SERIKALi ya Ujerumani imeahidi kuendelea kuisaidia mahakama ya Afrika ya watu na haki za binadamu,(AfCHPR) baada ya kuridhishwa na namna inavyoendesha shughuli zake.
Aidha imezihimiza nchi za Afrika kuridhia mkataba unaowawezesha mashirika yasiyo ya kiserikali, (NGO) na wananchi kuweza kufungua mashauri kwenye mahakama hiyo.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa wa Ujerumani, Heiko Maas alipotembelea mahakama hiyo na kufanya kikao pamoja na watendaji wake.
Alisema kuwa anaridhishwa na namna mahakama hiyo inavyosaidia katika kuhakikisha watu kutoka mataifa ya Afrika wanapatiwa haki jambo linalozidi kuimarisha utawala bora na unaozingatia sheria.
Awali Rais Mahakama hiyo, Sylvain ORE, alimweleza kuwa waziri mkuu huyo wa Ujerumani kuwa kwa sasa changamoto kubwa ya inayowakabili ni nchi nyingi za Afrika bado hazijaridhia wananchi wake kufungua mashauri kwenye mahakama hiyo kwani mpaka sasa ni nchi 10 tu ndizo zilizoridhia kati ya nchi 55.
Alisema kuwa ni miaka 10 sasa tokea mahakama hiyo ianzishwe lakini mpaka sasa inakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi na miundombinu kwani wanajiendesha kwa majengo waliyopewa kutumia kwa muda na serikali ya Tanzania.
ORE alisema kuwa wamefanya jitihada kuhakikisha wanapata ofisi za kudumu lakini hawajafanikiwa ambapo kwa sasa wanaendelea na jmazungumzo na serikali ya Tanzania juu ya suala hilo na tayari mwezi uliopita walifanya kikao na Katibu Mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Tanzania ambapo walikubaliana kuwa nchi mwenyeji itahusika kuzindua mfuko kwa ajili ya ujenzi huo unaotarajiwa kuchangiwa na marafiki wote wa mahakama.
Aidha aliishukuru serikali ya Ujerumani kwa mchango endelevu wanaowapatia katika kutoa mafunzo kwa watu wa kada mbalimbali kuilewa vema mahakama hiyo wakiwemo wandishi wa habari jambo aliloda kuwa anaamini wataendelea kuwasaidia katika ujenzi wa jengo la mahakama, kuimarisha utamaduni wa haki, demokrasia na utawala wa sheria.
0 Comments:
Post a Comment