NAMNA WAZAZI LUCKY VICENT WALIVYOTINGA MAHAKAMANI

KWA mara ya kwanza  wazazi wa wanafunzi 32 pamoja na mke wa dereva wa shule ya Lucky Vicent waliofariki kwenye ajali  wamehudhuria mahakmani kusikiliza shauri linalowakabili mmiliki wa shule, Innocent Moshi na mwalimu Mkuu Msaidizi, Longino Nkana.

Wazazi hao walikuwa wamekaa kwenye chumba cha mahakama kwa huzuni ambapo mara baada ya shauri hilo kuahishwa walionekana baadhi wakilia huku wenzao wakiwafariji.



Aidha mahakama ilielezwa kuwa mmiliki wa gari lililopata ajali likiwa na wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa shule ya Lucky Vicent, Swalehe Sadiki Kiluvia ambaye anadaiwa  alifanya kosa la  kupeleka gari wilayani Karatu bila kibali cha kubadili njia cha Mamlaka ya Udhibiti wa safari za nchi kavu na majini, (SUMATRA),  hajafikishwa mahakamani.


Afisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani hapa, Allen Mwandri, (41) aliyasema hayo jana mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, mahakama ya wilaya ya Arusha, Desderi Kamugisha wakati alipokuwa akihojiwa na wakili wa utetezi, Method Kimomogoro.
Akijibu maswali ya wakili Kimomogoro, Mwandri alisema kuwa aliyetenda kosa kwa kuacha  kwenda kuomba kibali cha kubadili njia ya basi hilo lililokuwa likifanya safari zake kati ya Arusha na Mererani ili liweze kufanya safari kuelekea Karatu ni mmiliki wa gari , Kiluvia ambaye si mmoja wa shitakiwa mahakamani hapo.
Aliendelea  kuieleza mahakama hiyo kuwa hamfahamu mmiliki wa gari hilo ambaye anatambulika kama  Kiluvia wala  hajawahi kumuhoji ni kwa nini alibadili njia bila kuomba kibali ambapo akiongozwa na wakili wa serikali shahidi huyo alisema siyo jukumu lake kumkamata mshitakiwa na kumhoji.
 Hata hivyo alisema kuwa leseni ya Sumatra ilitolewa Mei 16, 2016 kwa ajili ya kufanya safari kati ya Arusha na Mererani   ilikuwa imalize muda wake Mei 15, 2017  na bima ya gari hilo ilikuwa haijaisha muda wake wakati gari hilo likipata ajali.
Awali akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali, Nuda Khalili, Mwandri alisema kuwa alibaini gari hilo limebadili njia yake mara baada ya kufika eneo la tukio ambapo  alitumia simu yake ya kiganjani kupata taarifa za gari hilo zilizoonyesha  limesajiliwa kupita njia ya Arusha Mirerani.
Alisema kuwa gari lolote linaweza kukodishwa kubeba wanafunzi lakini linatakiwa kuomba kibali cha kubadili njia pale  linapoenda kufanya safari tofauti na njia iliyosajili Sumatra huku akisisitiza kuwa gari lililopata ajali lilikuwa la rangi ya njano lakini akataka ieleweke kuwa si magari yote ya njano ni kwa ajili ya kubeba wanafunzi kwani magari mengine wameingizwa nchini yakiwa na rangi hiyo.
Mwandri ni Shahidi wa nne kati ya mashahidi 15 wanaotazamiwa kutoa ushahidi wao kwenye shauri hilo ambapo tayari mashahidi watatu wameshafika mbele ya mahakama hiyo akiwemo, Mkuu wa Usalama barabarani mkoani Arusha, Nuru Seleman, (43), koplo Hamad na Afisa wa Idara ya Kazi mkoani Arusha, Wilfred Mdumi, (38).
Mwanasheria wa Serikali Nuda Khalili akiwafafanulia jambo wazazi nje ya mahakama mara baada ya shauri hilo kiahirishwa


Hakimu Kamugisha aliahirisha shauri hilo ambapo linatarajiwa kuendelea leo ambapo aliuagiza upande wa jamhuri kuleta mashahidi zaidi ya mmoja ili kuwezesha shauri hilo kumalizika mapema.
Awali katika kesi hiyo ambayo mmiliki wa shule ya Lucky Vicent, Innocent Moshi anakabiliwa na mashitaka manne huku mwalimu Mkuu msaidizi  Longino Nkana, (38) akikabiliwa na shitaka moja.

Shauri hilo namba 78/2017 linalovuta hisia za wengi jijini hapa washitakiwa wanadaiwa  kuruhusu abiria 13 waliozidi kuingia kwenye gari kinyume na utaratibu na sheria za usalama barabarani na kusababisha vifo vya wanafunzi 32,walimu wawili na dereva mmoja .

Nuda alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa kwanza anadaiwa  mnamo Mei 6, mwaka huu eneo la kwa Morombo  akiwa mmiliki wa gari aina ya Mitsubishi Rosa, lenye namba za usajili T 871 BYS, aliruhusu gari hilo kufanya biashara ya kubeba abiria likiwa halina leseni.
Alisema katika shitaka la pili Moshi anadaiwa kuruhusu gari hilo kuendeshwa bila kuwa na bima na shitaka la tatu ni kushindwa kuwa na mkataba na dereva wake ambaye kwa sasa ni marehemu,Dismas  Gasper.
Mmiliki huyo wa Lucky Vicent alisomewa shitaka la  nne  analodaiwa kuruhusu gari lake kubeba abiria waliozidi uwezo wa gari ambapo abiria 13 walizidi.
Mnamo Mei 6, mwaka huu wanafunzi 32 ,walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent waliofariki kwa ajali eneo la Rhotya ,wakielekea mjini Karatu katika shule ya msingi Tumaini kufanya mtihani wa ujirani mwema.

0 Comments:

Post a Comment