CHADEMA waitaka NEC Kuiondoa jimbo la Longido kwenye uchaguzi wa marudio

Katibu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini Mh. Amani Golugwa

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) mkoani Arusha kimeitaka tume ya taifa ya uchaguzi(Nec) kusitisha na kuliondoa jimbo la Longido kwenye uchaguzi wa marudio kwa kuwa kuna kesi ya msingi mahakamani.

Hivi karibuni Nec ilitangaza majimbo matatu kuwa wazi ambayo ni Longido,Singida Kazkazini pamoja na jimbo la Longido ambapo uchaguzi wa marudio umepangwa kufanyika mwezi ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya Chadema mkoani Arusha,katibu wa Chadema kanda ya kazkazini,Aman Golugwa aliitaka Nec kusitisha mchakato wa uchaguzi katika jimbo la Longido kwa kuwa kuna kesi ya msingi mbele ya mahakama ya rufaa kanda ya Arusha.

Golugwa,aliwaambia waandishi wa habari kwamba shauri hilo limewasilishwa mbele ya mahakama ya rufaa na kusajiliwa kwa kupewa nambari 35 mwaka 2017.

“Tunaiomba Nec iiondoe jimbo la Longido kwenye uchaguzi wa marudio kwa kuwa kuna shauri liko mahakama ,tunaiomba mahakama ya rufaa isikilize rufaa yetu kwanza na tunaamini katika misingi ya kisheria”alisema Golugwa

Amesema kwamba katika kusisitiza suala hilo Chadema tayari wamemwandikia msajili wa mahakama ya rufaa sanjari na ofisi ya mkurugenzi wa uchaguzi kumuomba aiondoe Longido kwa kuwa shauri hilo liko mahakamani.
Golugwa,alifafanua kwamba hukumu ya kesi ya ubunge wa jimbo la Longido ilitolewa mnamo mwezi oktoba 30 mwaka huu ambapo mahakama hiyo ilitoa muda kwa upande ambao haujaridhika na hukumu hiyo kuwasilisha rufaa ndani ya siku 14 ambapo mnamo Novemba 13 mwaka huu waliwasilisha rufaa hiyo na kisha kupokelewa.
Alifafanua kwamba wameshangazwa na hatua ya mahakama ya rufaa kanda ya Arusha kuwasilisha cheti mbele ya Nec mnamo Novemba 7 mwaka huu bila kutambua ya kwamba chama chao tayari kimeshawailisha kusudio la kukata rufaa dhidi ya   hukumu hiyo.

“Nec walipaswa kufuatilia kote kote walipaswa kuangalia je mbele mahakama ya rufaa hakuna rufaa yoyote iliyowasilishwa mbele ya mahakama hiyo ?sisi tunatarajia rufaa yetu muda wowote itaitwa mahakamani”alisema Golugwa

Hatahivyo,aliyekuwa mbunge wa jimbo la Longido,Onesmo Ole Nangole alisema kwamba linapokuja suala la haki mahakama haina budi kutenda haki na hivyo kuiitaka Nec kuiondoa Longido katika mchakato wa uchaguzi.

Ole Nangole alisema kwamba kumekuwa na ujanja ujanja unaofanywa katika kesi hiyo wa kutotaka kesi ya msingi isisikilizwe kwa kuwekwa pingamizi kila mara huku akisisitiza kwamba yeye haogopi uchaguzi wa marudio.

“Hatuogopi uchaguzi wao CCM ndio walienda mahakamani lakini upande wa pili wamekuwa wakipambana  kesi ya msingi isisikilizwe kwa kuweka pingamizi kila mara lakini nawahakikishia kesi siki ikisikilizwa ni aibu hakuna kesi pale”alisisitiza Ole Nangole

0 Comments:

Post a Comment