JESHI la polisi mkoani Arusha limefanikiwa kukamata bunduki tatu za
kivita zilizokuwa zikitumiwa na wananchi wa kabila la wasonjo na
wamasai kinyume cha sheria ,wilayani Ngorongoro katika mapigano
mbalimbali yaliyosababisha vifo kadhaa na majeruhi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kamanda wa polisi
mkoani hapa,Liberatus Sabas alitaja silaha hizo kuwa ni SAR yenye
namba za usajiri 20034823 ikiwa na risasi saba,SMG yenye namba NH-4200
ikiwa na magazine yenye risasi tano,pamoja na G3 yenye namba,D60365
kiwa na magazine yenye risasi 5.
Kamanda Sabas alisema kukamatwa kwa silaha hizo kumetokana operesheni
kambambe ya jeshi hilo kwa kushirikiana na wazee wa ukoo wa makabila
mawili ya Wasonjo na Wamasai katika vijiji vya Olorien na Mgongo
,wilayani humo.
Alisema kuwa operesheni hiyo imekuja kufuatia mapigano ya mara kwa
mara ya kulipiza kisasi baina ya makabila hayo,ambapo watu wa kabila
la wasonjo mnamo april 8 mwaka huu walivamia gari aina ya Landrover
linalodaiwa kumilikiwa na wamasai na kulishambulia kwa risasi .
Aliongeza kuwa tukio hilo lilisababisha vifo vya watu wawili akiwemo
mwanafunzi wa kidato cha tatu na kuwajeruhi wengine saba wakitoka
kwenye vijiji vinavyokaliwa na wasonjo.
Alisema tukio hilo lililenga kulipiza kisasi kwani kabla ya tukio hilo
mtu mmoja wa kabila la kimasai aliuawa wakati akitokea katika kijiji
cha Olorieni.
Alieleza kuwa baada ya mapigano hayo ambayo yamekuwa yakijitokeza mara
kwa mara wilayani humo,jeshi la polisi kwa kushirikiana na timu ya
wazee wa kimila kutoka makabila yote mawili waliunda tume ya
usuluhishi na kufanikiwa kupatikana silaha hizo.
Sabas alisema timu hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kurejesha hali
ya amani katika vijiji hivyo kwani baadhi ya wananchi walikubali
kusalimisha silaha zao walizokuwa wakitumia katika mapigano mbalimbali
ya makabila hayo mawili.
Alisema timu hiyo itasaidia kupatikana amani ya kudumu baina ya
makabila hayo hasimu kutokana na kujikita kwenye utatuzi wa migogoro
ya Ardhi ambayo imekuwa ikileta msunguano wa mara kwa mara na
kusababisha mapigano ya silaha za moto na jadi.
Alibainisha kuwa operesheni hiyo itakuwa endelevu na wataifanya muda
wote lengo ni kuhakikisha silaha zote zinazomilikiwa kinyume cha
sheria zinasalimishwa na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na
jeshi hilo kutoa taarifa za matukio ya viashilio vya uvunjifu wa
amani.
0 Comments:
Post a Comment