MASHIRIKA saba yasiyo ya kiserikali (NGO) nchini yanayojishughulisha na kutetea haki za watu wa jamii ya wafugaji yamejitokeza kuungana na serikali ya Tanzania kwenye shauri linaloikabili kwenye mahakama ya Afrika Mashariki inalozuiwa kujenga barabara ya Musoma-Serengeti-Arusha.
Shauri lililofunguliwa dhidi ya Serikali na taasisi isiyo ya kiserikali inayoshughulikia haki za wanyama ya Africa Network for Animal Welfare (ANAW) ya nchini Kenya inayopinga mradi huo kwa madai kuwa utafanya magari mengi kupitia njia hiyo na hivyo kuathiri ikolojia ya wanyama wanaohama kutoka hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania kwenda hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya kila mwaka
Akiongea na waandishi wa habari jana Mkurugenzi wa Mtandao wa mashirika yanayowatetea haki za jamii ya wafugaji (Pingo’s forum) , Edward Porokwa alisema kuwa tayari wameanza taratibu za kisheria ili waweze kuingizwa kama sehemu ya washtakiwa kwenye shauri hilo akizitaja NGO nyingine kuwa ni ALAPA, TAPHGO, NGONET, NYDA, CORDS na TPCF.
“Sisi tunawakilisha jamii za wafugaji ambazo ndiyo walengwa wa ujenzi wa barabara hiyo inayotarajiwa kuwanufaisha wananchi wanaoishi kwenye wilaya 10 kuanzia Arusha, Arumeru, Monduli, Longido, Ngorongoro, Serengeti, Tarime, Bunda mpaka Musoma inayopitia upande wa mashariki wa hifadhi ya Serengeti” alisema Porokwa.
Alisema kuwa wameamua kuungana na Serikali baaada ya kuona mpango wa mataifa ya nje ikiwemo Kenya una hila ndani yake hasa kutokana na ukweli kuwa kwenye hifadhi za nchi zao wamejenga barabara ndani ya hifadhi tena za kiwango cha lami huku wakikataa ujenzi wa kipande cha barabara ya kiwango cha changarawe chenye urefu wa wastani kilomita 50 kwenye hifadhi ya Serengeti.
Porokwa alitolea mfano kuwa Kenya imejenga barabara za lami kwenye hifadhi yake ya Masaimara inayopakana na hifadhi ya Serengeti kwa upande wa mashariki jambo alilohoji kuwa hayo madhara wanayodai kuwa yatawapata wanyama endapo barabara itajengwa Tanzania ni yapi ambayo wanyama hao hawayapati wanapoingia kwenye hifadhi hiyo ya Masaimara .
Porokwa alisema kuwa wanaamini jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi hizo ambazo mwaka 1953 zilihamishwa ndani ya hifadhi ya Serengeti ili kupisha uhifadhi wa wanyamapori wanahaki ya kunufaika na hifadhi hizo japo kwa kuboreshewa miundo mbinu ili waweze kupata huduma nyingine za msingi wanazozikosa ikiwemo huduma za afya na elimu ambazo kwa sasa si nzuri.
Kwa upande wake mratibu wa mtandao wa wafugaji nchini (TPCF),Joseph Parseko alisema kuwa wananchi wa maeneo hayo wanahaki ya kupata huduma za msingi kama ilivyo Watanzania wengine kwa kile alichodai kuwa tatizo la ukosefu wa barabara umekuwa mwiba kwa wakazi wa maeneo hayo akitolea mfano eneo la Loliondo ambapo mabasi ya abiria huanza safari saa 12 asubuhi na kufika Arusha mjini saa moja usiku huku nauli ikiwa ni shilingi 20,000 .
Alisema kuwa endapo barabara hiyo itajengwa itasaidia kupunguza gharama hizo pamoja na muda wa kusafiri kwa kile alichosema kuwa hata huduma za afya ni mbaya sana kwani wataalam wanapopelekwa huko hukimbia kutokana na mazingira duni na wagonjwa wanaohitaji kupata matibabu zaidi kwenye hospitali ya mkoa ya Maount Meru humbidi kusafiri kwa zaidi ya saa 10 jambo alilosema kuwa wakati mwingine hupekea wengine kupoteza maisha .
Alisema kuwa kukosekana kwa barabara hiyo kumechangia kufanya bei za bidhaa kuuzwa kwa bei ya juu sana akitolea mfano kuwa soda ambayo bei yake ni shilingi 500 lakini Loliondo huuzwa shilingi 1,500 na sukari ikiuzwa shilingi 3,000 .
Kwa upande wake mratibu wa masuala ya katiba kwa watu wa jamii ya wafugaji , William Ole Naasha alisema kuwa mhifadhi mkubwa wa hifadhi ya Serengeti ni wananchi wanaoizunguka hifadhi hiyo lakini inasikitisha kwa wao kushindwa kunufaika na hifadhi hizo kwani wamekuwa akijikuta wakichomewa nyumba zao ili kupisha uhifadhi lakini hawapatiwi huduma muhimu na ikitokea Serikali inataka kuanza kuwahudumia wanatokea watu wengine kupinga.
“kama wao ni wahifadhi kweli kwenye nchi zao wanyama wako wapi? Nyumbu walipotea Marekani miaka mingi iliyopita ilikuwaje wakashindwa kuwahifadhi kwo leo waje kudai ikijengwa barabara itaathiri mapito ya nyumbu kuelekea hifadhi ya maisaimara, Mbona wakiingia masaimara wanakuta barabara za lami au hayo madhara yatatokea endapo tu barabara itajengwa Tanzania?” alihoji Naasha.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya serikali ya Tanzania kubwagwa katika rufaa yake iliyokata dhidi ya uamuzi wa mahakama ya Afrika Mashariki ya kuzuia ujenzi wa barabara hiyo baada ya kitengo cha Rufaa cha Mahakama hiyo kwa madai kuwa uamuzi kufungua shauri hilo ulikuwa sahihi.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Tanzania kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata ilipinga hati hiyo kwa madai kuwa mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kufanya hivyo kisheria kwani suala hilo linahusu mambo ya ndani ya Tanzania na yalistahili kuwasilishwa na raia wa Tanzania au NGO ya Kitanzania mbele ya mahakama iliyo ndani na chini ya mamlaka ya nchi ya Tanzania.
Uamuzi wa jopo jopo la majaji watatu walioongozwa na Rais wao, Jaji Harold Nsekela na Jaji Emilie Kayites, ulisomwa na Jaji James Ogoola aliyesema kuwa kifungu cha 9 cha mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kinaipa mamlaka, haki kisheria Mahakama ya Afrika Mashariki kutoa hati ya zuio na hivyo kutupilia mbali rufaa ya serikali ya Tanzania.

0 Comments:
Post a Comment