Kamanda wa Usalama wa Barabarani mkoani Arusha, Joseph Bukombe akiongea na wamiliki wa mabasi ya abiria mkoani Arusha na Kilimanjaro, (AKIBOA).
Katibu wa AKIBOA, Locken Adolf akichangia kwenye mkutano huo
CHAMA Cha Wamiliki wa Mabasi nchini, (TABOA), kimelalamikia uwepo wa vituo vingi vya polisi vya ukaguzi wa magari walivyodai vinachangia magari hayo kushindwa kusafiri kulingana na ratiba waliyopangiwa.
Aidha wamedai matukio ya mabasi kuungua yawapo safarini husababishwa na matuta madogo mengi yaliyowekwa kabla ya tuta kubwa kwenye maeneo ya kuvuka waenda kwa miguu jambo waliloomba wakala wa Barabara nchini, (TANROAD), kutekeleza agizo la Rais John Magufuli aliyewahi kuagiza diku za nyuma matuta hayo yaondolewe.
Pia wametaka wamachinga wanaopika chakula kwenye kituo kikuu cha mabasi jijini Arusha kuondoka mara moja kwani wanahatarisha usalama wa abiria na magari hayo endapo itatokea magari hayo kushika moto na kutaka maduka yaliyo kwenye stendi hizo kutolewa kwa wenye mabasi yatumike kukatia tiketi.
Waliyasema hayo juzi kwenye kikao chao kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu na Katibu wa Chama cha wenye mabasi mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, (AKIBOA), Locken Adolf na kuhudhuriwa na Kamanda wa Usalama barabarani mkoani Arusha, (RTO), Joseph Bukombe pamoja na wawakilishi kutoka ofisi za serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.
Mrutu alisema ni vema askari wakawa wanatoa barua kuonyesha kuwa gari limeshakaguliwa kituo kikuu cha mabasi kabla halijaanza safari badala ya mfumo wa sasa ambapo gari likianza safari likaguliwa kila baada ya kilometa 10 au 20.
"Gari linaondoka stendi limekaguliwa na polisi likifika Philips linakaguliwa tena likifika Tengeru unasimamishea tena wanafanya ukaguzi ule ule uliofanyika vituo vya nyuma ukifika Usa River unakaguliwa tena hii si sawa hata kidogo," alisema Mrutu.
Aliwasisitiza madereva kuwa kituo cha mabasi Korogwe ndiyo lazima waingie lakini hawalazimiki kuingia kwenye vituo vya mabasi kwenye miji yote wanayopita labda kama wana abiria wanaohitaji kupanda au kushuka kwenye mabasi yao ambapo alisema hilo ni agizo la Rais Magufuli.
Kwa upande wake mmiliki wa mabasi ya Ibra Line, Ibrahim Shayo alisema kuwa hivi karibuni moja kati ya mabasi yake yanayofanya safari kati ya Arusha na Dar es Salaam aina ya Yutong liliteketea kwa moto ambapo baada ya kutafiti ilibainika chanzo ni matuta ya barabarani.
"Tunaomba Tanroad watekeleze maagizo ya Rais Magufuli siku za nyuma alishawahi kuagiza haya matuta yaondolewe, pia tunaomba hili suala la magari kutakiwa kutembea spidi 50 kwenye makazi ya watu na 80 liangaliwe hizi sheria zilitungwa wakati magari ya kizamani Leyland Daf," alisema Shayo na kuongeza.
Kwa sasa barabara zetu ni nzuri magari ni ya kisasa kama Yutong ambayo mbali ya kuwa na mwendo kasi lakini yametengenezwa kwa mfumo unaoyawezesha kusimama kwa haraka hata inapotokea jambo la kushtukiza hivyo tunashauri walau spidi iongezwe ifike 70 kwenye makazi ya watu na 100,".
Pia alitaka mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinachora mistari ya barabarani kila mara ili kuepuka kuwatoza faini madereva kuwa wameegesha magari eneo ambalo si sahihi wakati hizo alama hazionekani.
Akijibu hoja zilizoelekezwa kwa polisi, RTO, Bukombe alisema kuwa suala la ukaguzi wa magari haliepukiki kwani magari hayo hupandisha na kushusha abiria kila sehemu hivyo wanayakagua ili yasizidishe abiria ambapo ikitokea wamewaacha wazidishe abiria na kwa bahati mbaya yakapata ajali polisi ndiyo watakao laumiwa.
Akijibu madai kuwa wingi wa vituo hivyo vinatengeneza mazingira ya askari kupokea rushwa alisema kuwa hawezi kukubali au kukataa madai hayo huku akiwataka wale wanaotakiwa kutoa rushwa wakatae, "na nyie muwaambie hao madereva wenu hizo shilingi 2,000 wazibeba nyingi kwa ajili ya kutoa rushwa na wakati mwingine wanatoa bila kuombwa waache tena wakati mwingine wanatoa hata hawajakutwa na makosa,".
Bukombe alisema kuwa kwa suala la kiwango cha mwendokasi lipo kwa mujibu wa sheria hivyo polisi wanachofanya ni kuhakikisha sheria zinazingatiwa alizodai kuwa madereva wengi hawapendi kuzitekeleza ndiyo sababu yakaongezwa matuta.
Hata hivyo RTO Bukombe alikiri kuwa suala la machinga kuruhusiwa kupika ndani ya kituo kikuu cha mabasi ni hatari sana, " pale kuna magari yanatumia petroli na mengine dizeli ikitokea basi moja limeshika moto basi utasambaa kirahisi sana hata mimi nashauri waondolewe,".




0 Comments:
Post a Comment