MTANZANIA Paul Siniga akiapishwa kuwa spika wa bunge la vijana Afrika Mashariki na katibu wa bunge hilo, Brian Odero. Anayeshuhudia katikati ni mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Josephine Lomayan ambaye alimwakilisha spika wa bunge la Afrika Mashariki, (EALA) Martin Ngoga.
MTANZANIA, Paul Siniga amechaguliwa kuwa spika wa bunge la vijana la Afrika Mashariki baada ya kuwabwaga washindani wake wawili kwenye kinyang'anyiro hicho ambapo wajumbe walipiga kura moja kwa moja ukumbini na wengine kwa njiia ya mtandao.
Uchaguzi huo ulifanyika Novemba 11,2021kwenye ukumbi wa bunge la Afrika Mashariki (EALA) jijini Arusha ambapo mgeni rasmi alikuwa spika wa EALA, Martin Ngoga.
Siniga amepata kura 34 huku msindani wake Joyce Solomon kutoka Sudani Kusini akipata kura 14 na Bosco Kubwago kutoka Burundi akipata kura 12 huku kura nne zikiharibika.
Uchaguzi huo ulisimamiwa na Katibu wa bunge hilo la vijana, Brian Odero ambapo mara baada Siniga kutangazwa mshindi aliapishwa na ataongoza kikao cha bunge hilo kwa siku moja kisha siku inayofuata Joyce atakiongoza.
WATAKA BUNGE LA VIJANA LITAMBULIWE KISHERIA
Akifungua mkutano huo ,spika wa EALA Ngoga, aliwahimiza wabunge hao wa bunge la vijana kuhakikisha wanapaza sauti zao zisikike kila mahali Afrika Mashariki na watumie wingi wao kama vijana kutangaza zoezi la katiba ya EAC
“Ili katiba hiyo ibebe maono ya vijana, kwani vijana ni wengi zaidi ya asilimia 62 au 65 ya wakazi wote wa Afriaka Mashariki hivyo ni vema ndoto na maono yao yakaingizwa katika katiba ya EAC,” alisema Spika Ngoga katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Josephine Lomayani.
Alisema kuwa anawaelewa vijana hao wanapoomba chombo hicho kitambulike kisheria ila kuna michakato kadhaa inayoweza kufanyika ili kuhakikisha kwamba bunge la vijana linatambulika rasmi kama moja ya mihimili ya EAC.
“Wanaweza kuanza katika mijadala ya bunge lao kulizungumzia suala hili na sisi katika bunge letu (EALA) tunaweza kuendelea kupaza sauti zetu ili bunge la vijana litambulike kama nguzo au muhimili ndani ya EAC,” alisema Lomayani na kuongeza.
….Ili waweze kutambulika na kupata hadhi ya kisheria moja kati ya njia wanayoweza kuitumia ni kupaza sauti na kuweka mapendekezo yao yaingie katika katiba mpya ambayo inaanza kutengenezwa ya mtangamano wa EAC.
…Tunapoelekea hatua ya shirikisho la kisiasa, maoni ya wadau mbalimbali yatatolewa na walio katika mchakato huu wa kukusanya maoni yatatakiwa maoni ya vijana na wanaweza kuhuisha ombi hili la kutaka kuwa na bunge linalotambulika kisheria,”.
Awali akiongea kabla ya ufunguzi huo, Mkurugenzi wa taasisi ya Vision For Youth, Violet Ayoub alisema kuwa bunge la vijana limekuwa likitumika kuwaandaa na kuwajengea uwezo vijana kuingia kwenye bunge la EALA.
“Matarajio yetu kwa hizi siku mbili wabunge hawa vijana watakuja na mapendekezo yatakayoweka mkazo katika utekelezaji wa sera ya vijana ya EAC na nyingine zitapelekwa kwa majadiliano zaidi kwenye vikao vijavyo vya bunge,” alisema Violet na kuongeza.
…..Kuwa pamoja kama vijana wa EAC ni fursa ya kutengeneza mitandao, kujifunza na kubadilishana uzoefu na fursa miongoni mwao bila kujali tofauti ya umri, mipaka, rangi, lugha na tamaduni mbalimbali. Ni muda wetu vijana , sisi vijana hakuna linalotuhusu bila sisi,”.
Akiongelea mtandao wa vijana wa Afrika Mashariki, (East African Youth Network), Violet alisema kuwa mtandao huo ni mwavuli wa asasi za kiraia za vijana kwenye jumuiya hiyo pamoja na mabaraza ya Taifa ya vijana, Umoja wa wanafunzi wa Afrika Mashariki na majukwaa ya mabalozi kutoka makundi ya vijana.
Wabunge hao vijana wametaka chombo hicho kutambulika kisheria ili kiweze kuwa na nguvu ya kuwasemea vijana wa ukanda huo na yale wanayoyajadili na kuyaamua yafanayiwe kazi.
Bunge hilo hufanyika mara moja kwa mwaka na huwakutanisha vijana kutoka nchi tano zinazounda EAC na kujadili masula yanayowahusu vijana.
0 Comments:
Post a Comment