Wanajamvi,
Napenda nichukue fursa hii kuanzisha somo la siasa kwa Waswahili wote
wa Shirikisho letu tukufu la Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu
wa Zanzibar,
Hii itakuwa fursa kwa vijana wengi wanaochipukia katika siasa za kileo,
Mambo makuu muhimu nitakayofundisha ni:
1. Maana ya siasa.
2. Itikadi za vyama vya siasa
3. Katiba za vyama vya siasa
4. Siasa za kisasa
5. Maisha ya mwanasiasa.
Nitatumia lugha yetu adhimu ya kiswahili katika kuwafunza haya.
Sehemu ya Kwanza.
Siasa ni nini?
Siasa ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni
msingi kuendesha uchumi, utamaduni na mwenendo mzima maisha ya jamii
hiyo.
Kabla hatujaangazia itikadi za vyama, nataka tujifunze na tuelewe,
ITIKADI ni nini?
Itikadi ni mkusanyiko wa imani unaoshikiliwa na kikundi cha watu fulani.
Kuna aina kuu mbili za itikadi:
Itikadi za KISIASA, na itikadi za KIEPISTEMOLOJIA (ni sehemu ya
falsafa ambayo inahusu utafiti wa jinsi tunavyojua mambo).
Itikadi ya kisiasa ni upangiliaji unaohusu mawazo ya kimaadili na
vipi nchi itaendeshwa.
Itikadi za kiepistemolojia ni upangiliaji unaohusu mawazo ya
kifalsafa, ulimwengu, na jinsi gani watu wanapaswa kufanya maamuzi.
Kwakuwa somo letu linahusu siasa, hivyo nitajita kufundisha itikadi
ya kisiasa zaidi katika kipengele hiki cha itikadi.
ITIKADI ZA KISIASA.
Katika dunia ya leo, Itikadi za kisiasa zimegawanyika katika makundi
makubwa sita kama ifuatavyo:
1. Ukomunisti
2. Ujamaa
3. Ujamaa wa kidemokrasia
4. Uliberali
5. Uhafidha Liberali
6. Uhafidhiana
Mpangilio huu wa itikadi hutokea kushoto kuelekea kulia kama ifuatavyo:
Ukomunisti=>Usoshalisti=>Ujama a wa Kidemokrasia=>Uliberali=>Uhafi
dhina Uliberali=>Uhafidhina
Kwahiyo kwa mfano, itikadi ya kikomunist, na kijamaa zinatambulika
kama itikadi za mrengo wa kushoto, wakati itikadi ya uhafidhiana
inatambulika kama itikadi ya mrengo wa kulia.
Itikadi za mrengo wa kushoto (Ukomunisti, Ujamaa na Ujamaa wa
kidemokrasia), asili yake ni Karl Max ambae alidai kwamba Ubepari ni
muundo wa kinyonyaji na kikandamizaji. Wengi wetu tayari tunalielew
vizuri suala hili.
UKOMUNISTI
Utawala: Mamlaka yote ipo chini ya umma, Hakuna chaguzi kwani
serikali ya kikomunisti inakubalika na wote. Maisha yote ya jamii,
kuanzia utawala, uchumi na maisha binafsi, yapo chini ya serikali.
Hakuna soko wala ubadilishanaji wa aina yoyote; hakuna umiliki
binafsi wa mali; bidhaa na huduma zote zinagawanywa sawa katika jamii
bila ya ubaguzi wa aina yoyote.Hakuna matabaka ya aina yoyote miongozi
mwa wafanyakazi. Kuna mapinduzi yanayolenga kufuta uhaba na pia
umiliki binafsi wa mali. Wananchi hupatiwa huduma zote za msingi na
serikali bure, kwa mfano elimu, afya, n.k.
UJAMAA.
Masuala ya umma yanaendeshwa kwa nguvu za kimuundo iliyopo chini ya
muundo wa halmashauri, kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa. Ingawa mara
nyingi huwa na chama kimoja cha siasa, huwa kunakuwepo na chaguzi za
mara kwa mara, hivyo viongozi kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka juu
hutokana na watu. Kuna serikali za makusudi za kuunganisha serikali na
jamii nzima. Uwepo wa mishahara isiyotofautiana sana; Pia huduma na
bidhaa nyingi kwa umma hutolewa na serikali. Kuna muungano wa tabaka
la wafanyakazi; uwepo wa fursa sawa kwa watu wote bila kujali
matabaka. Kuna mapinduzi ya kuangamiza ubwanyenye. Umiliki wa umma wa
njia kuu za uchumi, na matumizi ya rasilimali ya taifa kwa manufaa ya
umma pamoja na upatikanaji wa huduma zote za msingi kwa watu wote.
UJAMAA WA KIDEMOKRASIA.
Masuala yote ya umma yanaendeshwa na viongozi waliochaguliwa kupitia
muundo wa kidemokrasia. Viongozi wa umma hutokana na chaguzi za mara
kwa mara zenye uwazi na uhuru kwa wapiga kura; Serikali thabiti
huitajika ili kuendesha mipango na sera za kugawanya keki ya taifa.
Ubepari unakubalika, na unashamiri kupitia muundo thabiti wa kugawana
keki ya taifa na upatikanaji wa huduma bora za kijamii. Kuna umoja wa
kitabaka miongozi mwa wafanyakazi kupitia taasisi zinazounganisha
tabaka hili. Mapinduzi hayahitajiki kwani ubepari unakubalika hivyo
kuendelea kushamiri. Msisitizo mkubwa ni uwepo wa a "Welfare State",
yenye Social security programs zinazolenga kutoa msaada kwa wote
wanaostahili - kama vile huduma ya afya, elimu, makazi, n.k. Pia
serikali hugawanya mapato kwa kutoza kodi za aina mbali mbali kwa
lengo la kupunguza tofauti za kiuchumi baina ya matabaka mbalimbali,
huku pia ikiweka kinga thabiti kwa watu wasio na ajira, wagonjwa, na
wastaafu..
Na sasa tuziangalie itikadi za mrengo wa kulia –Uliberali, Uhafidhina
wa Kiliberali, na Uhafidhiana.
1. ULIBERALI
Asili ya itikadi hii ilikuwa ni kupigania haki za watu katika jamii
za mataifa ya magharibi yaliyokuwa chini ya tawala za kifalme; tawala
hizi hazikutoa haki na fursa sawa za kiuchumi kisiasa na kijamii kwa
wananchi. John Locke ndiye (mwanzilishi), na wenzake walidai kwamba –
binadamu huru ndio msingi wa jamii imara yenye amani na utulivu; pia
walihimiza umuhimu wa kuwepo kwa serikali yenye wajibu wa kulinda haki
za msingi za wananchi; harakati hizi ndiyo zilizokuja kuzaa dhana
nzima ya demokrasia ya uwakilishi. Baadae harakati hizi ziilichochea
kuzaliwa kwa uliberali katika eneo la uchumi, muasisi wake akiwa Adam
Smith, ambae alihimiza umuhimu wa serikali kutoingilia shughuli za
kiuchumi, kwa mtazamo kwamba, serikali ikiachia shughuli za uchumi
zijiendeshe na kujisahisha zenyewe itapelekea ufanisi zaidi katika
uchumi. Katika dunia ya leo, Itikadi hii bado ina nguvu kubwa. Kuna
jamii nyingi duniani zinazo himiza umuhimu wa serikali kutojiingiza
katika shughuli za kiuchumi na kijamii, kwa mfano, serikali kukaa
mbali na na utoaji wa huduma za kijamii – afya, elimu n.k; na pia
serikali kutoshiriki katika uchumi kupitia mashirika ya umma, na
badala yake, mashirika binafsi pekee ndiyo yatawale shughuli za
kiuchumi.
2. ULIBERALI NA UHAFIDHINA
Itikadi hii ni mchanganyiko wa mawazo, sera na imani za uliberali na
uhafidhiana. Itikadi hii inaunga mkono ulegezaji wa masharti
mbalimbali ya kiuchumi na utandawazi, Pia inaunga mkono sera kali
zinazozuia uhamiaji.
Kiuchumi – itikadi hii inaunga mkono uwepo wa uhuru wa kiuchumi
miongoni mwa wananchi, hasa kuwapatia wananchi uhuru wa kujiamulia
mambo yao wenyewe. Itikadi hii haijihusishi sana na masuala ya kijamii
lakini kila inapobidi kufanya hivyo, huwa na msimamo wa kijamii ulio
sawa na ule wa kiliberali (rejea dhana ya uliberali hapo juu).
3. UHAFIDHINA.
Asili ya itikadi hii ni harakati za kupinga mapinduzi ya kumwondoa
mfalme wa Ufaransa katika karne ya kumi na nane. Uhafi maana yake ni
'kuhifadhi', hivyo wahafidhina hawaamini katika mabadiliko au
uharibifu wa desturi/utamaduni. Edward Burke ni muasisi wa itikadi
hii; yeye alipinga mapinduzi ya kumwondoa mfalme wa ufaransa kwa
mtazamo kwamba kitendo hicho kitaharibu desturi, imani na taasisi
zilizojengwa kwenye jamii kwa muda mrefu ambazo ni muhimu katika
maisha ya watu. Katika siasa za leo, wahafidhiana wanapinga ushiriki
wa serikali katika uchumi kwa madai kwamba, umaskini ndani ya jamii ni
matokeo ya serikali kuingilia maisha ya wananchi kwani kitendo hiki
hulea watu wavivu, na kuua dhana ya uchapa kazi na uwajibikaji katika
jamii. Badala yake, wahafidhiana wanahimiza kila mtu kujipatia riziki
yake kwa jasho lake, na sio kusubiri serikali kupitia huduma za
kijamii, n.k. wahafidhiana pia wanapinga uwepo wa mashirika ya umma
katika uchumi, na badala yake wanahimiza uchumi uendeshwe na mashirika
binafsi.
Katika siasa mpya, itikadi hizi kuu zimezaa itikadi nyingine tatu
kubwa ambazo ni: (1) Mrengo wa Kati; (2) Mrengo wa Kati-kulia; na (3)
Mrengo wa Kati-kushoto;
Ukomunisti>Ujamaa=>Ujamaa-wa-Kidemokrasia=>Uliberali=>Ulibe rali wa
Kihafidhina=>Uhafidhiana
1. Itikadi ya Mrengo wa Kati
Huu ni mrengo kati ya Uliberali na Ujamaa wa kidemokrasia. Kwa
kawaida, Itikadi ya mrengo wa kati inaamini na kuunga mkono mambo
makuu yafuatayo:
· Ongezeko la kodi linaloenda sambamba na ongezeko la vipato
vitokanavyo na shughuli za uchumi, Umiliki binafsi wa mali; Uhuru na
haki ya wananchi mbele ya sheria;
Uliberali wa kiuchumi na uliberali wa kijamii.
· Kuwapatia wananchi uhuru wa kujiendeshea shughuli zao bila ya
kuingiliwa na serikali; Umiliki wa mali binafsi; Serikali
kuratibu/rekebisha uchumi, lakini wanapinga serikali kukwaza uhuru wa
biashara na ushindani katika soko; wanaunga mkono sera za serikali za
kuondoa ukiritimba binafsi kwa imani kwamba ukiritimba huu unaumiza
wananchi maskini;
Uliberali wa jamii kwa maana
· Haki ya kijamii na uhuru kwa watu wote; Wajibu wa serikali kuinua
hali za maisha ya wananchi kwa njia kama vile – ajira, afya, elimu,
huku haki za wananchi zikizidi kuimarishwa.
2. Mrengo wa Kati-Kulia.
Huu ni mrengo uliopo katikati ya Uliberali na Uhafidhina-Uliberali.
· Kwa ujumla, itikadi hii inaunga mkono kanuni nyingi za soko huru;
lakini vilevile inapinga serikali kujiingiza kupita kiasi kwenye
shughuli za kiuchumi (kupitia mashirika ya umma); inapinga serikali
kujingiza kupita kiasi kwenye utoaji wa huduma za kijamii (kama vile
afya na elimu); na inaunga mkono umiliki wa mali binafsi;
3. Mrengo wa Kati – Kushoto
Huu ni mrengo uliopo kati ya Ujamaa wa Kidemokrasia na Ujamaa.
Mrengo huu unaamini katika yafuatayo:
· Jamii endelevu na serikali endelevu; Uliberali wa kijamii (rejea
hapo juu), na siasa za kijani, pia ina amini katika mchanganyiko wa
sekta ya umma na sekta binafsi kuendesha huduma za kijamii kama vile
elimu, afya n.k; Uwepo wa uhifadhi wa akiba ya kutosha kwa wananchi
wanaostahili tu (sio katika kiwango cha Ujamaa na Ukomunisti) ili
kupunguza kasi ya umaskini na kulinda 'vipato' vya wananchi wanaioshi
katika mazingira ya uzee (wastaafu), wagonjwa, walemavu na wasio na
ajira; mrengo huu pia una amini katika haki na fursa sawa kwa wote;
inaunga mkono uwepo na umuhimu wa taasisi za serikali zinazoratibu
sekta binafsi kwa nia ya kutetea wafanyakazi na walaji, kwa
kuhakikisha uwepo wa vyama imara vya wafanyakazi, na pia ushindani wa
haki katika soko; pia wanaunga mkono ongezeko la kodi linaloenda
sambamba na ongezeko la vipato katika uchumi, lengo kuu likiwa
kukusanya kodi ya kutosha ili isaidie kutoa huduma muhimu za kijamii
kwa wale wanaostahili
Sasa tuangazie itikadi za vyama vinne vyenye ufuasi mkubwa nchini
ambavyo ni NCCR MAGEUZI, CUF, CHADEMA na CCM.
1.NCCR MAGEUZI=>Mlengo wa KUSHOTO (Ujamaa wa kidemokrasia)
2. CUF=>Mlengo wa KULIA (Uliberali)
3.CHADEMA=> Mlengo wa KATI (Uliberali na Ujamaa wa kidemokrasia)
4.CCM=> Mlengo wa KUSHOTO (Ujamaa)
0 Comments:
Post a Comment