KINAPA,NEMC WAMPA SHAVU SHARON KAMPENI YA KUPANDA MITI


BALOZI wa Utalii Afrika Mashariki, sharon Ngowi akiwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi – Mawasiliano TANAPA, Pascal Shelutete 
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi KINAPA Angela Nyaki 

HIFADHI ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, (KINAPA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini, (NEMC) kanda ya Kaskazini wameahidi kushirikiana na balozi wa utalii wa Afrika Mashariki, Sharon Ringo, (11) kwenye mpango wake wa upanda miti milioni 2 nchini katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

 

Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi KINAPA, Angela Nyaki na Afisa Mazingira wa NEMC, Kanda ya kaskazini , Fransis Nyamhanga walitoa ahadi hiyo kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki walipokutana na mtoto Sharon kwenye jengo la kituo cha utalii cha Ngorongoro jijini Arusha.

 

Sharon ambaye aliambatana na baba yake, Ringo Mowo kwenye ziara hiyo, alisema kuwa yeye kama balozi wa utalii anaungana na Rais Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na  mabadiliko ya tabia ya nchi hivyo amejipanga kupanda miti hiyo kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

 

Alisema kuwa anatazamia kupanda miti 5,000 jijini Dar Es Salaam na kwa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha atapanda miti 2,000 kwenye kila mkoa.

 

Afisa Mazingira wa NEMC, Kanda ya kaskazini , Fransis Nyamhanga akiongea wakati balozi wa Utalii Afrika Mashiriki, Sharon  Ringo alipotembelea ofisi za NEMC

 

“Tunawaunga mkono kwa asilimia 100, na kwa hapa Arusha kuna wadau wa mazingira huwa tunashirikiana nao kama Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, (NCAA) hata mnapoona ofisi zetu za kanda zipo kwenye hili jengo lao la kituo cha utalii,” amesema Nyamhanga.  

 

Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi KINAPA, Nyaki amesema kuwa watashirikiana na balozi huyo wa utalii kupanda miti hiyo kwenye mlima Kilimanjaro mwanzoni mwa mwezi Desemba ambapo zoezi hilo litaenda sanjari na  kupandisha bendera ya Taifa kwenye killele cha mlima Kilimanjaro kwa ajili maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru.

Balozi wa utalii ukanda wa Afrika Mashariki, Sharoni aliishukuru KINAPA kwa kumpatia miti 2,000 anayotazamia kuipanda kwenye mlima Kilimanjaro pamoja na NEMC Kanda ya Kaskazini kwa kuahidi kufanya naye kazi za uhifadhi wa mazingira.

 

Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa  mataifa makubwa yanayozalisha kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa inayochafua mazingira, kuwa mstari wa mbele kutekeleza program mbalimbali za kutunza mazingira, ikiwa ni pamoja na kutoa misaada na mikopo nafuu kwa nchi zinazoendelea ili zitekeleze kwa ufanisi miradi ya utunzaji wa mazingira.

 

 

 

Aliyasema hayo jijini Glasgow, Scotland wakati akituhubia katika Mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa unaojadili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) na kuongeza kuwa Tanzania imeathirika vibaya na mabadiliko hayo ikiwa ni pamoja na kukumbwa na majanga kama mafuriko na ukame.

 

 

 

Ameongeza kuwa licha ya hatua thabiti zinazochukuliwa na serikali, lakini majanga ya asili yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, yanaendelea kutokea ikiwemo kuongezeka kwa kina cha bahari pamoja na kuyeyuka kwa theluji katika Mlima Kilimanjaro.

 

 

 

“Sisi Tanzania hatujasalimika na majanga haya. Kupanda kwa kina cha maji kunachukua ardhi yenye rutuba, fahari yetu Mlima Kilimanjaro unabaki mtupu kwa kuyeyuka kwa barafu na tunakumbwa na mafuriko na ukame usiotabirika,” alisema Rais Samia na kuongeza.

 

 

 

…Mabadiliko ya tabianchi yanamaanisha 30% ya Pato la Taifa la Tanzania ambalo linatokana na kilimo, misitu na uvuvi liko hatarini. Cha kusikitisha ni kuwa mikakati mikubwa ya kukabiliana na vyanzo na athari zake haijapewa uzito,

 

 

 

…Lengo la [Makubaliano ya] Paris la kufikia 1.5°C halijafikiwa, lakini bado makubaliano zaidi yanawekwa. Tunachotakiwa wote kukumbuka ni kwamba mabadiliko makubwa ya tabianchi yatakapotukumba hayatachagua eneo, imara au dhaifu, nchi tajiri au maskini. Muda wa kuchukua hatua ni sasa,” .

 

 

 

 

0 Comments:

Post a Comment