NA ARODIA PETER
CHAMA cha ACT Wazalendo kinatarajia kuzindua Sera ya Wamachinga itakayoainisha hatua ambazo serikali itapaswa kuzichukua ili kuhakikisha wafanyabiashara hao wanafanya shughuli zao kwa uhuru.
![]() |
| KATIBU Mkuu ACT-WAZALENDO, Ado Shaibu Ado wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 7,2022 kuhusu ziara yake na Sektretarieti ya chama hicho katika Jimbo la Mbagala. |
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam leo Julai 7,2022 na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu Ado wakati akizungumzia changamoto walizozibaini kwenye ziara ya Sekretarieti ya chama hicho kwenye kata 10 za Jimbo la Mbagala Dar es Salaam.
Amesema katika maeneo hayo wapo vijana wasomi wanaendelea kumiminika mtaani huku uchumi wetu ukiwa hauzalishi fursa za kutosha kuwawezesha wahitimu wote kuajiriwa na kujiajiri.
Ado amesema Sera hiyo itazinduliwa hivi karibuni ambapo amebainisha kuwa vijana waliojiajiri kwenye sekta ya bodaboda, wamachinga na wafanyabiashara masokoni, lakini Serikali haijaweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao.
Katika hatua nyingine Ado amesema wananchi hawaridhishwi na kasi ya Serikali katika kushughulikia hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili kwa sasa.
Amesema kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu za chakula, mafuta ya petroli, dizeli na vifaa vya ujenzi kumechangia kupanda kwa gharama za maisha na hali ngumu ya uchumi kwa wananchi hasa wa hali ya chini.
Ado amesisitiza kuwa kupanda kwa petroli na dizeli ndiko kunachochea kwa sehemu kubwa kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu na nauli.
Ado pia alizungumzia bei za bidhaa muhimu kama mchele, unga wa mahindi, mafuta ya kupikia na maharagwe akisema zimepanda sana ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana.
"Katika ziara hiyo tumetembelea maeneo ya masoko, vijiwe vya kahawa, bodaboda na kufanya mazungumzo na wazee, tumebaini mchele umepanda kutoka Sh 1200 hadi 2400, unga wa mahindi umepanda kutoka Sh 1000 hadi Sh 1600, mafuta ya kupikia kutoka Sh 3000 kwa lita hadi Sh 9000.
Bidhaa nyingine ni unga wa ngano umepanda kutoka Sh 1200 hadi Sh 2000, sukari kutoka Sh 1500 hadi Sh 3000 huku nyama ikipanda kutoka Sh 6500 hadi Sh 9000." alisema Ado.
Kufuatia hali hiyo ACT Wazalendo kimerejea kwenye ushauri wake kilioutoa siku chache zilizopita kwamba Serikali iondoshe Sh 500 kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli zinazokusanywa kama tozo ambapo itakuwa imeweka ruzuku ya Sh bilioni 152.5 kila mwezi badala ya Sh bilioni 100.
Aidha chama hicho kimesisitiza umuhimu wa Serikali kuingilia kati kwa kuyawezesha mashirika ya Maendeleo ya Petroli nchini (TIPPER) na TPDC kuagiza mafuta ili kuhakikisha unafuu zaidi unapatikana sambamba na kutenga fedha haraka kwa ajili ya kuongeza uwezo wa hifadhi ya mafuta ya petroli ili kuongeza siku zaidi tofauti na utaratibu wa sasa wa kuagiza kila mwezi.

0 Comments:
Post a Comment