WABUNGE EALA KUMSHTAKI SPIKA WAO KWA WAKUU WA NCHI

SIKU moja baada ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki,(EALA), Dk Magreth  Zziwa kuahirisha bunge hilo kwa muda usiojulikana, wabunge wameahidi kulifikisha suala hilo kwa wakuu wa nchi wanachama.

Aidha wanaendelea kutafuta ushauri wa kisheria kwa Katibu wa Bunge na Mwanasheria wa jumuiya hiyo ili kuona namna wanaweza  kutumia kipengele cha 56(b) cha mkataba wa uundwaji wa EAC  kuchagua mmoja wa wabunge miongoni mwao kuongoza shughuli  za bunge kwa muda.

Pia wamesema kuwa mchakato wa kumng’oa spika huyo wanayedai kuwa uongozi wake haufuati misingi ya utawala bora utaendelea pindi bunge hilo likiitwa tena.

Tamko hilo lilitolewa jana kwenye ukumbi wa bunge ambapo lilisomwa na mbunge, Abdullah Mwinyi kutoka Tanzania kwa niaba ya wenzake 36 waliosaini kuunga mkono kung’olewa kwa spika ambapo wachache walikuwa ukumbini hapo chini ya uenyekiti wa muda wa mbunge, Ombasa Kyangoi kutoka Kenya.

Alisema kuwa kwa pamoja wanalaani kitendo kilichofanywa na spika cha kuvunja kwa makusudi kanuni taratibu na sheria zinazosimamia bunge hilo na kuahirisha bunge kabla ya muda mkutano wa bunge kwa madai kuwa kitendo hicho kimesababisha hadhi ya chombo hicho muhimu kushuka.

Mwinyi alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa bunge hilo Spika Zziwa  hakupaswa kuongoza kikao kilichokuwa kikimjadili alipaswa apishe ili katibu wa bunge aongoze kikao ambapo wangechagua mwenyekiti miongoni mwa wabunge.

“Wakati Mbunge Muthuki, (Peter kutoka Kenya) akianza kusoma utaratibu ili aweze kuwasilisha hoja iliyokuwa kwenye utaratibu wa shughuli za bunge za jana (juzi) ya kujadili hoja ya kumtoa Spika ofisini aliingiliwa na mbunge Bidde akiomba muongozo na spika akamruhusu,” alisema Mwinyi.

Alisema kuwa walishangazwa na hatua ya Spika Zziwa kukubaliana na hoja ya mbunge, Fred Bidde kutoka Uganda aliyedai kuwa kuna shauri alilofungua kwenye mahakama ya Afrika Mashariki, (EACJ) kuhusiana na hoja hiyo ya kumng’oa spika hivyo isijadiliwe huku kukiwa hakuna taarifa yoyote ya maandishi mezani.


Mwinyi alisema kuwa Sipka Zziwa aliamua kuahirisha bunge kwa muda usiojulikana licha ya kuwa Mwanasheria wa EAC, Wilberd Kahwa alimpa ushauri wa kisheria kuwa suala ambalo bado halijaanza mahakamani haliwezi kuzuia shughuli za bunge kuendelea.

Pia alisema kuwa mwenendo wa uendeshaji wa kikao hicho cha Aprili mosi, mwaka huu haukuwa wa kawaida hasa utaratibu aliotumia spika wa kuingia bungeni saa 10:00 jioni badala ya muda wa kawaida wa saa 8:30 bila wao wabunge kupatiwa maelezo yoyote.

“Tutamwandikia spika kumweleza kuwa taratibu na kanuni zilikiukwa hivyo tunajipanga upya kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa kumuondoa kwenye kiti kwa mujibu wa sheria,” alisema Mwinyi.

Hata hivyo juhudi za kumpata spika Zziwa kuelezea sakata hilo hazikuzaa matunda baada ya wasaidizi wake kuwaeleza waandishi wa habari kuwa wamsubiri kwenye ukumbi wa Spika wa watu mashuhuri, (VIP) ambapo walimsubiri kwa zaidi ya saa moja.

Baadaye majira ya saa 7 mchana,  Afisa Uhusiano mwandamizi wa Bunge hilo, Bobbi Odiko aliwaeleza wanahabari hao kuwa Spika Zziwa spika atatoa taarifa rasmi saa 9 alasiri hivyo akawataka kutawanyika kwa ahadi ya kuwatumia taarifa hiyo kwa njia ya barua pepe ambapo mpaka trunaenda mitamboni haikuwa imetumwa.
Katika Hatua nyingine wabunge hao wamepinga madai kuwa wanataka kung’oa Spika Zziwa kwa kuwa amewabana katika matumizi ya fedha ikiwemo posho jambo walilodai kuwa madai hayo hayana ukweli kwani kwa nafasi yake Spika hana mamlaka ya kuwapangia maslahi wala posho.

Tokea kuanza kwa mkutano huu wa bunge Machi 25, mwaka huu kumekuwa na harakati za kumng’oa  spika ambazo zilikuwa zikiungwa mkono na wabunge idadi yao kwenye mabano Rwanda, (9) ,Burundi, (9) Kenya, (5),  Tanzania, (5) na  Uganda anakotokea spika huyo wabunge watano walisaini kuridhia kung’olewa kwa spika huyo.

 Kwa mujibu wa kanuni ya tisa ya inayosimamia bunge hilo inaeleza kuwa baada ya hoja ya kumuondoa spika kuwasilishwa kwa katibu wa bunge inatakiwa ijadiliwe bungeni ndani ya siku saba ambapo wakati kamati ya Sheria ikichunguza madai yanayompelekea kuondolewa spika anaweza kusimama mwenyewe , kuweka mwanasheri au mtu yeyote kutetea.

Kanuni hiyo inaeleza kuwa spika atapisha kwenye kiti kuruhusu uchunguzi huo ambapo ili kumng’oa itapigwa kura ambapo inatakiwa iungwe mkono na theluthi mbili ya wabunge wote 45 walio kwenye bunge hilo.

Madai ya msingi ya wabunge hao yaliyowasukuma kumkataa  Spika Zziwa ni kuwa amepwaya kwenye nafasi hiyo kwani ameshindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo hali kutokana na udhaifu mkubwa wa kiuongozi alionao ambao hauzingatii utawala bora.

Madai mengine ni matumizi mabaya ya ofisi, kutowaheshimu na kuwabagua wafanyakazi na wabunge mambo yaliyopelekea wabunge kukosa imani naye.


Mwanzo mwa wiki iliyopita Mwenyekiti  wa Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Uhuru Kenyatta alilamizimika kufanya kikao cha dharura na wenyeviti wa wabunge toka nchi tano zinazounda jumuiya hiyo kwa kile kilichodaiwa ni kujaribu kutuliza harakati za wabunge hao kutaka kumng’oa Spika, Dk. Banbtonbg Zziwa.
Kikao hicho ambacho hakikuwa kwenye ratiba iliyotolewa asubuhi ya siku hiyo kilifanyika mara baada ya Rais Kenyatta kumaliza kuongea na waandishi ambapo muda huo alitakiwa kushiriki chakula cha mchana na wabunge wa EALA.

Kikao hicho kilichofanyikia kwenye ofisi ya spika kilidumu kwa dakika 40 ambapo alipomaliza alitoka na kuwapungia mkono wabunge na wafanyakazi wa jumuiya hiyo na kuondoka huku wabunge wa EALA waliokuwa eneo hilo wakionekana kuweka mkakati wa pamoja kuhakikisha hawabadilishi msimamo wa kumng’oa spika.

0 Comments:

Post a Comment