MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, (DCI), Isaya Mngulu amesema kuwa siku baa ya Arusha Night Park maarufu kama Matako baa ilipolipuliwa majira ya saa 1:30 usiku, majira ya saa 6 usiku kifaa kingine cha mlipuko kilikutwa kimetelekezwa kwenye baa ya Washington ya jijini hapa.
Aidha amekanusha taarifa zilizowahi kutolewa na Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo kuwa Jeshi hilo limenasa mtandao wa watu walioingiza mabomu yaliyotumika kwenye matukio ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu, Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasite na Soweto kwenye mkutano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA).
Pia jeshi hilo limeahidi kitita cha shilingi milioni 10 kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa matukio hayo ya mabomu na milipuko.
Mngulu aliyasema hayo jana wakati akiongea na waandishi wa habari jijini hapa ambapo alisema kuwa wataalm wa jeshi la Wananchi Nchini, (JWTZ) na wale wa jeshi la polisi wanendelea na uchunguzi juu ya matukio hayo.
Alisema kuwa bomu hilo kwenye baa ya Washington lilikutwa sehemu wanayokaa wateja likiwa ndani ya begi dogo ambapo mpaka sasa polisi wanaendelea kulichunguza na hawajalipua.
Alisema kuwa taarifa za awali zinaonyesha mabomu yote hayo ni ya kutengenezwa kienyeji ambapo hupatikana zaidi maeneo ya machimbo ya madini ingawa hakutaka kufafanua malighafi iliyotumika kuyatengeneza kwa hofu ya kuwafanya wengine waige.
DCI alisema kuwa mpaka sasa hawajajua chanzo cha matukio hayo kwa kile alichoeleza kuwa bado wanaendelea na upelelezi kuweza kubaini na hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
"Hatufanyi kazi kama watabiri au waganga wa kienyeji, bado tunaendelea na upelelezi, mpaka sasa,hatuna majibu sahihi ya sababu za matukio haya tukiyabaini tutawaeleza.
"Hatuwezi kusema ni lini tutakamilisha upelelezi wa matukio ya mabomu ya Arusha, kama Marekani walimtafuta Osama Bin Laden kwa miaka mingi wakati walikuwa wanamjua sembuse sisi ambao tunamtafuta mtu tusiyemjua," alisema DCI wakati akijibu maswali ya waandishi.
Aliwataka wafanyabishara katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kuweka vifaa vitakavyosaidia masuala ya usalama ikiwemo kufunga mitambo ya kamera ya (CCTV) yenye uwezo wa kurekodi matukio muda wote kwa kile alichoeleza kuwa uwezo wa jeshi la polisi kulinda raia ni mdogo kwani idadi ya askari walio jiji la Arusha wamegawanywa kwa uwiano wa askari mmoja kulinda watu 2,000 .
Akielezea hali ya majeruhi wa bomu la watu waliokuwa wakiangalia mpira
kwenye bar hiyo, alisema kuwa watu 15 waliokuwa wamejeruhiwa na
kulazwa ,kati yao saba,wameruhusiwa na wengine nane wanaendelea
kupatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa Mount Meru.
Aliwataja wanaoendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo ni
,Evance Maleko,Evarist Richard,Petro James,Christine Zakaria,Pius
Shayo,Antelus Zakaria,Sudi Ramadhani na Mariam Juvenary Hans.
0 Comments:
Post a Comment