MILIONI 220 KUKARABATI KITUO CHA AFYA NDURUMA

HALMASHAURI  ya wilaya ya Arusha imetenga shilingi milioni 220 kwa ajili ya kuongeza vifaa na madaktari kitengo cha upasuaji kwenye  kituo cha afya cha Nduruma.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha, Dk Charles Mahela aliyasema hayo mwishoni wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya wauguzi duniani 

 Alisema kuwa wako kwenye harakati kuhakikisha kituo hicho kinakamilika ili kiweze kutoa huduma kwa ufasaha ambapo lengo kubwa ni kuhakikisha swala la afya linapata mwarobaini na kuondokana na changamoto mbalimbali. 

Aidha, Mahela aliwataka wauguzi kutumia nafasi zao vizuri katika kuhudumia wananchi huku wakitumia lugha nzuri Kwa wagonjwa ili Mwisho wa siku kazi yao iweze kupendwa na Watu wote. 


Muuguzi mkuu wa hospitali ya Seliani, Felix Samweli alisema wanahitaji ushirikiano kutoka serikalini pamoja na wadau wa afya kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali na kuweza kuziba mapengo yaliyopo ya ukosefu wa vifaa  ili kufanikisha majukumu yao . 

Akisoma risala kwa niaba ya waugui hao, Felix  alisema kuwa, wauguzi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa wauguzi na wakunga katika vituo mbalimbali vya afya. 

Alisema kuna upungufu mkubwa wa vifaa katika wodi za wazazi na wajawazito jambo ambalo linakwamisha utoaji mzuri wa huduma hizo,sambamba na vitanda vya kisasa vyenye uwezo wa kumgeuza mgonjwa. 

Kwa upande wake muuguzi  mkuu wa halmashauri ya wilaya ya arusha ,Augusta Komba alisema wanawake wengi wamejitokeza kupima ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ambapo wachache wamegundulika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo na tayari wamepatiwa tiba.

0 Comments:

Post a Comment