LIVE KUTOKA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI


BUNGE la Afrika Mashariki,(EALA) leo inaendelea na kikao cha siku ya pili baada ya jana kushindwa kuchagua spika kutokana na sintofahamu iliyoibuka juu ya ni nchi gani inapaswa kushika nafasi ya uspika baada ya wagombea kujitokeza kutoka Tanzania Rwanda na Burundi.

Aliyechukua fomu kwa Tanzania ni Adam Kimbisa ambapo baadhi wanapinga hatua yake hiyo kwani Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kushika nafasi hiyo hivyo hatua yake inaenda kinyume na mkataba wa kuanzishwa jumuiya ya Afrika Mashariki,(EAC) unaosema bayana kuwa nafasi hiyo itashikwa na nchi wanachama kwa mzunguko.

Hivyo Tanzania inapaswa isubiri nchi zote sita zishike nafasi hiyo ndipo iweze kuweka mgombea hoja ambayo Mjumbe mmoja kutoka Tanzania aliyeongea na blog hii kwa sharti la kutoandikwa jina lake alikiri ni kweli ila wamefikia uamuzi huo kwa maslahi ya EAC.

“Wakuu wa nchi za Rwanda na Burundi hawaelewani hivyo hata wa chini yao hawana mawasiliano mazuri hivyo kumweka spika kutoka moja ya hizo nchi kinaweza kukwamisha shughuli na utendaji wa bunge kwani hataweza kufanya mawasiliano na mkuu wa nchi ambayo mahusiano yao si mazuri sisi tumeamua kuweka mgombea ili kutatua hili tatizo na kuinusuru jumuiya ,” anasema mbunge huyo wa Tanzania.

Kwa upande wake Burundi, Le’ontine Nzeyimana amechukua fomu kugombea nafasi hiyo kwa hoja kuwa wao hiyo ni zamu yao na wanastahili kwani kwenye mkataba imeandikwa nchi zishike nafasi kwa mzunguko na wao hawajashika huku wakitaka waachiwe wagombee wenyewe kwa kuweka wagombea toka nchi yao kama ilivyofanyika kwenye awamu tatu zilizopita.

Hata hivyo walienda mbali zaidi wakitaka nchi zipangwe kwa alfabeti hivyo inayoanza ndo ipewe nafasi ambapo wao ndiyo wanakuwa mbele ya Rwanda hivyo katika kushinikiza hilo waliamua kutoka nje pamoja na Tanzania kila nchi ikitaka kupewa fursa hali iliyofanya kikao kukwama kwa siku nzima ya jana na huenda ikawa hivyo kwa siku ya leo.

 Rwanda mgombea wa nafasi hiyo akiwa ni Martin  Ngoga ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda hata ikitokea uchaguzi huo ukawahusisha wagombea wote muda wote alikuwa ndani ya ukumbi pamoja na wabunge wa Rwanda, Kenya, Uganda na Sudani ya Kusini ambao hii ni mara yao ya kwanza kuleta wawakilishi kwenye chombo hicho cha kutunga Sheri cha EAC.

Hata hivyo Rwanda wanadai kuwa hii ni nafasi yao kushika uspika wa EALA kwani kwa sasa Katibu Mkuu wa EAC, Liberati Mfumukeko anatokea Burundi hivyo haiwezekani spika ambaye anatakiwa kumsimamia naye akatoka nchi hiyo kwani zoezi hilo halitafanyika ipasavyo hivyo wanaona ni vema spika akatoka Rwanda.

Wanaenda mbali kudai kuwa Sudani ya Kusini wangeweza kuweka mgombea wasingepinga lakini kwa kuwa ni wapya hawana uzoefu hivyo hawawezi jambo walilosisitiza kwa bunge hili Rwanda ndiyo anapaswa kushika uspika.




0 Comments:

Post a Comment