Bodi ya wadhamini ya huduma ya Efatha, ambao
ni wamiliki wa shamba la Efatha, imemjibu
katibu mkuu wa CCM, Abdulrahamn Kinana
kutokana na kauli yake kuwa atahakikisha
Serikali inanyang’anya shamba hilo na
kulirejesha kwa wananchi.
Katika taarifa yake kwa umma, bodi hiyo
imesema mbali na kuwa hawakubaliani na
uamuzi huo, wanahoji kama mpango ni kuwapa
wananchi shamba hilo, ni lini wao (Efatha)
wamekoma kuwa wananchi wa Tanzania.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya waumini
wa Efatha ni wanachama wa CCM na wengine ni wafanyakazi wa Serikali iliyopo madarakani,
hivyo nao ni wananchi wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Efatha, shamba
hilo la Malonje lenye ukubwa wa hekta 15,000
lilikuwa linamilikiwa na Shirika la Maendeleo ya
Mifugo (DAFCO) na kwa mujibu wa sera ya
ubinafsishaji iliyopitishwa na Serikali
lilikabidhiwa kwa PSRC ili waliuze.
Baada ya kutotokea mnunuzi, PSRC waliamua
kutenga sehemu iliyokuwa na miundombinu,
lakini bado hakutokea mnunuzi ndipo
walipoamua kulikabidhi shamba hilo kwa Wizara
ya Maendeleo na Mifugo na Maji mwaka 2003.
Inaongeza taarifa hiyo kuwa mwaka 2004 wizara
ililikabidhi shamba hilo kwa Mamlaka ya Mkoa
wa Rukwa ili kuligawa katika vipande vidogo
ambavyo vingeuzika jambo ambalo pia
lilishindikana.
Inazidi kufafanua mwaka 2007, Serikali iliitisha
kongamano la wawekezaji na Efatha walipata
mwaliko na fursa ya kuomba kununua hekta
10,000 za shamba hilo kwa ajili ya kilimo na
mifugo, ombi lililokubaliwa kwa kununua
shamba hilo kwa bei ya Sh600 milioni.
Wiki iliyopita akiwa ziarani mkoani Rukwa,
Kinana alisema atahakikisha shamba la Efatha
alilodai limepokonywa kwa nguvu, linarejeshwa
kwa wananchi kwa madai kuwa Rais Kikwete
alishatoa agizo la kupatiwa hekta 8,000.
0 Comments:
Post a Comment