MAPYA YAIBUKA KESI LUCKY VICENT

Mmiliki wa shule ya Lucky Vicent, Innocent Moshi, (aliyeshika umashavu) akiongea na wakili wake, Method Kimomogoro mara baada ya kesi kuahirishwa
BIMA iliyokuwa kwenye gari lililopata ajali na kusababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa shule ya Lucky Vicent ilikuwa imefikia ukomo hivyo mmiliki wa gari (Kampuni ya Lucky Vicent Limited)  ndiyo anawajibika kulipa madhara yaliyompata mtu wa tatu.

Hayo yameelezwa jana na Meneja wa Shirika la Bima Zanzibar, Kanda ya Kaskazini, Mohamed Matumla,(36), wakati akiongozwa na Wakili wa serikali, Elizabeth Swai kutoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya wilaya Arusha, Desdery Kamugisha anayesikiliza shauri hilo linalovuta hisia za wengi.
Alisema kuwa wao walikuwa na mkataba wa bima ya mtu wa tatu ( third party) na mmiliki wa awali wa gari hilo, Swalehe Sadiki  Kiluvia ambapo mkataba huo ulikoma pale alipouza gari hilo kwa kampuni ya Lucky Vicent.
" Bima ikishafikia ukomo sisi (Zanzibar Insurance) hatuna dhima tena ya kulipa madhara ya mtu wa tatu jukumu hilo litamuangukia mmiliki wa chombo," alisisitiza Matumla.
Shahidi huyo alieleza mahakamani hapo kuwa Mei 9, mwaka jana alipokea barua kutoka kwa mkuu wa usalama barabarani, (RTO) mkoani Arusha akitaka kujua uhalali wa bima ya gari aina ya Mitsubishi Rosa lenye namba za usajili T 781 BYS wakiambatanisha na kadi ya gari , nakala ya mkataba wa bima na risiti ya malipo.
"Sisi kwenye gari namba T 871 BYS tulikuwa tumeingia mkataba na Swalehe Sadiki Kiluvia lakini kadi gari iliyoambatanishwa ilikuwa imeandikwa jina Lucky Vicent company Limited," alieleza shahidi huyo wa tano upande wa jamhuri na kuongeza.
"Niliwaeleza vielelezo vya bima walivyoambatanisha (kwenye barua ya RTO) ni vitu vilivyotolewa kwa Swalehe Sadiki Kiluvia na kuhusu uhalali wa bima niliwaeleza kama gari limeuzwa na umiliki umebadilika bima hiyo si halali,".
Alisema waliingia mkataba wa bima na Kiluvia Mei 17, 2016 ambapo bima hiyo ingemaliza muda wake Mei 16, mwaka jana lakini kwa mujibu wa mkataba wao unaeleza wazi kuwa endapo mteja wao ataamua kuuza gari basi ana wajibu wa kurejesha stika, mkataba na risiti kwao ndani ya siku saba kwani baada ya kubadilisha umiliki bima hiyo inakuwa imefika ukomo.
Akihojiwa na wakili wa Utetezi, Method Kimomogoro, Matumla alisema kuwa majukumu ya bima ya mtu wa tatu endapo mtu yule waliyeingia naye mkataba wa bima akisababisha ajali kwa mtu wa tatu na ikathibitishwa na polisi wa usalama barabara na mahakama basi ni wajibu wa bima kuwalipa waathirika kwa niaba ya mtu huyo.
Alikiri kuwa stika ya bima ya kampuni yake iliyokuwa kwenye basi hilo ndiyo iliyosababisha askari wa barabara wasilikamate basi hilo lilipopita kwenye barabara ya Makuyuni (wakati likielekea wilayani Karatu) hivyo kupita vituo kadhaa vya ukaguzi wa polisi (yeye alidai anakifahamu kituo kimoja cha ukaguzi cha Mesereni)  wasilikamate gari hilo kwa kudhani basi hilo lina bima.
Alisema mmiliki wa awali ndiye alipaswa kurejesha kwao stika, mkataba na risiti baada ya kuliuza gari hilo "alipoacha kuleta vitu hivyo alijidhulumu mwenyewe kwa sababu kuna kiasi cha fedha tunapaswa kumrejeshea kwa kuwa muda wa mkataba ulikuwa haujamalizika hivyo ameipoteza," .
Matumla ni Shahidi wa tano kati ya mashahidi 15 wanaotazamiwa kutoa ushahidi wao kwenye shauri hilo ambapo tayari mashahidi wanne wameshafika mbele ya mahakama hiyo akiwemo, Mkuu wa Usalama barabarani mkoani Arusha, Nuru Seleman, (43), koplo Hamad na Afisa wa Idara ya Kazi mkoani Arusha, Wilfred Mdumi, (38) na Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya usimamizi na Udhibiti wa safari na majini na nchi Kavi, (SUMATRA) Allen Mwandri.
Shauri hilo limeahirishwa mpaka Mei 17, mwaka huu kwa mawakili wa serikali kuendelea kuleta ushahidi wao huku Hakimu Kamugisha akiwahimiza mawakili wa Serikali kuleta mashahidi kwa wakati ili kutimiza malengo aliyojiwekea ya kuhakikisha shauri hilo linafika mwisho mwezi huu.
WAZAZI WA WATOTO WAONGEZEKA MAHAKAMANI
Wazazi wa wanafunzi pamoja na mke wa dereva waliofariki kwenye ajali wamehudhuria mahakamani hapo kwa siku ya pili huku idadi yao ikiongezeka kulinganisha na juzi ambayo ilikuwa siku yao ya kwanza kuhudhuria.
Wazazi hao ambao muda mwingi wamekuwa wakionekana watu wa huzuni walianza kuhudhuria mahakamani hapo siku moja baada hakimu anayesikiliza shauri hilo kutishia kulifuta endapo upande wa jamhuri wangefanya jambo lolote litakalosababisha shauri hilo kushindwa kuendelea.
Awali katika kesi hiyo ambayo mmiliki wa shule ya Lucky Vicent, Innocent Moshi anakabiliwa na mashitaka manne huku mwalimu Mkuu msaidizi  Longino Nkana, (38) akikabiliwa na shitaka moja.

Shauri hilo namba 78/2017 linalovuta hisia za wengi jijini hapa washitakiwa wanadaiwa  kuruhusu abiria 13 waliozidi kuingia kwenye gari kinyume na utaratibu na sheria za usalama barabarani na kusababisha vifo vya wanafunzi 32,walimu wawili na dereva mmoja .

Nuda alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa kwanza anadaiwa  mnamo Mei 6, mwaka huu eneo la kwa Morombo  akiwa mmiliki wa gari aina ya Mitsubishi Rosa, lenye namba za usajili T 871 BYS, aliruhusu gari hilo kufanya biashara ya kubeba abiria likiwa halina leseni.
Alisema katika shitaka la pili Moshi anadaiwa kuruhusu gari hilo kuendeshwa bila kuwa na bima na shitaka la tatu ni kushindwa kuwa na mkataba na dereva wake ambaye kwa sasa ni marehemu,Dismas  Gasper.
Mmiliki huyo wa Lucky Vicent alisomewa shitaka la  nne  analodaiwa kuruhusu gari lake kubeba abiria waliozidi uwezo wa gari ambapo abiria 13 walizidi.
Mnamo Mei 6, mwaka huu wanafunzi 32 ,walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent waliofariki kwa ajali eneo la Rhotya ,wakielekea mjini Karatu katika shule ya msingi Tumaini kufanya mtihani wa ujirani mwema.

0 Comments:

Post a Comment