KESI YA INAYOMKABILI MMILIKI LUCKY VICENT YAKWAMA




KESI inayomkabili mmiliki wa shule ya Lucky Vicent,  Innocent  Moshi, (56), imeshindwaa kuendelea leo baada ya hakimu mkazi Mfawidhi, Desder Kamugisha  anayesikiliza shauri hilo kutokuwa mahakamani.

Shauri hilo linalovuta hisia za wengi liliahirishwa na hakimu mkazi, Jasmine Abdul ambaye haueleza  sababu za hakimu Kamugisha kutokuwepo mahakamani hapo.

Wakili wa Serikali, Alice Mtenga aliieleza mahakama kuwa walikuwa wameleta mashahidi wawili ambapo mmoja alijitambulisha mahakamani hapo, Mohammed Mutumula kutoka kampuni ya uwakala wa bima ya Zanzibar.

Hakimu Jasmine aliahirisha shauri hilo mpaka novemba 16, mwaka huu litakapoendelea kwa upande wa Jamhuri kuendelea kuleta mashahidi wake kwani mpaka sasa ni mashahidi watatu wameshafika mbele ya mahakama hiyo Mkuu wa Usalama barabarani mkoani Arusha, Nuru Seleman, (43).

Nuru alipotoa ushahidi wake alidai kuwa gari lililokuwa limebeba wanafunzi wa Lucky Vicent na kupata ajali Mei 6,  mwaka huu wilayani Karatu lilikuwa na leseni ya kusafirisha abiria kati ya Arusha, Mbuguni  na Mererani wilaya Simanjiro.

Aidha, kwenye ajali hiyo iliyosababisha vifo vya wanafunzi 32 waalimu watatu, imeelezwa kuwa bima ya gari hilo ilikuwa haijamaliza muda wake ila ilikuwa inasoma jina la Swalehe Kiluvia aliyekuwa akimiliki gari hilo kabla ya kuliuza kwa kampuni ya Lucky Vicent Limited.

Nuru aliieleza mahakama kuwa leseni ya gari hilo ilimalizika muda wake Mei 15, mwaka huu hata hivyo alisema kuwa lilipaswa liwe na leseni ya muda ya kuwawezesha kuelekea wilayani Karatu.

"Gari lilipaswa iwe imeshakaguliwa na kupakwa ranging ya njano kwa ajili ya kubeba wanafunzi na ingekuwa na leseni ya Usimamizi ya Usafirishaji nchi kavu na majini, (SUMATRA), ya kubeba wanafunzi," alisema RTO Nuru akiongozwa na wakili wa Serikali, Nuda.

Shahidi wa tatu kwenye shauri hilo, Afisa wa Idara ya Kazi mkoani Arusha, Wilfred Mdumi, (38), aliieleza mahakama kuwa baada ya kuupitia mkataba wa kazi wa aliyekuwa dereva wa basi hilo, Dismas Gasper walibaini haukuwahi kuhakikiwa na kusainiwa na ofisa wa ofisi yao hivyo kukosa hadhi ya kuwa mkataba halali.

Kwa upande wake shahidi wa kwanza Koplo Hamad aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio yeye aliwahi eneo la tukio kwenye kijiji cha Thotia  baada ya kuarifiwa ambapo alikuta basi hilo likiwa limeanguka kwenye bonde la Marera.

Alisema alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kufika eneo hilo akiwa na gari la polisi aina ya toyota Landcruizer yenye namba za usajili PT 1839 ambapo aliwakuta watu wasiozidi sita kwenye eneo hilo wakasaidiana nao kutoa majeruhi na miili ya marehemu ambayo mingi ilikuwa imebanwa na gari.

Alisema baada ya kuwapeleka hospitali ya Lutherani majeruhi sita na miili ya watu 32 walikuwa wamefariki alirudi eneo la tukio na kuchora ramani ya eneo la ajali ambayo aliikabidhi makamani hapo.

 Awali katika kesi hiyo ambayo mmiliki wa shule ya Lucky Vicent, Innocent Moshi anakabiliwa na mashitaka manne huku mwalimu Mkuu msaidizi  Longino Nkana, (38) akikabiliwa na shitaka moja.

Shauri hilo namba 78/2017 linalovuta hisia za wengi jijini hapa wanadaiwa  kuruhusu abiria 13 waliozidi kuingia kwenye gari kinyume na utaratibu na sheria za usalama barabarani na kusababisha vifo vya wanafunzi 32,walimu wawili na dereva mmoja .
Nuda alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa kwanza anadaiwa  mnamo Mei 6, mwaka huu eneo la kwa Morombo  akiwa mmiliki wa gari aina ya Mitsubishi Rosa, lenye namba za usajili T 871 BYS, aliruhusu gari hilo kufanya biashara ya kubeba abiria likiwa halina leseni.
Alisema katika shitaka la pili Moshi anadaiwa kuruhusu gari hilo kuendeshwa bila kuwa na bima na shitaka la tatu ni kushindwa kuwa na mkataba na dereva wake ambaye kwa sasa ni marehemu,Dismas  Gasper.
Mmiliki huyo wa Lucky Vicent alisomewa shitaka la  nne  analodaiwa kuruhusu gari lake kubeba abiria waliozidi uwezo wa gari ambapo abiria 13 walizidi.
Mnamo Mei 6, mwaka huu wanafunzi 32 ,walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent waliofariki kwa ajali eneo la Rhotya ,wakielekea mjini Karatu katika shule ya msingi Tumaini kufanya mtihani wa ujirani mwema.

0 Comments:

Post a Comment