Na Grace Macha Hai
TAASISI ya Utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI) imetoa magari mawili aina ya Toyota Land Cruizer yenye thamani ya shilingi milioni 180 ili yatumike katika kutoa elimu kwa wakulima wa kahawa vijijini juu ya umuhimu na namna bora ya kutumia miche mipya chotara ya kahawa iliyogunduliwa na taasisi hiyo .
Magari hayo yalitolewa juzi na Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa TaCRI , Vedastus Ngaiza kwa viongozi wa vituo vya Mwayaya mkoani Kigoma na Lyamungo inachohudumia mikoa ya kanda ya Kaskazini muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa kikao wafanyakazi kwenye makao makuu ya taasisi hiyo yaliyopo Lyamungo , wilayani Hai .
Mwenyekiti huyo wa bodi aliwataka watumishi wa tassisi hiyo kuyatumia magari hayo vizuri kwa kuhakikisha wanawafikia wakulima kwenye maeneo husika ili waweze kuwasaidia katika kuwapatia elimu itakayowawezesha kujua njia sahihi za namna ya kulima , kutunza , kuandaa jambo litakalowawezesha kupunguza gharama za uzalishaji na kupata bei nzuri kwenye soko .
Aidha alieleza changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kutafiti na kuzalisha mbegu zinazoweza kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo kwa sasa maeneo mengi yanakabiliwa na ukame kwa kipindi kirefu cha mwaka .
Ngaiza alisema kuwa kwa sasa TaCRi wanafikiri namna ya kubuni namna endelevu ya kujiendesha kimapato tofauti na sasa ambapo wanategemea fedha kutoka serikali kuu na jumuiya ya Ulaya (EU) jambo alilosema kuwa litawasaidia kuendeleza na kupanua shughuli zao za utafiti hata wafadhili hao wakipunguza kiwango cha fedha wanachowapatia .
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu mtendaji wa taasisi hiyo , Prof. James Teri aliwataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa mshikamano huku akijivunia mafanikio ya kugundua aina 15 za mbegu mpya chotara za kahawa za Arabika na 4 za Robusta kwa kipindi cha miaka 10 tokea kuanzishwa kwa taasisi hiyo .
Naye Naibu Msimamizi wa fedha za Jumuiya ya Ulaya Nchini , Samuel Marwa aliipongeza taasisi hiyo kwa kutumia vizuri fedha walizopewa na jumuiya hiyo kwa ajili ya tafiti na kuboresha miundo mbinu jambo alilosema kuwa linaiweka kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kufadhiliwa kwa kiwango kikubwa .
MWISHO
0 Comments:
Post a Comment