wananchi arumeru wataka serikali iwamikishe ardhi

Na Grace Macha Arusha SAKATA la mgogoro wa Ardhi wilayani Arumeru limechukua sura mpya baada ya wananchi hao kuamua kufunga barabara kuu ya Arusha kueleke Kilimanjaro eneo la Shangarai karibu na mto Nduruma kwa zaidi ya saa mbili wakushinikiza kumilikishwa kihalali mashamba hayo ambayo kwa sasa yanamilikiwa na wawekezaji . Tukio lilitokea jana kuanzia majira ya saa tano asubuhi ambapo wananchi hao walifunga barabara hiyo kwa kuweka mawe makubwa na magogo hali iliyosababisha misururu mirefu ya magari yaliyosimama pande zote za barabara . Hata hivyo barabara hiyo ilifunguliwa majira ya saa saba mchana kwa msaada wa jeshi la polisi ambao walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao kisha kuyaondoa magogo na mawe hivyo kuwezesha barabara kupitika . Hata hivyo juhudi za kumpata kamanda wa polisi mkoani hapa, Thobias Andengenye kuongelea suala hilo hazikuzaa matunda kutokana na siku yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa. Hata hivyo afisa mmoja mwandamizi wa jeshi hilo ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini kutokana na kuwa si msemaji wa jeshi hilo alikiri kutokea kwa tukio hilo . Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa, Magesa Mulongo amewataka wawekezaji na wamiliki wa mashamba makubwa kutekeleza kikamilifu wajibu wa kusaidia jamii inayowazunguka ili kupunguza uhasama baina yao na wananchi . Aliyasema hayo jana alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya matukio ya uvamizi yanayoendelea wilayani Arumeru ambapo wananchi wamevamia mashamba ya Dolly na Machumba na kugawana. Mulongo alisema kuwa ni vema wawekezaji hao wakasaidia upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo zile za afya, elimu na maji jambo. Aidha Mkuu huyo wa mkoa aliunda timu ya watu watano itakayoongozwa na Mkuu wa Idara ya Miundombinu mkoani hapa, Jackson Ole Saibatahu ili kushughulikia kwa ukamilifu migogoro hiyo iliyoibuka baina ya wanavijiji na wawekezaji ambapo itatumia siku saba kuanzia kesho kumamilisha kazi hiyo. Mnamo April 14 mwaka huu baadhi ya wananchi kutoka vijiji vya Kitefu, Migadini, Maroroni na Ugoro walivamia shamba la Dolly linalomilikiwa Jerome Bruins na kufanya uharibifu wa miundombinu ambapo walivunja fensi ya umeme yenye urefu wa miza 2000 pamoja na kuchoma moto vibanda vya walinzi. Aidha siku inayofuata wananchi hao waliingiza makundi ya mifugo katika shamba hilo kwa ajili ya malisho. Tukio lingine lilitokea Aprili 21 , mwaka huu ambapo wananchi wanaokadiriwa kufikia 500 maeneo ya Nduruma, Nkoanrua na Akheri wilayani humo, walivamia shamba linalomilikiwa na kampuni ya Machumba na kuanza kukata miti huku kugawana kwa madai kuwa wanataka kurejeshewa ardhi yao iliyotolewa kwa wawekezaji huku wao wakikosa ardhi ya kuzalisha chakula kwa ajili ya familia zao. Mulongo alisema kuwa madai ya wananchi kutaka kurejeshewa kurejeshewa ardhi yao ni madai ambayo yanapaswa kushughulikiwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa kisheria kinyume cha hapo jeshi la polisi halitasita kuingilia kwa wale watakaofanya vitendo vya uvunjaji sheria. Hata hivyo alidai kuwa kuna taarifa za kuwepo kwa baadhi ya wanasiasa wanaochochea vitendo hivyo vya uvamizi ambapo aliwataka wajitokeze hadharani ili kupunguza msuguano baina ya wananchi na wawekezaji . “Kama yupo mtu aliyewaahidi wananchi hao kwamba atawagawia au kuwapa sehemu ya mashamba hayo wanayovamia basi ni vema wananchi wakamfuata mtu huyo ili aweze kuwaeleza ni kwa namna gani au njia ipia atatumia ambayo haikinzani na sheria kuhakikisha wananchi hao wanatimiziwa ahadia yao” alisema Mulongo. MWISHO

0 Comments:

Post a Comment