HATI YA MUUNGANO UTATA MTUPU HAIJULIKANI ILIPO

Utata umezidi kuibuka katika Bunge Maalumu la Katiba kutokana na kutopatikana kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.
Utata huo, umebainika katika Kamati kadhaa siku moja tangu wajumbe wa Bunge hilo waanze kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wake.
Jana Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa.
Nahodha alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano, Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali kadhalika.
Nahodha alisema baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.
Kauli hiyo ya Nahodha inapingana na kauli ya Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad ambaye jana alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kuipeleka bungeni Dodoma.
“Ile hati ya Muungano ipo Dar es Salaam, lakini tunahofia kuileta maana inaweza kupotea kwani ipo moja tu, sasa ambacho tutakifanya inaweza kutolewa nakala na kuthibitishwa na mawakili na ikaja nakala hapa Dodoma iwapo wajumbe wanahitaji,” alisema Hamad.
Nahodha alipoelezwa juu ya majibu ya Katibu wa Bunge kuwa hati hiyo ipo Dar es Salaam, alishikwa na mshangao na kusema wanamuomba Katibu huyo, aiwasilishe kama ipo.
Sheria za Muungano
Katika hatua nyingine, Sheria Namba 22 ya 1964 ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuridhia Muungano nayo haijulikani ilipo.
Baadhi ya wajumbe katika Kamati Namba 2 walidokeza kuwa, walipohoji kuhusu sheria hiyo walisomewa kitabu cha aliyewahi kuwa Mwanasheria wa Zanzibar, Abdul Jumbe na kuambiwa kwamba picha za ukumbusho zipo.


Nahodha ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, alikiri kuwa hata yeye hajawahi kuona sheria hiyo.
“Kwa Bunge la Tanganyika ushahidi tumeletewa hapa kuwa waliridhia Aprili 25, 1964 na waliosaini ni Julius Nyerere, Katibu wa Bunge hilo, Pius Msekwa na aliyekuwa Spika Adam Sapi Mkwawa, lakini kwa Zanzibar haupo,” alisema na kuongeza:
“Mimi nilikuwa mtendaji mkuu wa SMZ nilipaswa kujua, lakini nisingeweza tu kuanza kutafuta sheria, sheria ambazo zimetungwa Zanzibar ni nyingi, kwani ingeniwia kazi kubwa sana kuipata hati hii kwani msimamizi wake ni Ofisi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Ofisi ya Rais”.
Alisema Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman pia alisema hajawahi kuiona sheria hiyo.

0 Comments:

Post a Comment