PRINCE &PRIU YAWAINUA VIJANA KIUCHUMI


https://youtu.be/AbTJIkSXFVw


VIJANA wanaotoka kwenye familia duni wameishukuru kampuni ya Pince&Priu ya jijini Arusha kwa elimu na kuwapatia ajira hivyo kupata kipato kilichobadili kabisa maisha yao na wazazi wao.


Aidha, wamiliki wa makampuni na asasi za kiraia zinazoshughulika na kusaidia watu walio kwenye mazingira magumu wameshauriwa kufika kwenye maeneo ya vijijini kwani huko kuna watu wenye uhitaji zaidi ukilinganisha na wale walio mjini wanaopata huduma kutoka taasisi nyingi.


Hayo yalisemwa Novemba 12,2021 na baadhi ya vijana wanaofanya kazi kwenye mgahawa wa kampuni hiyo unaojulikana kama, Sanna Café uliopo kwenye jengo la Ngorongoro jijini Arusha wakati walipokuwa wakiongea na Balozi wa utalii wa Afrika Mashariki, Sharon Ringo.



Mmoja wa vijana, Neema Yaroti,(21) ambaye ni mwenyeji wa wa wilaya ya Hangang’ mkoani Manyara anasema kuwa anatoka kwenye familia duni kwani wazazi wake wanategemea kilimo cha jembe la mkono hivyo kufanya wawe na uwezo mdogo kuweza kukidhi mahitaji ya familia yenye watoto saba.


 


Alisema kuwa yeye ni mtoto wa pili kuzaliwa na umaskini wa familia ulimpa wakati mgumu alipokuwa akisoma hivyo akashindwa kufuatilia masomo ipasavyo ikamfanya asiwe anafanya vizuri kitaaluma jambo lililochangia yeye kupata matokeo yasiyo mazuri kwenye mtihani wake wa kidato cha nne.


 “Kabla ya kuja hapa Sana Café nilikuwa nakabiliwa na changamoto ya chakula na malazi lakini toka nimekuja hapa nakula na kulala mahali pazuri,” alisema Yaroti huku akilengwalenga na machozi.



Kwa upande wake kijana ,Justine Masondole (25)ambaye ni kitaaluma ni mwalimu na ana diploma ya fani hiyo alisema kuwa kwa sasa  yeye ni mtaalam wa kutengeneza kahawa kwenye mgahawa huo.


Alisema kuwa  kabla ya kuajiriwa na kampuni hiyo hakuwa ameajiriwa  hivyo katika pitapita yake kutafuta ajira akapita eneo hilo akaona huo mgahawa akaingia akawakuta wahusika akawaomba kazi.


 

"Waliniuliza maswali mengi ya kunihusu, nikawaleza hali ya familia yetu ni duni na naishi na mama ambaye naye hana kazi yupo nyumbani na nina mdogo wangu anayesoma sekondari na ananitegemea kwa ada,” alieleza Masondole.



Alisema kuwa licha ya kuwapa taarifa zake lakini wakurugenzi wa kampuni hiyo waliamua kuongozana naye mpaka nyumbani kwao wakakutana na kuongea na  mama yake, majirani na viongozi wa mtaa wa …….


Nilipofika hapa nilikuwa sijui chochote juu ya kuandaa kahawa ya kunywa  na hivyo walileta watu wa kutufundisha mimi pamoja na wenzangu na wakati nikifundishwa nilikuwa nalipwa kama tayari nimeshaanza kazi nawashukuru sana.


 


“Kama nilivyokwisha sema mama yangu hana kazi, hivyo malipo ya kwanza niliyoyapata Sana Café nilimlipia ada mdogo wangu ambaye yupo kidato cha nne. Ikamuwezesha kuendelea na shule kwani tayari alikuwa amesharudishwa nyumbani kwa kukosa ada,” alisema Masondole na kuongeza,



“Nawashukuru sana kampuni ya Prince & Priu kwani mbali ya kunipa ajira lakini wamenisaidia kupanua uwezo wangu wa kufikiri na kila siku wanatuhimiza kuwa bora zaidi ya vile ulivyo sasa, naamini hata nikitoka hapa nitaweza kufanya mambo yangu kwa usahihi,”.



Kwa upande, mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Pince Ongunjobi ambaye ni raia wa Marekani mwenye asili ya Nigeria alisema kuwa aliamua kuwekeza Afrika na akachagua Tanzania kwa kuwa  ina watu wakarimu na ushirikiano ukilinganisha na mataifa mengina ya afrika.


“Watanzania  wakisema hakuna matata wanamaanisha hicho ndiyo kimenifanya kuipenda,” alisema Ongunjobi na kuongeza.


….Niliamua kuwekeza Arusha, nimeona ni mahali panapofaa zaidi kwani hata Watalii wanapokuja Tanzania wanapendea kuja Arusha nadhani  ni rahisi kwa safari za porini kusafiri kuna uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro,(KIA) ,”.


Hata hivyo alisema kuwa kwa upande wake uwepo wa vivutio vya utalii, viwanja vya ndege si jambo lililomfanya avutiwe kuwekeza nchini bali ni ukarimu wa Watanzania.


 “Mimi natokea Hispania kuna vivutio vingi kuna milima kuna fukwe nzuri lakini kilichonifanya kuwekeza Tanzania ni ukarimu wa watu wake, watu wakiwa wazuri kwako unaweza kufanya shughuli zako vizuri,” alisema Ongunjobina kuongeza . 


…Kabla ya kuja Tanzania nilisoma na kuelezwa mengi kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo  lakini nilipofika Tanzania nikakuta watu wake ni wakarimusana. Anaweza kukuelekza eneo moja kwenda lingine ukitaka kumlipa anakwambia hakuna matata haitaji,”


… Mimi baba yangu asili ya ni Nigeria hivyo ningeweza kutumia muda mwingi kuisifia lakini watu wa huko si wakarimu kama Tanzania,” .


 


Ongunjobi  alisema kuwa kupitia Sana Café kampuni yao imelenga kutangaza kahawa ya Tanzania ambayo ina muonjo mzuri sana ukilinganisha na zile zinalimwa maeneo mengine duniani.


 



Naye Mkurugenzi mwenza wa Kampuni hiyo, Veronica Shayo alisema kuwa wameanzisha mgahawa wa Sanna miezi mitatu iliyopita ambapo mbali ya kupata kipato lakini wamelenga kuutumia kugusa maisha vijana kutoka familia duni hapa nchini.


 


“Tumelenga kugusa maisha ya watu wenye uhitaji hasa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 18,  ambapo tukishawapata tunaenda kutembelea familia zao kujiridhisha kama zinauhitaji kweli,” alisema Shayo.


 


Alisema kuwa baada ya hapo tunaongea na viongozi wa serikali kwenye eneo husika kisha wanamchukua kijana bila kujali kiwango cha elimu aliyo nayo hata kama hakuwahi kuingia darasani kupata elimu rasmi wao wanampatia mafunzo ili aweze kufanya vema kazi wanayohitaji aifanye.


Shayo alisema kuwa mradi huo wanautekeleza Tanzania Bara na Zanzibar wakilenga kuwawezesha watoto wanaotoka kwenye familia duni kupata ujuzi wa kuweza kuendesha shughuli zao ziwaingizie kipato binafsi na watunze familia walizotoka.


 


“Kampuni yetu inafanya mambo mbalimbali ikiwemo mgahawa huu wa Sanna uliopo kwenye jengo la Ngorongoro hapa Arusha. Tunauza kahawa ya kunywa, kahawa iliyofungashwa tayari kwa kutengeneza nyumbani na  vipodozi vinavyotokana na kahawa,” alisema Shayo.


 


Hata hivyo alitoa wito kwa makampuni mengine kuangalia uwezekano wa kwenda vijijini kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa huko badala ya kujikita kusaidia wale walio karibu na biashara zao kama sheria inavyowataka kwa kile alichoeleza hao walio maeneo ambayo hayana makampuni karibu wanauhitaji pia.


“Sisi tumekuwa tukienda vijijini na kusaidia pale tunapoweza, Kwa mkoa wa Kilimanjaro tumefika wilaya ya Moshi, Materuni , Marangu, wilayani Hai kwenye mji Mdogo wa Bomang’ombe, Kambi ya Nyuki ni eneo la Wamasai, mkoani Arusha LOngido na Nduruma,” alisema Shayo.

Alisema kuwa mpaka sasa wamesaidia vijana zaidi ya 100 kwenye maeneo hayo pamoja na jijini Arusha kwa kuwapa elimu na ajira, wengine wamewapatia chakula na sasa wanakamilisha taratibu ili kuweza kuwapatia mavazi kwani wana orodha ya wale wanaohitaji.

0 Comments:

Post a Comment