MAMBO MOTO KESI AJALI WANAFUNZI LUCKY VICENT


KESI inayomkabili mmiliki wa shule ya Lucky Vicent,  Innocent  Moshi, (56), imepangwa kusikilizwa mfululizo mpaka ifikie mwisho kuanzia Mei 7 mpaka 9, mwaka huu kwani limekaa muda mrefu mahakamani.


Hakimu mkazi Mfawidhi, Desder Kamugisha  anayesikiliza shauri hilo aliyasema hayo  jana wakati akiahirisha shauri hilo linaovuta hisia za wengi baada ya wakili wa utetezi, Method Kimomogoro kushindwa kufika kutokana na kubanwa na majukumu mengine.

Hakimu Kamugisha alimuagiza wakili wa Serikali, Alice Mtenga kuwaandaa mashahidi wake ili watoe ushahidi wao siku hiyo ambapo wakiweza kumaliza siku ya kwanza siku inayofuata upande wa utetezi wataendelea endapo wataonekana wana kesi ya kujibu.

"Hii ni ya muda mrefu na haikupaswa kuchukua muda mrefu hivyo. Mimi ' spirit' yangu ni hii kesi iishe nitaipangia siku ya kusikiliza mashahidi wote na siku nyingine ya kusikiliza upande wa utetezi kama watakuwa na kesi ya kujibu nataka mpaka mwezi ujao uamuzi uwe umetolewa na ninapopanga tarehe sitaki ' excuse' yoyote," alisema hakimu Kamugisha na kuongeza.

"Naipangia siku nzima ya tarehe saba tusipomaliza tutaendelea tarehe nane isipoisha tutaendelea tarehe tisa mpaka hili shauri lifike mwisho tusiendelee kulichelewesha kwa sababu haki i liyocheleweshwa ni haki iliyopita,".

Awali mshitakiwa wa pili, walimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo,  Longino Nkana, (38) aliiomba shauri hilo lipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea kutokana na wakili wao, Kimomogoro yuko kwenye majukumu mengine kwani mara ya mwisho waliambiwa hakimu hayupo na shauri hilo litaendelea hakimu atakaporudi.

Awali shauri hilo limekuwa likiahirishwa mfululizo tokea mwezi novemba mwaka jana kutokana na hakimu Kamugisha kutuwa mahakamani hapo kutokana  na majukumu mengine ya kikazi.

Tayari mashahidi watatu wameshafika mbele ya mahakama hiyo akiwemo, Mkuu wa Usalama barabarani mkoani Arusha, Nuru Seleman, (43), koplo Hamad na Afisa wa Idara ya Kazi mkoani Arusha, Wilfred Mdumi, (38),


Awali katika kesi hiyo ambayo mmiliki wa shule ya Lucky Vicent, Innocent Moshi anakabiliwa na mashitaka manne huku mwalimu Mkuu msaidizi  Longino Nkana, (38) akikabiliwa na shitaka moja.

Shauri hilo namba 78/2017 linalovuta hisia za wengi jijini hapa wanadaiwa  kuruhusu abiria 13 waliozidi kuingia kwenye gari kinyume na utaratibu na sheria za usalama barabarani na kusababisha vifo vya wanafunzi 32,walimu wawili na dereva mmoja .


Nuda alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa kwanza anadaiwa  mnamo Mei 6, mwaka huu eneo la kwa Morombo  akiwa mmiliki wa gari aina ya Mitsubishi Rosa, lenye namba za usajili T 871 BYS, aliruhusu gari hilo kufanya biashara ya kubeba abiria likiwa halina leseni.

Alisema katika shitaka la pili Moshi anadaiwa kuruhusu gari hilo kuendeshwa bila kuwa na bima na shitaka la tatu ni kushindwa kuwa na mkataba na dereva wake ambaye kwa sasa ni marehemu,Dismas  Gasper.

Mmiliki huyo wa Lucky Vicent alisomewa shitaka la  nne  analodaiwa kuruhusu gari lake kubeba abiria waliozidi uwezo wa gari ambapo abiria 13 walizidi.

Mnamo Mei 6, mwaka huu wanafunzi 32 ,walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent waliofariki kwa ajali eneo la Rhotya ,wakielekea mjini Karatu katika shule ya msingi Tumaini kufanya mtihani wa ujirani mwema.


0 Comments:

Post a Comment