KUTIMIZA MWAKA MMOJA: Princess Lounge Ya Arusha Kusimamisha Jiji Agosti Mosi, Ni Baada Ya Kutikisa Afrika Mashariki!


 


Na Queen Lema, Arusha

 

MKOA wa Arusha unatarajiwa kusimama miguu yote miwili kesho Agosti Mosi, wakati Princess Lounge, moja ya kumbi maarufu na zenye mvuto mkubwa wa kipekee barani Afrika Mashariki, itakapofanya maadhimisho makubwa ya kutimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.


 Akizungumza kuelekea tukio hilo la kihistoria, Mkurugenzi wa Princess Lounge, Catherine Urasa, amesema wameandaa sherehe kubwa na ya kukata na shoka itakayoweka historia mpya ya burudani mkoani Arusha.

Catherine amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake, Princess imekuwa nguzo kuu na kichocheo kikubwa cha sekta ya burudani, huku ikisifika kwa kulisha vyema hisia za wapenda bata na starehe mkoani hapa.

Alieleza kuwa kwa kuzingatia Arusha ni kitovu cha utalii nchini, Princess Lounge imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenda sambamba na hadhi hiyo kwa kutoa burudani na huduma za kiwango cha kimataifa zinazovutia wageni wa ndani na nje ya nchi.


"Tunatimiza mwaka mmoja sasa wenye mafanikio makubwa sana. Tunafurahi kwa upendo na mapokezi tuliyopata, na tunapenda kuwaahidi wateja wetu kuwa tumejipanga vyema zaidi kuendeleza na kuiboresha sekta hii ya burudani kwa viwango vya juu zaidi," alisema kwa kujiamini Catherine.


Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amejivunia namna biashara hiyo ilivyoweza kuwa mkombozi kwa vijana kwa kutengeneza fursa za ajira kwa wale ambao hapo awali hawakuwa na kazi kabisa.


"Kama mnavyojionea wenyewe, hapa tuna mabinti warembo na wachapakazi ambao ni sehemu ya nembo yetu. Pia tuna vijana mahiri wa muziki (DJs) na wataalamu wa kuchoma nyama tamu na zenye ladha ya kipekee, ambao wote kwa pamoja ndio siri na nguzo ya mafanikio ya Princess," aliongeza.


Kufuatia hatua hiyo, Catherine ametoa wito na mwaliko rasmi kwa Watanzania wote na wakazi wa jiji la Arusha kujitokeza kwa wingi kesho kusherehekea kwa pamoja mafanikio hayo, ambapo kutakuwa na mfululizo wa burudani za kusisimua, vinywaji vya kila aina, na vyakula vya kutosha.

0 Comments:

Post a Comment