MAHAKAMA YAELEZWA NAMNA LEMA ALIVYOSEMA RAIS MAGUFULI ANAWEZA KUSABABISHA MACHAFUKO


MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), amedaiwa kusema kuwa Rais John Magufuli akiendelea kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani Taifa litaingia kwenye umwagaji damu.

Wakili wa Serikali, Agnes Hyera, aliyasema hayo leo mbele ya hakimu mkazi Mfawidhi, Devota Msoffe wa mahakama ya wilaya ya Arusha, wakati akimsomea Lema maelezo ya awali.

Alieleza kuwa  Lema anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi  Oktoba 22, mwaka jana wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara eneo la Kambi ya Fisi,Kata ya Ngarenaro jijini Arusha.

"Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongwa upinzani iko siku Taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu.Rais yoyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria,katiba Rais huyo ataingiza Taifa katika majanga ya umwagaji damu, watu watajaa vifua wakiamua kulipuka polisi wala jeshi hamtaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza," wakili Hyera alimnukuu Lema.


Wakili huyo aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa maneno hayo yalikuwa yanasababisha uchochezi kwa watu yakiwa na nia ya kusababisha machafuko katika Taifa.

Wakili Hyera alisema baada ya mkutano huo kumalizika baadhi ya wananchi na askari polisi waliokuwa katika mkutano huo walitoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kati,jijini Arusha.

Aliieleza mahakama hiyo kuwa baada ya hapo mshitakiwa Lema alikamatwa na kufikishwa katika kituo hicho kwa mahojiano ambapo alikataa kutoa maelezo yake.


Wakili huyo wa Serikali alisema baada ya hapo hati ya mashitaka iliandaliwa na mshitakiwa alifikishwa mahakamani kujibu shitaka hilo lanuchochezi.

Lema alikana mashitaka hayo ambapo yupo nje kwa dhamana

Wakili Hyera alisema upande wa Jamhuri umejipanga kuleta mashahidi wasiozidi 10 ambao hakuwa tayari kuwataja majina.

Hakimu Msofe ameahirisha shauri hilo mpaka novemba 27, mwaka huu litakaposikilizwa siku tatu mfululizo mpaka novemba 29, mwaka huu.



0 Comments:

Post a Comment