LISSU ASABABISHA KESI ZA LEMA ZIAHIRISHWE


KESI mbili za uchochezi zinazomkabili mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), zimeshindwa kuendelea kutokana na mbunge hiyo kuwa Nairobi, Kenya alipoenda kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayepatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa kwenye tukio la gari lake kushambuliwa na risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana.
Wakili wa Lema, Sheki Mfinanga jana aliieleza mahakama mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha,Jasmine Abdul, kuwa mteja wake yuko nchini Kenya hivyo akaomba shauri hilo lipangiwe siku nyingine 

Mashauri hayo yalifika mahakamani hapo kwa ajili ya Lema kusomewa hoja za awali ambapo wakili wa Serikali, Fortunatus Mhalila alisema walikuwa wako tayari kwa ajili hiyo ingawa hakuwa na pingamizi la kuahirishwa kwa mashauri hilo.

"Kwa kuwa mshitakiwa hayupo na Hakimu Devotha Msofe aliyekuwa akisikiliza kesi hii hayupo, tunaomba mahakama iahirishe kesi na kupanga tarehe nyingine ili tuendelee na hoja za awali kwa Msofe," aliomba Wakili huyo.

Hakimu Jasmine aliahirisha shauri hilo mpaka Oktoba 24, mwaka huu litakaporudi kwa ajili ya Lema kusomewa hoja za awali.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo katika kesi namba 440/2016 kuwa mnamo oktoba 22, mwaka uliopita Lema akiwa maeneo ya Kambi ya fisi, Ngarenaro jijini hapa kwenye mkutano wa CHADEMA alitoa kauli za uchochezi.
" Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani ipo siku Taifa hili litaingia kwenye umwagaji damu...Rais yeyote ambaye aheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya katiba, Rais huyo ataingiza Taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza," wakili mkuu wa Serikali, Martenus Marando alinukuu maneno yanayodaiwa kuwa ni uchochezi wanayodaiwa kutolewa na Lema
Katika shauri namba 441/2016 Lema anakabiliwa na  mashtaka mawili ya uchochezi ambapo anadaiwa kutoa maneno yenye chuki na yenye kuibua nia ovu kinyume cha sheria ambapo  anadaiwa kutenda makosa hayo oktoba 23, mwaka jana.
Kosa la kwanza anadaiwa kulitenda Kwenye shule ya sekondari Buraa kata ya Buraa ambapo anadaiwa kusema " kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu elfu mbili na ishirini (2020), haitafika Mungu atakuwa amechukua maisha yake, Rais ana kiburi, rais kila mahali watu wanaonewa, wafanyakazi wa serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani, watu wananyanyaswa,".
Kwenye kesi hizo Lema, anawakilishwa na Wakili Sheck Mfinanga huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali,Riziki Maayu.

0 Comments:

Post a Comment