MBUNGE wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki (CCM), amemtuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuwa ameshindwa kumchukulia hatua aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Amani, ambaye amegoma kutii maagizo ya serikali.
Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu bungeni jana, Kagasheki alisema kuwa licha ya Rais Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kushughulikia mgogoro huo, ofisi ya waziri mkuu imekuwa kimya.
"Wananchi wa Manispaa ya Bukoba wako msibani, ofisi ya waziri mkuu haikuwajali. Tumekuwa na mgogoro wa meya na madiwani ambao umedumu tangu Aprili 2012 hadi leo Mei 2014.
"Rais tunamshukuru na CCM waliingilia kwa kuomba CAG afanye ukaguzi, ripoti ilikamilika na serikali ikatoa maagizo ya kumtaka Amani ajiuzulu na akafanya hivyo mbele ya naibu waziri wa Tamisemi, lakini baadaye akatangaza kuwa hakujiuzulu," alisema.
Kagasheki alisema kuwa kwa sasa manispaa hiyo imeingia kwenye vurugu, hakuna mipango ya maendeleo inayofanyika kwa sababu madiwani hawakutani, lakini ofisi ya waziri mkuu imekaa kimya.
"Aprili 30 mwaka huu, Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Kagera ameandika barua kwenda ofisi ya waziri mkuu, akieleza kuwa kwa uelewa wa mkuu wa mkoa, Amani alikwishajiuzulu nafasi ya umeya.
"RAS alitaka ufafanuzi wa waziri mkuu kuhusu utata huo, lakini hadi leo hakuna majibu. Hii ni aibu, uamuzi umefanyika lakini uwajibishaji hakuna. Tunataka majibu kama huyu ni meya au hapana," alisisitiza.
Kagasheki alisema kuwa hayo ni maneno ya wakazi wa Bukoba ambao hawafurahishwi na utendaji wa serikali wakati CAG alishafanya ukaguzi, lakini hakuna hatua zimechukuliwa kwa zaidi ya miezi mitano sasa.
"Hili jambo ni 'very serious' maana mimi nimekuwa waziri kwenye serikali, lakini nikafanyiwa hivi muda wote huu, sasa fikiria itakuwaje kwa mbunge wa kawaida?" alihoji Kagasheki huku akiuliza kama waziri mkuu anamsikiliza kwa vile alikuwa akisemeshwa.
Baada ya Kagasheki kuketi, Mbunge wa Viti Maalumu, Paulin Gekul (Chadema), aliomba mwongozo wa spika, akihoji inakuwaje waziri mkuu anasumbuliwa bungeni wakati masuala ya msingi yakizungumzwa.
"Malalamiko ya Kagasheki ni ya kweli, Manispaa ya Bukoba ina mgogoro na hata bajeti yake haikujadiliwa na kamati yetu maana iliandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa. Mgogoro kama huo uko pia Manispaa ya Ilemela.
"Sasa wabunge wanaeleza matatizo hayo halafu kuna wabunge wanakwenda kumpigisha stori," alisema Gekul na kisha Naibu Spika, Job Ndugai kuwataka wabunge wasiende kumsumbua waziri mkuu.
0 Comments:
Post a Comment