliruhusiwa kusikiliza shauri hilo wakati mwanasheria wa Serikali Sule akimsomea mshitakiwa maelezo ya kosa na orodha ya mashahidi 10 na vielelezo viwili wanavyotarajia kuleta mahakamani hapo.
Baada ya hapo hakimu Barro aliahirisha shauri hilo kwa muda ambapo mahakama iliporudi shauri hilo lilisikilizwa kwa faragha.
Mshitakiwa Nchemba anayetetewa na wakili, Steven Makwega alikana mashitaka hayo hivyo shauri hilo limeahishwa mpaka Machi 19, mwaka huu ambapo mshitakiwa Nchemba yupo nje kwa dhamana.
Wakili Suke aliwataja mashahidi wanaotarajia kuwaleta mahakamani hapo kuwa ni pamoja na Neema Onesmo, Happy Onesmo, Onesmo Shayo, Wilson Lazaro, Teresa Yuda, Anna Saitoti, Joyce Sigifred, Namnyaki Papenye, Dk Kasumuni kutoka hospitali ya mkoa Mount Meru na koplo Pudensiana.
Aidha wakili Sule alitaja vielelezo watakavyowasilisha mahakamani hapo kuwa ni pamoja na fomu ya polisi PF 3 na ramani ya eneo la tukio.
UMATI MKUBWA WA WANAWAKE WAFURIKA MAHAKAMANI
Umati mkubwa wa wanawake wakiwemo raia wa kigeni na makundi ya wanaharakati wa haki za mtoto kutoka asasi mbalimbali zisizo za kiserikali ikiwemo Sasa Foundation walifurika mahakamani hapo kuanzia majira ya asubuhi kufuatilia shauri hilo.
Wengi wa wananchi hao walitokea maeneo ya kata ya Moshono inapoishi familia ya mtoto huyo walijitokeza mahakamani hapo wakiwa wamevalia mavazi meusi kama ishara ya kuonyesha hisia zao za huzuni..
"Tunafurahi mahakama imesikiliza kesi hii leo, leo wanawake wa Moshono tumeacha shughuli zetu tukaona tumsindikize mwanamke mwenzetu kwenye hii kesi kwa sababu tumechoshwa na matukio ya unyanyasaji wa watoto wa kike njooni Moshono mjionee yapo mengi sana," alisema mmoja wa wananchi hao, Fatuma Mlacha.
mkurugenzi wa Sasa Foundation, Jovita Mlay, alikuwa ni miongoni mwa wananchi waliojitokeza mahakamani hapo ambaye alisema a anafarijika baaada ya mahakama kuanza kusikiliza shauri hilo.
Alisema shauri hilo litatumika kama chachu ya kuwabadili fikra wazazi ambao wamekuwa wakikataa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria pale watoto wao wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia aliodai kuwa ni wengi.
"Kata ya Moshono kunahitajika uangalizi wa kina hasa kwenye masuala ya uangalizi wa watoto wa kike, ukiangalia hata idadi ya watoto wanaoachishwa shule kutokana na kupata ujauzito ni kubwa," alisisitiza mkurugenzi huyo.

0 Comments:
Post a Comment