ufisadi halmashauri ya arusha

Wamachinga Arusha watozwa ‘ushuru’ bila stakabadhi

BAADHI ya watumishi wa Manispaa ya Arusha wanatuhumiwa kukusanya ushuru wa 20,000 kila mwezi kutoka kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga zaidi 1,000 bila kuwapa stakabadhi ili kuwaruhusu kuendesha shughuli zao katika mitaaa mbalimbali ya mji wa Arusha.

Fedha hizo zinazokaribia 20,000,000 kwa mwezi hazikatiwi stakabadhi na haziwahi kufikishwa ofisi za Manispaa kwa zaidi ya kipindi cha miaka mitatu.

Kugundilika kwa jambo hilo kulitokea juzi baada ya wafanyabiashara hao kugomea ongezeko la ushuru kutoka 20,000 hadi 40,000 kwa mwezi kitendo kilichosababisha askari wa Manispaa waliokuwa wakitumika kukusanya fedha kutoka kwao kukamata mali zao na kuzifungia kwenye depo la halmashauri eneo la Levolosi.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, Estomih Chang’a alithibitisha jana kuwepo kwa tuhuma hizo ambazo tayari zimeundiwa tume ya watu watano kuchunguza kubaini ukweli na wahusika kabla hatua za kinidhamu na kisheria kuchukuliwa.

“Nimepokea malalamiko ya wafanyabiashara hao kupitia kwa wawakilishi wao 30 waliofika ofisini kwangu kueleza jinsi walivyokuwa wakitozwa ushuru na baadhi ya watumishi wa Manispaa bila kupewa stakabadhi, nimeunda tume kuchunguza suala hilo na uchunguzi ukikamilika nitauweka wazi kwa umma,” alisema Chang’a

Pamoja na kuunda tume, Mkurugenzi huyo pia ameagiza mali za wafanyabiashara zilizokuwa zikishikiliwa kwenye ghala la halmashauri hiyo zirejeshwe kwa wenyewe bila masharti na kuwaomba wahusika wa pande zote kutoa ushirikiano kwa tume ili kufanikisha uchunguzi mapema.

Kabla ya kuonana na Mkurugenzi, wafanyabiashara hao waliandamana hadi ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoa wa Arusha ambapo walikutana na katibu wake, Amani Golugwa aliyewatuliza na kuwataka kutatumia njia ya vurugu kudai haki yao na kuwaunganisha na ofisi ya Mkurugenzi.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Golugwe alisema chama chake kimesikitishwa na kitendo cha watumishi hao wa Manispaa kuhujumu mapato ya halmashauri kwa kukusanya ushuru na kuziingiza mifukoni huku huduma za kijamii zikiendelea kuzorota kutokana na uhaba wa fedha.

Katibu huyo licha ya kumpongeza Mkurugenzi Chang’a kwa kukubali kukutana na kuwasiliza wafanyabiashara hao, lakini alidai ofisi yake imeonyesha udhaifu mkubwa kwa kushindwa kubaini na kudhibiti uhalifu huo unaodaiwa kutendeka zaidi ya miaka mitatu sasa.

MWISHO

0 Comments:

Post a Comment